Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kuridhia Ubadilishaji Hadhi Mapori ya Akiba ya Biharamulo, Burigi, Kimisi, Ibanda na Rumanyika – Orugundu kuwa Hifadhi za Taifa

Hon. Rev. Peter Simon Msigwa

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Iringa Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kuridhia Ubadilishaji Hadhi Mapori ya Akiba ya Biharamulo, Burigi, Kimisi, Ibanda na Rumanyika – Orugundu kuwa Hifadhi za Taifa

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Dhana nzima ya uhifadhi wa mazingira yaani Flora pamoja na Fauna wote kama Watanzania tunapenda sana, lakini masuala kadhaa katika mambo ambayo nimeyazungumza muda uliopita ni lazima kama Taifa tuwe tumejiuliza na kujihoji.

Mheshimiwa Spika, Serikali yetu imekuwa na mipango mingi sana na hasa Wizara hii, lakini kuna wakati mwingine mipango hii huwa haifiki mwisho. Kupandisha hadhi mapori ni jambo jema, lakini kabla hatujapandisha ni lazima tujihoji masuala ya msingi sana. Ni kweli kama wenzangu ambao tuko nao kwenye Kamati wamepongeza utendaji mzuri sana wa TANAPA, namna ya uhifadhi na kwa kweli TANAPA wanafanya kazi kubwa sana ya uhifadhi na kama Bunge tunapaswa tuendelee kuwaunga mkono, lakini bado nauliza swali lile lile ambalo wenzangu wameuliza.

Mheshimiwa Spika, TANAPA tunazidi kuiongezea mzigo kwa sababu haya mapori yalikuwa TAWA, TAWA tumeipa mamlaka, sasa TANAPA ambayo ni hifadhi zake tano tu ambazo zinaendesha hifadhi zingine 11. Swali ambalo tunapaswa kujiuliza kama Serikali na kama Taifa; pamoja na kwamba tunaongeza hizi hifadhi lakini lazima tuwe na mikakati ambayo itasababisha hifadhi hizi ziweze ku-generate income. Kama TANAPA ina hifadhi tano zinaendesha hifadhi 11 ni dhahiri kwamba mapato mengi ambayo yangeweza kuleta shughuli nyingine za kimaendeleo tunajikuta yanakwenda kuendeleza hifadhi zingine.

Mheshimiwa Spika, sasa niombe Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa ajaribu kutupa picha ni namna gani hizi hifadhi zingine ambazo hazija-break even kwa muda mrefu, ni nini mkakati za Wizara kwa hizi hifadhi zingine 11, time limit ni kwa kiwango gani hizi hifadhi zitaendelea kuwa tegemezi kwa hifadhi zingine au tutaendelea kuchukua kiwango kile kinachopatikana kwenye hifadhi zingine na kuendelea kutunzwa kwenye maeneo mengine. Hili ni jambo ambalo tunapaswa tujiulize kabla ya kwenda haraka haraka kufanya maamuzi tunayokwenda kuyafanya.

Mheshimiwa Spika, jambo kubwa ambalo tunapaswa tujiulize; kwenye Bunge la Bajeti Mheshimiwa Waziri alikuja hapa na tukapanga mipango mizuri sana ya kukuza utalii Kusini mwa Tanzania na mipango ilikuwa mizuri sana, Serikali ikaenda World Bank ikakopa pesa Dola bilioni 150 kuhakikisha maeneo ya Mikumi, Ruaha, Selou yote tunaiimarisha ili tukuze utalii upande wa Kusini. Ni maeneo machache tu, lakini kabla kabla hatuja-take off tumeanza tena maeneo mengine. Tunapenda Tanzania tuiunganishe yote kwa pamoja, lakini hatuwezi kufukuza sungura wawili kwa wakati mmoja. Waziri hajatoa maelezo ya kina ni kwa kiwango gani REGROW inaendelea mpaka sasa.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema tuna taarifa kwamba World Bank wame-pool out kwa sababu Serikali haiku consistency kwenye maamuzi yake. Wananchi wa Kusini wametutamanisha, wametupa imani, wakazi wangu wa Manispaa ya Iringa walikuwa na matumaini makubwa kwamba tunakwenda kuinua utalii sasa, wakazi wa Mbeya, wakazi wa Mikumi, hata Selou waliaminisha Taifa hili. Nakuwa na wasiwasi isije ikawa kama wakati ule wa gesi watu waliimba hapa gesi, gesi, gesi, gesi ikaenda, baada ya muda ikapotea tena.

Mheshimiwa Spika, napata tabu kwamba inaonekana hata hii REGROW inaweza ikawa kiini macho. Nimwombe Mheshimiwa Waziri atupe maelezo ya kina ni kwa kiwango gani na kwa namna gani kuboresha Southern Circuit. Haitaathirika na mipango mingine sasa tunayokwenda tena upande mwingine kabla huku hatujamaliza. Serikali ya Chama cha Mapinduzi imekuwa ni bingwa sana wa kuanzisha miradi na kuachia njiani kama ambavyo wanataka kufanya sasa hivi. Uwanja wa Nduli kwa mfano pamoja na kuongeza runway lakini bado tunahitaji kuwa na jengo la wageni, la wasafiri hatujaimarisha, bado tunahitaji kuwa na barabara kutoka Iringa Mjini kwenda Ruaha National Park. Wajumbe wa Kamati wataniambia ni tabu kweli kweli kusafiri kutoka Iringa Mjini kilomita 104 kutoka Iringa Mjini kwenda Ruaha National Park, haya mambo hayajafanyika.

Mheshimiwa Spika, tulizungumza mradi huu ulikuwa ukatengeneze barabara nzuri za kwenda Selous kwenye mahoteli na hela tumeshapata. Tumeanza ku-service mkopo, lakini sasa ghafla tumeongeza mambo mengine ambayo wakati bado hatujaimarisha. Niseme siwezi kusema naunga au napinga, lakini kuna maswali mengi yanaleta ukakasi, kwa nini hili jambo lije kwa haraka na haya mapori tunayo?

Mheshimiwa Spika, jambo lingine; wenzangu wanasema itasaidia kupunguza migogoro. Wote hapa ni mashahidi zimetokea kampeni mbalimbali mara tokomeza, mara nyingi, kugombana na wananchi, wafugaji hasa wanapoingia kwenye hifadhi na tumekuwa tukii-task Serikali kwamba lazima itenge maeneo ya wafugaji na uhifadhi. Sasa leo watu wanasema kwa kuongezewa hifadhi tutapunguza migogoro, sasa hii migogoro mingine yote iliyoko kwenye hifadhi imetokana na nini? Kwa sababu wananchi huwa wana-intrude kwenye maeneo ya hifadhi. Sasa ni kwa kiwango gani Serikali imeweka utaratibu ambao hatutaingia kwenye matatizo kwa sababu hifadhi zote za nchi hii ukienda karibu zote kuna ugomvi kati ya wafugaji na wahifadhi, kuna watu wanavamia maeneo ya uhifadhi.

Mheshimiwa Spika, sasa tusije tukawa tunakuja hapa kwa haraka haraka, halafu baadae tena tukaingia kwenye shida ambayo kimsingi tusipofanya vizuri tunaingiza gharama kwa TANAPA yenyewe kuijendesha, kwa sababu kwanza itaanza kugombana tena na watu. Tunaifanya TANAPA iwe adui kwa wananchi kwa sababu hatujapanga mipango vizuri. Watu wakiona magari ya TANAPA wanawachukia, watu wakiona mavazi ya TANAPA wanawachukia kwa sababu wanaona kama wanaumiza, wakati tulitakiwa tuweke utaratibu mzuri wananchi waone faida ya uhifadhi huu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo naomba Mheshimiwa Waziri lazima atuambie ni namna gani mpango huu hautaathiri mpango mzuri ambao umeanza upande wa Kusini. Kusini kuna maeneo, isiwe sifa tu kwamba Ruaha ni kubwa lakini uwekezaji mdogo. Naamini tukienda huku
TANAPA sasa, watahamisha pesa nyingi sana kuanza kubeba mzigo mkubwa huu wa Magharibi wakati Kusini hatuja-take off, hatuja-take off kwenye miundombinu, hatuja-take off kwenye mambo ya mahoteli, mambo ya customer service, mabo ya customer care, hospitality kwa ujumla iko chini, badala hizi pesa tungeweka kwenye vitu vya msingi ambavyo vingesababisha vitu vya juu vijichukulie vyenyewe, tunaongeza mzigo mkubwa.

Mheshimiwa Spika, nadhani kama Bunge kwa pamoja tungetafakari tusifanye haya mambo kishabiki, wote tunahitaji maendeleo, tunahitaji uhifadhi kama nilivyosema, siko kinyume na uhifadhi kabisa, lakini kama Taifa na kwa pamoja tunatakiwa haya masuala tuyaangalie wka upana, tuone yataleta tija gani. Kwa hiyo kwa ujumla, sikatai au siungi mkono ila nataka kwanza wote tutafakari kwa ujumla tuone ina tija gani hasa kwa kuzingatia REGROW naomba nipate majibu ya Mheshimiwa Waziri ili niweze kuwa comfortable kama mwakilishi wa Kusini. Ahsante sana. (Makofi)