Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Emmanuel Papian John

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kiteto

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. EMMANUEL P. JOHN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nipongeze Mawaziri ambao wametuletea bajeti yetu hii, Mawaziri wote wawili kwa ushirikiano mkubwa na bajeti nzuri ambayo imeweza kutusaidia kutupa malengo na mwelekeo wa 2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze kwa kazi nzuri na bajeti ambayo mmetutengea Kiteto kwa maana ya TARURA kutupa shilingi bilioni 1.6, secondary school shilingi bilioni 1.4, primary school shilingi bilioni 1.2, Kituo cha Afya cha Engusero shilingi milioni 200 na maboma yanaendelea kumaliziwa. Hongereni sana kwa kazi nzuri ambayo mnaendelea kutusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi hiki ambacho tunaelekea mwishoni mwa bajeti ya 2019 naomba tupate pesa za kumalizia jengo letu la Halmashauri ambalo limesimama muda mrefu. Mheshimiwa Waziri Jafo unajua kabisa hili jengo lipo ukingoni tunahitaji mtutengee pesa kwa haraka ili angalau katika hii miezi miwili mitatu tuweze kufanya kazi ambayo tunadhani kwamba ingeweza kutusaidia kumalizia hilo jengo ili tukafanyie uchaguzi mahali ambapo pako safi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo miradi hii ya kimkakati ambayo tumeomba pesa na miradi mingi ambayo inaendelea, naomba na kushauri Serikali kwamba kwenye miradi hii ya kimkakati Serikali ingeweza kuainisha maeneo ambayo yanaweza kuwa na miradi ambayo ni highly paying ili iweze kui-fund mapema inaweza kusaidia zile Halmashauri kutengeneza ile internal income yake na kusaidia kupunguza utegemezi Serikali Kuu, jambo hili linaweza kusaidia sana Halmashauri. Zile Halmashauri ambazo hazina miradi mikubwa wala vyanzo vya mapato, inaweza kuhamisha ile pesa ambayo ingeweza kuwa inaenda kwenye zile Halmashauri ikapunguza zile pesa zikaenda kwenye zile Halmashauri na kuhakikisha kwamba tunatengeneza uwiano wa mapato kwenye Halmashauri zetu na kuhakikisha kwamba tunasukuma gurudumu la maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utawala bora. Kwenye utawala bora pale Kiteto tuna nyumba yetu ya TAKUKURU imeharibika na imekwisha. Nilitaka kumwomba Waziri, Mheshimiwa Mkuchika ikikupendeza tuondoke hapa wakati wowote baada ya maswali na majibu ukaangalie hilo jengo, ikikupendeza ukitutengea shilingi milioni 15 tukitumia force account lile jengo tutalikarabati na litakuwa salama. Mimi nikuombe kwa hilo ukubaliane na mimi kabla hujaamua lolote twende kule uone halafu turudi tuweze kuamua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo jambo la TASAF. Katika kusaidia kaya maskini tuli-form mfumo ambao uliweza kusaidia watu kukatiwa bima ya afya. Watu wamekuwa wanakatwa pesa zao, bima za afya zinachelewa kuja, watu hawapati matibabu, pesa zinakwenda na mwaka unaisha halafu wanaendelea kupoteza hela zao. Naomba Mheshimiwa Waziri ujitahidi ulione hili na ni namna gani tunaweza kufanya kwa ajili ya kupata bima ya afya basi hizo pesa zinapokatwa bima ya afya iwahi na watu waweze kupata matibabu katika mwaka husika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kuzungumza juu ya suala la Madiwani. Madiwani wetu sasa hivi ni viungo muhimu sana na wanafanya kazi sana kwenye maeneo yetu. Madiwani hawa sasa hivi ndiyo wanaoweka pressure ya kusimamia kwenye Baraza la Madiwani na WDC zao kwa ajili ya kusukuma shughuli za maendeleo ya ujenzi wa hivi vituo vya afya vinavyojengwa kote nchini. Madiwani hawa ndiyo tunaowabana kwa ajili ya kujenga maboma na kusimamia pesa kwa kutumia force account ili waweze ku-manage zile fedha vizuri. Madiwani hawa ndio wanaosimamia miradi ya maji, ukusanyaji wa kodi, mapato na ushuru wa Halmashauri kwenye vyanzo vyetu ili kuona ni namna gani ya ku-push maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Serikali na Mheshimiwa Jafo mlione. Nilikuwa naangalia tuna Madiwani zaidi ya 3000 nchi nzima, Madiwani hawa tungewapa pikipiki. Mimi Diwani mmoja anatembea kilomita 120 kwenda na kurudi ni 240, huyo Diwani atakwenda wapi na wapi? Haiwezekani! Nina Diwani ambaye lazima akienda kwenye eneo lake la kijiji fulani lazima alale huko na kesho yake arudi, anapita maporini kuna incidence nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Waziri liangalie suala hili tupate pikipiki kwa sababu tume-afford kuwapa wataalam wa elimu kwenye kata zetu, tuone ni namna gani tunaweza ku-support hawa Madiwani wapate vyombo vya usafiri mafuta watajitegemea lakini tuone namna gani wanaweza kuwa motivated na kusukuma gurudumu la maendeleo kwenye maeneo yetu na maagizo mengi ambayo Wakurugenzi wetu wanawaagiza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la maboma; Kiteto tuna maboma 92 ya primary schools, secondary schools tumeshamaliza kwa kutumia mapato yetu ya ndani. Niombe tusaidiwe pesa haya maboma yaweze kumalizwa kwa wakati kwa sababu watoto wetu kutoka point moja kwenda nyingine anakwenda kilomita 56; hatuwezi kupeleka wale watoto kwenye hayo maeneo kwa kuanza primary school. Tuna watoto ambao hawawezi kusafiri umbali mrefu na kurudi nyumbani kwa jiografia ya Wilaya yetu maeneo ya kifugaji ya Ndido, Makame, Rolela, Sunya na kuna maeneo mengi ambayo ni makubwa na mapana ambayo watoto hawawezi kwenda shule na kurudi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeanzisha shule sikizi, zinawasaidia wale watoto kujua kusoma na kuandika, vinginevyo tusipofanya hivyo tuta-create mfumo wa kuwa na watu ambao hawajui kusoma na kuandika na mwisho wa siku wataogopa kwenda shuleni kwa kusubiri hizi shule zikafunguliwe. Niombe review progamme yenu ya kuangalia ni namna gani ya kusajili hizi shule, muangalie madarasa yanayofikiwa, mfumo upi utumike ili watoto wetu waweze kuanza shule na zile shule ziweze kufunguliwa, mpunguze aina ya vigezo ambavyo mnaona kwamba vinaweza kusaidia kuhakikisha kwamba hizi shule zinaanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kumalizia kwa kusema yafuatayo. Nimeona wenzetu watani zetu na wengine wanalalamikia Serikali na Rais kwamba hakuna utawala bora. Watu wanasema kwamba hapatatosha, patachimbika, naomba niwaambie Rais Magufuli ukimwambia kwamba kesho hapatachimbika patatokea fujo, anataka hapohapo. Ogopa Rais ambaye hawezi kurudi nyumba ana-change gear angani kukabiliana na mapambano, huyo ndiyo Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukishaona una kiongozi huyo hapo juu, wewe unachofanya always unakuja mezani mna- debate hoja yako, mnatatua mgogoro mnamaliza, ana-solve matatizo yako akimaliza mnapeana mikono kwaheri. Ukitangaza msuli kwa namna Rais wetu Magufuli alivyo na namna anavyotekeleza shughuli, bora akufyatue mambo mengine mtajadili baadaye. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwape mfano maana tunazungumza kwa mifano, Kibiti hapa juzi walisumbua mbele nyuma, amefyatua mapolisi waliokuwa wanalinda na ule upuuzi uliokuwa unafanyika pale. Amegeuza viongozi pale, amehakikisha amepeleka mtu mmoja tu amecheza vizuri sembuse mahali ambapo panawaka taa. Niwaombe tukae mezani, tuijenge Tanzania kwa kushauriana, tu-debate wote, tutafute solution ya issues zinazoikabili nchi kwa pamoja bila kutishiana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe niwaambie Tanzania ina demokrasia ya kutosha, nchi nyingine zinazotuzunguka, wapinzani na wabishi wote wanazungumzia ughaibuni na nje ya nchi. Unatoka hapa unazungumza mtaani na unarudi nyumbani unalala; unatoka hapo unatukana unarudi unalala, huyo Rais leo East and Central Africa, utampata wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, niwaambieni hapa ndiyo tunaagana, tunatafuta nani anaenda kibra kazaneni na sisi tunakazana, kesho kutwa 2020 mechi uwanjani biashara imekwisha, huko ni CCM, huku ni CCM kazi imeisha. CCM hoyee, Mungu awabariki sana. (Makofi)