Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Njalu Daudi Silanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Itilima

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hotuba ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Utawala Bora. Nianze kuwapongeza sana Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya wakiongozwa na Waziri na Katibu Mkuu, pamoja na Wataalam wote kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa ushauri katika sehemu ya Watumishi wanaolipwa mapato ya ndani. Watumishi wanaolipwa mapato ya ndani wanafanya kazi kubwa katika Halmashauri zetu. Ni vyema wangechukuliwa nao sasa walipwe katika Mfuko wa Serikali Kuu ili waondokane na suala la kusubiria fedha za mapato ya ndani. Kazi kubwa wanafanya, ni vyema sasa nao hawa wakaingia katika utumishi kama wengine kwenye maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa shukrani kubwa sana katika Wizara ya TAMISEMI. Kazi wanayoifanya ni kubwa sana. Ni mfano tosha katika kitabu hiki ukikiangalia kwenye jalada hili, Kituo cha Afya cha Magu na maeneo mengine na kwangu Ikindilo na sehemu nyingine, shilingi milioni 500 nakumbuka katika enzi zilizopita ilikuwa ni suala la kufanya upembuzi yakinifu, hela inaisha; lakini leo fedha hizi zinafanya kazi ya kuonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepata shilingi bilioni 1.5 kwenye Halmashauri zetu 67. Ukizunguka katika maeneo hayo, utakuta zile shilingi bilioni 1.5 ujenzi unakaribia kwisha kwa majengo saba. Niseme tu ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, viongozi wetu kazi kubwa wanazozifanya, tuwatie moyo na tuwatie nguvu. Wanafanya kazi kubwa ya kunusuru maisha ya Watanzania, lakini nao hawalali kwa ajili ya kutufanyia kazi zetu nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la elimu. Serikali ya Awamu ya Tano, pamoja na mengi tunayoyazungumza, lakini kama ni kazi, viongozi wetu wanafanya kazi kubwa sana na nzuri sana. Ni suala la kufika mahali nasi kama viongozi, kama Wawakilishi wa wananchi, tuwatie moyo na pale kuliko na upungufu tuwaongezee maarifa wafanye kazi yao vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haijawahi kutokea, nakumbuka mimi nikiwa kule kijijini, shilingi milioni 50, shilingi milioni 40 ilikuwa darasa moja na haliishi. Leo shilingi milioni 15, madarasa katika kitabu hiki utaona yapo mfano hapa katika Wilaya yangu ya Gangabilili, ni mfano wa kuigwa. Leo tukiingia katika Bunge hili tunaona kama kazi hazifanyiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Vituo vya Afya na Zahanati, nashukuru na ninaipongeza Wizara kwa kusajili Vituo vya Afya vinne Ikunguilipu, Mwamwita, Maderana na Ndoleji; na kwa ujumla naiomba Serikali pale itakapokamilika watupatie Wauguzi katika Kada hii ili wananchi waweze kupata huduma katika maeneo husika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Waziri ya Mkuu kuna Wabunge walichangia, wanasema Idara ya Maji, haijafanya kazi. Mimi nataka nitoe ushuhuda katika Mkoa wetu wa Simiyu hususan katika Jimbo langu la Itilima. Tangu nchi iumbwe, Makao Makuu ya Lagangabilili tulikuwa hatuna maji. Leo Laganganilili, Nkoma, Kabale, Mwamungesha na Habia yamejengwa machujio ya kuweza kubeba takribani lita 200,000. Kusema ukweli Serikali hii inafanya kazi kubwa na lazima tuipongeze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilayani kwangu pale Itilima tulikuwa hatuna nyumba ya watumishi, jengo la utawala. Tulipata shilingi bilioni 1.5, leo jengo limekamilika na watu wanaendelea kufanya kazi. Naipongeza sana Wizara imenitengea shilingi milioni 900 kwa ajili kumalizia vitu vingine vilivyopo mle. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kunitengea shilingi milioni 500 kwa ajili ya kumalizia Hospitali ya Wilaya. Nami nimhakikishie mwezi wa Nane au wa Kumi njoo ufungue Hospitali ya Wilaya ianze kuwatumikie wananchi wa Itilima. Haya ndiyo matunda tunayohitaji ya Serikali ya Awamu ya Tano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba TARURA ituongezee bajeti yake. Wilaya yangu ya Itilima ina mtandao wa barabara wa kilometa 562, fedha iliyotengwa ni kidogo, lakini vilevile yako maeneo korofi ambayo hayawezi yakaendana na bajeti hii. Naomba Ofisi ya TAMISEMI pale ambapo wataalam wetu watakapoleta maandiko, basi watusaidie katika maeneo mawili muhimu sana. Tuna daraja la solo ambalo linaunganika na kwa Mheshimiwa Ndassa na daraja la Mwabuki. Tukiunganishiwa hayo, tutakuwa tumefanya kazi nzuri katika maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba Wizara ya TAMISEMI imefaa. Zamani walikuwa wanasema mzigo mzito mpe Mnyamwezi, kumbe na Wazaramo wanaweza. Mnachapa kazi vizuri na kazi inaonekana na mwenye macho haambiwi tazama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)