Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Godfrey William Mgimwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalenga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia. Nitajikita zaidi kwenye Kamati yangu…

SPIKA: Dakika tano eeh.

MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nitajikita zaidi kwenye masuala ya UKIMWI kwa sababu na mimi pia ni Mjumbe wa Kamati hii ya UKIMWI. Nipongeze juhudi za Kamati ambazo zimefanyika, lakini vilevile nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri ambayo anaendelea kufanya kwa ajili ya Watanzania wote.

Mheshimiwa Spika, kwenye masuala ya UKIMWI lazima tufahamu kwamba, tatizo la UKIMWI ni kubwa katika nchi yetu, asilimia tano katika asilimia 100 ya Watanzania ndio wenye maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI, lakini tatizo tunalolipata ni bajeti ambayo tunakumbana nayo,
changamoto ya bajeti. Tumeshauri hapa kwenye Kamati kwamba, ufinyu wa bajeti sehemu kubwa au ni chanzo kikubwa sana cha kutoweza kuwafikia ndugu zetu ambao wana maambukizi ya virusi vya UKIMWI. Kwa hiyo, ingekuwa vizuri zaidi kwamba, Serikali tungeweza kujikita na kuzipeleka fedha, hasa fedha ambazo zinatoka Hazina kuelekea kwenye mifuko mbalimbali, hasa huu Mfuko wa TACAIDS ili tunapopeleka ujumbe wetu kwa ajili ya Watanzania na kuhakikisha kwamba, tatizo hili au ugonjwa huu wa UKIMWI unapungua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba, kuna mikanganyiko au mgongano kati ya Sheria ya UKIMWI na Sheria ya Ndoa, ambapo unakuta Sheria ya UKIMWI inamtaka mtoto mwenye miaka 15 aweze kuambatana na mzazi kwenda kupima, lakini Sheria ya Ndoa inasema mtoto mwenye miaka 14 kwa ridhaa ya mzazi anaweza akaolewa. Sasa ina maana mtoto huyu mwenye miaka 14 ameshaolewa, lakini vilevile arudi tena kwenda kupima akiwa na mzazi wake. Hilo jambo linaleta mkanganyiko kidogo, kwa hiyo, Sheria ya UKIMWI tuiangalie inavyokinzana na Sheria ya Ndoa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile kuna tatizo la takwimu. Kuna takwimu ambazo zinatolewa na NBS, kuna takwimu ambazo zinatolewa na TACAIDS, takwimu nyingine zinatolewa na wadau mbalimbali wa huko nje ya nchi, Ulaya na kadhalika ambao wanatoa fedha kwa ajili ya kuendelea kusaidia changamoto ya maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI. Kwa hiyo, niseme tu kwamba, ni vyema sasa ifike wakati hizi changamoto ziweze kupungua, ili kwamba, tunapopeleka takwimu tuweze kupeleka takwimu zinazoeleweka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna sehemu nyingine unakuta wanasema Nyanda za Juu Kusini, Mkoa wa Iringa tunaongoza kwa asilimia 13, takwimu nyingine zinasema 11, takwimu nyingine zinasema 10 kwa hiyo, kuna mkanganyiko namna hiyo. Kwa hiyo, lazima tupate takwimu ambazo zinaeleweka ili tuweze kuwaambia Watanzania ukubwa wa tatizo.

Mheshimiwa Spika, lingine nieleze, tatizo la UKIMWI ukubwa wake labda kwa takwimu tu, maambukizi kwa mwaka kwa Tanzania ni maambukizi 81,000. Ina maana kwa mwezi maambukizi ni 6,750 kwa wiki ni 1,687 kwa siku ni 241 na kwa saa ina maana ni watu 10 wanapata virusi vya ugonjwa wa UKIMWI kwa saa. Kwa hiyo, ukiangalia kwa upana wake na ufinyu wa bajeti ambao tunao bado tuko nyuma sana na tunahitaji tuweze kuweka mkazo ili changamoto hii iweze kupungua.

Mheshimiwa Spika, vilevile niseme tu kwamba, kwenye ule mkakati wa 90 90 90 ambao tunaenda nao mpaka mwaka 2020, ni kwamba, kwenye 90 ya kwanza Tanzania bado hatujafanya vizuri, tuko kwenye asilimia 52 ya malengo ya asilimia 90 ambapo hapa ndio kwenye changamoto kubwa ambapo watu wanashindwa kwenda kupima, hasa sisi wanaume tunakuwa wagumu sana kwenda kupima. Vilevile akinamama kwa sababu wanapata nafasi ya kwenda kupima wakiwa wajawazito, inaonesha kwamba, idadi ya akinamama ndio kubwa zaidi kwenye maambukizi, jambo ambalo inaweza ikawa lisiwe sahihi kwa sababu, wanaume tumekuwa ni wazito kidogo kwenda kupima. Kwa hiyo, changamoto hii lazima tui- address kwa wanaume pia kwamba, twende sasa tukapime kwa wingi. Nami Mbunge wa Kalenga nitakuwa miongoni mwa Wabunge wa kwanza kwenda kupima kuwaongoza Wabunge wengine wanaume katika majimbo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye 90 ya pili ni kwamba, kwenye masuala ya upatikanaji wa dawa; ni kweli kwamba, tuna tatizo, lakini kwa sasa hivi tatizo limeshapungua kwa kiasi kikubwa. Niishukuru Serikali kwa kazi nzuri.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda naomba niunge mkono hoja na nakushukuru sana. (Makofi)