Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Deo Kasenyenda Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makambako

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweza kuchangia. Kwanza naunga mkono hoja kwa kazi nzuri inayofanywa na Jeshi la Polisi ikisimamiwa na Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wanafanya kazi nzuri sana ya kutulinda sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jana nilikuwa nasikiliza wachangiaji wenzangu hasa upande fulani, hebu fikiria Jeshi la Polisi na Mahakama visiwepo angalau kwa siku moja nini kitatokea? Ni lazima tumpongeze Waziri kwa kazi nzuri ambayo anafanya kupitia Jeshi la Polisi la kutulinda sisi na mali zetu na nchi kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, Njombe tulipata tatizo la mauaji ya watoto. Jeshi la Polisi lilifanya kazi kubwa ya kuwakamata wahusika, hivi sasa wanajibu tuhuma walizozifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini nizungumzie kwenye Jimbo la Makambaku, mwaka 2016/2017 kulikuwa na mauaji vijana wengi walikuwa wananyang’anywa bodaboda zao na wanauwawa. Jeshi la Polisi limeweza kuwakamata wote waliokuwa wanafanya vitendo hivyo. Nampongeza Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama - Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya - Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama, RPC na OCD na wapelelezi wake wa Jimbo la Kiwilaya la Kipolisi pale Makambaku. Wamefanya kazi nzuri sana, walikamata mpaka magaidi pale Makambaku, wale ambao walikuwa wanafanya mauaji kule Kibiti wamekamatwa pale na Jeshi hili hili la Polisi. Kwa hiyo, ni lazima tulipongeze sana kwa kazi nzuri ambazo wanazifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili niwapongeze kwa kujenga nyumba za askari wetu kwa nchi nzima na hususan kwenye Mji wetu wa Makambaku. Tangu tupate uhuru hatujawahi kupata nyumba za Jeshi la Polisi, safari hii tumejengewa nyumba na wanaendelea kujenga nyumba nzuri za kukaa Askari wetu. Hata mimi Mbunge wao nimeweza kuchangia kwa asilimia kubwa kufanikisha nyumba zile ambazo Serikali ya Magufuli imetupa fedha. Nawapongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri ambayo mnaifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Makambaku ndiyo njia panda ya kwenda Songea, Mbeya, Iringa, tunaomba utupe gari ili Askari hawa waweze kufanikisha shughuli zao za kidoria kwenye Mji wetu wa Makambaku. Tunaomba sana tupate gari ambalo litasaidia kufanikisha shughuli za kiusalama katika Mji wetu wa Makambaku.

Mheshimiwa Spika, vilevile gereza liko Wilayani Njombe, kupitia Wizara hii ya Mambo ya Ndani tunaomba waone umuhimu wa kujenga gereza katika Halmashauri yetu ya Mji wa Makambaku. Sisi wa Makambaku tutawatafutia eneo la kujenga gereza kwa ajili ya wahalifu ambapo kwenda Njombe ni mbali. Kwa hiyo, eneo lipo, nikuombe sana Waziri mwenye dhamana uone namna ya kutenga fedha kwa kipindi kinachokuja ili kujenga gereza katika Mji wetu wa Makambaku.

Mheshimiwa Spika, nizungumze jambo la mwisho, pamoja na kazi nzuri si vizuri kuwataja hawa Askari lakini kupitia Bunge lako naomba niwataje kwa sababu ya kazi nzuri wanayofanya, akiwepo OCD wa Mji wa Makambaku, Mkuu wa Upelelezi pamoja na timu yake ya askari kadhaa wanaofanya kazi nzuri ambapo waliweza kufanikisha kukamata silaha mbalimbali katika mji wetu. Naomba muone namna ya kuwapandisha madaraja hawa askari kwa namna ambavyo wanafanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wapo askari kadhaa ambao labda wakati fulani wanaweza kuwa si wazuri …

SPIKA: Mheshimiwa Sanga, unawapongeza askari wako wa Makambaku lakini hapa Dodoma Wabunge wote mnakaa kwa amani kabisa, salama kabisa lakini RPC wa Dodoma hamumpongezi, hii inakuwaje? (Kicheko/Makofi)

Eendelea Mheshimiwa Sanga.

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, ni kweli na ndiyo nilikuwa nakuja huko kutokana na kazi nzuri wanazozifanya na hata sisi Wabunge hapa, sisi kule Iringa kuna msemo wanasema ‘tukikala kilega’, tukilegea ni kwa sababu ya usalama wa hawa wanaotulinda. Kwa hiyo na Dodoma hapa tunalindwa, tunakaa majumbani salama huko tunakokaa hakuna bughudha mitaani, tunatembea mpaka usiku wa manane ni kwa sababu ya Jeshi la Polisi. Kwa hiyo, tunawapongeza sana kwa kazi nzuri wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho baada ya maelezo haya, Mheshimiwa Waziri na timu yako kaza buti, endelea kuchapa kazi, askari mmoja anayeharibu si jeshi zima bovu. Kwa hiyo, hawa askari ambao wanataka kulichafua Jeshi la Polisi kupitia Kamanda wako Siro muendelee kuwadhibiti ili warudi kwenye mstari vinginevyo kazi ni nzuri na mnadhibiti vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata hili suala la mikutano ambalo wenzangu wamelizungumzia hapa, kwenye mikutano watu walikuwa wanafanya kazi ya kuja kutukana si kufanya shughuli za maendeleo. Sasa hivi mikutano tunafanya kila watu kwenye maeneo yao, shughuli zinakwenda vizuri, Waziri kaza kamba. Nikutakie kila la kheri katika shughuli hizi ambazo ziko mbele yetu, ahsante sana. (Makofi)