Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Livingstone Joseph Lusinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtera

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru sana Mungu kwa kunipa nafasi ya kuchangia leo katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kunipa afya na kutuwezesha sisi Wabunge kuweza kukutana mahali hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wengi wamempongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu na watendaji wote wanaofanya kazi kwenye ofisi yake na mimi nichukue fursa hii kukubaliana nao. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anazozifanya za kiutendaji lakini tumeona yeye na watendaji wake wakuu wote wakitembea na kuzunguka taifa zima ili kuchagiza maendeleo kwenye nchi yetu, tunasema hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shukrani za pekee zimuendee Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya kuiongoza Serikali hii ya Awamu ya Tano ambayo imejielekeza kabisa kwenye kuondoa changamoto zilizokuwa zikiwakabili wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi punde kuna Mbunge ametoka kuchangia hapa akiisifu Serikali ya Awamu ya Nne kwa kazi kubwa ilizofanya. Nina hakika Wabunge wengine watakuja kuisifu Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi nzuri inazofanya kwa sababu siyo wote tutaona mara moja, wengine wataona baadaye. Kwa hiyo, nina uhakika hata haya yanayofanyika sasa hivi baadaye watakuja kuyaona na kuyapongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nisimame kama shuhuda kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Mtera kuishukuru Serikali ya Awamu ya Tano imefanya kazi kubwa kutuletea pesa kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Mpwayungu. Wametuletea Sh.1,500,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya pale Mlowa Barabarani njia ya kwenda Iringa. Vilevile upande wa maji wamefanya kazi kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona Prof. Kitilya Mkumbo akitembea hata yeye kuangalia miradi kadhaa ya maji na kuikamilisha pamoja na Waziri na Naibu Waziri wamefanya kazi kubwa sana kuhakikisha Watanzania wanaondokana na dhiki ya maji. Kwa hiyo, mimi kama Mbunge ninayeongoza wananchi ambao wamechanganyika maskini wengi kuliko pengine matajiri, nachukua fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayofanya kuhakikisha kwamba nchi yetu inapata maendeleo makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuendelee kuomba mjielekeze zaidi kwenye kumaliza miradi ya maji ambayo haijakamilika. Vilevile kuanzisha visima vipya na kuna maeneo mengine visima vya zamani vimekauka tuweze kuvifufua ili akina mama wasipate adha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo niliamua wakati napewa nafasi hii kwamba nataka kusema na Waheshimiwa Wabunge wote kwa ujumla. Tumekuwa tukipokea misaada mingi sana, mingine kutoka nje lakini sisi wenyewe pengine Bunge hili lilishawahi lenyewe kujinyima fursa halafu likachukua pesa zake za Bunge tukaenda kununua madawati. Napongeza sana Bunge kwa uamuzi ule ambao tulijinyima tukasema tuchukue hizi pesa twende tukanunue madawati ya watoto wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema maneno haya? Nasema maneno haya kwa sababu tumepata misaada mingi sana ya kusaidia jamii yetu lakini sasa naomba Taifa hili hebu na sisi tujinyime jambo moja ili tuweze kutoa msaada mkubwa sana kwa nchi yetu. Jambo lenyewe ni hili, ukisoma kwenye ukurasa wa 7 utaona kuna mafanikio lakini ukienda kwenye hotuba ya Waziri Mkuu ukurasa wa 17 kuna habari za Tume ya Taifa ya Uchaguzi inategemea kuongeza vituo 858, hivi vituo vinavyoongezeka bado tunaongeza gharama kubwa kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini nachotaka kushauri? Tumeona uchaguzi mwingine tunaoufanya na wenzetu wamelalamika sana kwamba wakati mwingine tunaingia gharama kubwa bila sababu, naomba Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote hivi kwa nini mwakani tusifanye uchaguzi wa Diwani na Mbunge tu Rais tukaacha apite bila kupingwa? Kwa nini tusifanye hivyo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tutakuwa tumeokoa fedha nyingi wakati Rais anaapishwa tumkabidhi cheque ambayo Taifa hili limeokoa ili Rais aende akatumie hizo fedha kuondoa matatizo ya maji na barabara vijijini. Kuna faida gani kwenda kupoteza pesa chungu zima kwa uchaguzi wa Rais, Rais ambaye hana mpinzani? Hii ni kwa sababu tumeona hata mshindi wa pili aliyepata kura 6,000 ameunganishwa na 8,000. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ndugu zangu nataka niwashauri, naomba mitandao yote na wanazuoni wote hoja hii naiweka mezani tuangalie faida ambayo tunaipata na hasara zake tupime. Jamani sisi ni Wabunge tuliotokana na familia maskini, tusijisahau tunaongoza watu maskini; watu maskini wakati mwingine huwa wanajadili katika milo mitatu ambayo ni haki yake anaamua kukata milo miwili anakula mlo mmoja, sisi kwa nini tusile mlo mmoja? Tule mlo wa Udiwani na Ubunge, kwenye Urais tumuache Mzee Magufuli apite bila kupingwa. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi aliyoifanya Rais ni kubwa, Taifa hili sasa na lenyewe lijinyime kwenye upande huo badala ya kupoteza pesa bila faida tumkabidhi Mheshimiwa Rais pesa ambazo zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya uchaguzi wake tumwambie Rais kamata cheque hii ondoa shida ya maji kwa Watanzania. Mshindi namba mbili Ulipo Tupo tayari tayari yupo kule kule na Walipo Tupo wamemfuata huko huko, hivi kweli kuna chama nchi hii kinaweza kutengeneza mgombea Urais kwa miezi tisa (9) akamshinda Magufuli jamani? Ukweli tuuseme, haiwezekani! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, badala ya kupoteza muda mimi nawakaribisha tuje tushindane kwenye Ubunge na Udiwani, kwenye nafasi ya Urais tumpe heshima huyu mtu amefanya kazi kubwa. Ameonyesha kwamba yupo tayari kuondoa changamoto za Watanzania, kusimamia pesa za Watanzania na kuhakikisha mambo yanakwenda.

WABUNGE FULANI: Katiba.

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Hiyo Katiba ni ya kwetu sasa tuangalie faida ya Katiba na umaskini wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua kuna Wabunge wengine humu wanapiga kelele Katiba, kwa sababu Majimbo wanayoongoza hayana watu maskini lakini sisi ambao tunaongoza watu maskini ukiwauliza, ndiyo maana nimesema tujadiliane, naomba tujadiliane hasara na faida ya kufanya huo uchaguzi kwa sababu kwa vyovyote vile hakuna mtu atakayeweza kusimama 2020. Mimi naweka wosia kwenye Bunge hili siyo tu akamshinda, akamtikisa Mzee Magufuli, hayupo! (Makofi)

(Hapa baadhi ya Waheshimiwa Wabunge waliongea bila utaratibu)

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa sababu hiyo hatuna sababu ya kutumia mabilioni ya pesa kwenda kupoteza muda na kitu ambacho tuna uhakika. Katiba ni yetu, matatizo na changamoto ni zetu, tupime kama Watanzania. Ndiyo maana nimesema naruhusu mjadala huu na naomba Wabunge mtulie nasema makubwa sana hapa, mnaweza mkapata matatizo wengine hapa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza na nchi, tuangalie kwa namna nchi yetu ilivyo, ufadhili tunaopokea, na sisi tutoe ufadhili kwa nchi yetu. Tutakumbukwa kwa kitendo hicho kuliko kwenda kupoteza pesa bila sababu yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri Mkuu lakini nilikuwa nataka kuweka hoja hii mezani Watanzania waijadili waone faida na hasara zake halafu waamue kuniunga mkono au wasiunge mkono. Naunga mkono hoja hii asilimia mia. (Makofi)