Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Magdalena Hamis Sakaya

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Kaliua

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ambayo iko mbele yetu. Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa nafasi hii. Naomba niseme kwamba naipongeza Serikali kwa masuala ya afya kwa kuhakikisha kwamba wameweza kuimarisha huduma za uchunguzi wa magonjwa katika kufunga vifaa vya kisasa katika hospitali mbalimbali hapa nchini, lakini zaidi kabisa kuweza kufunga mashine za kisasa za MRI, CT-SCAN Digital X-Ray na Modern Ultrasound, katika Hospitali ya Moi Muhimbili.

Mheshimiwa Spika, nilisema tena wakati tumeletewa Mpango wa Bajeti na nikaiomba Serikali kitendo cha kuweza kufunga vifaa vya kisasa kwenye Hospitali ya Muhimbili kimeokoa sana sana watu wengi ambao walikuwa wanaumia na kupoteza maisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kuweza kuimarisha huduma kwenye Taasisi ya Moyo ya JK Kikwete. Cha kwanza nipongeze sana utendaji mzuri wa Taasisi ya Moyo ya JK Kikwete. Kama hujauguliwa au hujaugua huwezi kujua umuhimu wa Taasisi hii. Kama umeuguliwa au umeugua unaweza kuona umuhimu wa Taasisi hii.

Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kumpongeza kwa dhati Director wa ile Taasisi, Profesa Jinabi na Dkt. Kitenge na watumishi wengine wote na Madaktari wote, kwa kazi nzuri wanayoifanya. Kama unataka kwenda kujifunza huduma ya upendo wa dhati, huduma inayomponyesha mgonjwa kabla hajaipata, basi watumishi waende Taasisi ya Moyo. Kwa kweli, nisiposema haya, mawe yatasimama yatasema na nitaonekana sina maana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninachoiomba Serikali, baada ya kuhakikisha kwamba kuna huduma hizi za msingi kwenye ya JK pamoja na Hospitali ya Moi na maeneo mengine, naomba vifaa vya kisasa viende kwenye hospitali zote za Mikoa ya Tanzania, tuwekeze kwa mara moja. Serikali imesema iwekeza karibu shilingi bilioni 12. Ukiwekeza shilingi bilioni kwa mara moja kwa miaka zaidi ya kumi ijayo hujapoteza chochote. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Magdalena Sakaya, kwa makofi haya yaliyopigwa humu ndani kuhusiana na Taasisi ya Jakaya Kikwete, basi kwa niaba ya Waheshimiwa Wabunge tutaandika barua rasmi ya pongezi kwa Uongozi na Wafanyakazi wa Taasisi hiyo kuwapa moyo kwa niaba yenu Waheshimiwa Wabunge wote. Endelea Mheshimiwa. (Makofi)

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nashukuru kwa hatua hizo. Naiomba Serikali tuhakikishe tunatafuta fedha tuwekeze kwenye vifaa tiba na vifaa vya kisasa kwenye Hospitali za Mikoa. Inakuwa ni ngumu mtu kutoka labda Ruvuma au kutoka Tabora mpaka Muhimbili kufuata vifaa hivi vya kisasa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tukiwekeza kwenye hospitali zote za Rufaa za Mikoa, tukihakikisha tumeweza kuweka vifaa vya kisasa kuhakikisha tunakuwa na uchunguzi wa kisasa, tutaweza kupunguza idadi ya watu wengi wanaokuja Muhimbili. Pia tutaokoa sana wananchi wetu ambao wengi walikuwa wanapoteza maisha.

Mheshimiwa Spika, leo tumeokoa gharama kubwa ambazo watu walikuwa wanaenda India na maeneo mbalimbali, lakini leo huduma ambazo zilikuwa zinapatika India leo ziko ndani ya Tanzania pale Hospitali ya Moi. Nashukuru sana kwa ajili ya hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali imesema kwamba inajenga hospitali katika maeneo mbalimbali, nami napongeza kwa hatua hiyo. Naomba juhudi ziendelee. Pamoja na kuwa tunaongeza vituo, katika hotuba Mheshimiwa Waziri amesema wameongeza vituo 441, lakini kwa speed ya ongezeko la Watanzania, speed yetu ni kubwa kweli kweli, tunaongezeka sana na niliwahi kuomba mwongozo hapa kwamba angalau tuweke standard ya watoto, Serikali ikasema imeachia free watu wazaane tu. Speed yetu ni kubwa sana. Kwa hiyo, tunavyozidi kuongezeka ndivyo mahitaji ya Vituo vya Afya, Zahanati na Hospitali zinahitajika.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba bado speed ya kuongeza vituo vya iendelee kuongezeka. Nashukuru kwamba Serikali ilitoa agizo kupitia TAMISEMI miaka kama miwili iliyopita kwamba kila baada ya Kata mbili wajenge Kituo cha Afya kimoja. Sisi Kaliua tumeanza kujenga vituo vinne kwa mpigo. Tunaomba Serikali iongeze nguvu kwenye vile vituo.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli alipokuja Kaliua, alitoa shilingi milioni kumi kama mbegu kupanda kwenye Kituo kimoja cha Afya cha Usinge. Kwa hiyo, naomba Serikali isadie vile vituo ambavyo vimeanzishwa ili yale maboma yasibaki wazi, likamilike tuendelee kuongeza huduma za afya lakini pia kupunguza vifo vya akina mama na watoto.

Mheshimiwa Spika, pia Serikali imesema kwamba inaendelea kujenga hospitali, imekarabati hospitali nyingi na ina hospitali nyingi sana kwa ajili ya kujenga. Wilaya ya Kaliua tunajenga hospitali ya kisasa ya Wilaya kwa fedha za ndani, iko karibu asilimia 60.

Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali, Mheshimiwa Makamu wa Rais alipokuja ametupongeza, Mheshimiwa Waziri Mkuu ametupongeza, Mheshimiwa Rais ametupongeza; naiomba Serikali iongeze nguvu pale kwenye ile hospitali. Tumemaliza jengo la OPD, la ghorofa tumemaliza, jengo la akina mama na mtoto la kisasa tumemaliza mwaka huu. Tunaiomba Serikali itusaidie, kuweza kujenga jengo la wanaume na jengo la uchunguzi ili huduma pale ziweze kufunguliwa, hospitali ile ifunguliwe kazi ziendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nashukuru sana. La pili, naomba niende kwenye suala la mifugo. Watanzania tumejaliwa kuwa na mifugo mingi, lakini kiukweli hatujaweza kutumia fursa ya mifugo Tanzania kuongeza pato la Taifa inavyotakiwa. Hiyo ni wazi kabisa. Leo mifugo yetu mingi inakwenda kunufaisha Taifa la nje. Mimi mwezi wa 12 nilienda Nairobi kwa kutumia basi, kupitia Namanga. Nimefika pale Namanga niliweka mikono kichwani, nimekuta malori tisa yamebeba ng’ombe, mbuzi, kondoo.

Mheshimiwa Spika, nikawauliza wale watumishi wa pale, wakasema huu ndiyo utaratibu, kila siku malori tisa au kumi yanakwenda Nairobi. Sasa nikawa nasema mifugo kuanzia ngozi ni mali, kwato ni mali, damu ni mali, kila kitu ni mali. Leo yale yote yanakwenda kutoa faida kwenye Mataifa mengine, sisi tunabaki tu tunaambulia ile kodi kidogo inayotolewa pale.

Mheshimiwa Spika, bado tunahitaji kufanya mambo makubwa sana kwenye Sekta ya Mifugo, hatujaweza. Leo Mikoa ambayo inazalisha mifugo kwa wingi hatuna viwanda vya kuchakata masuala ya mifugo. Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne alizindua machinjio ya kisasa pale Ruvu.

Mheshimiwa Spika, niiulize Serikali leo, naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu tujue yale machinjio ya kisasa pale Ruvu ambayo yalipewa karibu shilingi bilioni mbili tangu mwaka 2008 mpaka leo yamebaki ni magofu, nini kinaendelea pale?

Mheshimiwa Spika, lazima tuwekeze kwenye viwanda vya mifugo, lazima tuhakikishe kwamba rasilimali ya mifugo inanufaisha Taifa. Leo kwa baadhi ya maeneo ya Mikoa mingine, mifugo inaonekana ni changamoto, inaonekana ni kero na siyo fursa, wakati hii ni mali. Tunatumiaje uwezo wetu Watanzania wa kuwa watatu kiafrika kuwa na mifugo mingi kuweza kuongeza pato la Taifa.

Mheshimiwa Spika, naomba sana kwenye Sekta ya Mifugo tuhakikishe tunawekeza vizuri. Leo Tanzania nzima, nilikuwa nazungumzia habari ya viwanda vya Tanganyika Packers, ni historia. Viwanda vyote ni historia. Mwanza kulikuwepo na viwanda vya nyama, leo ni historia.

Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali, ili tunufaike vizuri na pato hili; mimi nilijaribu kupiga mahesabu ya haraka haraka: Je, pale Kenya kwa kupokea magari tisa kwa siku, wanapata nini? Sisi tunakosa nini? Hiyo ni mifugo, bado maziwa, wanachukua. Sisi tumekuwa ni collecting Center. Pale Arusha ambapo kuna mifugo mingi imekuwa ni collection Center wanakusanya wanapeleka Nairobi.

Mheshimiwa Spika, tunakwenda kwenye uchumi wa viwanda, tunakwenda kwenye uchumi wa kati, hatuwezi kwenda huko kama hatuwekezi vya kutosha. Ndiyo maana nashukuru sana mchango wa mama yangu Mheshimiwa Anne Kilango, Sekta ya Uwekezaji, dada yangu Mheshimiwa Kairuki umepewa jukumu zito, ni lazima utumie nafasi hiyo kikamilifu.

Mheshimiwa Spika, nashukuru Mheshimiwa Rais alivyoweka hii Sekta chini ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Hii Wizara iliyoko chini ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Waziri Mkuu tunamjua utendaji wake wa kazi, tumwambie asimamie kikamilifu lakini walio chini yake wafanye kazi kikamilifu, wahakikishe wanaitendea haki Wizara hii. Hatuwezi kwenda kwenye uchumi wa viwanda, kwenye uchumi wa kati kama hatujaweza kusimamiwa vizuri suala la uwekezaji.

Mheshimiwa Spika, natoa mfano mmoja, kwanza tumekuwa wazito sisi Watanzania kwenye suala la uwekezaji na tumekuwa tuna vikwazo vingi, tumekuwa na urasimu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Nakuongezea dakika tano uweke vizuri uwekezaji huo. (Kicheko/Makofi)

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Tumekuwa na urasimu ambao saa nyingine hauna tija kabisa, urasimu ambao unakatisha tamaa wawekezaji, urasimu ambao unafanya mtu anazungushwa mwaka mzima; amekuja na mtaji wake au anakopa benki anataka awekeze, mwaka mzima anapigwa dana dana, nenda rudi nenda rudi, ameshapata ardhi, anaambiwa mpaka Environment Impact Assessment, inachukua miezi sita, anaambiwa sijui hiki, miezi sita.

Mheshimiwa Spika, wale wanaokuja kuwekeza wanakata tamaa, hawawezi kuwaambia walioko huko kwamba njooni. Kwa hiyo, ni lazima tuweke conducive environment kuhakikisha kwamba mwekezaji anapokuja tunampokea vizuri, akiwekeza anapiga simu, njooni Tanzania inawekezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwaka 2018 ulitutuma kwenda South Africa, bahati nzuri tukapata bahati ya kumtembelea Balozi wetu wa South Africa, tukajaribu kumwambia mojawapo ya tatizo katika nchi yetu, hatuna wawekezaji. Vile vile kazi mojawapo ya Mabalozi ni kuwa na diplomacy ya kuvutia wawekezaji kwenye nchi yetu. Wewe umefanya nini kuhakikisha kwamba tunapata wawekezaji kutoka South Africa?

Mheshimiwa Spika, alisikitika sana, akatuambia ndugu zangu mimi nasikitika sana. Nimepata wawekezaji South Africa. Kwanza alipata wawekezaji wanaotaka kuja kuwekeza Tanzania kwenye mashamba ya kulima parachichi Iringa, ametuma barua TIC mwaka mzima hakujibiwa. Wale wawekezaji wamesubiri mwisho wamekata tamaa wameondoka zao. Akapata wawekezaji wengine hata ile ku-reply kwamba tumepata barua yenu jamani tuna- respond, no response.

Mheshimiwa Spika, tunahitaji wawekezaji; lakini akapata wengine, akahangaika baba wa watu, kapata wawekezaji wa kuwekeza kwenye kiwanda cha ku-assemble Volkswagen hapa Tanzania, walitaka kuja hapa kuwekeza Tanzania. Walitaka kuweka kiwanda cha magari ku-assemble Volkswagen. Wamepigwa dana dana nenda rudi hawajibiwi; na wenzetu Wazungu wanakwenda kwa muda. Watu wana- invest kwa muda. Huwezi kuwa unataka uwekeze leo, unaambiwa kaingize mwakani. Mipango inabadilika, watu wanakwenda kwa malengo, ya jana siyo ya leo.

Mheshimiwa Spika, wamepigwa dana dana, Tanzania Investment Center imezubaa, haikujibu kwa wakati, wale wawekezaji wamekwenda kuwekeza kiwanda cha Volkswagen Kenya pale. Leo tayari uchumi ambao ungeingizwa na kile kiwanda kimoja cha Volkswagen, umekwenda Kenya.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hii ni mifano hai, ni namna gani ambavyo hatutumii fursa kama Watanzania. Kwa hiyo, Sekta ya Uwekezaji ni sekta muhimu sana. Hakuna Taifa lolote duniani linaweza kuendelea bila wawekezaji usidanganywe na mtu. Ukiona leo China imeendelea, ni wawekezaji, Malaysia, Singapore, kila mahali, hata Nairobi hapa ni wawekezaji.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ni lazima kama Taifa tuhakikishe kwamba tunaweka nguvu ya kutosha kwenye suala la uwekezaji ili lengo letu la kwenda kwenye uchumi wa viwanda, uchumi wa kati liweze kutimia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ni suala la kilimo. Wenzangu wamechangia sana suala la kilimo, lakini kwa kuwa ni sekta muhimu sana kwenye uchumi wetu na hasa uchumi kwenda uchumi wa kati, kwenda uchumi wa viwanda, naomba nami niweke inputs zangu.

Mheshimiwa Spika, bado uchumi wetu hatujaweza kuwekeza kikamilifu. Nilikuwa nasoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, amesema kwamba benki yetu ya Tanzania Agriculture Development Bank imeweza kukopesha shilingi bilioni 100. Mimi naona ni kidogo sana kwa wakulima wa Tanzania nzima, ni kidogo bado. Kwa sababu kuna watu ambao wana ekari 1000, kuna watu ambao wana ekari 2000 mpaka ekari 100,000. Ukiangalia hii shilingi bilioni 100 ni kidogo kwa watu hao, lakini tunataka ku-transform kilimo chetu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE.MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.