Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana nami kuniruhusu nichangie hotuba ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani vifungu 28, 29, 51 na 93.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kutoa pongezi nyingi kwa Mheshimiwa Rais Joseph Pombe Magufuli kwa kuliwezesha Jeshi la Polisi kufanya kazi kubwa ambayo linafanya. Pia pongezi kwa Wizara nzima ya Mambo ya Ndani na Jeshi la Polisi hasa kwa kuendeleza amani na utulivu hapa nchini, kwa kulinda raia na mali zao Ila nina jambo la kusema leo ambalo limenisumbua sana.. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu, upande wa pili kule wanaye Mnadhimu Mkuu au Msemaji wa Kambi ya Upinzani. Mnadhimu huyu, Mheshimiwa Tundu Lissu amekuwa anasema maneno mabaya kuhusu nchi hii, kuhusu Serikali, kuhusu Mheshimiwa Rais na wenzetu hawa wamekaa kimya. Huyu ndiye Msemaji wa Kambi ya Upinzani Bungeni. Kwa hiyo, anayoyasema kule ndiyo haya haya ambayo hawa wanayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka hawa waseme leo: Je, ni kweli mnamuunga mkono Tundu Lissu au mko tofauti? Mseme ili wananchi wajue mko upande wa watu wanaochukia Tanzania, wanaomchukia Mheshimiwa Rais, wanaochukia Serikali, wanaochukia maendeleo yote; wanachukia miradi ya nchi hii inayoletwa na Serikali ya Awamu ya Tano. Mseme wananchi wawajue ili wasiwape kura kwenye uchaguzi unaokuja. Hamfai kuongoza nchi. haiwezekani muishi kama popo upande huu mko ndani ya Bunge mnasema mnaipenda Serikali ya Jamhuri ya Muungano, mnachangia mtu anayekosoa Serikali. Sasa hivi mnawasema vibaya hawa hawa. Haiwezekani mkia uwe tofauti na kichwa kiseme tofauti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti hii wakati ilipofika Wizara ya Sheria na Katiba, wamesoma hotuba ya Mheshimiwa Tundu Lissu. Kwa hiyo, wanamuunga mkono yote anayoyasema, lakini nje hamwambii wananchi kwamba ninyi hamuipendi nchi hii, semeni. Msiendelee kukaa kimya, upande wa pili mnasema watu, nchi za nje ziinyime misaada Serikali yetu, lakini vilevile hamtaki misaada yoyote ije kwa watu ambao wanawasaidia, Serikali inayowasaidia dada zetu, mama zetu na kaka zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa sana upande wa Upinzani leo useme kwamba anayoyasema Mheshimiwa Tundu Lissu ni ya kwao au ni ya kwake? Ili wananchi wajue. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo sasa naomba nichangie. Namwomba Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani anipelekee salamu zangu kwa Mheshimiwa Rais za kuwapa pole familia za Askari waliofariki wakitetea amani na usalama wa nchi yetu. Askari hawa ambao wanabezwa na upinzani wamefanya kazi kubwa sana. Hakuna mtu kati yetu Bungeni humu aliyejitolea kufa ili jirani yake aishi. Askari wetu wamekufa. Wamekufa Rufiji, hata juzi wamekufa, wanapambana na majambazi ili kuleta usalama wa raia na mali zao. Iko haja ya kuwasifia sana lakini kutoa pole kwa familia zinazobaki, waliokuwa wanawategemea Askari wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati yangu ya NUU imefanya kazi ya kukagua miradi yote muhimu ya Jeshi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ikiwemo miradi muhimu, lakini kote kumekuwa na kilio, hakuna fedha iliyopelekwa kwenye maendeleo hata kidogo. Fedha iliyopelekwa ni kidogo, haiwezi kumalizia miradi ambayo ipo. Naiomba Serikali, Wizara ya Fedha iwapatie fedha miradi hii katika Jeshi la Polisi, Idara ya Zimamoto, Idara ya Magereza na Uhamiaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko suala la Sheria ya Sekta Binafsi ya Ulinzi. Sheria hii niliileta nikaipeleka kwa Mheshimiwa Spika na baadaye Serikali ikaiomba kwamba yenyewe itaileta kwa sababu ilikuwa inahusishwa kuanzishwa chanzo cha kupata kodi na Mamlaka ya Sekta ya Ulinzi Binafsi, (Private Security and Authority). Sasa zilikuwa siku, ikawa wiki, ikawa miezi, mwisho imekuwa ni miaka mitatu tangu sheria imechukuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda Mheshimiwa Waziri atapokuja alieleze Bunge hili, ni lini sheria hii italetwa? Sheria hii ni muhimu sana kwani italeta win win situation kwa makampuni yanayoendesha biashara hii ya ulinzi binafsi lakini pia Serikali itapata kodi kwa kudhibiti mapato yanayotengenezwa na makampuni ya ulinzi binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa mchoyo iwapo sitasemea suala linalompata mwenzetu Mheshimiwa Kadutu katika makazi ya wakimbizi kule Ulyankulu. Sisi tumekuwa na makambi ya wakimbizi kule Ulyankulu, Mishamo, Katumba na kwingineko. Wakimbizi hawa wanavyoishi na wanavyotenda ni kama vile wameanzisha nchi nyingine ndani ya nchi ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakimbizi hawa wamefikia kiwango cha kuchagua nani awe kiongozi wao wa kisiasa kwa nafasi zote; Diwani, Katibu nani, hata Mbunge wanayemtaka wao. Vilevile bahati mbaya Mwenyekiti iko haja kubwa ya kuangalia maslahi wanayopata hawa wakimbizi ambayo sasa wako kama raia wa Tanzania; na hawa wanapata elimu bure, wanapata maji bure, wanapata chochote ambacho Watanzania wanapata. Imekuwa mbaya zaidi, inahofiwa kwamba hawa wanaongezeka kwa wingi sana lakini pia wanasoma sana wanapata hata mikopo ya elimu ya juu na vilevile kuingia katika nafasi za kazi muhimu sana kwa ajili ya Tanzania. Hii ni hatari kwa usalama wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa na hayo ya kuchangia. Nakushukuru sana kwa muda ulionipa. Ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)