Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Khatib Said Haji

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Konde

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. KHATIB S. HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uhai wake nikaweza kusimama hapa jioni hii ya leo.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuongelea suala la ugonjwa wa UKIMWI. Asubuhi hapa nilimsikia Mheshimiwa mmoja akiongea kwamba ishara za wafadhili zinazoonesha kusita kutoa misaada ambayo kwa kiasi kikubwa inatusaidia katika sekta hii ya kuwahudumia wenzetu wenye maradhi haya ni kiwango ambacho ni kikubwa sana, jambo ambalo mazingatio tunayopaswa kuwa nayo kwa sasa ni kuona umuhimu kama Taifa kuanza kuona jinsi gani ya kufanya kuweza kukabiliana na hali hii.

Mheshimiwa Spika, kila siku zinavyokwenda mbele masharti ya wahisani wetu yanazidi kuwa makubwa. Masharti yanapozidi kuwa mengi na makubwa na mengine yanakuwa hayatekelezeki, ni fundisho tosha la kutufundisha sisi kuona sasa kidogo tunachokipata kuangalia maeneo muhimu. Kati ya maeneo muhimu ni maeneo yanayogusa uhai wa watu moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo hili la wagonjwa wa UKIMWI ni eneo ambalo kwa kiasi fulani tumepata mafanikio ya kupunguza maambukizi mapya kutokana na msaada mkubwa wa kifedha ambao wahisani wetu walikuwa wanatusaidia. Kutokana na hii hali ambayo imeanza kuonekana, masharti kila yanavyozidi kuongezeka yanatishia juu ya fungu hili la kusaidia wenzetu ambapo hakuna anayejijua lini litamkuta hili.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kama kuna maeneo ambayo tunapaswa kuyazingatia sana ni kuangalia namna gani tutaweza kukabiliana na tishio la wafadhili wetu kuacha kutusaidia katika mambo mazito na muhimu ya uhai ya wananchi wetu na sisi wenyewe kwa ujumla. Kwa hiyo, angalizo langu ni kwamba aomba Serikali kupitia Wizara ya Afya, katika mipango yake, sasa ijielekeze zaidi kutathimini maeneo haya ambayo kwa kweli yanasononesha na yanatishia sana.

Mheshimiwa Spika, nataka niongelee suala la pili ambalo ni kuhusu Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo. Asubuhi ya leo niliuliza swali kuhusiana na namna Zanzibar tunavyonufaika na misaada kutoka FIFA.

Mheshimiwa Spika, kama unavyofahamu na wote tunafahamu kwamba Tanzania ni Taifa moja na masharti ya Taasisi zile, Shirikisho la Mpira Duniani, FIFA na CAF yote kati ya masharti yao ni kwamba hawatambui, hawawezi kupokea nchi mbili kuwa wanachama wa taasisi zile.

Mheshimiwa Spika, hili lilitokea mwanzoni mwa miaka miwili iliyopita pale Zanzibar ilipobahatika kujiunga na wanachama wa CAF kwa jitihada kubwa zilizofanywa na mapenzi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa kusaidiana na washirika wa kimichezo hadi kuifanikisha Zanzibar kuingia katika wananchanma wa CAF, lakini kwa bahati mbaya haikuchukua zaidi ya miezi minne Zanzibar ikaondolewa katika Uanachama ule kwa masharti yale kwamba haiwezekani Taifa moja likawa na wanachama wawili. Kwa hiyo, hayo ni masharti ya Katiba zao na sisi hatukuwa na la kufanya.

Mheshimiwa Spika, hapa ninaongelea ni kwamba, asubuhi jibu nililolipata ni kwamba ZFA ni sehemu ya TFF, siyo sahihi. Kama ni sahihi, naomba Mheshimiwa Waziri tafadhali aje aliweke sawa jambo hili nione uhalali wa jambo hili. Kwa sababu kama nilivyosema na narudia kusema, Wizara ya Habari na Michezo ya Tanzania ni Wizara inayohusika na upande mmoja wa Muungano, kama ilivyo Zanzibar, Wizara ya Habari na Michezo Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, TFF ni chombo cha mpira wa Tanzania Bara na Zanzibar iko ZFA. Kwa hiyo, linapokuja suala la misaada kutoka nje ya kimichezo kupitia FIFA, inapoingia TFF, kama kuna kilichowahi kwenda, basi ilikuwa ni huruma TFF. Hakuna mfumo maalum wa kuona upande wa Zanzibar ambaye siyo mwanachama wa FIFA wala CAF anafaidika vipi na fungu la mgao kutoka FIFA?

Mheshimiwa Spika, hili ni suala ambalo naiomba sana Serikali iliangalie kwa umakini tusije tukazalisha kero ya ovyo katika Muungano, kwa sababu masuala ya michezo ni sekta inayogusa vijana wengi; na kama tunaavyojua, vijana wana mihemuko mingi. Leo kuliacha jambo hili ambalo taarifa zipo; kwa mfano, sasa hivi tunatarajia kama hazijaingia, zitaingia muda wowote, 1.25 billion Dollar msaada wa FIFA kwa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, katika hili, kabla haujafika huo mgao, napenda kutoa mapendekezo yangu kwa Mheshimiwa Waziri, waangalie kupitia Wizara yake na Wizara ya Michezo ya Zanzibar, ni namna gani kale kasungura ka michezo ambako kanatolewa na FIFA kwa nchi ya Tanzania? Tanzania ikijijua ni nchi yenye Muungano wa mchi mbili vilevile, kwa hiyo, hili jambo liwekewe mfumo maalum ili Zanzibar tuone tunanufaika vipi kupitia FIFA.

Mheshimiwa Spika, hili ni jambo na ambalo limekuwa na malalamiko makubwa kwa upande wa Zanzibar. Kwa hiyo, ni vizuri sana kuzingatia moja kwa moja isiwe ni kwa bahati mbaya; leo ukiongelea habari ya msaada wa FIFA kwa Zanzibar siku zote jibu linakuja, “tulisaidia Uwanja wa Gombani kuweka nyasi.” Hilo tu! Kuweka nyasi Uwanja wa Gombani imekuwa ni slogan ya kuonesha kwamba ilitosha kwa Zanzibar kufaidika na misaada ya FIFA. Hiyo siyo sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tungeweka mfumo ambao hautakuwa na mgongano wa kujua katika kinachopatikana kutoka FIFA wao Zanzibar moja kwa moja kifungu chao at list kitakuwa ni hiki na tuondoe huu mgongano ambao sioni umuhimu wowote wa kuweza kufikia hali ya kuwekwa nayo kama ni kero ya Muungano. Nadhani hilo limeeleweka.

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho na la muhimu sana, hapa kuna jambo linazungumzwa, lakini mara nyingi Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakilizungumza kana kwamba ni jambo la utani na ni jambo ambalo linachukuliwa kwa utani.

Mheshimiwa Spika, suala hili la tohara kwa wanaume, nilivyomsikia mchangiaji leo akisema madhara yanayopatikana kufikia kansa, siyo jambo la kulichukulia utani tena, ni jambo serious kwamba kwa sababu hilo jambo linagusa kila maisha ya mwanadamu, siyo jambo la kusema hapa tukawa tunacheka. Kama leo kuna ugonjwa, nilidhani labda ni kupunguza chachu ya mambo fulani, lakini sasa kuna gonjwa la hatari la kansa ambalo linapatikana kutokana na wanaume ambao hawajafanyiwa tohara. Hilo siyo jambo la utani tena. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ingekuwa ushauri wangu, akina mama wa Tanzania wananisikiliza, ningewaambia wawagomee wanaume wowote ambao bado hawajakubali kufanyiwa tohara. Wawagomee kabisa, wawaambie bila tohara hilo jambo haiwezekani, no! Kwa sababu leo unaenda kumwoa mke...

SPIKA: Mheshimiwa Khatib siyo fitina hiyo! (Kicheko)

MHE. KHATIB S. HAJI: Mheshimiwa Spika, hapana. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, siyo fitina kwa sababu leo mtu anaenda kuoa mke, kesho amegombana, anamuacha; wewe unaenda kuoa tena; kumbe yeye alikuwa na tatizo hilo kutokana na maradhi ya kujitakia.

Mheshimiwa Spika, mara nyingi nimewaambia wanaume ambao bado na tatizo hilo, tuulizeni tunafaidika vipi sisi ambao tulibahatika mwanzo kujaliwa kuwa na tohara? Leo nimekuja siyo faida pekee, bali ni madhara makubwa ambayo yanatokea kiasi cha kuwapatia ndugu zetu kansa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tusichukulie utani. Kama kuna ugonjwa mkubwa ambao dada yangu asubuhi ameutaja pale, hili jambo lazima tuwe serious kuona kwamba hili suala ni muhimu kwa tohara ya wanaume wote.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nasema ahsante sana, nashukuru sana. (Makofi)