Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Fakharia Shomar Khamis

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza sina budi kuwapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, IGP na Makamishna na hasa Kamishna wangu Mohamed Hassan wa Zanzibar, ambaye hivi karibuni kulitokea tokeo la vikosi kuingiliana katika majukumu ya kazi na wakaweza kulidhibiti na kukaa salama na shwari. Lazima niwapongeze kwa kazi yao nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna msemo watu wanapenda kusema ambao nitausema hapa leo, “domo, nyumba ya maneno.” Sisi watu wa Pwani tunapenda sana kuzungumza. Kuna baadhi ya watu wanapenda kusema mambo mengi wakailaumu Serikali, wakasema ovyo, baadaye wakamtafuta mchawi, kumbe mchawi anakuwa yeye mwenyewe ambaye amejidhuru kwa kauli zake alizozisema na hilo linatendeka humu ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kuna msemo mwingine unasema hivi, “kwa shujaa huenda kilio, kwa mwoga huenda kicheko.” Sasa baadhi yetu humu yakija yakiwakuta, wanapiga kelele kumbe amejifanya shujaa, yamemkuta, akina siye tuliokuwa waoga, tunamwangalia tunacheka. Sasa jamani tunapokuwa tunataka kusema mambo, lazima ufikirie kwanza nini athari yake ya mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia kuhusu ujenzi wa nyumba za Askari. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi hapa Tanzania kwa huruma zake kwa Wizara hii ambapo aliweza kuwapatia shilingi bilioni 6.3 kwa ujenzi wa nyumba 400 za askari, pia mkachagua mikoa minane katika mikoa minane na Zanzibar wakapata Unguja na Kaskazini Pemba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo ni jambo la fahari, la kujivunia, kwa uwezo iliyokuwanao Tanzania na kujali wapiganaji wake. Naomba Wizara pia mjiongeze. Mjipongeze vipi? Kwa sababu tunayo mifuko yetu ya jamii, mngekuwa mnazungumza nayo wakaweza kuwapatieni mkopo wa riba nafuu, mkaweza kujiongeza kwa kuwawezesha kujenga nyumba na katika mikoa mingine pia nao wakapata nyumba, Askari wetu wakajisitiri katika makazi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikizungumzia Jeshi la Magereza, Mheshimiwa Waziri alizungumzia katika ukurasa 28 na 29, Jeshi la Magereza kubuni ili kuweza kuzalisha chakula na pia kuzalisha mazao ya biashara. Sasa nasema wangejiongeza na wakatafuta na mifugo kwa sababu tayari wanao vijana, wanaingia kwenye magereza yetu hodari, wana nguvu, wana uwezo, ni shabab kabisa, takribani wengi wanakuwa vijana sio wazee. Sasa hawa isiwe kazi yao ni kula na kulala, wawatumie waweze kufanya kazi ili waweze kuzalisha na kuipunguzia mzigo magereza au kuipunguzia mzigo Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija katika mwaka 2017/2018, zilitengwa bilioni 5.8 kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi wa Ofisi ya Uhamiaji Mikoani, Wilayani vituo na kadhalika. Hata hivyo, hizi pesa hazikutoka, ujenzi haujakamilika, mfano tukienda Lindi na Mtwara, yale majengo hali yake ni mbaya, hayajamalizwa, ile ni hasara kwa pesa za wananchi na ni kodi zao. Kwa sababu ukienda ukiyaona hali ni mbaya na humjui umkamate nani uchawi? Tuwakamate Wizara ya Fedha, tuwakamate Wizara ya Mambo ya Ndani au tuwakamate Magereza, lakini hali ni mbaya na hili jambo lazima walingalie kwa upeo mrefu na liweze kufanyiwa kazi hiyo ya matengenezo ila majengo hayo watu wakae na kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitanzungumzia dawa za kulevya kwa upande wa Zanzibar. Hivi karibu Mheshimiwa Naibu Waziri alikwenda Zanzibar akazungumza na Wanahabari. Nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri, kazi aliyoifanya ni nzuri na akagundua udhaifu uliokuwepo na akasema udhaifu ulikuwa kwa viongozi wetu watendaji na kuna maneno alizungumza akasema na itakuwa si mbaya baadaye hili jambo akalizungumza kwa mapana tukaelewa sote kwa sababu wanaopata tabu ni watoto wetu na wanatajirika ambao wanaiharibu nchi kwa kutaka manufaa yao ya kupata hela. Sasa hilo jambo azidi kulisimamia ili huu udhaifu uondoke, kama amegundua kiongozi, basi huyo kiongozi ashughulikiwe au amegundua taasisi, hiyo taasisi ishughulikiwe, lakini hili jambo liweze kuangaliwa kwa mapana na tuweze kupata nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia kuhusu jengo letu au pale Mkoa wa Mjini Magharibi kuna sehemu panaitwa bomani, hilo boma ambalo ndio kambi kubwa ya mwanzo tulikuwa tunaitegemea pale Zanzibar maana ipo kwenye historia, maana hata wakizungumza hayo Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964 lazima boma lile lina historia. Hata limetungiwa nyimbo katika historia, lakini wanaliacha, boma lile majumba ndani hayapo sawa halishughulikiwi, njia zilipo ndani haziko sawa hazishughulikiwi. Utakuta mlango mkubwa kuna askari kasimama analinda. Sasa analinda nini wakati ule uzio wote mbovu, utaingia utatoka askari hana habari, utafanya unalotaka, askari hana habari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, naomba safari hii katika bajeti ya maendeleo watakayoomba, kama mwaka huu hawakuomba, wataomba mwakani wangefanya uzio na huo uzio usiwe wa waya, uwe wa matofali. Nasema hivyo kwa sababu pale pamezungukwa na majumba, zamani palikuwa nje ya mji, lakini sasa katikati ya mji, majumba yote yamezunguka, wanalofanya mle ndani mtu wa nje anawaona, sasa hiyo siri hapo iko wapi? Sasa naomba wakapaangalia, ile historia iliyokuwepo mle wakaiweka sawa na wanaijua ili watu waliokuwepo mtaani, au waliokuwa nje au mtu akidhamiria kufanya jambo kidogo apate shida ya kuingia mle ndani, asiingie kwa urahisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haya machache, naunga mkono hoja. (Makofi)