Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Katiba na Sheria

Hon. Mohamed Omary Mchengerwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rufiji

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Katiba na Sheria

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema kwamba amani na utulivu wa Taifa letu ni misingi iliyoachwa na Waasisi wa Taifa hili katika kuimarisha Serikali, Bunge kusimamia Serikali na Mahakama kuachwa kuwa huru katika kuamua mashauri mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwalimu Nyerere miaka ya themanini aliwahi kusema kwamba zipo kazi ambazo kila Mtanzania anaweza kufanya, lakini miongoni mwa kazi hizo, siyo kuwa Hakimu au kuwa Jaji. Mwalimu Nyerere alizingatia kwamba Katiba yetu ya mwaka 1977 lakini nyakati za upatikanaji wa uhuru, yako mambo mengi ambayo Watanzania pengine wangependa kuwa nayo. Nachukua fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ameendelea kufanya uteuzi wa Majaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi kifupi kilichopita, tumepata Waheshimiwa Majaji vijana kabisa na tunaipongeza Serikali kwa sababu Waheshimiwa Majaji hawa wataweza kufanya kazi kwa zaidi ya miaka 20 na kupata uzoefu mrefu zaidi kuliko kuteua mtu ambaye amekuwa mtu mzima na anashindwa kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, Msemaji ame-challenge mamlaka ya Mheshimiwa Rais kuteua Majaji akiishutumu Tume ya Utumishi wa Mahakama aki-cite Ibara ya 113 kwamba inashindwa kumshauri vyema Mheshimiwa Rais. Naomba nimkumbushe msemaji kwamba ajiongoze katika Ibara ya 109, ibara ndogo ya (7) pamoja na ibara ndogo ya (8). Mheshimiwa Rais hafungwi na masharti katika uteuzi wa Waheshimiwa Majaji. Mheshimiwa Rais ana uwezo wa kumteua Jaji yeyote, kwa kuzingatia masharti yaliyowekwa katika ibara ndogo ya (7) au vile atakavyoona yeye mwenyewe inafaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imezungumzwa katika taarifa ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu demokrasia. Msemaji katika ukurasa wa 15 amesema kwamba Tanzania haifuati misingi ya demokrasia iliyoainishwa katika chapter mbalimbali za Umoja wa Mataifa pamoja na Afrika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimkumbushe Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani kwamba demokrasia siyo Coca Cola. Niseme haya kwa kuwakumbusha Watanzania wote kwamba hotuba iliyotolewa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baba wa Taifa, kwenye Mkutano Mkuu Maalum wa Chama cha Mapinduzi, hotuba hii ilitolewa tarehe 18 mwezi Februari, 1992 naomba ninukuu baadhi ya maneno ambayo Mwalimu Nyerere aliwahi kuyasema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwalimu Nyerere alisema kwa sauti yake kwamba “Utaratibu wa kidemokrasia uliobora kwa nchi yoyote, yaani utaratibu utakaofaa kwa nchi hiyo utatofautiana wakati wowote kati ya nchi moja na nchi nyingine na hata kati ya nchi moja, utaratibu utakaofaa utatofautiana kipindi kwa kipindi. Demokrasia si bidhaa kama Coca Cola ambayo nchi moja inaweza kuagiza kwa fedha za kigeni kutoka nchi nyingine na nchi zote duniani zikawa zinakunywa Coca Cola ile ile; na ole wake nchi yoyote ambayo haina fedha za kigeni.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni maneno ya Julius Kambarage Nyerere aliyowahi kuyasema wakati huo. Naomba niwakumbushe tu wenzangu kwamba demokrasia zinatofautiana, nami napenda niishauri Serikali kutoridhia mikataba ya namna hiyo kwa sababu hatuwezi kufanana. Demokrasia iliyopo Tanzania haiwezi kufanana na demokrasia iliyopo Misri pamoja na nchi nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nitoe ushauri. Tanzania kuna Wilaya zaidi ya 169, lakini kati ya Wilaya hizo, Wilaya 27 tu pekee ndiyo zenye Mahakama za Wilaya ambazo ziko katika mamlaka ya usikilizwaji wa mashauri katika wilaya hizo. Wilaya zaidi ya 87 zinaazima majengo mbalimbali katika maeneo husika. Pia Wilaya zaidi ya 23 wanategemea kutoka kwenye mamlaka ya wilaya za jirani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali, kwa kuwa mamlaka ya uanzishwaji wa mikoa na wilaya ni mamlaka ya Serikali, naiomba Serikali, wakati inaandaa mpango mkakati wa kuanzishwa wilaya, basi pengine wafikirie ni namna gani wanaweza kuisaidia Mahakama kwa kuanzisha majengo ya Mahakama, lakini wakati fulani inakuwa ni aibu kwa Mahakama kwenda kununua ardhi au kutafuta ardhi ya kujenga Mahakama za Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Serikali wakati inafikiria kwenda kuanzisha Mamlaka za Wilaya na Mikoa, izingatie pia kwamba ipo Mahakama ambayo imetamkwa kwenye Ibara ya 107 kwamba ni muhimu kuwepo kwa Mahakama katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kushauri ambalo nimejaribu kulieleza katika taarifa yangu, ni marekebisho ya sheria Na. 2 ya mwaka 2018 ambayo yamempa mamlaka makubwa Mkurugenzi wa Mashtaka. Naiomba sana Serikali, namwomba Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuona uwezekano wa kuleta marekebisho ili Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, basi iweze kupata proceeds ya kiasi cha fedha ambayo inaokoa wakati wa uendeshwaji wa mashauri yale ya uhujumu uchumi na mashauri mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili nimelizungumza vizuri sana kwenye taarifa yangu na naomba nisisitize kwa Serikali, Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuona uwezekano wa kuleta marekebisho ya sheria au kwa kutumia kanuni ili mwongezea mamlaka Mkurugenzi wa Mashtaka kuweza kupata kiasi cha fedha kidogo ambacho kinaweza kusaidia. Eneo hili, siyo tu kwa Mkurugenzi wa Mashtaka, hata vyombo vingine vinanufaika na maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kusisitiza ni kuhusu mlundikano wa mahabusu. Wiki kadhaa zilizopita tulimsikia Mheshimiwa Rais akitoa maelekezo kuhusu moja ya kesi za jinai ambazo mtu mmoja alishitakiwa kwa kosa la mauaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, lakini pia tuiombe sana Mahakama. Sheria Na. 2 ya mwaka 2018 imetoa maelekezo fasaha kabisa kuhusu jukwaa la haki jinai. Nami niseme kwamba Mahakama imepata bahati kubwa sana kwa kumpata Jaji Kiongozi ambaye aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka, ana ufahamu mzuri sana kwenye eneo hili. Sheria hii imeelezea utaratibu wa haki jinai. Tumwombe Mkurugenzi wa Mashtaka atumie jukwaa hili ili kupunguza mlundikano wa mahabusu Magerezani na maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia imezungumzwa kuhusu...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Mchengerwa kwa mchango wako.

MBUNGE FULANI Mwongozo, mwongozo wa Spika.

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)