Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Raphael Michael Japhary

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Moshi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia Makadirio ya Bajeti ya Hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Jambo la kwanza ninalotaka kuishauri Serikali, ni suala la mapato ya Serikali ikiwa ni pamoja na kuimarisha uwekezaji katika sekta binafsi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maoni yangu, mojawapo ya eneo ambalo limekuwa ni kikwazo cha kuimarisha sekta binafsi katika nchi hii, ni viwango vya kodi katika nchi yetu. Viwango vyetu vimekuwa ni kichocheo kikubwa cha kufanya wafanyabiashara wengi na wawekezaji wengi wakwepe kodi. Bahati nzuri nimeshaona jitihada zinazofanyika kusukuma hili suala la kupunguza viwango vya kodi. Nilikuwa naiomba Serikali ilifanye jambo hili kwa haraka iwezekanavyo ili iweze kuwa kichocheo cha wananchi kulipa kodi na kwa maana hiyo kuwekeza kwa kiwango kinachoridhisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kodi katika nchi hii imekuwa kama ni silaha ya kuadhibu baadhi ya watu ambao inawezekana wakawa na maoni tofauti au wakawa na mitazamo tofauti na Serikali hii. Sasa badala ya kodi kuwa sehemu ya kichocheo cha kuhakikisha kwamba nchi yetu inapata mapato ya kuendelea na kuweza kujiendeleza vizuri, kodi imekuwa sasa ni sehemu ya kuonyesha kwamba kama mtu ametofautiana na Serikali au ametofautiana na mtu yeyote katika Serikali, basi inakuwa kama ni adhabu, kwa sababu viwango vyake vimekuwa vikubwa, kwa hiyo, vinamfanya kila mtu akikutana na mtu wa TRA, aone ni afadhali angekutana na simba kuliko kukutana na mtu wa TRA.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nadhani ni vizuri tuvirekebishe viwango vyetu vya kodi ili vilipike na visiwe ni kichocheo cha kuwa kama adhabu kwa watu wengine ambao wanaonekana kwamba wanapingana na mitazamo fulani na fikra fulani za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili katika suala hili hili la uwekezaji, ni namna ambavyo kodi imekuwa ikilipwa na kundi fulani la watu wachache katika nchi hii. Bahati nzuri nimesikia Mheshimiwa Rais juzi akitoa takwimu kwamba mpaka sasa hivi tunavyozungumza Tanzania ina watu wasiozidi 2,700,000 kati ya watu milioni 55 ambao ni walipa kodi. Maana yake bado tuna kundi kubwa la watu ambao bado wako nje ambao hawalipi kodi. Inawezekana hatujafanya jitihada kubwa za kuwafanya hawa watu waingie.

Mheshimiwa Naibu Spika, rai yangu ni kwamba, kwa sababu kuna huo msisitizo wa Mheshimiwa Rais ni vizuri tuhakikishe kuwa tunasukuma ili watu wengi zaidi waingizwe kwenye utaratibu wa kulipa kodi ili tupunguze mzigo huu kwa watu wachache ambao sasa imefanywa kodi kuwa kama adhabu kwa watu fulani katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nizungumzie suala la vitambulisho vya wajasiriamali wadogo. Kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu amedhani kwamba mpango huu utasaidia makusanyo ya mapato katika Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika na Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kuwaambia kuwa vitambulisho hivi kwa sasa tena siyo msaada kwa Halmashauri zetu bali ni tatizo kwa Halmashauri zetu kuhusu suala la mapato. Kwa sababu wazo la vitambulisho vya wajasiriamali wadogo lilipokuwa limetolewa na Mheshimiwa Rais nilidhani lilikuwa limetazama Wamachinga wanaozunguka barabarani na mitaani, lakini leo tunavyozungumza, vitambulisho vya wajasiriamali wadogo wadogo vimeenda mpaka masokoni kwenye ambavyo ni vitega uchumi vya Halmashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa wafanyabiashara wadogo wadogo walioko kwenye masoko, leo nao wanapaswa kupewa vitambulisho vya Mheshimiwa Rais. Kwa misingi hiyo, ina maana kwamba hata mapato yaliyokuwa yakipatikana kwenye masoko yetu, leo hayapatikani kwa ajili ya kuendesha Halmashauri, masoko hayana utaratibu sahihi wa kufanyiwa usafi. Kwa hiyo, mwisho wa siku zoezi hili linaweza likasababisha uchafu katika maeneo yetu mengi na masoko yetu mengi na Halmashauri zetu nyingi kukosa mapato na pia kushindwa kusafisha maeneo yao muhimu sana katika Halmashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni vizuri suala hili liangaliwe. Pamoja na nia yake njema ya kusaidia wafanyabiashara wadogo wadogo kwa maana ya Wamachinga, wale wanaotembea na vitu kichwani ili watambulike, ili wasibugudhiwe, lakini ni lazima tuone namna gani mpango huu unaendelea kuzibakishia Halmashauri mapato ili dhamira hii ambayo Mheshimiwa Waziri Mkuu ameonyesha kwenye hotuba yake kwamba lengo ni kusaidia Halmashauri zipate mapato badala ya kuathirika kuhusu mapato yake. Kwa sababu kwa hali ilivyo sasa hivi hapa, mpango huu unaziathiri sana Halmashauri nyingi ambazo zilikuwa zinatumia baadhi ya maeneo kama masoko kama sehemu ya vyanzo vyake vya mapato.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu amesema kwamba hali ya demokrasia nchini anaona inaimarika. Inawezekana hali inaimarika kwa mtazamo wa tawala, lakini kwa uhalisia na kama wote mnamwogopa Mungu, hali ya demokrasia katika nchi hii imekuwa mbaya sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tulipokuwa tupo kwenye Serikali ya Awamu ya Nne na zilizokuwa nyuma yake hali ilikuwa angalau ni nzuri hata kama ilikuwa na matatizo kidogo kidogo kuliko hali ilivyo sasa. Kwa kujidanganya kwamba hali ya demokrasia katika nchi hii inaimarika, kujidanganya kwamba chaguzi zilikuwa huru na haki, ni kujidanganya sisi wenyewe kama vile hatuoni. Kimsingi ni kwamba hali ya demokrasia katika nchi hii imekuwa ni mbaya zaidi kuliko wakati wowote mwingine katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri, tungejitathmini vizuri bila kuwa na ushabiki wa kisiasa. Katika Taifa hili hatuna ubaguzi wa kidini, hatuna ubaguzi wa kikabila, lakini tumekuwa na ubaguzi mkubwa sana wa kiitikadi. Leo kuna watu ambao katika nchi hii, kwa kuwa katika itikadi tofauti na Chama Tawala wanaonekana kama vile sio watu wenye haki na Taifa la Tanzania. Wanaonekana kwamba hawastahili kukaa Tanzania. Tumejikuta tunatengeneza mbegu ambayo mwisho wa siku itakuwa ni tatizo kubwa katika Taifa hili na inaweza ikaliumiza sana Taifa hili kwa kubaguana kiitikadi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi wote ni Watanzania tuonane kwamba tuna haki ya kuishi Tanzania na kufaidi rasilimali za Watanzania. Leo tunavyozungumza hapa, Serikali yenyewe mtazamo wake ni kwamba kimaendeleo inaweza ikadhani kwamba kupeleka maendeleo maeneo yaliyochagua CCM ni sahihi zaidi kuliko kupeleka maendeleo maeneo yaliyochagua Upinzani, wakati Upinzani uko kwa misingi ya Katiba ya nchi hii, tumekubaliana wenyewe kwamba lazima Vyama vya Siasa viwepo na wananchi wana haki ya kuchagua anayeona anafaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri tuheshimu haya mambo tuliyokubaliana kwa mujibu wa Katiba yetu ya nchi hii, kuliko kuanza kubaguana kwa misingi tuliyojiwekea wenyewe. Tunatengeneza kizazi ambacho kitakuwa ni cha ubaguzi kisichopendana bila sababu yoyote ya kimsingi. Kazi yote aliyoifanya Mwalimu Nyerere na wenzake katika nchi hii mwisho wa siku itaishia mahali pasipojulikana. Ni vizuri turudishe umoja wetu, itikadi iwe kichocheo cha maendeleo isiwe sababu ya kubaguana baina yetu sisi wenyewe kwa wenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kutoa rai yangu kwa Serikali kwamba hebu rudini nyuma tazameni kwamba hivi tuko katika mstari sahihi? Hivi kweli ni sahihi kusema kwamba demokrasia imeimarika?

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana, naomba kuwasilisha. (Makofi)