Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, awali ya yote, naomba nichukue nafasi hii kukushukuru kwanza kwa kunipa hii nafasi, lakini nichukue nafasi hii pia kuwashukuru Wabunge wote ambao kwa namna moja ama nyingine mmechangia katika taarifa ya Kamati hii. Pia naomba niunge mkono taarifa ya Kamati zote mbili, lakini kipekee niwapongeze Wajumbe wa Kamati ya Kilimo. Ripoti yao imesheheni mambo mengi mazuri na ya msingi sana ambayo sisi kama Serikali tutayafanyia kazi na tutaona namna ya kuweza kushirikiana na Waheshimiwa Wabunge hawa ili tuweze kufikia hii azma ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee namshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na Viongozi wengine wote Wakuu pamoja na Mawaziri kwa kuendelea kukiunga mkono kilimo cha nchi hii. Hapa Waheshimiwa Wabunge wote naomba mniunge mkono kwa sababu ningi wote ni wadau wa kilimo. Kama muda ungetosha, najua mngepata nafasi ya kuzungumza. Wote hapa ni wadau wa kilimo, wote hapa tumekula chakula ndiyo maana tunaongea. Kwa hiyo, wote kwa namna moja ama nyingine ni wadau wa kilimo.

Mheshimiwa Spika, hoja nyingi zimetolewa, lakini naomba nianze kwa hoja chache, bahati mbaya naona Mheshimiwa Zitto hayupo, lakini naomba nianze na hii hoja yake. Hoja ya kwanza ambayo ameisema, ni kuhusu chanzo cha fedha ambacho Benki yetu ya Kilimo imepata, labda naomba niweke takwimu vizuri, siku fulani hapo juzi nilisema, Benki yoyote duniani inayoitwa Benki ya Biashara, benki yoyote inategemea mitaji yake katika maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, kuna mtaji unaowekeza na wenye hisa na ukiangalia mtaji wa wenye hisa, ni mtaji ambao unawekezwa na ule mara nyingi ni kwa sababu ya taratibu za kibenki inakuwa kama dhamana; na mara nyingi unawekwa Benki Kuu. Benki baada ya kuanzishwa, iki-comply na zile taratibu za kuanzishwa, inatakiwa itafute fedha mahali popote zilipo nyingi ilete iweke na ipeleke mahali zinapotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitoe mfano, nianze na CRDB. Ukichukua mtaji wa CRDB wa wenye hisa, ni shilingi bilioni 65,296; lakini angalia mali walizonazo, wana mali zaidi ya shilingi trilioni 6,038,571. Wana shilingi trilioni sita, mtaji shilingi bilioni 65. Kwa hiyo, pale siyo kwamba wanafanya biashara kwa kutumia hela za mtaji, kazi yao ni ku mobilize fedha kutoka ziliko, wanakuja kufanya biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukichukua NMB, wana mtaji wa shilingi bilioni 20, lakini angalia mali zao walizonazo; asset za NMB ni zaidi ya shilingi trilioni tano. Ni shilingi trilioni 5,706,110. Kwa hiyo, ina maana hawa wanafanya kazi ya biashara. Vivyo hivyo Benki yetu ya Kilimo, ina mtaji mkubwa kuliko hata NMB. Benki yetu Serikali iliwekeza shilingi bilioni 60, nayo inaendelea kufanya kazi na kutafuta fedha na kuendesha na tunataka hii benki iendelee kutoa mikopo kwa wakulima wa nchi hii ili kilimo kiweze kusonga mbele.

MBUNGE FULANI: Shule hiyo!

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kwa kuanzia ndiyo maana benki hii imetafuta fedha. Ilikopata mimi sijui, imetafuta. Ninachokijua, wametoa fedha kwenye Bodi yetu ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko. Wametoa mkopo; na mkopo lazima ulipwe. Bodi yetu inalipa. Tumekopa Benki ya Kilimo ambayo kazi yake ni kufanya biashara.

Mheshimiwa Spika, nataka niseme kwamba kazi yetu sisi ni kukopa na hiyo Bodi yetu ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko imekopa, inaendelea kukopa, inafanya biashara, imenunua korosho, kazi yake ni kununua, kuchakata na kwenda kuziuza hizo korosho. Hiyo tutaifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu nilotaka kulizungumzia na bahati nzuri amesema Mheshimiwa Zitto na Waheshimiwa Wabunge wengine wamechangia, naomba niseme, Serikali yoyote duniani iko pale kwa mujibu wa Katiba na kwa mujibu wa sheria.

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, tusikilizane. Hii ni shule, msikilize vizuri. (Makofi)

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kazi ya Bunge ni kutunga sheria. Sheria hizo zikishatungwa, kazi ya Serikali ni kuzitekeleza hizo sheria. Sasa mwaka 2009, Bunge lako Tukufu lilitunga sheria inayohusu Zao la Korosho. Ilipotunga sheria, iliweka vifungu mbalimbali. Kwa sababu ya muda, naomba niweke vizuri ili tuelewane. Ukisoma hiyo Sheria ya Bodi ya Korosho, Kifungu cha 12 (1) kinasema hivi: “every cashew nut dealer, being a buyer, processor, importer, exporter, wherehouse owner or operator shall be required to register with the Board.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mtu yeyote anayegusa, anayeshughulika na korosho kwa namna yoyote ile, lazima kwanza aandikishwe na Bodi. Ukisoma Kifungu cha 15(4) kinasema hivi: “a person shall not buy,” naomba Mheshimiwa Zitto uishike vizuri. “A person shall not buy, sell, process, own or operate a wherehouse or exports any cashew nuts on commercial basis without a licence issued by the Board.” Huu ndiyo msingi ambao tunautumia sisi kusimamia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, unapokuja na hoja unasema sijui kuna Kangomba sijui wafanye nini, mwaruhusu, kazi yako ya kwanza kama Mbunge, itisha turekebishe hii sheria. Kama hatujarekebisha, sitaisimamia hii. Kama unataka korosho zinazotoka nje, zinazotoka popote zije, zifuate utaratibu ulioandikwa kwenye sheria. Kwa hiyo, huo ndiyo msimamo ambao sisi kama Serikali tutaendelea kuusimamia na tutaendelea kuhakikisha kwamba haya yote yanazingatiwa.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumzia kuhusu kilimo, nami nakubaliana kabisa. Zipo hoja za msingi mlizosema namna ya kuboresha kilimo chetu. Kilimo chetu hiki ili tuweze kukiboresha vizuri, jambo la kwanza ambalo lazima tuangalie ni mifumo yetu ya pembejeo nchini. Hilo nakubaliana na Kamati imetoa maoni, imeshauri, tutayafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, inaendana na tija; ni ukweli usiofichika. Kwenye kilimo chetu, tija bado iko chini. Ukiangalia tija bado iko chini; ukiangalia upatikanaji wa mbegu bora, bado hata hatujakaa vizuri. Hili ndiyo suala tunalolifanyia kazi. Pembejeo viuatilifu na madawa mengine hivi vyote ndiyo msingi, lakini pia kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, watu wetu katika maeneo mengi, ukiangalia mashamba tunayolima yaliyo mengi, uzalishaji wake uko chini, tija iko chini, ndiyo maana tunaona kuna hasara. Kazi yetu kama Wizara, ni kuhakikisha kwamba tunafanya utafiti wa kutosha.

Mheshimiwa Spika, labda niliseme hili, wengi wamesema kwa mfano kuhusu mbolea, nami nakubaliana. Wengi wanasema kuhusu pembejeo, lakini kazi ya kwanza ambayo tunatakiwa tuifanye na ambayo sasa tunaifanya, naomba niliambie Bunge lako hili, ni kufanya utafiti wa ardhi yote ya nchi hii ya kilimo ili kuiona ina virutubisho gani? Ina kitu gani kinachokosekana ili tujue aina sahihi ya pembejeo zinazohitajika kwenye lile eneo. Siyo suala la ku-apply tu mbolea, ni suala la lazima kufanyike utafiti.

Mheshimiwa Spika, Kituo chetu cha Mlingano kile cha Tanga karibu kinakamilisha hiyo kazi ya kufanya mapping. Tukishajua hilo, tutajua aina ya mbolea inayotakiwa, tutajua kumbe inawezekana siyo hiyo CAN tunayoisoma au siyo DAP. Lazima tuangalie ni madini gani yanakosekana pale, ndiyo tutengeneze, ndiyo tulete hiyo mbolea.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, mtazamo wa mbolea sasa hivi ndiyo ulioharibu ardhi kwa kiwango kikubwa katika nchi yetu. Sasa hivi wataalam wanasema, inawezekana tukifanya utafiti tutahitaji kuzalisha chokaa ya kutosha ambayo iko nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwapongeze, Dodoma kuna kiwanda kinazalisha chokaa. Ile chokaa tungekuwa na uwezo, baada ya kufanya utafiti wa ardhi yetu, tukaenda tukaitumia kwenye mashamba yetu, tusingehitaji kutumia mbolea hata siku moja. Kwa sababu kutumia mbolea maana yake nini? Ukisoma ile mbolea ni sulpher sijui nitrogen; ni madini yaliyokosekana kwenye ardhi.

Mheshimiwa Spika, maana yake nini? Maana yake uchachu (acid) uko juu. Sasa ili kuupunguza uchachu, unahitaji alkaline. Kwa sababu unahitaji alkaline, ile lime ndiyo inaweza ikapunguza hicho kitu chote kikapotea. Kwa kwa mantiki hiyo, inawezekana tusihitaji kabisa hizo mbolea, tutaweka mkazo katika kuhakikisha hiki kiwanda kinazalisha chokaa ya kutosha na tutoe elimu kwa wananchi ili waweze kuanza kujua kutumia chokaa badala ya kufikiria tu kununua mbolea.

Mheshimiwa Spika, nakubaliana kwamba kilimo ndiyo kitatoa mchango mkubwa kwenye viwanda vyetu ambavyo tunasema, nasi kama Serikali tutaendelea kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha kwamba viwanda vyetu vinapata malighafi. Sote tunajua, viwanda vyetu vinategemea asilimia 66.5 ya malighafi zinazotokana na kilimo.

Mheshimiwa Spika, kazi yetu sisi sasa Wizara ya Kilimo ni kukaa na wenzetu wa Viwanda ili watuambie ni aina gani ya malighafi wanaihitaji yenye ubora wa kiwango gani kusudi tuhamasishe uzalishaji unaoendana na mahitaji ya soko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakubaliana na wale wote waliosema kuhusu masoko, siku za nyuma hatukuweka mkazo wa kutosha, hatukuweka msisitizo wa kutosha kwenye upande wa masoko, na hapa ndiyo tatizo. Wananchi wengi walikuwa wanazalisha mazao lakini walikuwa hawajui wapi kwa kuuza. Ndiyo maana kama Wizara kwa kushirikiana na Wizara na taasisi nyingine sasa hivi tumeweka mkazo kwamba lazima suala la masoko lipewe kipaumbele ili kujua masoko ya kila zao yako wapi na wananchi wanapoambiwa kuzalisha basi tuwaambie hili soko liko huku na bei zake ziko hivi. Hiyo tutakuwa tayari tume-link pamoja uzalishaji na masoko yaliyoko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimesikitika mdogo wangu Mheshimiwa Haonga anaposema hatujashughulikia mazao, tumeshughulikia mazao yote. Tulipoingia tumesaini mkataba mkubwa wa tani 36,000 ambapo Mheshimiwa Rais wetu ameshuhudia wa kununua mahindi ambapo WFP wamenunua; lile lote ni soko la mahindi. Unaposema kwamba eti hatujashughulikia utakuwa unazungumza vitu vya ajabu. Wizara kila mahali tunatafuta masoko, sasa hivi tumepata soko DRC lakini tumepata vikwazo mahali pa kupitisha kule nchini Zambia ambapo tunaendelea na mazungumzo ili kusudi watu wetu waende kuuza kule nchini Kongo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wamezungumzia Tume ya Ushirika kwamba inawafanya kazi wachache, haina uwezo, nakubali kweli wafanyakazi ni wachache na kazi yetu kubwa ni kuijengea uwezo Tume ya Ushirika ili iweze kufanya kazi iliyokusudiwa kwasababu ndiyo tarajio la wakulima wengi wa nchi hii na ndiyo njia pekee ya kuweza kutatua changamoto zao mbalimbali. Haya matatizo tunayozungumzia kwenye mfumo wa usambazaji wa pembejeo na mambo mengine ni kwa sababu ushirika wetu haujasimama imara. Ni imani yetu tukiusimamisha vizuri haya mambo yatapungua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo basi, mwaka huu tunategemea kama mambo yataenda kama tulivyopanga tutapata watu 86 ambao tutawaajiri kule kwenye ushirika. Hata hivyo, bado tunaendelea kushauriana na TAMISEMI ili wale wanaushirika walioko chini ya TAMISEMI waweze kuhamishiwa kwetu kusudi waweze kufanya kazi za ushirika.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Waziri.

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru lakini kama zitahitajika taarifa zaidi tuko tayari kutoa taarifa ili Bunge lako liweze kujua na takwimu nyingi bado tunazo. Nakushukuru sana kwa nafasi. (Makofi)