Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Jaku Hashim Ayoub

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

House of Representatives

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante sana kwa kuniruhusu kuchangia bajeti hii muhimu ya Waziri Mkuu. Kabla sijaanza kuchangia kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu aliyenipa nguvu za kuweza kusimama hapa na kuchangia, uwezo huu si wangu, wala maarifa yangu, wala nguvu zangu, ni neema zake yeye Mwenyezi Mungu. Ndio pale aliposema katika kitabu chake kitukufu “Wakhulka l-insaanu dhwaif” maana yake tumemuumba mwanadamu kuwa ni dhaifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kwa dhati kumshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na timu yake kwa umakini wa hali ya juu kwa kutuletea ripoti hii. Namjua Mheshimiwa Waziri Mkuu umakini wake, lakini mchango wangu utalenga katika sehemu tatu: Kwanza sehemu ya Muungano; pili, sehemu ya Bunge; na tatu, TRA. Nitajikita zaidi kwenye Muungano ukurasa wa 81 ambapo tunakaribia kutimia miaka 55 ya Muungano wetu huu ambao ni mfano kwa dunia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Muungano wetu huu ni matokeo ya mahusiano kihistoria kwa pande zote mbili, kwa hiyo hatuna budi kuheshimu na kulinda ili kuendeleza kudumu kwa faida ya watu wetu. Katika kuimarisha Muungano wetu Serikali zote mbili zinaendelea kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazoukabili. Tarehe 21 Januari, 2019 kilifanyika kikao cha Baraza la Mawaziri kilichohusu utozwaji wa kodi wa thamani (VAT) cha 0%. Hili jambo niendeleee kulishukuru tena kwa mara ya pili ndani ya chombo hiki na huu ndio Muungano, sio upande mmoja. Limepata suluhu na kiana yake niendelee kumshukuru sana Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa aliyofanya pamoja na Mawaziri

Mheshimiwa Naibu Spika, sitawafanyia haki Mheshimiwa January Makamba na Naibu Waziri wake katika sekta hii ya Muungano, Mheshimiwa Mussa Sima kama sitawapongeza kwa jitihada walizozifanya. Hata hivyo, kuna baadhi ya hizi kero za muda mrefu za 4.5%, kwanza naishukuru Benki Kuu kwanza hapa Waziri wa Fedha naomba a-take note hapa kidogo kwa faida ya wananchi wa Zanzibar; 4.53 toka dunia ilipoanza mpaka muda na mwanzo ilipokubaliana IMF, formula hii ni ya muda, sasa Zanzibar imekua, watu wameongezeka, mahitaji ya barabara yamekuwa makubwa, hii muingalie tena upya na hii ilikuwa ya muda 4.5. Zanzibar ishakuwa kubwa kupita kiasi kwa muda huu, ifike mahali walitatue tatizo hili, ni la muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, ajira katika sekta ya Muungano, upande wa Jeshi, upande wa Mambo ya Ndani, Migration, Polisi na Mambo ya Nje wanawashirikisha Zanzibar lakini waangalie formula nyingine, sasa hivi ajira imekuwa ngumu, pamoja na kuwa Tanzania bara ni kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine la kusikitisha, formula iliyokuwepo zamani Marais wengi wamekuwa wakitumia, viongozi waliokuwa wakifika Tanzania Bara walikuwa wakifika Zanzabar, sasa hivi hatuwaoni. Hili niliombe, viongozi sitaki kuwataja, ni wengi wamefika Tanzania Bara, viongozi mashuhuri, lakini wengine hawafiki Zanzibar. Hili halileti picha nzuri, hili naomba sana ifike mahali viongozi wanaofika huku wawapeleke Zanzibar.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuhusu bidhaa za Zanzibar kuingia katika soko hili la Tanzania bara, hiki ni kilio cha muda mrefu sana na wengine wameanza kufunga biashara zao. Itafutwe formula, maziwa hayafiki huku, sukari ipo Tanzania Bara, huku hailetwi, tunalinda viwanda vya Tanzania, sio vya Tanzania Bara. Tanzania ikiwepo Zanzibar, tuwe wakweli, tutafute formula itakayoweka sana. Zanzibar inategemea karafuu, ndio uchumi wake, ukiacha karafuu, pili ni utalii.

Mheshimwa Dau alizungumza pale hajui watalii wanaofika Zanzibar ni wangapi karibu laki saba kwa mwezi au zaidi ya hapo kama sikosei.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ifike mahali tuangalie formula hii inavyokwenda. Zanzibar kipato chake kikubwa sasa hivi ni utalii, tufike mahali tuangalie, watusaidie. Bidhaa inayitoka Zanzibar ikafika huku, suala hili tumepiga kelele muda mrefu jamani, waitafutie formula, TRA ni moja Tanzania. Leo hesabu inaanza moja ndio ije mbili. Mtoto akizaliwa leo hatembei siku hiyo hiyo hutambaa, akakamata kibambaza akaanguka, hili halileti picha nzuri jamani. Niombe sana suala hili liangaliwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa Tanzania mambo mengi Tanzania Bara imeiga Zanzibar bila kuficha, Mheshimiwa Waziri wa Fedha hapa nataka aliangalie na Benki Kuu awafahamishe, formula inayokuja ya Bureau De Change nasikia itakuwa ngumu na Zanzibar ni ndogo na inategemea sana utalii itawasumbua. Vigezo vya formula hii Tanzania Bara wameiga toka Zanzibar, waangalie masharti yatakayokuwepo yawe na uwiano.

Narudia tena Zanzibar itategemea utalii, watalii watapata shida, kwa hiyo formula ya Bureau De Change zinazokuja waziangalie ili angalau kuwe na uwiano, nafikiri hii formula itawasokota sana wananchi. Kwa hiyo, jambo hili waliangalie.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kwa kumalizia, namwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu na Ofisi yake tunamhitaji Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa upande wa Tanzania Bara angalau na sisi atutembelee, roho ina choyo, tunaomba sana. Kachanguliwa na Tanzania ikiwepo Zanzibar tunamwona kwa wenzetu, hili tunaliomba sana, tupelekeeni salam kwa wahusika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Jaku, lakini umezungumza lugha moja hapo kuhusu mtoto kushindwa kukimbia naamini hukukusudia kuita Zanzibar mtoto. Kwa kuwa hukukusudia hayo maneno kwenye Taarifa Rasmi za Bunge yasi…

MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niweke hansard sawa unajua Kiswahili cha kwetu pwani mtoto akazaliwa haendi mbio siku hiyo hiyo hutambaa akakwetwa, maana yake haya mambo yawe na formula maalum kwa upande wa Zanzibar.

NAIBU SPIKA: Hiyo hiyo kauli ndio sitaki iingie kwenye taarifa rasmi za Bunge kwa kuwa Zanzibar sio mtoto wala hajaanza jana Muungano ni wa muda mrefu.

MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ni hivyo au kama imefahamika hivyo nafuta kauli hiyo.