Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Mbaraka Kitwana Dau

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa fursa hii. Nianze kusema kwamba naunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu jana kwa namna nzuri sana aliyowasilisha makadirio ya Wizara yake kwa uweledi mkubwa sana. Jana mama yangu Mheshimiwa Anna Kilango alizungumza suala la uwekezaji na nashukuru kwa kuwa suala la uwekezaji hivi sasa lipo katika Ofisi ya Waziri Mkuu na tuna Waziri pale wa Nchi, nami katika mchango wangu nitajikita kwenye maeneo hayo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la utalii, kuna kitu kinaitwa uwekezaji wa utalii wa katika eneo linaloitwa Southern Circuit, eneo la Ukanda wa Kusini. Nimeipitia ile document, sina uhakika sana kama Mheshimiwa Waziri wa Utalii yupo lakini kwa kiasi kikubwa sana hakuna maeneo yoyote yanayozungumzia ama kujadili utalii katika fukwe za pwani. Utalii kwa Kanda ya Kusini kuanzia Tanga mpaka Mtwara kule Msimbati, tuna fukwe nzuri sana kwa ajili ya utalii lakini hii document inayohusiana na Southern Circuit hakuna sehemu yoyote inazungumzia utalii wa fukwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, unapozungumzia utalii wa fukwe huwezi kukiacha kukizungumzia Kisiwa cha Mafia. Kisiwa hiki ni miongoni mwa visiwa vizuri sana katika pwani ya Afrika Mashariki. Kina maeneo ya fukwe mazuri kabisa, kuna scuba diving, sport fishing, ni maeneo mazuri sana kwa uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa masikitiko makubwa sana Kisiwa cha Mafia ambacho sisi wenyewe tunaita ni New Zanzibar, kina offer mambo mazuri yote ambayo Zanzibar ina offer na pengine hata mimi naonekana ni Mbunge ninayetokea Zanzibar kwa sababu Kisiwa cha Mafia kinanasibishwa sana na mambo yanayoendelea kule Zanzibar. Tunatakiwa tuwekeze ili tuifungue Mafia kwani haitambuliki. Pamoja na vivutio vyote vizuri, Mafia inapata watalii wasiozidi 6,000 kwa mwaka wakati Zanzibar inapata watalii kwa malaki, sina takwimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nini kifanyike? Pengine huo ndiyo ushauri wangu ambao Mheshimiwa Waziri wa Uwekezaji katika Ofisi ya Waziri Mkuu ningeomba unisikilize. Tunahitaji kufungua Kisiwa cha Mafia lakini unafikaje Mafia wakatu usafiri ni shida? Tuna kiwanja cha ndege pale kina urefu wa ran way ya kilomita 1.6 ambayo katika hali ya kawaida ndege kubwa haziwezi kutua. Ningeomba sana Waheshimiwa na nimekuona Mheshimiwa Naibu Waziri wa Uchukuzi pale Kwandikwa, kwa nini msiangalie uwezekano wa kuongeza ran way ya Uwanja wa Ndege wa Mafia kutoka kilometa 1.6 kwenda mpaka kilometa 3 na kuruhusu ndege kubwa ziweze kutua pale na kuweza kukifungua kisiwa cha Mafia kwa utalii? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Zanzibar inapata watalii wengi kwa sababu hiyo. Watalii wanakuja na ndege moja kwa moja kutoka nchi za Magharibi na kutua pale Zanzibar lakini ili ufike Mafia lazima utue Dar es Salaam halafu tena uingie kwenye ndege ndogo ndogo na kuja Mafia ambapo watalii wengi hawapendi kadhia ya aina hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kushauri sana katika namna nzuri na bora ya kufungua Kisiwa cha Mafia ule uwanja wa ndege uangaliwe. Kuna terminal building ndogo sana, runway yetu pale ni ndogo sana Mheshimiwa Naibu Waziri uweze kuangalia ni namna gani mnaweza mkaongeza runway ili Kisiwa cha Mafia kiweze kufikika kwa urahisi na ndege kubwa ziweze kutua sambamba hata na ndege yetu ya bombardier. Kwa urefu tuliokuwa nao sasa hivi, ndege ya bombardier inaweza ikatua pale lakini bado hawajaanza hizo safari.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni accessibility kupitia kwenye bahari. Tuna ugomvi wa gati pale wa muda mrefu kidogo, gati la Nyamisati. Tunaishukuru sana Serikali imetutengea fedha na ujenzi umeshaanza pale na tunatarajia ujenzi ule utakamilika ndani ya miezi miwili au mitatu ijayo lakini kukamilika kwa gati la Nyamisati kutakuwa hakuna maana yoyote iwapo Serikali haitatupatia boti ya kisasa ili watu sasa waweze kulitumia gati la Nyamisati sambamba na gati la Kilindoni ili kuunganisha maeneo haya mawili na wananchi waweze kusafiri bila matatizo yoyote.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni barabara. Ndani ya Kisiwa cha Mafia kuna barabara yenye urefu wa kilometa 55, inaitwa Kilindoni kwenda Rasi Mkumbi. Usanifu na upembuzi wa kina umeshakamilika. Naishukuru sana Serikali mambo haya yamekamilika kama miezi miwili, mitatu iliyopita. Sasa kilichobaki ni kutengewa fedha kwa ajili ya kuwekewa lami. Hii nimelisema sana, tatizo linakuja pale kwamba periodical maintenance ya barabara ile inakuwa ni gharama kubwa sana kwa sababu kile ni kisiwa, kuweza kupata udongo, udongo unakaribia kwisha. Itafika wakati sasa ili kufanyia periodical maintenance, inabidi udongo uutoe Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunamwomba sana Mheshimiwa Kwandikwa nimemwona, waangalie uwezekano wa kuiwekea lami barabara hii ili haraka sana tuweze kuondokana na kadhia hii ya kuwa na wasiwasi labda huenda huko mbele udongo ukaisha tukashindwa kufanya periodical maintenance. (Makofi)

Lingine ni suala la Uwekezaji katika bahari kuu. Namshukuru sana Mheshimiwa Spika katika ile Kamati yake ya kuangalia namna gani nchi inaweza ikanufaika na rasilimali yetu ya bahari kuu; mimi nilikuwa ni mmoja wa Wajumbe wa Kamati ile. Tumeyaona mambo mengi sana na nimekuona ndugu yangu Mheshimiwa Ulega. Tulizungumza sana na wewe mwenyewe unalifahamu sana hili suala la blue economic. Kwanini Serikali sasa tusinunue meli ya uvuvi yetu wenyewe?

Mheshimiwa Naibu Spika, meli ya uvuvi gharama yake haitazidi sana, ni baina ya dola milioni moja mpaka dola milioni sita, hapa katikati kulingana na uwezo wetu wa kibajeti. Ninaamini kwa Serikali yetu hii hatushindwi kununua walau meli mbili ama tatu. Suala la uwekezaji katika Bahari Kuu ni zuri sana. Kule huhitajiki kulima kama vile unavyoandaa shamba. Mwenyezi Mungu ameshalima, wewe unakwenda na kapu lako kuvuna tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Muda wako umekwisha Mheshimiwa. Kengele ya pili imeshagonga. (Makofi)

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, nakushukuru sana.