Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niwe mmojawapo ambao wamepata fursa ya kuchangia hoja na kupata fursa ya kujibu baadhi ya hoja ambazo zimeletwa na Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kipekee nianze kwa kushukuru kamati yetu ya Utawala na TAMISEMI kwa maelekezo ambayo wamekuwa wakitupatia lakini pia Waheshimiwa Wabunge katika michango yao yote ya kujenga. Kama kuna Wizara ambazo zimetendewa haki ni pamoja na Wizara yetu. Kwa ujumla nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja ya kuhusiana na TARURA ambayo imeongelewa na Waheshimiwa Wabunge wengi kuanzia kamati yetu, lakini pia Kambi Rasmi ya Upinzani imeongelea juu ya suala zima la TARURA kuongezewa fedha, lakini kama siyo kuongezewa fedha, pia wameongelea suala zima la kutaka mgawanyo wa fedha utazamwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika na Waheshimiwa Wabunge wote ni mashuhuda, hali tuliyoanza nayo kuhusiana na suala zima…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Hawanisikilizi eeh!

Mheshimiwa Naibu Spika, wewe ni shuhuda jinsi ambavyo tulianza Waheshimiwa Wabunge wengi walikuwa wanalalamikia jinsi ambavyo utendaji kazi wetu wakati matengenezo ya barabara yalikuwa chini ya Halmashauri. Kila Mheshimiwa Diwani na Wabunge sisi tukirudi kule ni Madiwani, kila mmoja alikuwa anaomba kipande angalau kilometa moja kitengenezwe. Kwa hiyo, value for money ilikuwa haionekani.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tupokee pongezi ambazo tumepokea kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge juu ya utendaji bora wa TARURA. Wengi wamesifia juu ya chombo hiki, lakini ni ukweli usiopingika kwamba tuna safari ya kuhakikisha kwamba tunaimarisha TARURA ili ule upungufu ambao Waheshimiwa Wabunge wamesema uweze kurekebishika.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia ni ukweli usiopingika kwamba kilometa ambazo zinahudumiwa na TARURA, chombo hiki ambacho tumekianzisha sisi wenyewe, takribani kilometa 108,000 ni nyingi. Pia wameomba ikiwezekana mgawanyo ubadilike kutoka asilimia 30 kwa 70. Zipo sababu za msingi kwa nini tulikwenda kwenye hiyo formula? Nasi Serikali tumesikiliza kwa Waheshimiwa Wabunge, imeundwa Tume ambayo inafanya tathmini kupitia upya ili pale ambapo tukija na majibu ya uhakika tushirikishe Bunge letu katika kuwa na formula ambayo itahakikisha kwamba TARURA inafanya kazi nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna suala zima la ukosefu wa vitendea kazi ikiwepo magari. Ofisi ya Rais, TAMISEMI imeliona hili na ninaomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba tumeanza kununua magari ili kuhakikisha maeneo yote ambayo hakuna gari ziweze kufikishwa. Tumeanza na gari 22 katika kipindi kilichopita na safari hii tunaenda kununua gari 22. Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge maeneo yote ambayo yana uhitaji mkubwa wa magari tutayazingatia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala zima la ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya. Kipekee naomba nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tumeweza kupata kiasi cha shilingi bilioni 100.5 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya na hospitali. Tumeanza na hospitali 67 na Waheshimiwa Wabunge wote ni mashuhuda kwamba katika bajeti ambayo tutaomba baadaye watupitishie tunaenda kuongeza tena hospitali 27. Ni kazi kubwa na nzuri; ni wajibu wa Serikali kuhakikisha kwamba huduma ya afya inasogezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba waheshimiwa Wabunge tusaidiane tuhakikishe kwamba tunasimamia malengo ambayo tumeweka Ofisi ya Rais TAMISEMI kufika tarehe 30 mwezi Juni, yale majengo saba yawe yamekamilika na wananchi wa Tanzania waanze kupata huduma ya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hilo halitoshi, pia tunaenda kuongeza hospitali nyingine 27. Fedha imetengwa na ninaamini muda siyo mrefu Waheshimiwa Wabunge watapitisha ili tuweze kwenda kujibu kijibu kiu kubwa ya Watanzania kuhakikisha kwamba wanapata huduma ya afya umbali usiokuwa mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala zima ambalo napenda niongelee kidogo kuhusiana na usafiri wa mabasi ya mwendokasi kwa Dar es Salaam. Hili limechangiwa sana na Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam. Naomba niwahakikishie azma ya Serikali ya kuhakikisha kwamba msongamano wa usafiri kwa Dar es Salaam unapungua, iko pale pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mchakato ambao tulikuwa tumeanzisha wa kumpata mwendeshaji wa mwanzo ambaye kwa mujibu wa mkataba interim operator ilikuwa a-oparate na mabasi 140, lakini ndani ya mwezi huu Aprili tutahakikisha kwamba kandarasi inatangazwa na ukifika mwezi wa nane Mwenyezi Mungu akijaalia tutakuwa tayari tumeshampata mkandarasi wa kuendesha mabasi hayo na yataongezeka kutoka mabasi 140 mpaka mabasi 305. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, naomba niwahakikishie kwamba mchakato tutahakikisha unakwenda vizuri. Kama hiyo haitoshi, tunaenda kujenga barabara ya kuanzia katikati ya Mji wa Dar es Salaam kwenda Kilwa Road kwenda Gongolamboto kwenda Tegeta. Ni azma ya Serikali ambayo inaongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kuhakikisha kwamba wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam wanapunguziwa adha ya usafiri kwa maana ya msongamato.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hilo halitoshi, kuna suala zima la DMDP, naomba niwahakikishie Wabunge na hasa Wabunge wanaotoka Dar es Salaam, tupo vizuri tumejipanga muda siyo mrefu wao wenyewe watajionea jinsi ambavyo mchakato unakamilika na barabara hizi zinaanza kutengenezwa ili kuhakikisha kwamba Dar es Salaam inaendelea kuwa mahali salama pa kuishi na wananchi kufurahia matunda ya chama chao cha CCM.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala zima limeongelewa kuhusiana na asilimia 10 ambayo inatakiwa itolewe kwa ajili ya akinamama, vijana na watu wenye uhitaji maalum kwa maana ya watu wenye ulemavu. Wewe ni shuhuda kwamba tumepitisha sheria, kwa hiyo ni takwa la kisheria kwa Wakurugenzi wote kuhakikisha kwamba wanatenga asilimia 10 kutokana na mapato yao ya ndani. Tayari kanuni zilishakuwa tayari, muda wowote ndani ya mwezi huu kanuni zitakuwa zimetoka, kwa hiyo Mkurugenzi yeyote hatakuwa na kisingizio kwa nini hatengi hizo fedha na kuhakikisha kwamba fedha hizo zinakwenda kuwafikia Watanzania tuliowakusudia, ikiwa ni akinamama, vijana na watu wenye ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mengi, naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wote, kila Mbunge ambaye alitoa hoja yake tutaijibu kwa maandishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukru sana kwa muda wako. (Makofi)