Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Dr. Raphael Masunga Chegeni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busega

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niungane na wenzangu wote ambao wameweza kutoa pongezi na hasa katika Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuandaa bajeti hii vizuri na naomba tumpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu. Nina sababu kuu mbili za kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu; katika Mawaziri Wakuu ambao wameshapita katika nchi hii, huyu namwona Waziri Mkuu wa kipekee kwa sababu kwanza anazunguka, kuifahamu nchi na kuwatumikia Watanzania vizuri zaidi, lakini pia anafuatilia vizuri sana utekelezaji wa miradi ya Serikali na shughuli za Serikali kwa ujumla. Tunatakiwa tumpongeze kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa huyu ndio kiongozi wa shughuli za Serikali hapa Bungeni, niunge mkono vilevile, kwamba hotuba yake hii ya bajeti ya bilioni mia moja na arobaini na nane tumpatie bila hata kupunguza hata shilingi moja, kwa sababu anahitaji hizi fedha ili kwatumikia Watanzania. Serikali ya Awamu ya Tano imejipambanua kwa mambo mengi sana, wanasema mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu, hivi ni wapi ambapo leo hii katika nchi hii hutaona shughuli zinaendelea? Iwe za miundombinu, za maji, za elimu, za afya na kadha wa kadha. Hii imesaidia sasa kuwafungua Watanzania na ndiyo maana kuna siku hapa Mheshimiwa Mbunge Profesa Tibaijuka alisema kwamba, unapopanua huduma ndiyo watu wanahitaji zaidi. Kwa hiyo, Watanzania sasa tunahitaji zaidi maendeleo, kwa sababu tumeanza kuona maendeleo yanakuja. Awamu zote zilifanya kazi vizuri sana, lakini Awamu ya Tano kwa muda wa miaka mine, nadhani kila mmoja anaona na kama anaona, basi kuna kila sababu ya kupongeza shughuli za zinazofanywa na Serikali yetu ya Awamu ya Tano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia katika miradi mingi kwa mfano ya miundombinu, tumeona barabara nyingi zinajengwa, miradi ya umeme tumeona, mradi wa REA sasa hivi katika nchi hii, tunalalamika kwamba baadhi ya vijiji havijafikiwa, lakini karibu kila kijiji miradi hii imeshaanza kutekelezwa. Hii ni hatua moja muhimu sana na naomba tupongeze sana kwamba Serikali inafanya kazi yake vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika yote haya nataka niseme kwamba tunahitaji kuifungua nchi vizuri tuwe na priorities za kimkakati ili tuweze kuendelea tunahitaji kufungua nchi vizuri zaidi, maeneo ambayo ni ya kimkakati tuyaendeleze zaidi. Mheshimiwa Rais alikuwa kule Mtwara, amezungumza vizuri sana namna ya kufungua korido ya Kusini; kuna korido ya Mbeya, uwanja wa ndege wa Songwe, naomba sana sana hicho ni kitega uchumi cha muhimu sana katika nchi yetu hii. Kwa hiyo, lazima ukamilishwe kwa wakati na uweze kutoa huduma, uwanja wa ndege wa Mwanza ukamilishwe vizuri ili uweze kutoa huduma vizuri zaidi, kwa sababu umechukua sehemu kubwa ya mahitaji na watu ambao wanahitaji kuutumia na kwa kiuchumi uko kimkakati zaidi. Pia uwanja wa ndege wa Mtwara na viwanja vingine ambavyo vimetajwa ikiwepo Simiyu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itasaidia sana kufungua nchi yetu, lakini tukiangalia Serikali hii ya Awamu ya Tano tumeweza kuwapata wawekezaji wa umma na wa sekta binafsi, uwekezaji wa umma hadi sasa hivi Serikali imewekeza zaidi ya trilioni 54.8 na mwaka jana kwa mara ya kwanza tumepata gawio la shilingi bilioni 830. Tunapaswa tupongeze sana Serikali hii kwa sababu kuna baadhi ya makampuni na mashirika yalikuwa hayawezi kutoa gawio kwa Serikali, lakini yameweza kutambua umuhimu huu, sasa yanachangia kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Hii ni jitihada muhimu sana kwa Serikali yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto ambazo zipo na Waheshimiwa Wabunge nadhani wamezungumza na wengine pia tuzungumze, kuhusu ukamilishaji wa miradi, najua kuna vipaumbele vingi lakini vile vile tunapoanzisha miradi tuikamilishe. Kwa mfano, majengo ya halmashauri hizi mpya za wilaya, kwa mfano Wilaya yangu ya Busega tumejenga jengo huu ni mwaka wa nne halijakamilika. Ukiangalia gharama zinaongezeka. Kwa hiyo ningeomba kwamba Serikali iweke utaratibu majengo ambayo kwa wilaya ambazo hazijawahi kujengewa majengo mapya basi zijengewe majengo hayo yakamilike ndani ya muda ili kusudi tuepuke kuongezeka kwa gharama za ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maboma ya Zahanati, Waheshimiwa Wabunge wamezungumza hapa na madarasa, wananchi wamechangia nguvu ningeomba sana Serikali kupitia bajeti hii tuelekeze nguvu zetu kuhakikisha maboma haya ya zahanati pamoja na maboma ya madarasa yanakamilishwa ili kusudi tupange kingine zaidi. Mnapoanza kitu msipokamilisha mnaanza kingine, inakuwa ni tatizo kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ya maji; mimi na wewe nadhani tupongeze sana Serikali hii kwa sababu tuna mradi mkubwa sana wa maji kutoka Ziwa Victoria. Chanzo cha maji kinaanzia pale Busega, mradi huu ni wa kitaifa na utahudumia vijiji vingi na mikoa mbalimbali. Naomba miradi huu utekelezwe kwa wakati, kwa sababu mradi huu fedha zake zinatoka kwenye Climate Fund, basi ukamilishwe kwa wakati. Naomba taratibu zote za ujenzi zifanyike na uweze kukamilika

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika miradi ambayo bado najiuliza sana ni TARURA. TARURA Waheshimiwa Wabunge nadhani mtaniunga mkono, wanahitaji kusimamiwa vizuri. TARURA tumewapa majukumu lakini hata na Halmashauri hawako pamoja, hawaingii kwenye vikao inavyotakiwa. Pili, wanafanya miradi hata Madiwani hawajui miradi inavyotekelezwa. Naomba sana kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, suala la TARURA liangaliwe vizuri zaidi ili kusudi liweze kuwa na tija katika kutekeleza miradi yetu ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunahitaji maisha bora, tunayapataje, ni lazima tuwekeze na sekta binafsi lazima iangaliwe. Nashukuru sana Mheshimiwa Rais ameunda Wizara ya Uwekezaji na wamepata Waziri mahiri, naamini Waziri huyu akipewa ushirikiano atafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi tumeona wawekezaji wengi wanakuja hapa Tanzania halafu wanaondoka bila kuwekeza kwa sababu ya ukiritimba. Pia bado kuna vitu ambavyo vinakinzana kati ya vitu ambavyo vinampa mwekezaji incentives au vivutio vya uwekezaji ambavyo ukienda TRA kwa Mamlaka ya Kodi vinakuwa vinakinzana, matokeo yake mwekezaji anasumbuliwa. Bado kuna vitu vingine ambavyo vinafanya mwekezaji ili aweze kuwekeza vizuri anapata shida sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la vibali vya ufanyaji kazi. Mheshimiwa Jenista Mhagama analifahamu hili, tunaomba sana kuwe na coordination nzuri. Kwa sababu huyu Waziri wa Uwekezaji kama Waziri ameshaomba vibali vya wawekezaji lazima mshirikiane, msomane vizuri zaidi kwa sababu tuta-frustrate wawekezaji ambao ni genuine kwa sababu ya vibali, kumbe masikini hamjapata taarifa sahihi tu. Huyu atajitahidi kutafuta wawekezaji wanakuja hapa nchini, anaongea nao vizuri zaidi, ana wa-assure kwamba Serikali itawapa kila aina ya msaada inapokuja suala la vibali, kunatokea sintofahamu ya hapa na pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kama nchi tusafiri pamoja, kama Serikali msafiri pamoja ili kusudi tusi-frustrate wawekezaji. Ukishampoteza mmoja umepoteza karibu 100. Hii kwetu sisi inatu-cost sasa hivi, unakwenda kwenye nchi ambayo haina chochote wala lolote wanasema eti uwekezaji ni mzuri zaidi kuliko kwetu sisi. Naomba tuondokane na dhana hii na naomba sana Mheshimiwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)