Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Hamidu Hassan Bobali

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii. Kwanza nianze kwa shukrani na kupongeza hatua ya Serikali ya kutatua tatizo la umeme kwa Mikoa ya Lindi na Mtwara. Kiukweli kabisa mimi nimekaa kule karibu miezi miwili sikuwahi kushuhudia hata siku moja umeme ukiwa umekatika tena kijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambasamba na hilo, naomba Mheshimiwa Waziri wa Nishati atusaidie, najua Mheshimiwa Naibu Waziri alikuja mwezi Februari katika Mkoa wa Lindi na alisema kwamba mkandarasi wa State Grid anafanya kazi zake taratibu sana, yuko very slow. Ni kweli kabisa katika Jimbo la Mchinga nakotoka mimi katika kipindi chote cha Phase II na III huyu mkandarasi hajawahi kabisa kuonekana. Viko vijiji ambavyo vimeingia kwenye mradi lakini miaka yote tangia 2016 mpaka leo 2019 hajawahi kuleta hata nguzo moja.

Kwa hiyo, naomba jambo hili lichukuliwe kwa kipaumbele sana kwa sababu hivi vijiji viliingia kwenye mradi na tulishawaeleza wananchi na wananchi wamejiandaa kwa siku zote kusubiri umeme lakini umeme haufiki. Kwa bahati mbaya sana wakienda kwenye vijiji jirani ambako umeme unafika wanaukuta na haukatiki. Tuna umeme wa uhakika sana lakini kuna vijiji ambavyo havijapata hiyo stahiki ya umemeā€¦

T A A R I F A

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Haya taarifa.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Nataka nimpe taarifa mzungumzaji, huyu State Grid anayemzungumza hatufahi kabisa kwa Mkoa wa Lindi kwa sababu mimi kwenye Jimbo langu la Liwale ameweza kuwasha umeme katika vijiji viwili kwa muda wa miaka miwili sasa. Kwa hiyo, huyo mkandarasi hatufai.

SPIKA: Unaipokea taarifa hiyo Mheshimiwa Bobali?

MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Spika, ahsante, nimeipokea taarifa hiyo. Ni kweli Waheshimiwa Wabunge wote wa Mkoa wa Lindi tunamlalamikia mkandarasi huyu na hata Naibu Waziri, Mheshimiwa Subira Mgalu alikuja na yeye akamlalamikia.

Mimi nafikiri ifike wakati hatua zichukuliwe kwa sababu kama mkandarasi yuko site miaka mitatu hajawahi kwenda hata kwenye kijiji kimoja kupeleka nguzo mkandarasi huyo hafai, lakini siku zote yupo, ukifika Lindi pale Mkoani unamkuta, ana makabrasha yake, kubwa analokuambia sijalipwa, lakini taarifa za Serikali zinasema kwamba amelipwa. Naomba sana Serikali walichukue hili jambo huyu mkandarasi kwa kweli hatufai kabisa watubadilishie watupatie mkandarasi mwingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nishukuru pia juzi nimemsikia Mheshimiwa Rais akiwa Mkoani Mtwara ametupongeza Wabunge wa Mkoa wa Lindi na Mtwara namna tulivyosimamia na namna tulivyolisemea zao la korosho. Nashukuru kwa sababu Mheshimiwa Rais ame-recognize juhudi yetu ambayo tulikuwa tunaifanya ndani ya Bunge na sisi tunashukuru na tunapongeza kwa hatua zilizochukuliwa na Serikali kulipa wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo hili la mwaka huu liwe fundisho kwetu wote. Kwenye suala la korosho kuna changamoto nyingi sana. Nafikiri Mheshimiwa Rais mwenyewe amejionea na zingine amekuwa akishangaa kama zinatokea katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wako watu wengi wamekatwa fedha zao, mtu badala ya kulipwa ile fedha yake halali analipwa anakatwa Sh.300. Yako maagizo mengine Mheshimiwa Rais ameyatoa lakini nachosisitiza jambo lililotukuta kwenye msimu wa korosho uliopita liwe fundisho kwetu sote. Jambo hili kwa kweli limetupotezea fedha nyingi. Mimi nashukuru kwamba Mheshimiwa Rais ame- recognize na ametambua juhudi zetu namna Wabunge tulivyolisemea zao la korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambasamba na hilo kuna zao la ufuta, ndiyo ile hoja ya uwekezaji ambayo imezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge wengi hapa, ufuta unalimwa kwa wingi sana Mkoa wa Lindi. Ukizungumza na matajiri wanasema ule ufuta wa Lindi ambao kwa jina unaitwa Lindi White ni ufuta bora sana kwa sababu una mafuta mengi. Mafuta ya ufuta ni miongoni mwa mafuta bora na ni mazuri yanatumiwa na watu wenye fedha zao. Hapa Tanzania sidhani kama tuna kiwanda cha kukamua mafuta ya ufuta. Ufuta wote ambao unazalishwa kwenye nchi hii unasafirishwa kupelekwa nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, hivi sasa naposema tayari wakulima wanakaribia muda wa mavuno, najua tayari matajiri wameshajiandaa kuja kuchukua ufuta, tunapoteza fedha nyingi sana za kigeni kuagiza mafuta ya kupikia, kwa nini tusifanye mpango ufuta unaozalishwa ukawa umewekewa utaratibu pale Lindi tukapata kiwanda cha kukamua mafuta, tukaongeza ajira, kuna tatizo kubwa la ajira ingesaidia pia kupunguza tatizo la ajira la vijana. Kwa hiyo, hili jambo la uwekezaji ni muhimu sana na nashukuru umekuwa ukisimama zaidi ya mara mbili kulisisitiza. Jambo hili linahitaji lichukuliwe kwa tahadhari kubwa sana kwa misingi ya kutaka kupata maendeleo kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, nitoe rai pia viongozi wetu, Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa wasifanye harassment kwa wawekezaji. Kuna jambo la kusikitisha lilitokea hivi karibuni katika moja ya Mikoa ya Kusini mwa Tanzania, Mkuu wa Mkoa anaonekana anaweka ndani mwekezaji, anachukuliwa anasekwa mule, mambo kama haya yanaharibu taswira nzima ya uwekezaji na mtu mwingine ambaye alikuwa ana nia ya kutaka kuja Tanzania hawezi kuja. Kwa hiyo, jambo hili lazima lichukuliwe kama ni sensitive na iwe ni ajenda ya Taifa kwamba tunakwenda kwenye kuvutia wawekezaji, sheria zibadilishwe, miongozo iwekwe sawa ili wawekezaji warahisishiwe namna gani wanaweza wakaja wakafanya shughuli zao vizuri kabisa lakini bila kubuguziwa, kuwekwa ndani saa 24 na kadhalika. Mambo haya kwa kweli yanatutia doa wote.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii. (Makofi)