Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi)

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika kwanza naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyenzi Mungu kwa kunipa fursa hii ya kuweza kusimama hapa katika Bunge lako Tukufu ili nami niweze kuchangia katika Wizara ya Mambo ya Ndani.

Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. John Joseph Magufuli kwa kuona umuhimu wa kutenga fedha bilioni 10 kwa ajili kwenda kuboresha makazi ya askari wetu. Hali kadhalika vituo vya polisi vingi vimetengewa fedha kwa ajili ya kuendeleza ujenzi huo na Wabunge wengi wamesimama humu wametoa ushuhuda na mpongeza sana Mheshimwia Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika,nimpongeza Waziri mwenye dhama ya Wizara hii ndugu Kangi Lugola unafanya kazi nzuri sana chini ya majeshi yako yote ya Polisi, Magereza, Uhamiaji pamoja na Zima Moto. Ukisikia jirani yako anapiga kelele ujue sindano zinaingia vizuri na unafanya kazi vizuri. Itakuwa ni ngumu sana kwa jeshi la polisi kupewa sifa ya kwamba mnafanya vizuri yaani mpokuwa mnaambiwa hamfanyi vizuri kwa upande wa pili kwamba mpo sawasawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwasihi kwamba kamanda Sirro endelea kufanya kazi sisi wenye nia njema tunaona kabisa kazi unayofanya ni nzuri ulinzi umeimalika katika nchi yetu ya Tanzania watu wamekuwa na nidhamu kazi zinafanyika kwenye maeneo mbalimbali hata vijana waliokuwa wanashinda vijiweni vibaka nao pia wamepungua sana hongera sana kama Sirro. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie suala la kasma ya mafuta kwa jeshi la polisi, magereza na maeneo mengine. Pesa imekuwa inatengwa kidogo kuelekea kwenye maeneo hayo ili waweze kutimiza shughuli zao. Inafika kwa muda mfupi sana unakuta pesa inaisha wanashindwa kutimiza wajibu wao. Kwa hiyo, naomba majeshi haya yote yatengewe fedha ili waweze kufanya shughuli zao kwa maana ya kupata mafuta yanayotosheleza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia kasma ya vipuli magari yameongezwa nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kuongeza magari katika jeshi la polisi. Lakini pia vipuli navyo viongezwe kwa sababu vipuli bado ni vichache kwa hiyo wanashindwa kufanya mategenezo pale inapotokea magari yanapata uharibufu.

Mheshimiwa Spika, zipo stahiki za maskari ambazo wanashindwa kuzipata kwa mfano kuna suala plain clothes ambalo ni allowance kwa ajili ya CID. Hii allowance hawaipati kwa hiyo nilikuwa naomba sana watengewe fedha kwa ajili ya kupata hiyo allowance ili waweze kufanya kazi yao vizuri. Lakini pia kuna house allowance, house allowance inatakiwa 15% ya mshahara wa kila askari lakini hawapati kwa hesabu hiyo ya 15% naomba wapigiwe kwa 15% ili waweze kupata allowance hiyo.

Mheshimiwa Spika, mafao ya askari polisi, askari polisi wamekuwa wakipata mafao lakini hayo mafao yanachewa sana, siku za nyuma walikuwa wanatumia karibu mwaka mmoja na nusu ili waweze kupata mafao baada ya kustaafu. Lakini sasa hivi imepungua walau mwaka mmoja. Niombe Serikali ipunguze zaidi sababu askari wetu wanapokuwa wamestahafu kuendelea kukaa katika hali ya manung’uniko hawapati fedha zao kwa wakati nayo pia haileti tija kwa sababu kazi yao ni gumu na wanafanya kazi pia wakati mwingine katika mazingira magumu wamapate fedha zao kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, lakini pia hawa askari inapotokea askari amefariki wanaobaki ndugu zao kuhusu suala la mirathi wanapata shida sana wanatumia muda mrefu sana kupata mirathi ya ndugu zao. Kwa hiyo, naomba sana Serikali izingatie suala hili hasa pale tunapojua kwamba umuhimu wa jeshi la polisi kama ambavyo Wabunge wengine wamezungumza humu kwamba jeshi la polisi linafanya kazi nzuri na sisi tumo humu ndani kwa utulivu kwa sababu jeshi la polisi linafanya kazi yake barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie pia suala la fidia kwa askari magereza na askari polisi. Inapotokea kwa majeshi haya inapotekea amepata madhara kazini, ameumia kazini sheria ya tume ya polisi namba 25 inaeleza kwamba askari huyu baada ya kuumia alipwe pesa apate fidia. Lakini haielezi kwamba fidia ile anayoilipwa inatoka katika fungu gani? Sasa leo hii naomba nishauri Serikari yangu, kwamba kwanini Serikali isikae pamoja na jeshi la polisi wakazungumza na wakaweza kuchukua utaratibu wa hawa askari wote wakaunganishwa kwenye mfuko wa fidia badala ya hawa askari baada ya kupata matatizo wanajikuta kwamba wanasubiri yale mafao ambayo hayajulikani yanatoka fungu gani ni mpaka waombe benki kuu. Kwa hiyo, naomba sana suala hili lisimamiwe na lizingatiwe.

Mheshimiwa Spika, askari wetu hawa nao pia ni binadamu, ambao wameumbwa kwa mfano wa kila binadamu hapa ndani kwa maana ya Mungu. Hawa askari hawana moyo wa chuma wana moyo wa kibinadamu, wana moyo wa nyama.

Mheshimiwa Spika, inapotokea mtu anasimama humu katika Bunge lako hili Tukufu anawatuhumu askari. Jana amesimama Mbunge mmoja humu ndani akazungumzia suala la askari kuwabaka, kuwalawiti wanawake wanaokwenda kwenye vituo vya polisi. Miongoni mwa vituo ambavyo alivitaja ni pamoja na kituo cha Mtakuja Dar es Salaam na Staki shari na vingine lakini miongoni mwa hivyo. Sasa najiuliza ni kweli askari hawa wanafanya vitendo vya aina hii? Na kama ndivyo ni kwa nini aleze kwa maana askari wote…

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. JACQUELIN N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, na kama ndivyo kwa nini asichukuliwe akatoa ushahidi?

SPIKA: Mheshimiwa Jacqueline kuna taarifa.

T A A R I F A

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, napenda kutoa taarifa yangu kwanza nisikitike, anayechangia ni mwanamke. Jana nimechangia nikasema mabinti wanabakwa, wanatendewa kinyume na maumbile wanaambukizwa na UKIMWI niseme tu hii sio mara ya kwanza nimeongelea Bungeni. Alikuwa anakuja RCO kutoka Kanda Maalum gerezani tulimueleza na mifano. Nilipotoka tu gerezani niliongea na waandishi wa habari nilisema sasa ukiona Mbunge anabisha badala kwenda kusema!

SPIKA: Ulisema kwamba?

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, kwamba kuna mabinti wanatendewa ndivyo sivyo na wapo wanabakwa, wanaingiliwa kinyume na maumbile wanaambukizwa na UKIMWI na nikataja maeneo ya vituo ambavyo wametaja, na walivyokuja gerezani walisema wanaenda kufuatilia. Sasa na RCO kutoka Kanda Maalum sasa ukiona Mbunge ambaye amekuja kuwatete wananchi anatetea vitu anapindua, inabidi aombewe na inasikitisha sana. Polisi nimetoa taarifa ni chombo ambacho tunaongea huku Bungeni, wataeenda watafuatilia wataona the validity ya hiyo kitu na sio vinginevyo. Naomba sana Bunge hili litumike kushauri na kukemea na sio kutetea. (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana, nafikiri ulikuwa unampa taarifa

MHE. ESTHER N. MATIKO: Kama mnawapenda polisi mgeweza kubadilisha hata leo bajeti tukaingoza tukawajengea majumba wanateseka au tukawaongezea mshahara.

SPIKA: Ahsante sana inatosha Mheshimiwa Msongozi unapokea taarifa hiyo!

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, ninayezunguza ni Mwanamke na nina uchungu na wanawake wenzangu na walionileta ndani ya humu ndani ya Bunge hili ni wanawake. Siwezi kufurahia mwanamke mwenzangu analawitiwa, amekuwa na haraka ya kuyadaka maneno kabla ya kusikiliza nini ninachokisema angesubiri akaona concern yangu nini. Nasikitika sana kwa kudaka daka maneno. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nataka niseme hivi, huyo Mbunge ambaye ameeleza habari hii kama kweli vitendo hivyo vipo awataje hao polisi wanaofanya hivyo ili waweze kuchukuliwa hatua, kwa sababu vitendo hivyo kwa wanawake wenzetu sisi hatukubaliani kama wanawake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini isiwe kwamba Askari wote wanapakwa matope hayo, a-specify ni nani na nani? Ina maana kwamba leo hii kwa watu ambao wamesikiliza ile clip wanawake wote wataogopa kwenda kwenye Vituo vya Polisi, wanaogopa kubakwa na kufanyiwa vitendo vya ulawiti. Kwa hiyo, a-specify. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, naomba hili suala lisichukuliwe kimzahazaha asaidie Polisi ili kutoa ushuhuda wa kina ili Polisi na Serikali walifanyie kazi kwa sababu mwisho wa siku isiwe ni katika hali ya udhalilishaji kwa Jeshi la Polisi.

Mheshimiwa Spika, naomba niseme hivi, nakubaliana na wale wote ambao hawakubaliani na suala la maandamano, lakini pia hawakubaliani na suala la mikutano holela holela. Sisi kama Wabunge ziko kazi tumepewa na wananchi kwenda kuzifanya. Nashangaa sana Mbunge anasimama hapa, toka lilianza Bunge yeye anazungumzia maandamano tu. Naweza nikafananisha na mnyama mmoja anaitwa nyumbu.

Mheshimiwa Spika, tabia ya mnyama anaitwa nyumbu anafanana hivi; mmoja akiongoza njia kwenda, basi wote wanakwenda huko hata kama kule kuna samba, wote wataelekea huko; hata kama kuna shimo, wote wataelekea huko. Sasa hivi humu ndani ya Bunge hamna agenda nyingine, ni kuongelea tu suala la maandamano, suala la Askari wamefanya nini.

Mheshimiwa Spika, suala la mikutano nasema nampongeza Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, mikutano yote isiyokuwa na tija ikomeshwe. Hakuna mikutano, watu wakafanye kazi. Watu walikuwa wamezoea kuchukua vijimambo vidogo vidogo, anabeba kama dili anaenda nalo kwenye mkutano kupotosha watu na kufanya mambo yasiyostahili.

Mheshimiwa Spika, naomba sana nipongeze Jeshi la Polisi, Kamanda Sirro kazia hapo hapo, endelea kufanya kazi yako, tuko nyuma yako. Sisi tutakutetea na tutakusaidia.
(Makofi)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, tunataka nchi iwe na amani, nchi iwe na utulivu badala ya watu kufanya mambo yao binafsi.

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Jacqueline Msongozi.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja asilimia kwa asilimia mia moja. (Makofi)