Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Rev. Peter Simon Msigwa

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Iringa Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nijaribu kutoa maoni yangu kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania siyo kisiwa. Tanzania ni miongoni mwa nchi nyingi zilizoko duniani na kwa kuwa Tanzania siyo kisiwa kwa hiyo ni taifa ambalo tunategemeana na mataifa mengine. Muda siyo mrefu sana na miaka ya nyuma kama Wabunge na kama Kambi ya Upinzani tumetoa ushauri mwingi sana, sana, sana hasa kwa Mheshimiwa Mpango. Kabla sijaendelea kuchangia nilitaka nipate majibu kwa sehemu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujua Mheshimiwa Mpango, tumekuwa tukiambiwa mara kwa mara kwamba uchumi unakua, ukiangalia exchange rate kwa sasa hivi (ukwasi) kati ya Shilingi na Dola, ameondoka Mheshimiwa JK hapa Dola moja tunalipa kwa Sh.1,600 na tukawa tunakusanya shilingi bilioni 800 lakini leo tunaambiwa uchumi umekua makusanyo yako shilingi trilioni 1.3 mpaka 1.4 lakini exchange rate kwa mfano jana ilifika mpaka Sh.2,400. Hii inamaanisha nini katika masuala ya uchumi wakati tunambiwa uchumi unakua?

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwenye masuala ya mapato, tumeambiwa mapato tunakusanya sana na suala la GDP kwamba linaongezeka. Nilitaka nijiulize au tujiulize wote kwa pamoja tunapojadili haya masuala, masuala ya revenue, ni kweli hiki tunachokusanya ni revenue kwa wafanyabiashara wetu? Vyanzo vya mapato ni vipi ambavyo tunakusanya hii pesa? Au tunakusanya tozo na faini? Kwa sababu kuna uwezekano mkubwa…

T A A R I F A

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujua Mheshimiwa Waziri haya mapato tunayoyakusanya ni tozo au kweli ni vyanzo vya biashara tulivyonavyo? Kwa sababu takwimu zinazoonyesha kwamba biashara nyingi katika nchi yetu zinafungwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi navyozungumza kwa mfano Arusha Mjini kuna watu zaidi ya 650 wanafunga biashara, hawafanyi biashara. Sasa hizi tunazitegemea ni tozo au ni revenues na ni sustainable kwa siku zinazokuja au tunapiga kelele tu kwamba uchumi unakua? Mnatoza faini nyingi kwa wavuvi halafu tunasema tunakusanya kodi, hivi ni vitu ambavyo siyo sustainable. Lazima haya mambo tutafakari kama Wabunge na kama Silinde alivyosema tusiletewe taarifa ambazo ni za kubumba hazitusaidii kama Taifa ili tuweze kulishauri Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ni kweli uchumi unakua? Hilo ndiyo suala la kujiuliza. Kwa nini kuna tofauti kati ya economic growth na development growth? Kwa sababu kama kuna economic growth tungeona development growth inakuwa reflected lakini katika maisha ya watu hatuoni hayo mabadiliko pamoja na pambio na nyimbo nyingi za kwamba uchumi unakua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbona vyumba vya madarasa mashuleni hakuna kama uchumi unakua? Sasa hivi tunahangaika kwenye Halmashauri zetu vyumba vya madarasa tunashindwa kupeleka watoto kama huo uchumi unakua kwa nini hatupeleki hizo pesa? Kwa nini huduma za afya zinadidimia kama uchumi unakua? Haya ni mambo ambayo yanatugusa moja kwa moja. Kwa nini matatizo ya maji yameendelea kuwepo kama uchumi unakua? Haya masuala lazima tujiulize kama wawakilishi wa wananchi. Uchumi unakua kwenye makaratasi lakini kwenye mazingira ya uhalisia hauonekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la lingine tunaambiwa kwamba uchumi unakua kama ambavyo nimesema Mheshimiwa Mpango tumemshauri sana miaka iliyopita, twende kwenye Halmashauri zetu ndugu zangu Wabunge sijui wengine, mimi kwenye Halmashauri yangu ya Iringa pesa inayokuja ni ile ya kusukumasukuma elimu bure lakini pesa zote za maendeleo hazirudi. Mheshimiwa Mpango tulikukataza hapa usichukue mabango tuliyokuwa tunayategemea kwenye Halmashauri, tulikukataza hapa usichukue property tax, mlisema hapa kwa mbwembwe nyingi kwamba tunachukua vyanzo vya mapato, property tax, mlisema mnachukua mabango, mkasema hiyo hela itakuwa inarudi saa hizi hamjarudisha hiyo hela. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, TRA tuliwaambia hapa hata mimi nilisema hawana capacity ya kukusanya hizo pesa, hawawezi kukusanya pesa, hela hairudi, mmerudisha mara moja. Haya ni mambo tunatakiwa tujadiliane sasa huo uchumi unakuaje na hiyo hela hamrudishi kule? Utaratibu huu una-cripple D by D, Halmashauri zinashindwa kujiendesha halafu tunafichama hapa tunapongezana pongezana kitu gani? Huo uchumi unaokua unakuaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema mwanzoni kwamba sisi siyo kisiwa tunahitajiana duniani. Haya yote tunayapata ni kwa sababu tumeshindwa kuwa na mahusiano ya kimataifa. Haya ni matokeo ya kutokuwa na mahusiano mazuri, diplomacy yetu imeporomoka kwa kiwango kikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti yetu ya Taifa asilimia 40 tumetegemea wafadhili ambao mara nyingi kwenye chama chenu na kwenye tv yenu mmekuwa mkiwabeza, mkiwaita mabeberu lakini asilimia 40 ya bajeti yetu tunategemea mabeberu. Jambo analolifanya Mheshimiwa Rais la kusema tujitegemee ni jambo jema lakini tunajitegemeaje? Tunajitegemeaje wakati muda wote tumekuwa tukiwatukana na kuwakebehi wafadhili.

T A A R I F A

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, donors wetu ambao toka tumepata uhuru nchi za Ulaya zimetusaidia sana katika maeneo mbalimbali ya elimu, afya ambao kwa sasa hivi wametoa masharti kwamba nchi yetu haina masuala ya kidiplomasia, nchi yetu haina utawala bora na demokrasia katika nchi yetu haipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba mnasema sisi tunataka tujitegemee nakubaliana lakini ushahidi kuonyesha kwamba hatuwezi kujitegemea na matusi mnayowapa wafadhili na kila siku Waziri wa Mambo ya Nje hapa akisoma bajeti yake huwa anataja nchi wafadhili, wahisani waliotusaidia katika nchi hii, sipingi kujitegemea lakini namna gani tunahama kutoka kutokujitegemea kwenda kujitegemea. Hawa wahisani ambao wamekuwa wakitusaidia leo tunasema mabeberu lakini demokrasia haifanyiki, nani atakuwa na ujasiri wa kuja kuwekeza katika nchi yetu. Serikali ambayo haiwezi hata kumheshimu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani ambaye ana kura milioni sita inamweka ndani kwa ajili ya bail, ni mwekezaji gani kutoka nje atakuwa na confidence ya kuja kuwekeza katika nchi hii? Anayekuja kuleta mamilioni kama bail ya mtu mwenye wafuasi milioni sita anawekwa kienyeji kienyeji ndani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mnaongea kwa ujasiri hapa, mtuambie ni kwa nini Waziri wa Mambo ya Nje, Profesa Kabudi na Dkt. Slaa walienda kupiga magoti kule nchi za Ulaya kama mnaweza kujitegemea? [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

Kama tunaona tunaweza kujitegemea, tumesema masharti hatuwezi, hawa ni watu ambao tunatakiwa…

KUHUSU UTARATIBU

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisema nasema uongo unanionea. Vyombo vya habari vimesema na hawajakanusha na kanuni zinataka kwanza yeye aseme kama mimi nasema uongo. Yeye athibitishe kama mimi nasema uongo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachosema, uchumi wa nchi hii tutaimba pambio hapa, tutapongezana, TBC itawasifu sana, lakini duniani kote nimesema Tanzania siyo kisiwa. Ili uchumi wetu uweze kukua tuimarishe demokrasia, na utawala bora…

KUHUSU UTARATIBU

MWENYEKITI: Mheshimiwa Peter Msigwa kwa vile huna ushahidi na hilo naomba ufute kauli yako.

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Dkt. Kabudi, Dkt. Slaa na Mheshimiwa Mahiga walisimama walipokwenda Ulaya kuomba misaada, hawakupiga magoti. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoweza kusema…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Peter Msigwa.

Kwa hiyo kauli yako ya mwanzo umefuta? Haya sema nimefuta kauli yangu ile ya kupiga magoti.

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Hiyo ya mwanzo nimefuta, imebaki ile ya kusimama. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mpango, Mheshimiwa Silinde hapa amezungumza hapa kwamba atayekuwa wa kwanza kwenda gerezani ni Katibu wa Hazina, lakini hata wewe Mheshimiwa Mpango hakitakukosa kikombe hiki kwa sababu mambo mnayoyafanya nje ya utaratibu katika Serikali hii yamekithiri kuliko kawaida na jinai huwa haifi. Msishangilie tu mambo haya kama hatuwezi kufuata utaratibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe hii bajeti mnayohangaika na kusema haiendi vizuri, naomba nikuulize Mheshimiwa Mpango, kama wafadhili wanatoa hiyo asilimia 40 wanaotuletea pesa mnawaita mabeberu na huko barabarani ukipita unaona barabara kwa hisani ya watu wa Marekani, ukikuta daraja kwa hisani ya watu wa Marekani, UKIMWI kwa hisani ya watu wa Marekani, condom hisani ya watu wa Marekani, malaria hisani ya watu wa Marekani, mama na mtoto hisani ya watu wa Marekani, kama wafadhili wakiondoa asilimia 40 kwa moyo mweupe kabisa, hiyo asilimia 40 kwa mpango wenu wa Serikali mnaitoa wapi ili tuweze kujitegemea? Kweli tujitegemee hamna mtu anayekataa lakini mnajitegemea, mnaondoka kwa mbwembwe na matusi wakati uwezo huo wa kupata asilimia 40 hatuna. (Makofi)