Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Sonia Jumaa Magogo

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. SONIA J. MAGOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia. Awali ya yote ningependa kuupongeza uongozi mzima wa Chama changu cha Wananchi (CUF) ukiongozwa na Mwenyekiti wetu mahiri kabisa, Profesa Ibrahim Haruna Lipumba kwa kuaminiwa na Wanachama wote na kupewa tena ridhaa ya kukiongoza chama chetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niende moja kwa moja kuchangia kwenye hoja na nitaanza na suala la uwekezaji. Katika kuwekeza, Serikali pia inawekeza kwenye Mashirika ya Umma ambayo yapo nchini kwetu na inaweka mtaji wake kwa lengo la kupata gawiwo ambalo litakuja kuisaidia Serikali katika shughuli zake mbalimbali za kuinua uchumi pamoja na huduma mbalimbali za jamii na tumeona mwaka jana baadhi ya Mashirika haya yametoa gawio zuri kwa Serikali. Ndhani kama Ofisi ya Msajili wa Hazina ambayo ndio msimamizi mkuu wa mashirika haya, ikiwezeshwa vizuri na kupewa bajeti ya kutosha na kwa wakati ikayasimamia zaidi haya mashirika gawio hili litaongezeka maradufu ya lile ambalo tulipata mwaka jana.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ningependa kuongelea kuhusu wazee waliokuwa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Wazee hawa waliitumikia nchi yetu kwa uaminifu, walisaidia kuleta mahusiano mazuri baina ya nchi yetu na waliokuwa Washirika wetu wa Afrika Mashariki, lakini bado wazee hawa wanahangaika kila kukicha na madai ambayo bado hayajapata suluhu mpaka leo. Kumekuwa kuna kesi mbalimbali wanaendesha, kwa hiyo, inabidi wakati mwingine watoe michango kwa ajili ya zile kesi, wakati mwingine inabidi wasafiri kutoka sehemu mbalimbali kuja Dar es Salaam kwa ajili ya mikutano yao ya kukutana kufuatilia madai na ukizingatia wazee hawa hali yao ya kiuchumi siyo nzuri. Kwa hiyo napenda kuishauri Serikali katika suala hili watoe tamko rasmi kwa hawa Wazee. Kama kuna chochote ambacho wanadai basi Serikali iwalipe ili waweze kupumzika na kama hakuna madai vilevile lingetoka tamko ili wakajua ni nini ukweli wa haya madai ambayo wanafuatilia kila siku.

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine bado nipo kwa Wazee na nazungumzia suala la pensheni wanayopata kila mwezi. Kwa kweli pension wanayopata kila mwezi baadhi ya Wazee ni ndogo. Kumlipa Mzee pension ya chini ya kiwango cha laki moja kwa mwezi ni kama unamwonea. Tukilinganisha hali ya maisha tuliyonayo kwa sasa na kile kiwango wanachopata, wazee wale wana familia, wazee wale wanatunza wajukuu lakini kile kiwango wanacholipwa kwa ajili ya kuendesha maisha yao ni kidogo sana. Hivyo naiomba Serikali iangalie inawasaidiaje ili kuongeza hiki kiwango cha pensheni ya kila mwezi hawa wazee waweze kujikwamua na umasikini ambao wanao.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi nikizingatia wazee hawa pia hawana mfuko maalum kama walivyo vijana, walemavu, wanawake ambao wanapata asilimia 10 kwenye Halmashauri zao, lakini kwa upande wa Wazee wao hawamo katika hii asilimia 10. Kwa mujibu wetu ni kwamba vijana wanaishia miaka 45. Kwa hiyo, kuanzia miaka 46 tunasema tunawachukulia kwamba wapo kwenye kundi la Wazee, lakini bado ni watu ambao wana nguvu, wanaweza kuitumikia nchi yetu, wanaweza kujenga uchumi. Kwa hiyo, wakiwezeshwa na Serikali kama wanavyowezeshwa vijana, akinamama na walemavu nao wataweza kuchangia kwenye uchumi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni vijana; mara nyingi tumekuwa tukiwalaumu vijana kwamba wana akili mgando ya kutaka kuajiriwa hawataki kujiajiri. Hata hivyo, hili mimi nalitazama kwa mtazamo mwingine kwamba, je, hawa vijana tunawaandaa vipi ili waje kujiajiri? System yetu ikoje kuanzia shule ya msingi, sekondari hata vyuoni, wanaandaliwa vipi ili baadaye wanapomaliza elimu yao waje kujiajiri na kuondokana na lile wimbi la kuwaza kwamba nitaajiriwa, nitaajiriwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, hapo hapo kuna wale ambao wana mawazo yale ya kujiajiri lakini mazingira yenyewe ya kujiajiri yanakuwa ni magumu. Mlolongo wa kuanzisha mathalan biashara au sehemu yake ya kazi unakuwa ni mrefu sana au unakuwa na gharama ambazo yule kijana anashindwa kuzikidhi na kuweza kufungua biashara yake na kujiajiri. Pia wakati huo huo tuna mapori mengi sana katika Tanzania yetu. Ingewezekana Serikali kuwakusanya wale vijana kwenye makundi, kuwapatia zana za kilimo ama kwa kuwakopesha au kuwasaidia wakaweza kuanzisha kilimo na kuweza kuendeleza uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kwenye ndugu zetu walemavu; kumekuwa na kesi mbalimbali za walemavu na wengine wanasababishiwa ulemavu huo na watu ambao ni wageni katika nchi yetu, labda wawekezaji ama watu mbalimbali. Hata hivyo, zinapokwenda zile kesi za hawa ndugu zetu walemavu na ukiangalia na mazingira ambayo wanakuwa tayari wanayo zile kesi zinachukua milolongo mingi sana, zinakuwa na ucheleweshwaji ndani yake hivyo kuwasababishia kuwa na maisha magumu zaidi. Hivyo, ningependa pia Serikali iwasaidie hawa ndugu zetu kwa kuwasimamia kwenye kesi zao na kuwahakikisha ufumbuzi unapatikana haraka kwenye hizo kesi ili waweze kuendelea na harakati za maisha yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.