Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Sonia Jumaa Magogo

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. SONIA J. MAGOGO: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuipongeza Wizara kwa wasilisho zuri pia jitihada za dhati kabisa za kusimamia tasnia hizi za Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri nianze kwa kuchangia upande wa vipaji ambavyo vinahitaji kuendelezwa. Watoto wengi hasa mikoani (vijijini) wana vipaji lakini wanakosa mtu wa kuwashika mkono, mfano, ni Kituo cha Michezo cha Manga, Wilayani Handeni, Tanga ambao wamefikia kutoa mtoto mmoja anayeshiriki timu ya under 17, lakini hawana uangalizi ambao laiti ungekuwepo tungepata wachezaji bora kabisa wa mpira wa miguu. Pia vipaji mashuleni viufuatiliwe na kuendelezwa.

Mheshimiwa Spika, pia tunaona kumekua na wimbi la vijana wengi wakijiunga na ajira ya online TV. Hili limesaidia katika kupunguza tatizo la ajira. Ila vijana hawa wanakwamba kwenye ada za kujisajili, Serikali ingeangalia uwezekano wa kuwasaidia angalau waruhusiwe kufanya kazi zao ili mradi wanafuata taratibu na sheria za nchi na hizo ada za usajili zikatwe katika mapato yao ya kila mwezi au wapewe muda walipe taratibu hadi wakamilishe huku wakiendelea na shughuli zao na kujiingizia kipato.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mitandao kusaidia sana katika shughuli mbalimbali za kila siku za jamii kujiingizia kipato, burudani na hata kupashana habari mbalimbali bado kuna wimbi la wanaotumia mitandao vibaya kama vile kutuma ujumbe mfupi unaolenga kutapeli, kufanya biashara za ngono, kutukana katika mitandao, vitu ambavyo nashauri Serikali iweke adhabu kali na zitangazwe hadharani ili wengine waogope wasione kama ni maneno tu bila vitendo.

Mheshimiwa Spika, pia Serikali iboreshe viwanja vya mpira hasa mikoani. Viwanja vingi vipo katika hali mbaya na vinahitaji maboresho hasa uwanja wa Mkwawani, Tanga ambao ni uwanja wa siku nyingi na moja ya viwanja vikubwa hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, bado mikataba ya wasanii wetu haiko vizuri na wanachopata hakilingani na kazi wanazofanya. Serikali ingeangalia uwezekano wa kuwa na mkataba maalum unaotoa maelekezo ya ujumla kwa wasanii wote, mfano, kama msanii atatumika katika tangazo au kazi ya aina fulani malipo yake yaweje ili kuondoa ukandamizaji unaotokea kwa wasanii wetu.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.