Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

TAARIFA YA KAMATI YA HAKI, MAADILI NA MADARAKA YA BUNGE KUHUSU SHAURI LA KUDHARAU NA KUDHALILISHA BUNGE LINALOMKABILI MHE. HALIMA JAMES MDEE (MB)

Hon. Emmanuel Adamson Mwakasaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

TAARIFA YA KAMATI YA HAKI, MAADILI NA MADARAKA YA BUNGE KUHUSU SHAURI LA KUDHARAU NA KUDHALILISHA BUNGE LINALOMKABILI MHE. HALIMA JAMES MDEE (MB)

MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA HAKI, MAADILI NA MADARAKA YA BUNGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba niweze kujibu baadhi ya hoja ambazo zimetolewa na Waheshimiwa Wabunge kuhusiana na shauri hili la Mheshimiwa Halima Mdee.

Mheshimiwa Naibu Spika, naanza na Mheshimiwa Masoud, yeye aliongelea zaidi suala la nidhamu katika Bunge kwamba nidhamu lazima iweze kupewa kipaumbele ili sisi tuwe mfano pia kwa wale wanaowaangalia Wabunge na aliunga mkono hoja. Nashukuru na sina la kuweza kuzungumzia zaidi ya hapo, huo ndiyo ukweli wenyewe kwamba nidhamu ni kitu muhimu na ndiyo maana kuna Kamati hii ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia suala la Mheshimiwa Godbless Lema siwezi kulizungumzia kwa kuwa yeye tayari anasubiri kuitwa kwenye hii Kamati hii hii ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge kwa maneno ambayo kayatumia humu ndani ambayo ni kinyume na maadili.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mlinga amezungumzia kwamba tuna viongozi wetu humu mbalimbali upande wa Chama cha Mapinduzi lakini pia na upande wa Upinzani yupo Kiongozi wa Upinzani. Hawa ndiyo wanatakiwa wawe viongozi katika kuelekeza mambo yanayohusiana na maadili kwa Waheshimiwa Wabunge mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia siyo kweli kwamba Wabunge ambao wamekuwa siku zote wanapewa adhabu ni wa Upinzani peke yake. Katika nyaraka/kesi mbalimbali ambazo sisi tumezipitia katika kumbukumbu ya kesi zilizopita (precedents) hata Wabunge wa Chama cha Mapinduzi wapo ambao kwa miaka ya nyuma wamewahi kupewa adhabu na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa kusimamishwa vikao mbalimbali akiwemo Mheshimiwa Richard Ndassa ni wa Chama cha Mapinduzi miaka ya nyuma amewahi kusimamishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nizungumzie suala ambalo amelisema Makamu Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Ishengoma. Ni kweli ukiangalia mwenendo wa Mheshimiwa Halima Mdee kwa muda mrefu, Kamati kwa kiwango kikubwa imempunguzia adhabu na hasa kwa kuzingatia muda mfupi wa uhai wa Bunge uliobaki. Kwa hiyo, Kamati ile hatukai tu kwa ajili ya kukomoa watu mbalimbali, ndiyo maana nimetoa majina ya Waheshimiwa mbalimbali ambao waliletwa kwenye Kamati hii na wakasamehewa akiwemo Mheshimiwa Aikael Mbowe ambaye ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, siyo kwamba inamtia hatiani kila mmoja lakini Mheshimiwa Halima Mdee ameletwa mara nyingi sana. Hata hii adhabu tuliyompa ni kwamba tuliangalia pia na body language yake alivyokuja kwenye Kamati, tunaangalia vitu mbalimbali. Hata yeye alikuwa anaonyesha kabisa hali ya wasiwasi kwanza kutokana na muda wa Bunge uliobaki mpaka ilifika mahali akasema mimi kweli nimekuja tena humu. Hata yeye mwenyewe anaona kabisa kwamba sasa amezidi kuletwa kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge. Kwa hiyo, adhabu hii tuliyompa kwa kweli ni ndogo lakini pia kuna huruma kama alivyosema Makamu Mwenyekiti kwa sababu tu ya uhai wa Bunge ambao umebakia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Bunge likubali taarifa pamoja na Azimio linalohusu Mheshimiwa Halima Mdee. Naomba kutoa hoja.

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.