Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Amina Nassoro Makilagi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nimshukuru Mwenyenzi Mungu muweza wa yote aliyenipa fursa ya kuweza kusimama kutoa mchango katika Wizara hii nyeti, Wizara ambayo kwangu mimi naiita moyo wa taifa kwa sababu bila amani hakuna chochote tunachoweza kufanya katika taifa letu. Naomba nipingane na wale wote wanaosema majeshi yetu ikiwepo Jeshi la Polisi kwamba ni ugonjwa wa kansa, mimi naendelea kusema Mwenyezi Mungu awasamehe kwa sababu hawajui watendalo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na naomba nipingane na wale wote wanaosema majeshi yetu ikiwemo Jeshi la Polisi kwamba ni ugonjwa wa kansa, naendelea kusema Mwenyezi Mungu awasamehe kwa sababu hawajui watendalo. Na wote hawa wanaozungumza ni kwa sababu hawajawahi kuchimba handaki, hawajawahi kulala kwenye handaki, hawajahi kushuhudia vita ndio maana leo wakisikia mtu amekamatwa wanasema amani hakuna lakini kumbe kuna watu ambao hawalali kwa ajili yetu na si wengine Jeshi la Polisi ni Jeshi la magereza, jeshi la uhamiaji ni jeshi la zima moto. Ninawaomba muwasamehe maana hawajui watendalo na akutanaye hakuchagulii tusi na ukiwa kwenye maji unaoga akija mwendawazimu haumfukuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri Kangi Lugola na timu yake yote kwa kazi njema wanayoifanya. Kusema ukweli mnyonge mnyongeni haki yake apewe, Mheshimiwa Kangi na timu yako na taasisi zako zote mnafanya kazi nzuri na ndio maana leo Wabunge tunazungumza tutakavyo kwa sababu amani imedumishwa mnalinda mali na raia, mnazima moto tunapopata majanga, mnatulinda na katika mipaka yetu ndio maana leo tunasema Mungu awape Baraka zake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze Kangi kwa kuandaa ripoti nzuri na timu yake kwa kweli taarifa hii ya Wizara ya Mambo ya Ndani imeandaliwa vizuri, imechanganuliwa vizuri ninapongeza kweli inajieleza yenyewe na sio tu na kazi inafanyika vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizi pia naishukuru Serikali kwamba kwa bajeti iliyokwisha 2018/2019 ilipeleka fedha vizuri kwenye Wizara ya Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani kwa kiwango cha asilimia 86 nimejaribu kupiga heshabu hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nataka nitoe ushauri. Wizara hii ya Mambo ya Ndani ndio moyo wa Taifa letu, ninaomba Serikali mko hapa mnisikie tutenge fedha za kutosha kwa ajili ya wizara hii. Wizara hii ina majukumu makubwa sana ya dharura ambayo hata hayatarajiwi, unamkuta OCD yuko Kiteto anaongoza kilometa zaidi ya 200 lakini mafuta anayopewa kwenye gari ni lita 100 kwa mwezi. Lakini unakuta hata service za magari wanatakiwa kwenda doria watulinde Wabunge, walinde doria, watembee kwenye mipaka yetu, watembee kulinda ujambazi na amani itokee lakini hata magari na matairi yao ya magari hayana uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine hata service zenyewe na hata namna wenyewe wanavyoweza kujikimu na hata kulala kwenye majanga kwenye maeneo mengine. Kwa kweli naomba na Waziri wa Fedha namwona yuko hapa na Kamati ya Bajeti mko hapa nawaomba wizara hii hebu iangalieni kwa jicho la pekee kwa sababu fedha zinazotengwa hazilingani na kazi wanayoifanya na ugumu wa kazi waliyonayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia magari ya zima moto ni magari ya zamani yamechoka. Juzi mliona moto hapa Dodoma unatokea hayafanyi kazi sawasawa wanaunulieni magari ya kisasa, tunaona kabisa Serikali imenunua magari nchi nzima imepeleka karibu Ma-OCD wote wana magari. Lakini hata matairi ni yale mapya yaliyokuja nayo hata mafuta ya kuweka kwenye hayo magari hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba jamani hebu tupigie kelele Serikali yetu na najua Serikali yetu ni sikivu na Rais wetu amekuwa mstari wa mbele kulinda vyombo vyetu hivi kama ambavyo anavyofanya kwenye majeshi na vyombo vya ulinzi na usalama jeshi la polisi, magereza, zimamoto watendewe haki kwa kuongezewa bajeti na hata fedha waliotengewa mwaka jana yote iende kama ambavyo imekusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nimejielekeza kuongelea maslahi ya askari, hata anayezungumza na mimi na maslahi na askari. Familia yote ya Mzee Makilagi tuko watoto 24 mimi peke yangu ndio raia na mimi niliponea chupuchupu. Kwa hiyo, nachozungumza hapa nazungumza tukiwa ndani ninaomba nitoe ushauri askari wetu wote wa polisi magereza, zima moto, uhamiaji wanafanya kazi ngumu katika mazingira magumu. Ninaomba sisi kama Bunge hebu tuielekeze Serikali tujaribu hata kuwaongezea mishahara na hasa askari wa kiwango cha chini. Mishahara yao ni ya zamani kwa kweli haiendani na mazingira ya sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile askari wetu wanafanya kazi kwenye mazingira magumu, posho zao za kujikimu, posho zao za likizo, posho zao za uhamisho hawapati. Askari anakwenda kila baada ya miaka mitatu anakwenda likizo lakini sasa hivi hata nauli wakati mwingine wanajitegemea tunapeleka wapi jeshi, tunawasaidiaje hawa vijana wetu ambao ndio walinzi wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tuangalie kwa macho ya huruma kwa sababu askari tumewaambia wasichukue rushwa, askari huyu hana muda hata wa kufanya biashara, hana muda wa kukaa wa kufanya mambo yake binafsi muda wote anatulinda sisi, sasa anapokwenda mpaka likizo anajitegemea kwa kweli sio sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie posho zao. Posho zao tunamshukuru Rais wetu na hata Awamu ya Nne, na hata Awamu ya Tano wanapata posho kujikimu ya chakula kila tarehe 15 wanapata shilingi 300,000.

Sasa hivi umekuja utaratibu eti wanapewa kila mwezi ninaomba ule utaratibu wa kupewa kila tarehe 15 ya kila mwezi wawe wanapewa kwa sababu ile tarehe 15 anapopata ile fedha inawasaidia kupunguza zile changamato ndio maana hawatakwenda kukamata huko ndio maana hawatajiingiza kwenye mambo mabaya lakinii unapolimbikiza mpaka mwisho wa mwezi sio nzuri. Ninaomba tuwaongeze pia kwa sababu tangu tulipowaongeza ilikuwa ni mwaka 2010 sasa ni 2015 tuwaongeze askari wetu toka hii 300, 000 ifike hata ikiwezekana 500,000 kwa sababu wanafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilitaka nizungumzie ni ma…

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, na ninataka nimshauri Mheshimiwa Kangi tena nafurahi kwa sababu wewe…

MWENYEKITI: ngoja

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nani kanipa taarifa huyo nani alete.

MWENYEKITI: Subiri kidogo taarifa.

T A A R I F A

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana naomba kumpa taarifa mzungumzaji kwamba pamoja na kwamba anasema askari wanapewa posho lakini yeye alikuwa miongoni mwa Wabunge waliokataa maaskari kuongezewa mshahara hapa Bungeni na wafanyakazi wote kwa ujumla. Kwa hiyo, ni taarifa tu kwamba anapozungumzia hilo akumbuke kwamba alikataa wafanyakazi kupandishiwa mishahara na maaskari wakiwa ni miongoni mwa wafanyakazi katika nchi hii. (Makofi)

MWENYEKITI: Haya Mheshimiwa Makilagi

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya huwa siongeagi na watoto nimekusikia, kwa hiyo, ataongea na size yake mimi sio size yake. Mimi naongea na baba yako umesikia mwanangu eeh!

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee kwa kusema kwamba askari wetu tuangalie maslahi yao kwa sababu wanalinda Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba tuzungumzie maslahi ya askari, vitendea kazi sasa hivi ipo changamoto kwa uniform za askari na sio kwa jeshi la polisi peke yake mpaka zimamoto, magereza, ukikutana na askari sio kama yule wa zamani uniform zake zinatofautiana. Ninaomba kwenye fedha za OC kwa ajili ya shughuli mbalimbali hebu tuongeze bajeti hii ili vyombo vyetu vya Serikali viweze kununua uniform…(Makofi)

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu.

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumza nao wanasema wakati mwingine hata wanaambiwa wanunue wao wenyewe.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Selasini kuhusu utaratibu kanuni ya ngapi.

KUHUSU UTARATIBU

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba utaratibu kwa mujibu wa kanuni ya 64(1)(g) mzungumzaji wakati anajibu taarifa alisema kwamba haongei na watoto. Sasa licha ya kwamba hii sio kauli ya kibunge lakini kama kiongozi wa Kambi hii siongozi watoto, ninaongoza Wabunge, watu wazima na watoto wamebaki nyumbani. Sasa i baba yao ninaomba ieleweke hivyo… (Kicheko)

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Haya Mheshimiwa Makilagi endelea.

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa sababu Mbunge anayezungumza ndio baba mwenyewe ninayemzungumza tutakaa pamoja kuwalea watoto kwa pamoja. Na ndio jukumu letu sisi kama wazazi ndani ya Bunge hili kuwalea watoto ili wazazi wanapokuwa wanazungumza watoto wanakuwa na utulivu na wanaweka heshima kwa wazazi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maslahi ya askari, leo nimesema najielekeza kwenye maslahi ya askari wetu, Rais wetu anawapenda askari kila anapopita mnamwona anawapenda askari na alipokwenda Arusha mwaka jana alitoa shilingi bilioni 10 kwa ajili ya kujenga nyumba za askari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa mujibu wa taarifa ya waziri nyumba zinaendelea kujengwa na baadhi yake nimezitembelea kwa kweli nichukue nafasi hii kumshukuru Rais kwa kazi njema. Ushauri wangu katika jambo hili pamoja na kazi nzuri ya kutenga hizo fedha bilioni kumi nataka nimwambie Mheshimiwa Kangi tena ambaye ni askari na wewe hebu sasa njoo na mkakati wa kujenga nyumba za askari za kutosha kwa nchi nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushauri kila unapofanya ziara usiache kutembelea kambini fika na pale feed force Mkoa wa Mara, fika na pale Mwanza Mabatini, fika na hapa Dodoma uone askari wako mahala wanapolala. Ninaomba mje na mkakati maalum na sisi Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sisi Wabunge wa CCM tuko wengi na wengi tunapenda askari tuko tayari kupitisha mpango huu ili nyumba za askari zijengwe nchi mzima na zilete tija kwa askari wetu walale mahala pazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na nawashauri pia hata ramani ya nyumba za askari ziangaliwe tena kwa sababu nyumba zilizojengwa zamani zilikuwa ni kwa ajili ya familia ambazo hazina watoto, sasa hivi askari wetu wanaishi vizuri wana watoto vile vinyumba haviwastahili hebu njooni na ramani ambayo inavutia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Mheshimiwa Waziri kuna kitengo cha ujenzi kwa upande wa magereza na kwa upande wa polisi. Sifurahii kuona kuna kazi imetokea jeshi la polisi, kazi wanapewa jeshi la wananchi, sifurahii kama mtoto wa askari kwa sababu nimeshiriki kujenga handaki, nimeshiriki kujenga hata nyumba za askari. Zamani familia za askari tukishirikiana na magereza, tukishirikiana na kitengo cha ujenzi tulikuwa tunajenga nyumba wenyewe. Hiki kitengo kimekwenda wapi? Na bahati nzuri jeshi la polisi lina wataalam waliobobea katika weledi wa ujenzi, lina Ma- engineer, lina wachoraji, lina kila kitu, mageraza ina rasilimali watu, Mheshimiwa Waziri hebu sasa uache legacy katika nchi hii. (Makofi)

MWENYEKITI: Asante sana Mheshimiwa Makilagi.

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante sana naunga mkono hoja (Makofi)