Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Usimamizi wa Matumizi ya Fedha za Umma katika Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2017

Hon. Catherine Nyakao Ruge

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Usimamizi wa Matumizi ya Fedha za Umma katika Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2017

MHE. CATHERINE N. RUGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii na nimi niweze kuchangia. Napenda kujikita kwenye Taarifa ya Kamati ya PAC na ningependa kuzungumzia issue ya 1.5 trillion. Kabla sijachangia, napenda kumnukuu aliyekuwa Rais wa 16 wa Marekani, Marehemu Abraham Lincolin ambaye alisema; “You can fool all people some of the time, but you cannot fool all people all the time.” (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali amelithibitishia Bunge, lakini pia ameuthibitishia umma kwamba kulikuwa na tofauti ya 1.5 trillion kwenye Mfuko Mkuu wa pesa za Hazina ambazo hazikukaguliwa wakati anafanya ukaguzi wake kwa hesabu zilizoishia Juni, 2017. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Kamati ya PAC kwa kumtaka CAG aweze kufanya verification na kujua tofauti ya 1.5 trillion na leo kuleta taarifa ya Bunge ambayo tunaijadili sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na verification kufanyika, badala ya hoja ya 1.5 trillion kufungwa, zimeibuka hoja nyingine na sasa hatuzungumzii 1.5 trillion, tunazungumzia 2.4 trillion. (Makofi) [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niweka records clear, siyo kazi ya CAG kusema kama kuna wizi. Kazi ya CAG ni kufanya ukaguzi na kutambua upungufu uliopo na mamlaka husika inatakiwa i-take charge. Kuna hoja mbalimbali ambazo zimeibuliwa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwenye hii ripoti ya ukaguzi maalum.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa kuna issue ya overdraft ya shilingi bilioni 290.7, Hazina wanasema hii ilikuwa ni overdraft na majibu yao wanasema zilikuwa ni pesa zilizokwenda kwenye miradi ya maendeleo na hazikupita kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina, lakini Mkaguzi hakupata vielelezo kuthibitisha hii hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkaguzi alienda mbali zaidi akaamua kuomba confirmation letter kutoka BOT kuthibitisha hiyo balance ya shilingi bilioni 290.67. Kuna confirmation letter kutoka BOT hii hapa ambayo wame-confirm kwamba kulikuwa na zero balance wakati Hazina inafunga mahesabu yao Juni, 2017. Pia taarifa za Ukaguzi za Hesabu za BOT za Juni, 2017 zinaonyesha balance ya overdraft ya Central Government ilikuwa ni 1.5 trillion. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina Hansard hapa ya tarehe 20 Aprili, 2018, ukurasa wa 22 mpaka 25. Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango alisimama hapa kutoa maelezo ya Serikali kuhusu tofauti ya 1.5 trillion. Alisema; overdraft ilikuwa shilingi bilioni 79.1. Sasa hapa tuna figure nne za kutoka kwenye Serikali moja, tuamini ipi? ya BOT ya 1.5, confirmation letter ya zero balance, maelezo ya Naibu Waziri ya shilingi bilioni 79.1 au taarifa za hesabu za BOT za 1.5 trillion? Yaani kwa kifupi hapa naona Serikali ilipoteana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya pili, ni kuhusu shilingi bilioni 976.96 ambazo zilifanyiwa reallocation kwenye vote mbalimbali kutoka kwenye mfuko wa Hazina kwenda kwenye vote 20 na fedha hizi hazikupitishwa na Bunge. Lakini pia reallocation hiyo haikupata approval ya BoT. Hizi pesa zimeenda vote 20 ambako ni Ofisi ya Rais. Wote tunatambua, vote 20 haikaguliwi. Kwa hiyo, Serikali imefanya vote 20 ni kama kichaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa masikitiko makubwa, mpaka leo…

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Catherine Ruge, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere.

T A A R I F A

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Catherine Ruge, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. CATHERINE N. RUGE: Mheshimiwa Naibu Spika, siipokei, naomba niendelee kuchangia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee nilipoishia. Hizi pesa ninazozizungumza zilizoenda vote 20 hazikupata approval ya CAG pamoja na reallocation iliyotokea. Kinachonisikitisha zaidi, hoja hii haiko kwenye Taarifa ya Kamati, lakini pia, Hazina mpaka leo hawajatoa majibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee kueleza jinsi gani Mheshimiwa Naibu Waziri alilipotosha Bunge lako tukufu aliposimama na kusema kwamba kulikuwa na receivable kwenye pesa ambazo zilikuwa zimekusanywa na Hazina.

MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

T A A R I F A

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Catherine Ruge, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. CATHERINE N. RUGE: Mheshimiwa Naibu Spika, siipokei hiyo taarifa na ninaomba unilindie muda wangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme, ripoti ya PAC ni matokeo ya taarifa ya CAG na taarifa ya CAG ni public document.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee.

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

T A A R I F A

MHE. CATHERINE N. RUGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba niendelee.

Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 20 Aprili, 2018 Naibu Waziri alisimama mbele ya Bunge lako tukufu na kulihadaa Bunge kwa kusema kulikuwa na receivable za shilingi bilioni 687 ambazo zilisababisha tofauti ya 1.5 trillion na akasema hii ilitokana na Hazina kuanza kutumia mfumo wa IPSAS Accrual. Taarifa ya Mkaguzi hii hapa haionyeshi hiyo hoja, haijaongelea kabisa receivable. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa wahasibu na tax administrators tulioko humu ndani, tunajua kabisa, hakuna pesa tarajiwa zinazokwenda kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina. Hakuna non cash item, kule zinakwenda cash tu. Mapato yote yako on basis of cash. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ni hoja ya hati fungani. Hazina walikuja na vielelezo ambavyo vilikuwa kwenye excel na CAG amesema hizi taarifa haziaminiki na haziko credible. Naomba ni-quote taarifa ya CAG; “The weaknesses continue during the verification of the difference,
the document were required as to meet numerous types from various department also it took a long time to locate and extract information most of which was in MS Excel spread sheet in different location. Kwa hiyo, kwa statement hii, hakuna credibility ya hii information.

Mheshimiwa Naibu Spika, kinachonishangaza, hivi inakuwaje Hazina inaweza kutumia excel kuweka hesabu zake ambayo inaweza ikabadilishwa, ikaongezwa kitu, ikatolewa kitu bila traces? Sasa kweli tuko serious? Hazina ambako tunaamini inalinda pesa za walipakodi wanyonge, lakini ndiyo tunaona haya matatizo na uongo mkubwa na weaknesses za mfumo na udhaifu mkubwa wa Hazina! Tusipofanyia kazi udhaifu wa mfumo wa Hazina, haya matatizo yataendelea kuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa…

MHE. OMARI M. KIGUA: Taarifa.

T A A R I F A

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Catherine Ruge, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. CATHERINE N. RUGE: Mheshimiwa Naibu Spika, siipokei.

MBUNGE FULANI: Pokea.

MBUNGE FULANI: Usipokee.

MHE. CATHERINE N. RUGE: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea hii taarifa na naomba nikwambie, I am a Certified Public Accountant, najua ninachokizungumza. Inawezekana hiyo syllabus yako uliyosoma ilikuwa ya zamani, mimi I am very current. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ilikuwa ya hati fungani ambapo hizi hati fungani zilionekana zimeiva na zikawa rolled over. Lakini vielelezo hivyo pia vimeletwa kwenye excel na ukiangalia hii taarifa, ukijumlisha kwanza hizo hati fungani, haziji-figure hiyo ya shilingi bilioni 656, zinakuja shilingi bilioni 853. Angalieni hii taarifa. Kwa hiyo, kuna tofauti ya kitu kilichosemwa na kitu ambacho CAG amekizungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukitaka kujua figure ya bonds unakwenda kuangalia kwenye taarifa ya BOT; na kwenye taarifa ya BOT zimeonyeshwa bonds zote. Sasa naomba Serikali ikija hapa ituambie, hizo bonds zilizo-mature 2016/2017 Juni, ni bonds gani? Za muda gani? Zilikuwa zina kiasi gani na zililipwa lini?

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)