Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Usimamizi wa Matumizi ya Fedha za Umma katika Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2017

Hon. Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Usimamizi wa Matumizi ya Fedha za Umma katika Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2017

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza binafsi napenda kuchukua fursa hii kukupongeza wewe kwa kutuongoza. Pia nishukuru Kamati zote kwa kazi kubwa waliyofanya na niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, yangu ni michache sana, kubwa zaidi kwanza naomba nishukuru kwa mchango wa Kamati ya Bunge ya LAAC kwa kazi kubwa tunayoendelea kuifanya kwa pamoja. Nikiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, niishukuru sana Kamati hii toka tulipoanza kufanya kazi pamoja, mimi mwenyewe binafsi nashuhudia mapinduzi makubwa sana katika usimamizi hasa wa rasilimali fedha, kwa upande wangu naishukuru sana Kamati. Kwa kweli kwa upande sisi hata utapoona leo hii kuna mabadiliko makubwa sana ya jinsi gani rasilimali fedha na upatikanaji wa hati safi mpaka zimefikia asilimia 90, hili si jambo haba ni Kamati imefanya na Serikali tumetekeleza katika baadhi ya mambo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue mapendekezo ya Kamati yalivyotoka kwa ajili ya kwenda kuyafanyia kazi kwa sababu lengo kubwa ni kwa ajili ya kuboresha utendaji wa Serikali katika maeneo mbalimbali. Hata hivyo, niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao, kwa sababu wamechangia mambo mbalimbali na naamini lengo lao ni kuongeza ufanisi katika usimamizi wa rasilimali fedha. Ndiyo maana tunaona hata ripoti ya CAG inavyotoka na hata Kamati inavyotushauri tumeamua kuchukua hatua mbalimbali katika vipindi tofauti, takribani toka ripoti zilivyotolewa tumechukua hatua kwa watumishi takribani 343. Hili siyo jambo dogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikwambie hakuna jambo kubwa katika maisha kama kuchukua hatua kwa watu ambao wamefanya makosa na tunajua kwamba watu hawa wana familia zao, lakini kama viongozi lazima tufanye maamuzi na hili niseme tumechukua hatua mbalimbali; kuna watu wengine wamefukuzwa kazi kabisa, kuna watu wengine wamepewa onyo na kuna wengine wamepelekwa Mahakamani hivi sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, unakumbuka hata ripoti ya CAG ilivyotoka siku ile ile unakumbuka, kwamba maelekezo yalitoka na karibu Wakurugenzi watatu siku ile ile walipoteza kazi, tukiangalia Halmashauri ya Ujiji, Halmashauri ya Kigoma na hali kadhalika Halmashauri ya Pangani. Hata hivyo, sisi kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunatekeleza maelekezo ya Kamati, kama Kamati ilivyosema kwamba pale tumeanzisha Kitengo ambacho kinaitwa Follow up and Investigation Unit, kitengo ambacho kimetusaidia kwa kiwango kikubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, unakumbuka hata juzi juzi kulikuwa na tukio kule Ulanga ambapo unaona kwamba ni maamuzi na mwelekeo sahihi ya kitengo hiki. Lengo letu ni kuhakikisha kwamba, tunaboresha katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa na mwisho wa siku tuhakikishe kwamba zile rasilimali fedha zinaenda kusimamiwa vizuri katika maeneo haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nikuhakikishe kwamba Ofisi yangu itaendelea kutekeleza maelekezo ya Kamati kwa kadri iwezekanavyo, lengo kubwa ni kwamba rasilimali fedha zielekezwe katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa, ziende zikajibu matatizo ya wananchi. Katika kipindi hiki cha karibuni tumeweza kuchukua maamuzi mbalimbali, kwa mfano, ukiangalia kule Nyang’wale, Nkasi na Tunduru na maeneo mengine mbalimbali. Haya yote tumeyafanya tukiwa na lengo kwamba, basi zile hoja mbalimbali zinazotolewa ziweze kufanyiwa kazi kwa ajili ya mustakabali na Serikali yetu iweze kwenda vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja ilijitokeza katika suala zima la Mfuko wa Vijana hasa upande wa kanuni na ni kweli tulitunga sheria hapa. Bahati nzuri sheria yetu iko very straight forward, kwamba sheria yetu inatekelezeka moja kwa moja. Hata hivyo, ofisi yangu mchakato wa kanuni sasa hivi uko hatua za mwisho, wadau mbalimbali wameshashiriki, tuko katika stage ya mwisho kabisa ambayo nina imani na kupitia ofisi yangu pale tunatarajia huenda mwishoni mwa mwezi huu mchakato huu utakuwa umekamilika. Kwa hiyo jambo hili litakuwa tayari utekelezaji mzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishukuru sana hasa niwashukuru wenzetu wa Wizara ya Fedha. Zamani kwa vipindi tofauti tumeona tatizo la upelekekaji wa fedha lilikuwa kubwa sana, lakini hivi sasa nadhani kutokana na maelekezo yanayotolewa na Kamati ya LAAC, leo hii ninavyozungumza zaidi ya kati ya shilingi 1.3 trillion ambayo ni development budget iliyopaswa kwenda katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa zaidi ya shilingi bilioni 640 zimeshafika, ni wastani wa asilimia 48.8, mpaka hivi sasa ndani ya kipindi hiki mpaka mwezi Desemba. Naona trend hii mpaka tukapofika mwezi wa Sita hali itakuwa ni shwari sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo katika jambo hili Waheshimiwa Wabunge naomba niwaambie katika suala zima la utekelezaji wa ripoti ya CAG, lakini halikadhalika maelekezo ya Kamati, jambo hili sasa nina imani linaenda vizuri zaidi. Maana yake leo hii ukizungumza zaidi ya shilingi bilioni 640, ambayo katika kipindi cha nyuma inawezekana hiyo ndiyo fedha ya mwaka nzima, leo hii Waheshimiwa Wabunge mbalimbali wanashuhudia katika Wilaya zetu jinsi gani zaidi ya shilingi bilioni 105 zinaenda kujenga hospitali 67, haijawahi kutokea ndani ya muda mfupi zaidi ya shilingi bilioni 105 inatoka. Pia zaidi ya shilingi bilioni 23 inaenda kuhakikisha tunajenga majengo ya halmashauri katika halmashauri zetu, lengo kubwa Watendaji wapate ofisi rafiki, hii haijawahi kutokea. Zaidi ya shilingi bilioni 1.4 watu ambao wako kandokando ya ziwa na bahari, ambao ilionekana kwamba tatizo kubwa lilikuwa ni boti, fedha hizo zote zimeshatoka kwa asilimia 100. Hii ni fahari kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge kwamba, Serikali kwa upande wake hasa katika upelekaji wa fedha na nikiangalia trend hivi sasa mabadiliko yamekuwa makubwa sana. Hata hivyo, juzi juzi tumepeleka zaidi ya bilioni 54 kwa ajili ya Sekta ya Elimu, tukiboresha miundombinu ya elimu, hii ni kazi kubwa sana ambayo nina imani jambo hili zamani halikuwepo. Kwa hiyo tukiri wazi kwamba ,Serikali imendelea kutekeleza maelekezo ya CAG, halikadhalika maelekezo ya Kamati yetu ya Bunge ambayo inatushauri vyema katika kipindi chote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja nyingine kuhusu ripoti ya ukaguzi maalum uliofanyika kule Kaliua. Naomba niwaambie kwamba, ofisi yangu iliamua hivyo kwa sababu ukiangalia idadi ya watumishi ni wengi zaidi ya watumishi 60; watumishi 60 siyo jambo dogo na halitaki maamuzi ya nanihi. Naishukuru sana Kamati imetuelekeza vizuri na hata hivyo tuliunda timu maalum ambayo ilienda kule site na Jumapili, ina maana keshokutwa hapa itatolewa ripoti ya watumishi wale 60 jinsi gani kwa kadri iwezekanavyo hatua kwa wale kuhusu labda suala zima la kinidhamu, mtu apelekwe wapi, kama mtu ana mambo ya kijinai. Mambo hayo yote yako katika utekelezaji, hata hivyo Kamati ilielekeza wale watumishi mbalimbali wengine waweze kurudishwa na hivi sasa Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumeanza kulitekeleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikuhakikishie wewe na Wajumbe wa Kamati, jukumu letu sisi kubwa ni kuhakikisha kwamba ripoti ya CAG lakini maelekezo ya Kamati tutaendelea kuyatekeleza kwa kadri tutakavyoona inafaa. Lengo kubwa ni kuonyesha jinsi gani nchi yetu tunakwenda kujibu matatizo ya wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali yao hivi sasa, Serikali hii ambayo kwa sasa ukiangalia trend ya utendaji wake wa kazi tumebadilisha utaratibu wetu wa kazi, tunakwenda kujibu matatizo ya wanachi kwa kubaini changamoto na kuzitafutia majawabu. Hili ndiyo jambo la kushukuru. Hali hii zamani haikuwepo hivi lakini sasa hivi tunaona jinsi gani uwajibikaji umekuwa mkubwa sana, nidhamu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa sasa imebadilika tofauti na mwanzo watu walikuwa wanafanya kazi kwa mazoea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru Kamati imetushauri jinsi gani tuongeze kada ya watumishi mbalimbali kwa ajili ya kuhakikisha tunapata watumishi wa kuweza kutenda vyema katika maeneo yetu. Ndiyo maana hapa karibuni tumeajiri zaidi ya watumishi 21,000 katika sekta mbili tu ya afya ambayo tumeajiri zaidi ya watumishi 8,800 hali kadhalika sekta ya elimu zaidi ya watumishi 13,000. Najua kwamba bado matatizo yapo na ndiyo maana Serikali inajieleza kuhakikisha katika kila eneo tunatatua matatizo haya kwa kadri iwezekanavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumeona changamoto ya idadi ya Wakaguzi wa Ndani na kuweka mifumo. Hili jambo tumelipokea lakini naomba niseme, Ofisi ya TAMISEMI sasa hivi imejiimarisha katika mifumo ya TEHAMA na sasa hivi kuna mifumo ya GoT-HoMIS na mifumo mingine ya ukusanyaji wa mapato. Katika vituo vyetu vya afya vyote fedha zinakwenda moja kwa moja na eneo hili tumeajiri zaidi ya watumishi 530, hawa ni wahasibu. Lengo kubwa ni kuhakikisha fedha zote zinazofika katika kituo cha afya ziweze kusimamiwa vyema.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wajumbe wameshauri, inawezekana technicalities za watumishi wetu uwezo bado mdogo. Ndiyo maana jambo hili tumeendelea kutoa maelekezo na hivi sasa wataalam wangu wengine wako Morogoro pale kwa ajili ya kutoa mafunzo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo machache, nikushukuru sana lakini niseme kwamba Ofisi yangu itaendelea kufanya kila iwezekanavyo kwa mustakabali mzuri wa nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)