Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

TAARIFA YA KAMATI YA HAKI, MAADILI NA MADARAKA YA BUNGE KUHUSU SHAURI LA KUDHARAU NA KUDHALILISHA BUNGE LINALOMKABILI NDUGU PROF. MUSSA ASSAD, MDHIBITI NA MKAGUZI MKUU WA HESABU ZA SERIKALI

Hon. Freeman Aikaeli Mbowe

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Hai

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

TAARIFA YA KAMATI YA HAKI, MAADILI NA MADARAKA YA BUNGE KUHUSU SHAURI LA KUDHARAU NA KUDHALILISHA BUNGE LINALOMKABILI NDUGU PROF. MUSSA ASSAD, MDHIBITI NA MKAGUZI MKUU WA HESABU ZA SERIKALI

MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumza kwa kifupi sana kwa sababu natambua kwamba Azimio ambalo mnakusudia kulipitisha mahali hapa mmeshalifanyia maamuzi na historia ambayo mnaiandika leo itawahukumu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge mnajipa utukufu na utukufu ni wa Mungu peke yake. Mnataka kuwaziba Watanzania midomo, watu wasiseme, watu wasi-comment wakati sisi hapa Bungeni tunafanya maamuzi yanayowaathiri Watanzania. Tunataka kupoka haki za msingi za watu kwa sababu sisi tuna mamlaka ya kufanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ninukuu Katiba ya nchi yetu kuhusu haki na uhuru wa mawazo. Ibara ya 18 ya Katiba inasema nini? Inasema hivi:

“(a) Kila mtu akiwemo CAG, kila mtu, ana uhuru wa kuwa na maoni na kueleza fikra zake.

(b) anayo haki ya kutafuta, kupokea na kutoa habari bila ya kujali mipaka ya nchi. (Makofi)

(c) anao uhuru wa kufanya mawasiliano na haki ya kutoingiliwa…”

T A A R I F A

MHE. GOOLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.


WABUNGE FULANI: Aaaaa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbowe kuna taarifa, Mheshimiwa Mlinga.

MHE. GOOLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimpe taarifa Mheshimiwa Freeman Mbowe anayezungumza kuwa kifungu ambacho ananakili kuwa kila mtu ana haki ya kutoa taarifa na kupokea taarifa, Profesa Assad siyo mtu kama watu wengine, Profesa Assad ni kiongozi mkubwa katika taasisi kubwa katika nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

WABUNGE FULANI: Aaaaa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbowe unaipokea taarifa hiyo?

MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, hii taarifa naipokeaje? Mimi naona niiache tu wala nisi- comment kuhusu taarifa hiyo na haya ndiyo mambo ya kufanya utani kuhusu mambo ya msingi ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipengele cha (c) kinasema nini? Kinasema: “anao uhuru wa kufanya mawasiliano na haki ya kutoingiliwa katika mawasiliano yake.

(d) anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia kuhusu masuala muhimu ya jamii.” (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huo ndiyo msingi wa Katiba na Katiba ni sheria mama. Sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge haiwezi ikavunja Katiba ya nchi. Kifungu ambacho kimemtia hatiani Profesa Assad kinavunja Katiba ya nchi, hilo ni jambo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili na naomba iingie vilevile kwenye record za Bunge kwamba katika siku za usoni tunapounda hizi Kamati za Maadili kama tuna nia njema na nchi yetu tuangalie kwa makini composition ya Kamati za Maadili. Kwa sababu composition ya Kamati ya Maadili leo haiwezi ikafanya justice kwa vyama vya upinzani au kwa watu ambao wanaonekana pengine wanaikwaza Serikali. (Makofi)

T A A R I F A

MHE. BONIFACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. FREEMAN A. MBOWE: Kamati hii ya Maadili...

MHE. BONIFACE M. GETERE: Taarifa.

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, hiyo itakuwa ni taarifa ya mwisho, Mheshimiwa Getere.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. BONIFACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kutoa taarifa kwa Mheshimiwa Mbowe, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumpa mtu adhabu au kwa nidhamu aliyoifanya kumpa adhabu hiyo siyo kwamba unakwenda kumtesa.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. BONIFACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, leo ningeona Bunge au upande mwingine wa Bunge wangekuwa jasiri kama msingi wa CAG uliopo sasa hivi ulikuwa ni kuzungumzia shilingi trilioni 1.5.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. BONIFACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, kama Kamati ya PAC na CAG mwenyewe amekubali kwamba matumizi ya shilingi trilioni 1.5 hayana matatizo yoyote katika nchi hoja ya kuja kusema kwamba Bunge ni dhaifu inatoka wapi?

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. BONIFACE M. GETERE: Angekuwa jasiri kama angekubali mambo yote kwamba matumizi ya shilingi trilioni
1.5 ni hovyo na sasa yeye hawezi kukubali hoja hiyo. Ameleta matumizi ya shilingi trilioni 1.5 kwamba yako sawa, udhaifu wa Bunge unatoka wapi?

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbowe unaipokea taarifa hiyo?

MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, napokea nini hapo? Yaani kuna nini cha kupokea hapo? Maana sijui Mheshimiwa Mbunge, aaah, nafikiri niachane naye. Naomba tu unilindie muda wangu, mimi hiyo taarifa siipokei kwa sababu hata sielewi anataka kusema nini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nazungumzia composition ya Kamati ya Maadili, ushauri wangu kwa Bunge na kwa Mheshimiwa Spika na Wabunge wote, tukitaka maadili ya Bunge yasimamiwe sawasawa kwa haki, uangaliwe uwezekano wa kufanya balance kwa members wa Kamati ya Maadili. Mkiendelea kuiongoza hii Kamati ya Maadili mnavyoipeleka leo, perception ya umma na nasisitiza, perception ya umma inaona Kamati ya Maadili ni Kamati ya Chama na maamuzi yanafanyika nje ya Bunge watu huku pengine tunakuwa tunaelekeza tu maelekezo tuliyopewa. Caucus ya Chama ndiyo inafanya maamuzi kwa niaba ya Bunge and this is dangerous, tuna-set precedent ambayo ni mbaya zaidi na zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama mnafikiri ni Profesa Assad mwenyewe anaona Bunge hili ni dhaifu ruhusuni Bunge live. Hamtaweza kuwazuia Watanzania kuliona Bunge ni dhaifu kama tutatunga sheria ambazo zinawaumiza wananchi na kama tutafanya maamuzi ambayo yanawaumiza wananchi na kama tutaendelea kuzuia uwazi na ukweli na transparency katika shughuli za Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa ya CAG tuna-deal na matawi tunaacha ku-deal na tatizo la msingi. Hoja ya shilingi trilioni 1.5 ambayo imekwenda mpaka shilingi trilioni 2.4 haijapata majibu ya kuridhisha katika Bunge hili na huo ndiyo mtazamo wa nchi. Mnamkaanga Profesa Assad anayeisaidia nchi hii kuokoa mabilioni na matrilioni ya fedha kwa sababu ametumia neno dhaifu. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, Hebu niulize...

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbowe kengele ilishagonga hapa.

MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, muda wangu walinipotezea sana.

NAIBU SPIKA: Mimi hapa mbele sina saa, saa iko kwa wataalam wangu na wanasema muda umekwisha.