Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Grace Victor Tendega

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kupata nafasi ya kuchangia katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kumpongeza Mwenyekiti wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe kwa kazi kubwa yenye changamoto anayoifanya na sisi tuko nyuma yake tutaendelea kufanya kazi naye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanzia katika sehemu ya lishe, nazungumzia suala la udumavu. Tanzania ni nchi ya tatu Afrika inayoongoza kwa udumavu na ni nchi ya kumi duniani inayoongoza kwa udumavu wa kiakili na kimwili na vilevile zaidi ya asilimia 42 ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano wana udumavu wa kiakili na kimwili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini ninazungumzia hili? Ninazungumzia hili kwa sababu tunataka tujenge Taifa lenye watu ambao hawana udumavu, tunataka tujenge Taifa ambalo watu wake watakuwa na maamuzi sahihi, tunataka tujenge Taifa ambalo tutaendeleza kizazi na kizazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahatma Gandhi alisema; “Ishi kama utakufa kesho na fikiri kama utaishi milele.” Hii ina maana gani? Tunayoyatenga hapa katika bajeti yetu, tunayoyapitisha katika bajeti yetu, basi yaende yakafanye kazi kubwa ya kuweza kuendeleza vizazi na vizazi na siyo ya kuangalia miaka mitano mitano, tuangalie nini mwisho wa kizazi cha Tanzania hii? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, udumavu huu ninaozungumza unaendana na changamoto nyingi za kukosa elimu hasa kwa hawa watu walioko vijijini na hata wa mijini. Utaona hata sisi wenyewe Waheshimiwa Wabunge tupo tunavyoenda kula pale canteen tunakosa kujua ni vipi tule vitakavyokuwa na uimara katika miili yetu na katika afya zetu. Sasa je, wale walioko vijijini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia bajeti inayotengwa, kwa mfano, Sekta ya Maendeleo ya Jamii ambao ndio wanaotakiwa kuelimisha watu katika maeneo ya vijijini, hawaajiriwi. Wanatakiwa waajiriwe Maafisa Maendeleo ya Jamii 4,000 sasa hivi wako 1,700, tuna upungufu wa takribani Maafisa Maendeleo ya Jamii asilimia 57.5. Sasa hii kuonesha kwamba tutaendelea kuwa na kizazi chenye matatizo ya udumavu. Mikoa mingi ambayo ina udumavu wa kimwili na kiakili ni watu ambao pia wana vyakula, ni mikoa ambayo inazalisha chakula, lakini wanakosa upangaji mzuri wa vyakula. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maziwa yamekuwa ni anasa katika familia zetu, mayai ni anasa katika familia zetu, mtu anaweza akawa na maziwa hanywi maziwa. Wenzetu nchi ya Kenya wanapanga kabisa mtu yeyote lazima anywe lita kadhaa kwa wiki. Sisi Serikali yetu mmejipangaje kuhakikisha hawa wananchi wanapata hiyo elimu? (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli itakuwa ni vigumu sana kwa Serikali yetu hii kufikia malengo tunayohitaji ya milenia yale tunayosema kama hatuwekezi mkakati mzuri wa kutokomeza hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakwenda katika suala lingine, kuna ahadi ya Waziri wa TAMISEMI ambayo aliitoa mwezi Juni, 2018 wakati wa matokeo ya Kidato cha Tano yalivyokuwa yanatoka. Alisema atapeleka shilingi bilioni 29 kujenga madarasa 478 na mabweni 269 kwa watoto waliofaulu kwa Kidato cha Tano. Napenda kujua, wamefikia wapi katika utekelezaji? Tuambiwe tujue wamefikia wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya mabweni mnaiona, watoto wa kike, walemavu na wengine wote, mnawaona. Nimekwenda kwenye shule moja unakuta walemavu wanapata changamoto, hakuna uzio kwenye hizo shule, kwa sababu kuna elimu jumuishi. Wale watoto kuna wengine ni Albino, wanataka kuibiwa, Serikali mnajipangaje kuhakikisha hiyo elimu jumuishi, hawa watoto wanasoma na wenzao, hawawezi kuibiwa? Hilo ninaomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kufanya majumuisho ni vizuri wakatuambia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni taulo za kike. Mwaka 2018 Mheshimiwa Waziri wa Fedha hapa alitutamkia na tukafurahi kwamba wanafunzi wa kike taulo zitaondolewa VAT. Imekuwa ni changamoto, hatujauona mkakati mzuri unawekwa watu wakajua ni zipi ambazo mmeamua zipi salama, zipi siyo salama na wapi na kiasi gani? Hakuna utaratibu unaojilikana. Kama inashindikana, basi tupelekwe kwenye capitation grants ili tujue kwamba kule watapata shuleni, maana hilo ndiyo lilikuwa lengo kubwa la TWPG na wote ambao tulikuwa tunashiriki katika hilo. Tunaomba ufafanuzi wa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni hili la vitambulisho vya ujasiriamali. Napenda kuuliza, hivi mlifanya utafiti kwamba hawa wajasiriamali shida yao kubwa ni vitambulisho? Mlifanya utafiti kweli! Kwa sababu akina mama na vijana wanaofanya biashara ndogo ndogo, amebeba ungo ameweka maembe, ameweka mchicha na kila kitu, anatakiwa atozwe hicho kitambulisho atoe shilingi 20,000/=. Sasa mnasema hivi, mliahidi shilingi milioni 50 kila kijiji. Hizo shilingi milioni 50 ziko wapi? Hamjapeleka, leo mnakuja na vitambulisho. Huyu mama anaishia kukimbia. Anavyofanya vile, anataka ajikimu kimaisha, akauze mchicha ili akalishe watoto, akauze mchicha ili aweze kusomesha watoto. Ninyi mnakwenda kuwadai hao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kupata kauli ya Serikali, mlifanya utafiti? Utafiti ulisema wapate vitambulisho? Kama siyo, utekelezaji huo, ni kweli? Kama ni kweli unafanyika hivyo, ndivyo mlivyodhamiria kuwakomboa hao wananchi wanyonge kama mnavyojinasibu? Hao wananchi wanyonge kweli watakomboka hapo? Maana tunakwenda tunaona wanazidi kudidimia kwa umasikini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nasema udumavu ni tatizo, tukiwa watatu Afrika ni shida, tunapaswa tufikiri zaidi, tuone kwamba ni biashara gani, ni mambo gani ya muhimu ambayo tunatakiwa tuyafanye kuleta maslahi mapana ya Serikali, lakini siyo kwenda kukamata hawa wajasiriamali wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la uwekezaji. Mnazungumzia uwekezaji lakini changamoto kubwa ya uwekezaji katika nchi hii, mazingira ni magumu mno na ni mabovu mno na yanasababisha watu kushindwa kufanya biashara na kuwekeza katika nchi. Kumekuwa na kauli za viongozi za kukatisha tama. Wawekezaji wengine wanaonekana ni kama wanakuja kuchukua mali na kila kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri lazima aangalie hili. Wawekezaji ndio watakaosaidia Sekta ya Ajira ipatikane. Kama mtawawekea mlolongo mkubwa wa kodi, mtawawekea mazingira magumu ya kuweza kufanya kazi zao… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)