Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Venance Methusalah Mwamoto

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilolo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii niweze kukushukuru kwa niaba ya Bunge Sports Club, nami mwenyewe. Kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri kwa kazi nzuri ambayo wamekuwa wakiifanya na kutusaidia kupelekea timu zetu nyingi kufanya vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nianze kuchangia, nitajielekeza zaidi kwenye ushauri kuhusu michezo. Tulikuwa na mfumo mzuri sana wa kuwapata wachezaji kwenye timu zetu za Taifa toka zamani. Tulikuwa tuna michezo ya UMISETA, UMISHUMTA, SHIMUTA, michezo ya majeshi na michezo mingine. Huko ndiko ambako timu zetu za Taifa zilikuwa zinapatikana na ndizo academy zetu zilikuwa, lakini leo hivi vyote havipo, tumeua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ule uwezekano wa kupata timu nzuri umeanza kuwa shida. Kwa sababu ukiangalia pamoja na kuwa tumefanya vizuri kwenye Timu ya Taifa ambayo bahati mbaya jana na juzi imefungwa, jinsi walivyopatikana wachezaji inaonesha kabisa bado mfumo siyo mzuri, kwa sababu wale wachezaji wamepatikana kwenye academy.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika wachezaji ambao wako kwenye timu ya Taifa ile ya vijana; ni vijana wanane wanatoka kwenye Shule ya Alliance, Mwanza. Kwa hiyo, tungekuwa na academy au tungekuwa na michezo mingine mingi, maana yake tungepata wachezaji kutoka nchi nzima, lakini leo wanatoka sehemu moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naweza kusema kwamba hatuwezi kuwa na timu nzuri ya Taifa. Kwa hiyo, naomba, tuangalie ni mfumo gani sasa Serikali itaingia nao ili kushirikisha vijana wetu toka wadogo na wa kati mpaka kupata wanamichezo wazuri. Michezo yote; ukiangalia kwenye riadha sasa hivi the way jinsi ambavyo wanapatikana ni kubahatisha, lakini zamani ilikuwa unawapata kirahisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Serikali itoke iangalie ni mfumo gani ambao tunaweza tukatoka nao. Kwa sababu ukisema academy ni gharama na siyo rahisi ukawa na academy nchi nzima, lakini kuna vitu ambavyo tukikaa na kubuni vinaweza vikatusaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, labda nichangie tena kitu kingine ambacho nimekuwa nikisema siku zote, TFF bahati nzuri wapo. Niliwahi kusema kwamba Uingereza naweza kusema ndiyo nchi yenye ligi bora, lakini Timu ya Taifa ya Uingereza siku zote siyo nzuri kwa sababu ya utitiri wa wageni. Kwa hiyo, Tanzania, sipingi sana, mwanzo nilipendekeza kwamba tupunguze idadi ya wageni kwenye timu zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kinachosikitisha zaidi ni kwamba bidhaa zinapoletwa Tanzania zinakaguliwa, kuna chombo kabisa kimeundwa kwa ajili ya kukagua zile bidhaa ambazo zinaingia nchini, zile ambazo zinakuwa siyo bora zinateketezwa. Wachezaji wanaotoka nje kuja kucheza Tanzania leo hawana ubora. Kwa hiyo, Watanzania hakuna wanachojifunza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, bado narudi kusema hivi, tuweke sheria kama nchi nyingine wanavyofanya, kwamba mchezaji anapokuja kuchezea kwenye nchi yetu, lazima angalau awe anachezea Timu ya Taifa kwenye nchi yao. Leo wachezaji wanaokuja kuletwa hapa ni wachezaji ambao kule wameshindikana, hawachezi; wakija hapa ni majeruhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia upande wa Simba, kuna wachezaji wawili au watatu; Kagere, Okwi labda na Chama. Ukija upande wetu wa Yanga, unamkuta yuko mmoja tu pale, sasa wengine hata benchi hawakai.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nafikiri hebu TFF mtusaidie ili tuweze kuboresha timu zetu za Taifa. Bila kufanya hivyo, hatutakuwa na Timu ya Taifa nzuri hata siku moja. Tutakuwa tunaendelea tu kuzifurahisha Simba na Yanga, Azam lakini Watanzania watakuwa wanaendelea kukasirika kwa timu yao ya Taifa. Kwa hiyo, naomba tulifanyie kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia wenzetu juzi kwenye benchi la ufundi la Timu ya Taifa ya Nigeria, pale kwenye benchi la ufundi kulikuwa kuna wachezaji ambao walicheza Olympic mwaka 1996 alikuwepo mtu anaitwa Mateo Atepigu na Peter Lufly walikuwa kwenye benchi la ufundi, lakini ukiangalia Timu yetu ya Taifa kocha umri wake analingana karibu sawa na wale vijana.

Mheshimiwa Naibu Spika, wenzetu huwa kwenye timu ya vijana wanaweka mtu ambaye ana umri mkubwa kwa ajili ya kuwalea kama watoto wake, watamwelewa. Sasa unaweka kijana ambaye ana umri unafanana.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni ahadi. Wale watoto ni wadogo unapomwahidi gari, unaahidi fedha nyingi, wale watoto wanachanganyikiwa. Afadhali tungewaahidi basi kwamba utasomeshwa, nakadhalika. Ukiangalia kwenye Timu ya Nigeria wachezaji wanane wanacheza nje professional, lakini wa kwetu wale kama unavyoona. Kwa hiyo, hatulaumu, lakini tulipofikia siyo pabaya isipokuwa tujirekebishe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mashindano mengine yanakuja. Kuna Mashindano ya Walemavu ya Afrika Mashariki, tunapata heshima tena kama ambayo tumeipata hii. Kwa hiyo, kwa sababu tunapata hiyo heshima, haya ambayo yanaendelea siyo rahisi tena kushinda, tukishinda basi Mungu atakuwa ametusaidia, lakini yanakuja ya walemavu. Afrika Mashariki tumepata heshima hiyo tena na wanatupa heshima hiyo kwa sababu ya amani na usalama wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiomba Serikali, Mheshimiwa Mwakyembe, tusiende kama tulivyokwenda ile, kwa sababu ile timu ndogo Taifa maandalizi ya AFCON yalikuwa siyo mazuri. Wenzetu walianza miaka mitatu kuziandaa hizi timu, sisi tumefanya miezi sita au mitatu tu. Kwa hiyo, hii timu ya walemavu angalia, inaitwa Tembo Warriors, tuangalie jinsi ya kuwasaidia sasa angalau tutoke na hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna vijana wenye mtindio wa ubongo hapa, wamechukua dhahabu kadhaa. Wale wazima wanashindwa kutuletea chochote; tuendelee basi tuwasaidie hawa wenzetu ambao wana uwezo. Kama hawa wenye mtindio wa ubongo na walemavu wengine ambao tuna uhakika wanaweza kufanya vizuri, michezo mingine imetushinda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, TBC, namwomba ndugu yangu, Mkurugenzi, rafiki yangu, kuna hawa wenzetu wenye ulemavu wa usikivu, kuna mtu ambaye anatakiwa apewe kazi pale kwa ajili ya kutafsiri alama zile ili wapate haki ya habari na wenyewe. Ni muda mrefu toka tumeomba, lakini bado hajaajiriwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba hebu tuwatendee haki ili tuweze…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, lakini usikivu pia TBC kule Nkasi na Kibondo bado siyo mzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba niunge mkono hoja. (Makofi)