Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Hassan Elias Masala

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nachingwea

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kukushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Niungane na wenzangu waliochangia kwa kutoa pongezi kwa mawasilisho yaliyofanywa, lakini pia kwa upekee kabisa, nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Wasaidizi wake wote ambao wanamsaidia majukumu ya kutekeleza mambo mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha tunawatumikia Watanzania ambao wametupa ridhaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo bado pia naomba nichukue nafasi hii kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, takribani siku nne sasa amefanya ziara ndani ya maeneo ya Kanda ya Kusini. Wote mtakuwa mashahidi amefika Mkoa wa Mtwara na kwa muda mrefu sana, sisi wananchi tunaotoka katika ukanda huo tulikuwa na hamu kubwa sana ya kumwona Mheshimiwa Rais anakuja kule. Ujio wake kwetu umekwenda kutupa faraja kubwa sana, yako maelekezo mengi ambayo Mheshimiwa Rais ameyatoa kwa ajili ya kuhakikisha Watanzania wanapata zile huduma zote muhimu, lakini hapa kubwa ambalo ningependa nipongeze ni suala zima linalohusiana na korosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, korosho kwa Mikoa ya Lindi na Mtwara ni sehemu ya uchumi wetu, ni sehemu ya maisha, lakini ni sehemu ya changamoto ambazo kwa wakati fulani kidogo tulipitia. Hata hivyo, kupitia ziara aliyoifanya ameenda kutuachia faraja kubwa sana na mimi kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Nachingwea na kwa niaba ya wananchi ambao wanalima korosho tutakuwa watovu wa fadhila kama hatutathamini na kupongeza kile ambacho Mheshimiwa Rais amekielekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa sababu yeye ndiye msaidizi, tunaomba atufikishie salamu hizi kwa Mheshimiwa Rais na Watendaji wake wote wakiwemo Mawaziri wa Kilimo, ambao walichukua mawazo yetu na waliyafanyia kazi yale ambayo sisi tuliyashauri kwa niaba ya wananchi ambao wametupa nafasi ya kuwepo katika eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenye ukurasa wa 27 mpaka 30 kwa sehemu kubwa wamezungumzia suala zima linalohusu kilimo. Ningependa nizungumzie zaidi kwenye eneo la kilimo kwenye namna bora ambayo tutakwenda kujipanga wakati tunaelekea kwenye msimu ujao hasa katika zao hili la korosho, ambalo ndilo hasa linalotuletea uchumi na ndilo ambalo hasa linatuletea kipato kama nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto tulizozipitia sehemu kubwa ili tuweze kuzirekebisha yako mambo ambayo ningependa nishauri kupitia hotuba ambayo imetolewa. Jambo la kwanza ni suala zima la kuhakikisha wakati tunajiandaa na msimu mpya wa 2019/2020, tuone namna gani ambavyo tunaweza kwenda kusambaza pembejeo za kutosha hasa sulfur pamoja viuatilifu vingine ambavyo tumekuwa tunavitumia katika kufanya uzalishaji. Jambo hili na kupitia Serikali yetu, naamini iko dhamira ya dhati kabisa ambayo tayari imeshaonekana hasa katika msimu uliopita wa 2018/2019, lakini zipo changamoto ambazo tungependa awamu hii wakati tunajiandaa tungeona mabadiliko makubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mfumo uliotumika 2017/2018 wa kutoa pembejeo bure au karibu na bure au kuleta pembejeo ya ruzuku, ningependa kushauri watu wanaohusika ili waweze kuona namna sasa tunavyoweza kwenda kupata hizi pembejeo ili wakulima wetu waongeze uzalishaji katika zao hili la korosho ambalo kwa muda kidogo sasa ni kama hatufanyi vizuri sana kwenye uzalishaji. Kwa hiyo pendekezo langu kubwa ambalo ningependa kulitoa ni hilo kwa wale ambao wanahusika na zoezi hili la utoaji wa pembejeo na hasa ukizingatia katika hotuba hii suala la kilimo pia limegusiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado pia tunahitaji tuone maandalizi ya haraka sana, tuone namna ambavyo wadau wanaohusika na zao la korosho wanavyoweza kukutana na kuanza kufanya tathmini ya changamoto ambazo tumezipitia katika msimu. Ziko hoja za masoko, lakini pia ziko hoja zinazohusiana na namna bora ya kuendesha msimu kupitia Vyama vyetu vya Ushirika. Niwaombe watu wanaohusika waweze kupanga ratiba za haraka, lakini pia waweke katika kalenda za vikao tuweze kukutana mapema, tuweze kujadiliana yale yote ambayo mwaka huu yamejitokeza katika huu msimu, basi tuhakikishe msimu ujao wa 2019/2020, mambo haya machache ambayo yamejitokeza hayatojirudia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko suala kubwa ambalo limezungumzwa kwa muda mrefu sana kuhusiana na korosho suala zima la kangomba, kangomba ime-trend sana, imezungumzwa sana, lakini yako maelezo ambayo sisi tunashukuru kupitia hotuba aliyoitoa Mheshimiwa Waziri Mkuu na kupitia Bunge lako, tungependa sasa tushauri ili tuepukane na kangomba kwa kadri ya maelekezo yaliyotolewa. Yako mambo ya msingi ambayo yakifanyika tunaamini suala la kangomba msimu ujao, na maelekezo yaliyotolewa halitojirudia na kubwa ni hili la kupeleka pembejeo, kwa sababu sulfur zinavyokosekana hili limechochea wakulima wetu kuingia katika majaribu ya kuwapa wafanyabiashara korosho zao ili waweze kuhudumia mikorosho yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali ili kuliepuka hili na kuwaepushia wakulima adha walioipata safari hii, basi ni vizuri sana tukaona namna ya kutengeneza hayo mazingira wezeshi ya kupanga vikao, ya kupanga bei, lakini pia ya kutoa pembejeo kwa wakati na kwa gharama nafuu ambazo zitaepusha wakulima kukutana na wafanyabiashara au watu ambao hawana nia nzuri ya kuwasaidia wakulima ambao kwa muda mrefu wamekuwa wanapata changamoto katika uzalishaji wa zao hili la korosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaishukuru sana Serikali kwa namna na nia njema waliyoonesha katika kuendelea kufungua na kuboresha Viwanda vya Kubangua zao la Korosho. Juzi Mheshimiwa Rais akiwa Newala kule Tandahimba amezindua na kuona Kiwanda kile cha Iyuri, lakini bado tuna maeneo mengine ambako kuna Viwanda ambavyo vilikufa na tayari Serikali imeshaonesha nia ya kuvirejesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Nachingwea tunacho Kiwanda cha Mamlaka ya Korosho, bado Kiwanda kile kinacho uwezo mkubwa wa kuweza kuzalisha na tayari wapembuzi wameshafanya kazi ya kukikagua ili waweze kuona namna ya kukirejesha, lakini bado Mtama kuna Kiwanda na Lindi Mjini bado kiko Kiwanda ambavyo hivi vyote vikitengenezewa mazingira mazuri azma ya kubangua korosho ndani ya maeneo yetu itakuwa ni kubwa na hivyo tutaenda kuongeza thamani ya zao la korosho na pia tutaenda kuongeza ajira kwa vijana wetu na kuboresha mfumo mzima wa upatikanaji wa korosho katika mazingira yetu. Kwa hiyo, haya niliona niyazungumze kama sehemu ya mapendekezo ambayo ningependa Serikali iyachukue.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nataka nizungumzie ni suala zima la zao la mbaazi, bado wakulima wetu sisi ni wazalishaji wakubwa wa zao la mbaazi. Hapa tunapozungumza tuko kwenye msimu wa maandalizi, naomba kupitia Wizara ya Kilimo, ambayo iko chini ya Ofisi pia ya Waziri Mkuu na kwenye hotuba imezungumziwa, waone namna wanavyojipanga katika kuhakikisha hatuyumbi tena katika upatikanaji wa masoko hasa wa zao hili ambalo kwetu sisi ni muhimu sana na linazalishwa kwa wingi sana. Miaka mitatu iliyopita zao la mbaazi hatujafanya vizuri, kwa hiyo naamini wakati tunaelekea kwenye kuhitimisha hizi bajeti basi, tutapata maelekezo mazuri ya namna ambavyo tunajiandaa kwenda kununua zao la mbaazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, naomba nizungumzie suala zima la miundombinu, Jimbo la Nachingwea, Jimbo la Liwale, Jimbo la Masasi kwa sehemu kubwa ndiyo wazalishaji lakini pia miundombinu yake sio rafiki sana. Naipongeza Serikali kwa sababu imeonesha nia ya dhati ya kujenga barabara ya lami kutoka Masasi kwenda Nachingwea, Nachingwea kwenda Ruangwa, Ruangwa kwenda Nanganga na tayari utaratibu wa kuitangaza hii barabara kwa ajili ya kupata mkandarasi ulishafanyika. Hata hivyo, mpaka sasa hivi ninavyozungumza bado sijaona taratibu zozote ambazo zinaendelea, kwa hiyo wakati tunaendelea kutaka kupitisha bajeti hii, niwaombe sana watu wanaohusika watoe maelekezo ya kina ya namna ambavyo wamejipanga kuanza ujenzi wa barabara hii ambayo ina kilomita karibu mia moja…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Masala.

MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)