Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami nichangie katika Wizara ya Mambo ya Ndani. Namtanguliza Mwenyezi Mungu katika mchango wangu, lakini nami niungane na mchangiaji aliyepita kwanza kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuwachagua hawa Mawaziri na viongozi wote waliopo katika Jeshi hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Kangi Lugola; Naibu Waziri, Mheshimiwa Masauni; Makatibu Wakuu na Watendaji wote wa Wizara hii ya Mambo ya Ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niwapongeze makamanda wote kwa kazi nzuri sana ambayo wamekuwa wakiifanya, IGP Sirro, SGP Kasike, Zimamoto, SGP Andengenye na Uhamiaji SGI AP Dkt. Makakala ambaye kwa kweli ni mwanamke aliyetuwakilisha wanawake wote na amefanya kazi nzuri sana. Katika ripoti ya Mheshimiwa Waziri tumeona amepewa tuzo katika passport. Kwa hiyo, tunaona kwamba sisi wanawake tumewakilishwa vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na kazi nzuri ya mama huyu, nafikiri hata mtandao wa Polisi, sasa uangalie wanawake na wenyewe wale wanaoweza, basi wapatiwe vyeo vya juu ili waendelee kutuwakilisha vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Askari wetu wanafanya kazi nzuri sana lakini tukikutana na bajeti finyu wamekuwa wakifanya kazi kwenye mazingira magumu sana. Kwa hiyo, nilikuwa naomba Serikali iwaangalie, kuna changamoto ambazo wanakumbana nazo. Wanadai posho zao muda mrefu, uhaba wa watumishi, pensheni zao zilipwe kwa wakati, promotion zao wapatiwe kwa wakati ili kuwatendea haki na wawe na ari ya kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Rais pia kwa kuona changamoto zilizopo katika nyumba za Maaskari wetu, naona ameanza kuzifanyia kazi pale Ukonga. Nami namwomba katika Mkoa wetu wa Iringa Askari wetu wanakaa katika nyumba chakavu sana. Ukiangalia pale Iringa Mjini, Mufindi, kule Kilolo ndiyo hakuna kabisa nyumba za Askari Polisi na wengine wanakaa nje ya makambi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Serikali iangalie. Pamoja na uchakavu walionao, kuna akina mama kuna watoto ambao wamekuwa wakiishi kwenye mazingira magumu sana. Kwa hiyo, tunapozungumzia makazi ya Polisi, tunaangalia hata akina mama na watoto walioko katika nyumba zile. Kwa hiyo, naomba hili lizingatiwe kwa umuhimu wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya yetu ya Kilolo, toka ianzishwe Makao Makuu ya Wilaya, OCD hajawahi kujengewa Ofisi katika Makao Makuu ya Wilaya. Kwa hiyo, kumekuwa na changamoto kubwa sana. Tunawashukuru sana TAZAMA Pipeline ambao wamempatia ofisi, lakini ni mbali sana na ilipo Mahakama. Kwa hiyo, utakuta wakati mwingine wanapata shida sana kuwapeleka mahabusu kwenda kwenye Mahakama kwa sababu ni karibu kilomita 70.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba waangalie, kuna gharama kubwa kila siku zinatumika. Wangeangaliwa changamoto iliyopo katika Wilaya ya Kilolo ili Mahakama ijengwe yalipo Makao Makuu ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, nikizungumzia Jeshi la Zimamoto wana changamoto nyingi sana na wanafanya kazi vizuri sana katika mkoa wetu lakini pia posho zao wanakuwa hawalipwi kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni uhaba wa magari ya Zimamoto. Utaona katika Wilaya ya Mufindi kuna msitu ambapo mara nyingi moto umekuwa ukitokea lakini hakuna gari la Zimamoto. Vilevile Wilaya ya Kilolo hakuna gari la Zimamoto na mara nyingine kumekuwa kukitokea ajali nyingi katika mlima Kitonga na hakuna hata gari la uokozi (crane) kwa ajili ya kusaidia kunapotokea ajali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna upungufu mkubwa wa Askari katika Wilaya zote. Jeshi la Magereza vilevile kuna madeni ya posho, kuna madeni ya Wazabuni ambao wamekuwa wakisaidia kuwalisha wale wafungwa, gharama za kuwasafirisha mahabusu na wafungwa wanaostahili kwenda kusikiliza kesi zao pia ni tatizo. Kwa hiyo, naomba Serikali ingeangalia pia haya Majeshi ili wapatiwe fungu la kutosha katika Mkoa wetu wa Iringa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu sasa. Naomba nitoe ushauri kwa Serikali kuhusiana na Jeshi la Zimamoto. Zile pesa za makusanyo (fire inspection fee) kwenye nyumba, biashara, viwanda, ma-guest, migodi, pengine ingekuwa hata asilimia kumi zinaenda kununua hivi vifaa vya Zimamoto ingeweza kusaidia upungufu ambao upo katika hili Jeshi la Zimamoto kuliko ambavyo sasa hivi pesa zote zinachukuliwa na Serikali wakati wao wenyewe wanakuwa wana matatizo kabisa ya upungufu wa vifaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika Jeshi la Magereza, Magereza iwe kama Chuo cha Mafunzo, waongezewe vifaa vya mafunzo ili wale wafungwa waliopo kule wawe wanapatiwa mafunzo. Vilevile wapewe vifaa vya kilimo kama matrekta, yatasaidia; na waweze kufundishwa hata uvuvi na wapatiwe mkopo usiokuwa na riba ili waweze kujiendesha wenyewe. Kwa hiyo, itasaidia.

Mheshimiwa Mweyekiti, nimeona hata Mheshimiwa Rais anasema kwamba haya Magereza yangekuwa yanajiendesha yenyewe katika kulisha wafungwa na kusaidia changamoto zilizopo. Kwa hiyo, kama tukiziwezesha kupata mikopo, inaweza ikasaidia sana zikawa zinajiendesha zenyewe; na wapewe kazi za ujenzi. Kwa hiyo, utaona kwamba tutakuwa tumezisaidia, tutakuwa hatutumii tena ruzuku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naweza kutoa mfano, nimeshatembelea pale Magereza nikakuta wana kiwanda, lakini wana changamoto ya fedha. Namshukuru Mkurugenzi aliweza kuwakopesha shilingi milioni kumi na sasa hivi wanajiendesha tu vizuri katika gereza letu la Mkoa wa Iringa. Kwa hiyo, iwe mfano hata katika Magereza nyingine, bado tunaweza tukaziwezesha Magereza zikaweza zikajiendesha zenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu lingine, Mkoa wetu una changamoto ambao kuna mwingiliano mkubwa sana kati ya Gereza la Mkoa na Hospitali ya Mkoa. Hili nimekuwa nikilizungumzia mara nyingi sana; na ningeomba labda sasa hivi hebu mlipe kipaumbele kwamba kwa sababu Gereza lina eneo kubwa nje ya mkoa, basi lihame ili kupisha hospitali iweze kujenga majengo na nyumba za Madaktari iweze kusaidia wagonjwa wetu na msongamano uliopo katika Hospitali ya Mkoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia Jeshi la Magereza liwe linawapatia hati maalum wadau wanaosaidia Jeshi la Polisi. Kwa mfano, katika mkoa wetu kuna wadau ambao wameweza kusaidia sana ujenzi wa Vituo vya Polisi, ujenzi wa madawati, wamekuwa wakisaidia hata ukarabati wa majengo mbalimbali, kwa mfano, yuko huyu Mheshimiwa ASAS ambaye ni mmiliki wetu pale Mkoa wa Iringa, kuna Besania, kuna Mbarak kuna Ruaha National Park, Zakharia Hanspop ambaye pia kwa kweli ametupatia magari ya Zimamoto na Ambulance. Sasa uwepo utaratibu mzuri wa kuwapatia hati ambayo inatambulika kwamba wamesaidia Jeshi letu la Polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata mimi mwenyewe nilijenga Kituo cha Polisi pale Kihesa, pia ni vizuri nikatambulika mchango wangu kwa kupatiwa hati maalum kwa sababu nimelisaidia Jeshi la Polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nizungumzie kuhusiana na vitambulisho vya Taifa. Hivi vitambulisho nafikiri Wabunge walio wengi pia wamezungumzia kwamba wengi walishakwenda kupiga picha, wamefanyiwa kila kitu, lakini sasa vitambulisho bado havijawafikia; na mara nyingi sasa hivi kila sehemu unatakiwa uwe na hicho kitambulisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna ufinyu wa bajeti, basi Serikali iangalie uwezekano wa kutoa pesa ya kutosha ili kuhakikisha kwamba hivi vitambulisho wananchi wanapewa haki yao, kwa sababu kila unapotaka kwenda lazima uwe na kitambulisho. Hata ukisafiri nchi za nje lazima uwe na kitambulisho cha Taifa. Vilevile ukitaka labda kuomba passport lazima uwe na kitambulisho. Kwa hiyo, wananchi wamekuwa wakipata shida sana wanapotakiwa kupata hivi vitambulisho.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante. Muda wetu ndiyo huo.

MHE. RITTA E. KABATI: Naomba niunge mkono hoja hii. Ahsante. (Makofi)