Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Livingstone Joseph Lusinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtera

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutuzawadia tena pumzi yake leo bure ili tuweze kukaa kwenye Bunge lako Tukufu na tuweze kuchangia hoja za Wizara mbili; ile ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na ile ya Utawala Bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wengi wamesema juu ya Waheshimiwa Watendaji Wakuu wa Wizara hizi; nami nachukua fursa hii kuwapongea sana ndugu yangu Mheshimiwa Selemani Jafo, Waziri; pamoja na Mheshimiwa George Huruma Mkuchika, Waziri; pamoja na Waheshimiwa Manaibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Mary Mwanjelwa; pamoja na ndugu yangu Mheshimiwa Waitara na Naibu Waziri mwenzake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mawaziri hawa wanafanya kazi kubwa sana. Tunaona namna wanavyopambana na shida za watu wetu, siyo vizuri sana kuwavunja moyo, wakati mwingine tuwapongeze kwa kazi nzuri wanazozifanya. Mheshimiwa Jafo pamoja na timu yake ya Watendaji wametusaidia sana sisi wa Jimbo la Mtera kutuletea pesa kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Mpwayungu. Wametupa shilingi milioni 700 pale, wakatupa shilingi bilioni 1,500,000,000/= kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya; vilevile wametusaidia miradi ya maji yenye thamani karibu ya shilingi bilioni mbili hivi na ushee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunawashukuru sana ingawa nina ombi maalum kwa ajili ya ambulance ya Tarafa ya Mpwayungu, ilipata ajali na ikachakaa kabisa, lakini tunamshukuru Mungu haikuua. Tunaomba tusaidiwe kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Tarafa ya Mvumi, kile Kituo cha Handali ili kwa kushirikiana na Kituo cha Mpwayungu, hospitali ya wilaya iweze kupumua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile timu ya ukaguzi wa zahanati, naomba Mheshimiwa Jafo hii aitilie maanani sana. Huko vijijini kuna zahanati nyingine hazina sifa hata za kung’oa meno, lakini wanang’oa meno. Hatujui vile vifaa kama viko katika hali ya ubora. Kuna magonjwa mengi sana ya kuambukiza ambayo ni hatari sana kama zahanati zile hazikugaliwa sawasawa hasa kwenye upande wa tiba ya kinywa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maneno mengi yemezungumzwa, nami bahati nzuri nimepewa kazi ya kupiga penalty ya mwisho. Unapopiga penalty ya mwisho lazima uwe umetulia. Ndugu zangu tunapozungumzia habari ya utawala bora kwanza tukubaliane mambo ya msingi. Utawala Bora, vyama vya siasa vinashindana kwa sera. Kila chama kinapeleke sera kwa wananchi kwenda kuomba kichaguliwe. Uchaguzi Mkuu umepita, chama kilichochaguliwa ni CCM, ndiyo kimechaguliwa kwa wingi. Chama hiki hakichaguliwi kwa rangi zake tu, kinachaguliwa pamoja na ubora wa sera zake. CCM ndiyo inapewa nafasi Serikali itafsiri ilani yake kwa miaka mitano bila kujali kwamba Jimbo hili la CHADEMA wala Jimbo hili la NSSR, wala Jimbo hili la chama gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ilani inayotekelezwa pale ni ilani ya mshindi wa ujumla. Wapinzani wanapewa kazi ya ku- oppose, kuleta sera mbadala kama wanazo, lakini wetu hawa kwa sababu hawana, ndiyo maana mnasikia madudu haya. Kama wangekuwa na sera mbadala, wangekuwa wanaeleza kwa hoja. Unasikia hoja, hivi ni Serikali gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi namwombea sana Mheshimiwa Rais, Mungu ambariki aendelee kutumia hekima. Nyie Mawaziri, mwendelee kutumia hekima. Hivi ni Waziri gani anatukanwa, anasemwa vibaya halafu tena anatakiwa apeleke maendeleo kwenye Jimbo la huyo anayemtukana? Hii iko Tanzania tu. Ndiyo maana mnaona tunapata tatizo kwa sababu uchaguzi ukiisha, wale walio shinda ndio wanakuwa na kazi ya kutafsiri ilani yao ya uchaguzi kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa leo upinzani wa Tanzania mnaona wanapiga kelele, wanataka kufaidi kwenye kushindwa. Mimi sijawahi kuona. Ninyi mmeshindwa, mnataka kufaidi nini? Mmeshindwa, lazima m-face problem, lazima m-face utulivu, lazima mkae muwaache walioshinda watekeleze ilani ya uchaguzi. Sasa leo eti timu imefungwa bao tatu bila, hiyo hiyo inataka ishangilie. Nyie mbona mnachekesha! Mimi sijawahi kuiona hii. Hii naiona Tanzania tu. Mtu anasimama anasema, ohoo, tunanyimwa hiki, tunanyimwa hiki. Si mmeshindwa, mtulie. Lazima... (Makofi)

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Bwege kaa chini, Mheshimiwa Lusinde endelea.

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ndiyo maana unaona kunaundwa Kambi ya Serikali na Kambi Rasmi ya Upinzani na wanaundwa Mawaziri wa Serikali na Mawaziri Kivuli. Leo wanaona aibu hata kutaja Wizara zao, kwamba huyu ni Waziri Kivuli. Hawasemi, kwa sababu wanajua kivuIi hakiaminiki. Nani ataamini kivuli? Wanajua kivuli saa sita kiko sawa na mtu, saa saba kinaanza kuwa kirefu, saa 12 kivuli ni kirefu kuliko mtu, wanajua. Wewe uliwahi kuona wapi Mbunge unasimama unampangia Mheshimiwa Rais kitu cha kufanya? (Kicheko/Makofi)

Jamani hii nchi mbona hatuna heshima, unampangia Rais kwamba akija kwangu afanye moja, mbili, tatu, hivi nyumbani kwako hata baba yako mzazi unaweza kumpangia wewe kwamba, leo baba tule hiki, inawezekana? Haiwezekani, kwanza hamjasoma vizuri Katiba ya nchi, Rais wa nchi ni mkuu wa nchi, Rais wa nchi ana madaraka makubwa ambayo hata kikatiba hajayatumia, mnapiga kelele; Rais hayo madaraka yake akiyatumia hamponi ninyi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio maana mimi sasa nawaomba Watanzania hebu mwakani tukubaliane, unajua wakati mwingine kuwahi sana nalo ni tatizo, kuwahi sana nayo ni shida.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaambiwa kwamba, kuwahi sana ni tatizo. Tunaambiwa hata mtoto wa kike wakati mwingine asubiri akomae via vyake vya uzazi ndio abebe ujauzito, kinyume cha hapo ataugua. Upinzani wa Tanzania uliwahi sana, kwa hiyo, nahisi umepata matatizo, uliwahi sana. Kwa hiyo, sishangai kuwaona Kambi nzima ya Upinzani badala ya kujenga hoja za kisiasa zenye muelekeo wa kusisimua Serikali mnaleta hoja za udumavu; angalia upinzani ulivyodumaa kwa sababu ya kuwahi, wamewahi sana kabla ya wakati wao wamejikuta wamedumaa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natangaza kwenye Bunge hili, tatizo tulilonalo tuna upinzani mdumavu. Wamedumaa kisiasa, wamefika mahali hawawezi kujenga hoja mbadala, kazi yao ni kulalamika na kupiga kelele kama unavyowasikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri nchi yetu Mheshimiwa George Mkuchika kwenye utawala bora ashikilie hapohapo. Hakuna nchi yenye utawala bora usio na mipaka, haipo duniani. Wameng’ang’ana wanataka kufanya maandamano ya nini? Mbona mazoezi asubuhi hawaendi sembuse maandamano? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna Serikali ya namna hiyo duniani, uruhusu watu wafanye fujo tu. Eti mtu anasema ooh, mimi nataka niende nikahutubie mkutano, wewe jimbo lile umeshindwa ukahutubie kitu gani? Utaeleza nini? Huna sera, huna ilani, huna kazi unayoifanya pale unataka ukahutubie ueleze nini? Kama sio kufanya kampeni kabla ya wakati? Ninyi mnataka mpate ruhusa ya kwenda kufanya kampeni kabla ya wakati, sisi ndio washindi jamani tunashindwa hata na Miss Tanzania? Kachaguliwa mrembo mmoja, wengine wote wamekaa kimya, wamekaa kimya, lakini hawa wanashindwa; sisi ndio washindi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakasikia kadada kamoja kanasema Lusinde nakupenda, tulia dawa iingie. Mimi nina mke na watoto watano, tukikutana nao kwenye chai wanaongea maneno ya unafiki kabisa, ooh tunaunga mkono, mnachapa kazi vizuri, tunaunga mkono. Tukija humu ndani wanajifanya ooh, Mwenyekiti patachimbika, pachimbike kwa hawa? Hakuna kitu cha kuchimbika hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali ishikilie hapohapo. Angalia kuna watoto wanawaona wanavyozomea, wanawaona ni watu wamechanganyikiwa kabisa. Humu ndani ya Bunge kuna watu wanakuja kujifunza uendeshaji bora wa Bunge, wao wameongea sisi tumenyamaza…

MBUNGE FULANI: Umechanganyikiwa wewe.

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: …sisi tunawapa dawa, ooh, ooh. Watoto wadogo hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nakusihi, tunaomba Serikali kwenye kusimamia sheria isiangalie huyu mpinzani, isiangalie huyu CCM, wote kula kichwa, wakivuruga amani weka ndani, hizo siku 120 walizosema ni kidogo. Kwa hiyo, nataka nikwambie dawa yake ukitaka nchi inyoke, sheria zifanye kazi asiwepo mtu wa kubembelezwa. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hiyo dawa kuingia naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)