Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata muda huu kuweza kuchangia kwa maandishi. Namshukuru Mwenyezi Mungu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa pongezi sana kwa Mheshimiwa Rais, Makamu wa Rais na Mheshimiwa Waziri na Makamu wa Waziri kwa kazi nzuri wanayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Viumbe Vamizi. Kuhusu hasa gugu la Kongwa ambalo linaharibu malisho ya mifugo ni la muda mrefu sasa ingawaje Serikali inajitahidi kukabiliana nalo, lakini bado ni tatizo. Mheshimiwa Waziri nashauri jitihada zaidi zitumike ili kutokomeza kabisa gugu hili la Kongwa. Naomba maelezo zaidi kwa niaba ya wafugaji na Serikali na hasa kuhusu gugu hili lililoenea katika Ranch ya Kongwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu gugu karoti ambalo linaenea kwa kasi hasa Mikoa ya Kaskazini. Gugu hili ni hatari, Mheshimiwa Waziri anafahamu gugu hili linahatarisha na hasa katika kilimo mazao na malisho. Mheshimiwa Waziri ningependa kujua kwa niaba ya wakulima na wafugaji mikakati inayoendelea ya haraka ili kutokomeza gugu karoti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu vyanzo vya maji na upandaji miti rafiki ya vyanzo vya maji. Natoa pongezi za jitihada zinazoendelea kunusuru vyanzo vya maji. Nashauri elimu izidi kutolewa kuhusu vyanzo vya maji na kupanda miti rafiki ili kulinda vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Morogoro tuna matatizo ya maji na hasa Halmashauri ya Morogoro Manispaa. Sababu mojawapo ikiwa ni uharibifu wa vyanzo vya maji na ukataji miti katika Milima ya Uluguru. Mheshimiwa Waziri kwa jitihada zake za kulinda mazingira, naomba akaliangalie tatizo hili, ili kunusuru vyanzo vya maji milima ya Uluguru (Morogoro) kwa madhumuni ya upatikanaji wa maji na uhai wa mito kama ilivyokuwa zamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais, Waziri Mkuu na Mheshimiwa Waziri kwa kulisimamia suala hili la mifuko ya karatasi. Kama Mheshimiwa Waziri alivyoelekeza kupitia kwenye mkutano (15/04/2019) na kwenye hotuba yake ya bajeti. Nashauri Mheshimiwa Waziri na watalaam wake walisimamie kwa ukamilifu ili tuweze kuondokana na tatizo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la ukataji miti na uchomaji mkaa bado ni tatizo. Elimu zaidi inatakiwa kwa wananchi kuhusu faida na hasara za kutunza mazingira, hasa kwa kupanda miti na kukata miti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, gunduzi kuhusu nishati mbadala na hasa zinazooneshwa wakati wa maonesho ya Siku ya Wakulima – Nane Nane zipewe kipaumbele kwa kuwaendeleza na kuwawezesha wagunduzi hawa wa nishati mbadala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo la fedha katika ofisi hii ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira). Nashauri fedha zote zilizoombwa wakati wa bajeti hii zitolewe kwa wakati ili waweze kufanya kazi zao vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.