Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Amina Nassoro Makilagi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli nilitaka kusema kama ni dakika tano niongee kesho kwa sababu nina salamu za wanawake wa Tanzania ambao mimi ndiyo wapiga kura wangu.

MWENYEKITI: Basi utaongea kesho, Mheshimiwa Mbogo malizia dakika kumi hizo. Mheshimiwa Richard Mbogo, umejitoa? Sikusikii, naona unainama, unakaa.

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ameomba niendelee, amenipa zake zimekuwa kumi.

MWENYEKITI: Haya.

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na nimshukuru sana kaka yangu Mheshimiwa Mbogo na nichukue nafasi hii kukupa pole na msiba mkubwa uliokupata wa kuondokea na mama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaona maneno mengi yanazungumzwa humu ndani sasa nimesimama Mbunge ninayewakilisha wanawake wa Tanzania na Jimbo langu ni Tanzania nzima. Hapa naleta salama za wanawake wa wa Tanzania ambao wamekuwa wakifariki kwa kujifungua kwa sababu ya kukosa huduma, ambao wamekuwa wakitembea umbali mrefu kwenda kutafuta huduma za afya, ambao vituo vilikuwa ni duni havitoi huduma kikamilifu, wakienda leba wanafariki, kwa uongozi wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli Serikali imewajengea vituo zaidi ya 350.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamenituma nilete salama za ahsante kwa Mheshimiwa Rais. Wanasema ahsante kwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi na wanamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na wanasema achutame maana ukiwa kwenye maji unaoga akija mwendawazimu haumfukuzi na akutukanaye hakuchagulii tusi. Wanaosema Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli hajafanya kitu tuwasamehe maana hawajui watendalo, ndiyo salamu walizonipa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanamshukuru Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa sababu Mikoa ya Geita, Simiyu, Kigoma, Mwanza, iko sita ambayo wanawake walikuwa wanafariki kwa kujifungua kwa sababu ya kukosa huduma, kwenye taarifa ya Mheshimiwa Jafo imeeleza ambavyo Serikali inakabiliana na changamoto hizo. Kwa hiyo, ukisikia mtu anabeza tena bahati mbaya wanaongea ni wale ambao hawakwenda leba, tunasema akutukanaye hakuchagulii tusi na ukiwa kwenye maji unaoga akija mwendawazimu haumfukuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumwambia Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli endelea na kazi, tunakuona unahangaika Nyanda za Juu Kusini, leo umefungua vituo vya afya, umekwenda Mikoa ya Mtwara, leo uko Njombe, umekwenda Ruvuma na unakwenda Katavi, unakwenda Tanzania nzima kuwaletea wananchi maendeleo. Chapa kazi baba, tuko nawe na wanawake wa Tanzania na leo nimekuja na book hili ndiyo kazi ulizozifanya na nimewauliza wanasema tukipiga kura leo anashinda kwa asilimia 100. (Makofi)

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kuhusu Utaratibu.

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasema atapita bila kupingwa.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kuhusu Utaratibu.

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo, napenda kuchukua nafasi hii…

MWENYEKITI: Kuhusu Utaratibu.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti...

MWENYEKITI: Kanuni.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kanuni ya 64(1)(a), inasema: “Bila kuathiri masharti ya Ibara ya 100 ya Katiba yanayolinda na kuhifadhi uhuru wa mawazo na majadiliano katika Bunge, Mbunge, hatatoa ndani ya Bunge taarifa ambazo hazina ukweli”. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa anayechangia ametoa taarifa ambazo si za kweli. Tunajua kwamba Tanzania tuna kata zaidi ya 4,000 na kwa Sera ya Afya inatakiwa kila kata iwe na kituo cha afya. Kwa takwimu tu alizozitoa mwenyewe amesema vimejengwa vituo mia tatu thelathini na kitu na nadhani vilikuwa kama 400 hivi. Kwa hiyo, ukitoa utaona zaidi ya kata 3,000 ambazo zina suffer wanawake wanakufa. Hata ukipitia taarifa vifo vya mama na mtoto ni vingi sana kama Taifa bado hatujavipunguza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, pamoja na kwamba amepotosha anazungumzia wanawake wote ambao…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Mheshimiwa kaa chini.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Mheshimiwa kaa chini. Mheshimiwa Makilagi, endelea. (Makofi)

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, inabidi nicheke tu kwa sababu ni mwanangu ana stress naomba tumsamehe kwa sababu ni juzi tu alikuwa na shida. Mimi kama mama nina kazi ya kufanya counseling nitaendelea kwa sababu kama angekuwa…..

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ana uchungu na anajua kuna pengo angeanza kuonesha Tarime ambayo inapata fedha nyingi kutokana na madini lakini…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, afute kauli yake.

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee nimesema kama mama nitaendelea kumlea mwanangu, nitazungumza naye…

MBUNGE FULANI: Afute kauli yake.

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Ni juzi alikuwa na shida nahitaji kumsaidia.

WABUNGE FULANI: Afute kauli yake.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee kwa kusema kwamba Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli amefanya kazi nzuri…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Sophia Mwakagenda, Mheshimiwa Salome Makamba last warning.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Kiti hakijasikia bado.

MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Maryam, kaa chini.

MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nikae vipi chini?

MWENYEKITI: Hutaki kukaa chini?

MBUNGE FULANI: Huyo mama ajiheshimu.

MWENYEKITI: Sema tena hutaki kukaa chini?

WABUNGE FULANI: Sema.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Makilagi, endelea na mchango wako.

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Naomba niendelee kujielekeza katika mchango wangu kama ambavyo nimejiandaa. Naendelea kumpongeza Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi mzuri, Tanzania nzima maana kwenye Ilani ya CCM aliahidi na ametekeleza kwamba tutajenga sekondari, shule za msingi, watoto watasoma bure na ukisikia watu wazima wanapiga kelele wameshikwa pabaya, leo nimekuja na takwimu zinazoonesha kila shule imepata nini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Mkoa wetu wa Mara peke yake Serikali yetu imetupelekea zaidi ya shilingi bilioni 1.7; kwenye hospitali zetu zote za Wilaya kila kila Halmashauri tumepata shilingi bilioni 1.5; kwenye vituo vya afya, hivi ninavyozungumza anajiandaa kujenga siyo hivi vilivyomalizika sasa hivi vingine vipya kwenye Mkoa wa Mara peke yake shilingi bilioni 2 zinakwenda na Mikoa yote ya Tanzania karibu shilingi bilioni 65. Tumpe nini Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli zaidi ya kumpa kura za ndiyo uchaguzi utakapofika? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipongeza Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi na nichukue nafasi hii kuipongeza Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya maelekezo ya Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli alisema tuwawezeshe wanawake kiuchumi. Tumewahamasisha wamejiunga katika vikundi vya vijana na wanawake na watu wenye ulemavu na kupitia Bunge hili tulipitisha sheria ili sasa suala la kutoa fedha kwa asilimia kumi ya wanawake na vijana isiwe jambo la hiari liwe ni la lazima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua nafasi hii kusema karibu Halmashauri nyingi zinafanya vizuri. Hata hivyo, naomba nitoe ushauri, kuna Halmashauri wanakaidi kutekeleza agizo hili, naomba nitumie nafasi na Mheshimiwa Jafo tunakuamini ni mtendaji hodari na mahiri, hebu orodhesha Halmashauri zote ambazo zimeshindwa kutekeleza Azimio la Bunge na matakwa ya sheria ya kutenga asilimia 10 kwa ajili ya vikundi vya wanawake na vijana ili hatua zinazostahili ziweze kuchukuliwa na vikundi vya wananwake na vijana viweze kupata mkopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya Halmashauri zetu ziko taabani, hazina vyanzo vizuri vya mapato kutokana na hali halisi ya Mikoa yao. Nashauri…

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Makilagi kwa mchango mzuri. (Makofi)

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, mengine nitachangia kwa maandishi. (Makofi)