Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami nashukuru kupata muda wa kuchangia Wizara hizi mbili, kwanza kabisa nitaanza kuzungumzia TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya asilimia 60 ya fedha za elimu zinaenda katika Wizara hii ya TAMISEMI na hasa kwa ajili ya majengo na infrastructure zote za mambo yanayohusu elimu. Sisi sote tunafahamu TAMISEMI inashughulika na elimu ya msingi na sekondari na hapo ndiyo kwenye msingi hasa wa kutengeneza Taifa la kesho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ripoti ya CAG ya mwaka 2016/2017, inaonesha mapungufu yaliyopo katika Wizara ya TAMISEMI ambapo asilimia 85 ni madara, asilimia 52 ni upungufu wa madawati, asilimia 86 ni vyoo na mashimo na matundu lakini asilimia 88 ni kwa ajili ya mabweni. Tunapozungumzia infrastructure kwa ajili ya elimu ya watoto wetu wa msingi na sekondari, ni lazima kama Wizara ijipange upya na kujua kwamba watoto hawa ambao tunawatengeneza kuwa Taifa zuri la kesho tuwawekee mazingira mazuri ya kuweza kujisomea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa bajeti tunayopitisha sisi Wabunge, ndugu zetu wa TAMISEMI hawapati zote. Naomba Serikali wanavyokuja kujibu waniambie kwa nini bajeti haiendi yote maana tunapopanga bajeti sisi kama Wabunge, tunataka kusaidia jamii na hasa wananchi tunaowaongoza waweze kufikia malengo tuliyoyakusudia. Kwa hiyo, natoa ushauri kwa Wizara na Serikali pia, tunahitaji asilimia 25 zaidi ya bajeti iliyopangwa ili iweze kukidhi mahitaji yanayohitajika katika Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule za msingi zina upungufu, na hii natoa kwenye ripoti ya CAG ya mwaka 2016/ 2017. Katika shule za msingi kuna upungufu wa madarasa zaidi ya 85,000. Hii ni idadi kubwa sana kwa nchi yenye watu wengi kama Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2018, Serikali kupitia Waziri wa TAMISEMI, aliahidi kujenga madarasa mapya 10,140 lakini mpaka leo hakijafanyika chochote. Serikali inapoahidi na ilizungumzia kwamba itatoa zaidi ya shilingi bilioni 29 lakini mpaka leo hazijatolewa. Tunajua kweli tunanunua ndege na vitu vingine lakini usipowapa elimu watoto wako na tayari tuko kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki, ushindani wa ajira utakuwa mgumu sana miaka mitano au kumi ijayo. Ndiyo hapo tunakuja kusema lazima tuwe na mipango ya muda mrefu kwa ajli ya kusaidia kizazi chetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejaribu kuainisha vitu muhimu na vipaumbele kama Taifa tunavyotakiwa kuvifanya. Kwanza lazima bajeti iongezwe na mazingira ya kujisomea lazima yawe mazuri. Walimu ambao wao ndiyo wanaosimamia hawa watoto, muda mrefu hawajapandishwa madaraja, mishahara haijaongezwa, tusitegemee hawa watu watafanya kazi kwa bidii na kwa ubunifu. Sote tunafahamu mwalimu anayefundisha mtoto wa darasa la 1 mpaka 5, ni lazima awe mwalimu anayejitolea na kujituma na kufanya kazi kwa uaminifu ili kujenga msingi wa mtoto mdogo. Sisi Wabunge hapa wengi tunapeleka watoto wetu kwenye shule ambazo zinalipa vizuri labda ndiyo maana hatuoni uchungu kwa ajili ya watoto ambao wako chini na wanasoma bila kuwa na mpangilio mzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tuongeze ajira kwa walimu, uwiano wa watoto na walimu ni tofauti. Mwalimu mmoja shule standard watoto 30 - 35, naijua Shule ya Msingi Majimatitu ina watoto 200 mwalimu mmoja, hiyo siyo sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ni muhimu kuweka uwazi wa Wizara katika programu na mipango mbalimbali endelevu kwa ajili ya kusaidia watoto wetu. Tunaomba Wizara husika itafute wadau iweze kujifunza, pamoja na kukataa takwimu ambazo sisi Bunge tulikataa lakini bado tunahitaji wadau watupe hali halisi ya takwimu kule chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye elimu tulizungumzia habari ya kuondolewa kwa VAT katika taulo za kike Bunge lililopita. Hakuna utekelezaji uliofanyika wa kupunguza bei kwenye taulo za kike. Tunaiomba Wizara aidha, irudi nyuma tena, irudishe VAT lakini itamkwe kwamba tunatoa VAT kwa wale wanaopeleka taulo za kike kwenye shule za msingi na sekondari tu, vinginevyo tumewapa faida wafanyabiashara ambao wameendelea na lile punguzo la tozo ya VAT lakini wakati huo huo watoto wetu hawapati huo msaada wa taulo za kike. Tunaomba Serikali na hasa Wizara ya TAMISEMI isimamie suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie posho za Wenyeviti wa Serikali za Mitaa pamoja na Madiwani. Hawa watu ndiyo wanakaa na wananchi chini zaidi kuliko sisi Wabunge lakini posho zao, mpaka sasa kuna baadhi ya Halmashauri zimekopa, Madiwani hawajalipwa vikao mbalimbali, ikiwemo na viongozi wetu wa vitongoji na vijiji na Serikali za Mitaa. Tusitegemee ufanisi wa kazi kama hatuwezi kuwalipa, sisi Wabunge maslahi yetu tunayapigania na yanafanikiwa. Tunaomba pia Serikali muwatazame watu hawa muweze kuongeza posho na mishahara yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende kwenye suala la utawala bora. Tatizo la viongozi sisi Watanzania, tunafikiri tuonavyo sisi ndivyo ambavyo na watu wa kawaida wanaona. Watanzania wa leo siyo wa jana, watu wa Tanzania wanaona, tuna teknolojia, watu wanaangalia simu nchi nyingine wanafanyaje. Leo hii mkutano wa Chama cha Upinzani unazuiliwa, mita 15 kutoka kwenye huo ukumbi unaozuiwa watu wa CCM wanafanya mkutano, tusijenge chuki zisizokuwa na maana. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)