Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Usimamizi wa Matumizi ya Fedha za Umma katika Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2017

Hon. Juma Kombo Hamad

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Wingwi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Usimamizi wa Matumizi ya Fedha za Umma katika Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2017

MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi, nichukue fursa ya kuwapongeza Wenyeviti wote wawili wa Kamati ya LAAC na PAC kwa kuwasilisha ripoti kwa ufasaha na ufanisi mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nirudi kwa kaka yangu pale Mheshimiwa Allan Kiula kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilitoa maelezo juu ya fedha ulizodai kwamba zilipelekwa Zanzibar na Serikali ilijibu kwamba, hakuna fedha waliyopokea kwa, ile fedha ambayo ilitajwa na CAG. Hii fedha… (Makofi)

MHE. ALLAN J. KIULA: Taarifa.

MHE. JUMA KOMBO HAMAD:… hii fedha hakuna, otherwise utupatie document ambazo zinathibitisha kwamba fedha ile ili…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Juma Kombo kuna Taarifa. Mheshimiwa Kiula.

T A A R IF A

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Juma Kombo unaipokea Taarifa hiyo?

MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, tuache unafiki na uwongo. Hii fedha Waziri wa Fedha alikuja hapa akatuambia kwamba fedha hii ilikwenda Zanzibar na, baada ya kushindwa kuthibitisha ndio mara nyingine akaja tena hapa akatuambia kwamba, fedha hii imekusanywa Zanzibar.

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, tusilishane uongo kwa jambo ambalo halipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye hoja...

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Kombo naomba ukae kidogo.

Waheshimiwa Wabunge, twende sawasawa, kwanza tusikilize kwa sababu tunajibizana kwa michango na kwa taarifa iliyoko hapa mbele, tuwe tunasikilizana vizuri ili tusikatishane pale ambapo hakuna sababu. Tusikilizane vizuri, mtu anayechangia kwanza umsikilize vizuri ili unapojibu usizungumze kile ambacho hajasema tunafikia hapo.

Nafikiri hilo limeeleweka, tusikilizane vizuri ili tuweze kwenda sawasawa, tusikilizane kwa makini. Kama unataka kumjibu mwenzio msikilize kwa makini. Mheshimiwa Juma Kombo.

MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, kuna falsafa ya uongo ambapo muongo anatakiwa awe na kumbukumbu, ili asisahau kile ambacho kwamba anakizusha.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye hoja na nianze na ku-declare ni Mjumbe wa Kamati ya LAAC. Na nianze na upungufu ambao tuliuona wakati wa kukagua hizi Halmashauri kwamba pungufu moja ambalo tumeliona ni suala la upungufu wa watendaji katika Halmashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika changamoto kubwa ambayo tunaenda nayo kama Tanzania ni suala la ajira, lakini kila halmashauri ambayo ilikuwa inakuja mbele ya kamati basi unakuta kama kuna kila kitengo kina upungufu wa watumishi au wafanyakazi. Niombe kwa Serikali na TAMISEMI kwamba, suala hili ni vyema walishughulikie kwa sababu, Watanzania wengi hawana ajira na kama hawana ajira kila Halmashauri inayokuja pengine ina upungufu wa asilimia zaidi ya 50 ya watendaji katika Halmashauri, hiki ni kitendo cha aibu kwa Tanzania kwamba, vijana wako wamemaliza chuo, wamemaliza kusoma, lakini nafasi za ajira Tanzania kwenye Halmashauri zetu zipo, lakini kila siku wanapiga kelele ajira hakuna, ajira hakuna, lakini nafasi za vijana kuwaajiri zipo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Serikali kupitia TAMISEMI ambao ndio responsible kwa Halmashauri zetu walitizame hili kwa kina na kwa sababu vijana wapo ambao hawana ajira, hawana kazi, basi wawaajiri ili waende wakatumikie wananchi wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu nyingine ambayo naomba niizungumze ni suala la udhibiti wa mfumo wa wa fedha, Kitengo cha Udhibiti wa Fedha za Ndani. Na hapa pia, kuna changamoto hiyo hiyo kwamba, katika kila Halmashauri, takribani Halmashauri 50 ambazo sisi tumejaribu kuzihoji, basi unakuta kitengo kinahitaji watu wanne, lakini ama kuna mtu mmoja, ama kuna wawili.

Mheshimiwa Naibu Spika, huu ni udhaifu mkubwa ambao unajitokeza, lakini pia, kitengo hiki hakina facility yoyote. Kina upungufu wa watendaji, kina upungufu wa fedha, kina upungufu wa vifaa kama vile gari, kamera na vitu vingine. Kwa kweli ni jambo ambalo na ukizingatia Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani ni kitengo muhimu na ndio jicho la halmashauri, ndio jicho la Mkurugenzi wa Halmashauri. Sasa kama hawezeshi na bahati mbaya sana ya Halmashauri nyingi utakuta mkurugenzi anamfanya kama yule Mkaguzi wa Ndani kama ni adui, kwa maana ya kwamba hataki kumpa taarifa za kina, kwa hiyo, hawezi kumuwezesha kwenye kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo na kwenye vitabu vya fedha wakati mwingine anamwekea vikwazo mbalimbali na kwa sababu yuko chini yake inakuwa Mkaguzi wa Ndani hana nguvu za kuweza kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vyema Serikali ikaanza kufikiria kwamba wale watu Wahasibu, Wakaguzi wa Ndani kama ikiwezekana na inayowezekana basi wawe nje ya mfumo wa uajiri wa Halmashauri ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi, waweze kuwakabili Wakurugenzi na kuwahoji juu ya masuala ya matumizi ya fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kutokutekelezwa kwa maagizo ya Kamati. Utakuta kila Halmashauri kama imepewa maagizo kumi, basi ikija imetekeleza maagizo mawili na hii ni aibu sana kwamba Kamati ya Bunge ambayo ipo kwa niaba ya Bunge imetoa maagizo kwenye Halmashauri, maagizo kumi, lakini Halmashauri inakuja mara nyingine au mwaka mwingine imetekeleza maagizo mawili au matatu. Kwa kweli hii ni dharau kubwa na Halmashauri lazima TAMISEMI isimamie vizuri suala hili, Ofisi ya CAG isimamie vizuri suala hili, lakini na Bunge litoe maagizo makali na maazimio makali juu ya suala hili la utekelezwaji wa maagizo ya Kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati ya Bunge ni Bunge, kwa sababu, Kamati ya Bunge ipo kwa niaba ya Bunge haipo kwa niaba kwamba labda ni Mheshimiwa Vedasto au ni Mheshimiwa Mama Kaboyoka, hapana, ni Bunge. Kwa hiyo, maagizo yanayotolewa pale yanatolewa na Bunge. Sasa halmashauri kwenda kukaa kitako wakajishughulisha nyingine bila kutekeleza maagizo yale hii kwa kweli si jambo jema na ni jambo la aibu ambalo mwisho wa siku linakuwa halileti ufanisi mzuri kwa maendeleo ya Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo naomba kulizungumza… eeh! Vipi sasa? Hata tano bado!

Mheshimiwa Naibu Spika, ni suala la Mfuko wa Wanawake, suala hili lina changamoto nyingi, juzi hapa/ mwaka jana tumepitisha sheria na uko mfumo wa 4:4:2 kwamba asilimia 4 iende kwa waawake, asilimia nne kwa vijana na asilimia mbili kwa watu wenye ulemavu kwa kweli, ilikuwa ni jambo zuri na jambo jema. Lakini halmashauri zote ambazo tumezikagua zimebakia na madeni makubwa katika kipindi hiki kabla ya sheria hii kuipitisha. Ni vyema Serikali itafakari upya kama ikiona kwamba ni jambo la busara basi madeni yale ya nyuma, sio mikopo maana kuna vitu viwili tofauti, kuna mikopo ambayo wamekopa, lakini kuna na madeni ambayo yamebebwa na Halmashauri ambayo kimsingi hayalipwi wala hayatalipwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iangalie utaratibu mzuri hapa wa kuweka jambo hili, ikiwezekana na ikionekana ni jambo la busara, basi Halmashauri, Taasisi za Serikali zisamehewe madeni yale ya nyuma na sasa tuanze upya na mfumo huu wa 4:4:2 ambao upo kisheria. Na mfumo huu ukisimamiwa vizuri basi tutaweza kuleta ufanisi kwa makundi haya ya akinamama, vijana pamoja na watu wenye ulemavu kuliko kuhangaika sasa na madeni yale ya nyuma ambayo kimsingi hayalipwi na yanatumiwa kama ni muamvuli au ni kichaka cha kujificha kwa hii 4:4:2 ambayo ipo sasa hivi kisheria. Naomba Serikali iliangalie hili vizuri na ikiwezekana walifanyie utaratibu, ili liweze kwisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende na sakata hili la Halmashauri ya Kaliuwa. Kaliua kuna kashfa kubwa na fedheha kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika watumishi 66 ambao walibainika na ripoti ya CAG kwamba wamehusika na ubadhirifu wa shilingi bilioni 3.3 ni watumishi wawili tu ambao hadi sasa wamechukuliwa hatua, bahati mbaya sana na hapa nakuwa najiuliza inawezekana wengine wasiridhike, lakini huu ndio ukweli. Nakuwa najiuliza huo utakatifu wa Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli uko wapi? Kwa sababu ni lazima tujiulize hata ikiwa kuna watu litawananihii, lakini huo utakatifu unaozungumzwa humu tena na Wabunge wa Serikali hii uko wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, tuishauri Serikali ili iwachukulie hatua watu ambao waepiga fedha za Serikali. Kama shilingi bilioni 3.3 zimepigwa halafu mtumishi/ Mkurugenzi ambaye yuko pale kipindi hiki fedha hizi zinapigwa, alikuwa Mtendaji baadae akawa Mkurugenzi leo ni Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, halafu tunakuja hapa tunajisifu kwamba sisi ni watakatifu, Rais anatumbua. Hebu tumuone basi, leo kwa ripoti hii ambayo imemtoa Mkurugenzi huyu kwa Tume ya Uchaguzi ambaye anaitwa Athumani Kihamia, tumuone Rais Dkt. John Pombe Magufuli katoka na kauli na leo kamtumbua. (Makofi)