Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kuridhia Ubadilishaji Hadhi Mapori ya Akiba ya Biharamulo, Burigi, Kimisi, Ibanda na Rumanyika – Orugundu kuwa Hifadhi za Taifa

Hon. Risala Said Kabongo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kuridhia Ubadilishaji Hadhi Mapori ya Akiba ya Biharamulo, Burigi, Kimisi, Ibanda na Rumanyika – Orugundu kuwa Hifadhi za Taifa

MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika hii mada muhimu iliyoko mezani. Hoja ya kupandisha hadhi Mapori ya Akiba ya Biharamulo, Burigi, Kimisi, Ibanda na Rumanyika, Orugundu kuwa Hifadhi za Taifa ndiyo hoja ambayo tumekuwa kukiijadili muda mrefu katika Kamati yetu ya Maliasili na Utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikiri tu kuwa mimi ni Mjumbe wa Kamati hiyo na kwamba nichukue fursa hii kipekee kumpongeza sana, Mkurugenzi wa Hifadhi za Taifa TANAPA, Ndugu Allan Kijazi pamoja na timu yake kwa kuendelea kusimamia maeneo ya Hifadhi za Taifa TANAPA, yenye hifadhi 16, mapori ya akiba 28, mapori tengefu 42 yanayosimamiwa na TAWA. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mapori ya Akiba yanayopandishwa hadhi ni miongoni mwa mapori 42 yanayosimamiwa na TAWA. Kumekuwepo na jitihada mbalimbali za kukabiliana na changamoto za ujangili wa mapori kwenye maeneo yanayopakana na mapori ya akiba. Maeneo mengine yanayokuwa na changamoto ni sehemu ya ujambazi ambao umekithiri maeneo ya mipakani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, changamoto nyingine ni uvuvi haramu ambao umekuwa ukikabili mapori haya na uingizaji wa silaha za kivita ambazo pia zimekuwa zikiingizwa kupitia kwenye mipaka ya mapori haya. Kumekuwa na malengo mbalimbali ambayo yamesababisha kupandisha mapori haya kuwa hifadhi za Taifa. Malengo hayo ni pamoja na kuimarisha uhifadhi wa maliasili kama tulivyoona kwenye Kamati yetu, hususani pia wanyama pori, mimea adimu, mazalia ya samaki, viumbe wengine na ndege wa aina mbalimbali ikiwemo korongonyangu.

Mheshimiwa Spika, kuimarisha ulinzi wa mipaka yetu imekuwa ni hoja muhimu pia ya kufanya maporo haya kupandishwa hadhi. Sambamba na hilo ni kuimarisha mifumo ya kisheria ambayo itakwenda kusimamiwa na hifadhi za Taifa TANAPA. Vilevile kuongeza pato la Taifa kupitai shughuli za utalii ambazo zitakwenda kuendeshwa katika ukanda wa hifadhi za Magharibi. Kwa kuwa shughuli za kijamii hazitaruhusiwa kuendeshwa katika mapori haya wakati eneo hili linapandishwa kuwa Hifadhi za Taifa, napenda kushauri masuala yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa hii inaweza kupelekea kuendelea kuwa na migogoro mingi ambayo imekuwa ikitokea katika maeneo mengine kama haya, wananchi wa maeneo haya ambao ni wafugaji kulingana na Sheria za Hifadhi hawataruhusiwa kuendelea kufanya shughuli za kijamii kama kufuga, kuokota kumi na kuvua samaki. Hivyo, sambamba na kupandisha hifadhi hizi, mapori haya ningependa kushauri mambo yafuatayo ili Serikali iweze kuyatekeleza:-

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa sasa hii ni fursa ya miji ya jirani kama Geita, Biharamulo, Bukoba na Ukerewe, napenda kushauri kuweko na mikakati ya kuendeleza miji hii. Hivyo, viwango vya utoaji huduma viwe vinakidhi mahitaji ya soko la utalii ili kuwezesha wananchi wanaopakana na Mikoa ile kuweza kufaidika na hili suala la upandishaji hadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala langu la pili ningependa kushauri Serikali ijenge mazingira kuiwezesha TANAPA kuyaendeleza mapori haya yatakayopandishwa hadhi. Suala la tatu, napenda kuishauri Serikali kusaidia miundombinu ya kufika hifadhi, iboreshwe. Suala la nne, naomba Serikali isaidie kuondokana na urasimu wa kutoa misamaha ya kodi kwa wafadhili wanaotoa pesa kusaidia maeneo hayo, hasa kwenye suala la miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda pia kushauri Serikali kuwe na bajeti ya kutosha kusaidia shughuli za uendeshaji kwa kuwa mpaka sasa kati ya Hifadhi 16 za Taifa ni hifadhi tano tu ambazo zinajiendesha zenyewe, hifadhi nyingine zote ni tegemezi. Kwa hiyo, kwa kuwa tunaenda kwenye kipindi cha bajeti, kuwe na bajeti ya kutosha kusaidia hifadhi hizi kujiendesha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali ione kuna haja sasa ya kufanya Wizara ya Maliasili na Utalii kuwa ni kipaumbele cha Taifa kwa kuwa Wizara hii sasa imekuwa ikichangia pato kubwa la Taifa na kwamba ni miongoni mwa Wizara zinazoingizia pato kubwa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, kwa kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja hii ya kupandisha hifadhi hizi za Magharibi kuwa na hadhi ya TANAPA kwa kuwa kupandisha hadhi hifadhi hizi zitaisaidia sana wananchi wanaozunguka maeneo haya ya Magharibi kuendelea kiuchumi, lakini pia kusaidia mipaka yetu ambayo inayozunguka nchi jirani. Vile vile, kama tulivyoona, itasaidia ulinzi katika nchi yetu na kuzuia migogoro mingi ambayo inatokana na nchi zinazozunguka katika hifadhi zetu.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)