Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Selemani Moshi Kakoso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpanda Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata nafasi ya kuchangia kwenye Wizara hii. Awali ya yote nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya ya kulinda amani ya nchi hii. Pia nimpongeze Waziri mwenye dhamana na Msaidizi wake kwa kufanya kazi kubwa ya kusimamia Wizara ambayo ni kubwa na ina majukumu mapana sana. Tuwapongeze Wakuu wa Vyombo vya Usalama, Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Jeshi la Uhamiaji, Jeshi la Zimamoto. Wamefanya kazi kubwa, naamini kila mwananchi anashuhudia ile kazi ambayo imefanyika chini ya uzimamizi wa Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Polisi wamefanya kazi kubwa sana, wamedhibiti mianya ya uingizaji wa madawa kulevya na kufuta kabisa nchi yetu iliyokuwa inaonekana kwamba ni eneo la uchochoro wa kupitisha madawa ya kulevya, hapa wamefanya kazi kubwa sana, tunawapongeza kwa dhati. Hata hivyo, wamedhibiti matukio ya ujambazi nchini ambayo yalikuwa yameshamiri kwa muda mrefu sana. Jeshi la Polisi wamefanya kazi ya kudhibiti hivyo vitendo na sasa hivi matukio yamepungua kwa kiwango kikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado katika eneo hilo la Jeshi la Polisi wamedhibiti vitendo vya kuhujumu uchumi wa nchi yetu. Tumeshuhudia Jeshi la Polisi likidhibiti utoroshwaji wa dhahabu ambao ulikuwa unafanywa na raia wasioitakia mema nchi yetu. Wamefanya kazi ambayo kimsingi Serikali imedhibiti vile vitendo ambavyo vilikuwa vinadhoofisha uchumi wetu. Pamoja na hayo Jeshi la Polisi pamoja na jitihada linalofanya na kazi inazolifanya ni kubwa, lakini bado kuna changamoto kubwa ambazo zinatakiwa zifanyiwe kazi, vitendea kazi hawana, tunaomba sana Mheshimiwa Waziri tuangalie kwenye maeneo ya vitendea kazi. Jeshi la Polisi hawana magari ya kutosha, Jeshi la Polisi hawana nyumba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kwenye eneo la jimbo langu, tumeshukuru Serikali wanajenga nyumba za askari zipo sita, lakini bado pamoja na kwamba wanajenga hizo nyumba, lakini hakuna Kituo cha Polisi cha Wilaya. Niombe sana Mheshimiwa Waziri alingalie hili na naamini ninachokiongea anakifahamu, alishafika kwenye maeneo husika, tunaomba kituo cha polisi. Zile nyumba anazojenga hazitakuwa na maana kama hakutakuwa na kituo cha polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vipo vituo vya polisi ambavyo vipo mpakani, tuna Kituo cha Polisi Ikola na Kituo cha Polisi Karema, hivi vituo ni ambavyo havina hadhi inayofanana, tuombe sana Mheshimiwa Waziri ahakikishe hivi vituo wanavipelekea vitendea kazi. Hata hivyo, baadhi ya vituo vya polisi hata uwezo wa kupeleka silaha hakuna, askari polisi analinda kituo akiwa na rungu, kwa sababu hana nyumba ya kuweza kuhifadhi silaha. Naomba Mheshimiwa Waziri apeleke silaha kwenye maeneo ambayo ni mpakani ili yaweze kulindwa, na ajenge mazingira ambayo yatakuwa salama kwa ajili ya vile vituo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nizungumzie Jeshi la Magereza, Jeshi la Magereza linafanya kazi kubwa na jimboni kwangu Wilaya ya Tanganyika tuna Gereza la Kilimo la Kalila Nkulukulu. Gereza hili ni la muda mrefu, ni chakavu, tunaomba likafanyiwe ukarabati sambamba na kujenga nyumba za watumishi hasa askari wanaofanya kazi kwenye gereza hili. Yapo maeneo mengine ukifika unawaonea huruma, hata hao watumishi unaowapeleka kwenye eneo hilo, unajua tu kwamba wanafanya kazi kwa sababu ni wito.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo Gereza la Kilimo la Kalila Nkulukulu lina eneo kubwa sana la uzalishaji. Kwa bahati mbaya sana vitendea kazi hawana. Tulikuwa tunaomba Waziri wanunulie treka Gereza la Kilimo la Kalila Nkulukulu ili liweze kuzalisha chakula cha ziada. Tuna matumaini makubwa sana wakiwapelekea vifaa na vitendea kazi watafanya kazi kubwa ambayo itawasaidia kuzalisha na kupata ziada ya chakula. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimboni kwangu nina wakimbizi, lipo eneo la Mishamo lina wakimbizi zaidi 60,000, kati ya hao walio wengi walishakuwa raia na wengine hawajakubaliana na kuwa raia wa nchi hii. Sasa kuna vitu ambavyo vinakuwa tofauti kwenye eneo moja, kwa maana linakuwa na utawala wa aina mbili; utawala wa makazi unaosimamiwa na Afisa anayetambuliwa na Wizara ya Mambo ya Ndani lakini utawala mwingine ni ule ambao ni wa kawaida. Kwa hiyo kuna tawala mbili kwenye eneo moja, mkuu wa makazi analinda wale wakimbizi wachache waliobaki. Kwamba ni mali ya kwake, wanatambuliwa na Umoja wa Mataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niombe Serikali itoe maamuzi, wale wachache ambao hawakuchukua uraia wawahamishe wawapeleke kwenye maeneo mengine ambapo watakaa kwenye maeneo rasmi. Tukiwaacha hivyo tuna mashaka makubwa sana baadaye, tutaendelea kupokea wakimbizi kupitia hawa hawa ambao wapo kitu ambacho hatukitegemei tena. Si Mishamo tu, hata Katumba wapo. Kwa hiyo tunaomba hili walishungulikie na tunapata wakati mgumu kwenye Serikali za Mitaa katika uchaguzi ujao. Kuna hati hati ya kutokushiriki wananchi hao wa Mishamo, Katumba, Ulyankulu wanaweza wasishiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa sababu ya mwingiliano wa utawala. Naomba hili walishughulikie na walifanyie kaziā€¦

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)