Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Selemani Said Bungara

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Kilwa Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nashukuru kwa kunipa nafasi hii leo na kwa kuwa umeniambia taratibu basi leo nitakuwa taratibu kabisa. Pili, namshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amewapa akili Watanzania na akili kazi zake mbili tu, kujua ukweli na uongo, ndiyo kazi ya akili, hayo mengine kupata Uprofesa na nini, hayo mengine tu, lakini kazi ya akili ni kujua ukweli na uongo, nyeupe na nyeusi, ndiyo kazi yake hiyo hiyo tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naanza kwa kusema tunamnukuu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mungu amuweke mahali anapostahili, alisema ili tuendelee tunahitaji vitu vinne; ardhi, watu, siasa safi na uongozi bora. Nchi hii vitu vyote hivyo vinne vipo, ardhi ipo ina kila kitu, watu ndiyo wengi tu, tunafika milioni 50 na ngapi sasa hivi, siasa ipo na tangu mwaka 1961 mpaka leo chama cha siasa kinachoongoza katika nchi hii ni Chama cha CCM, kwa hiyo siasa ipo na uongozi upo, lakini unaotakiwa ni uongozi bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mipango yote mnayopanga hii, yote hii, kama siasa haikuwa safi na uongozi haukuwa bora, sawasawa na hakuna. Tangu nimeingia Bunge hili mwaka 2010 mipango inapangwa kweli kweli lakini utekelezaji hakuna. Kwa hiyo, mimi ni mwanasiasa na huwezi ukaendelea kama siasa ikiwa mbaya. Naomba sana Mheshimiwa Dkt. Mpango na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali sikivu, huu uwanja wa siasa kama tukiuchezea hali itakuwa mbaya sana katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mipango yote hii wanayopanga, angalia sasa hivi, tumepanga mipango mikubwa, limekuja jambo hili la kununuliwa Wabunge, hela zote ambazo tulipangia katika mambo ya maendeleo zinakwenda katika bajeti ya kufanya uchaguzi.

KUHUSU UTARATIBU

HE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema fedha zimetumika katika uchaguzi. Uchaguzi ambao ulikuwa hauna sababu yoyote na hiki kitabu cha Mheshimiwa Dkt. Mpango, mwenyewe kasema katika ukurasa wa 44 kwamba fedha trilioni tisa hazikupatikana na mambo mengi ya maendeleo hayakufanyika, lakini fedha hizo zilienda katika uchaguzi. Sasa unachosema kwamba kununuliwa hata mimi si nilifuatwa! Hata mimi mwenyewe nilifuatwa, sasa ukitaka ushahidi anaitwa nani yule Mheshimiwa Jenista uje, tukutane baadaye nikwambie walikuja nani na nani walitaka kuninunua mimi nikakataa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana Mheshimiwa Dau alisema jambo kubwa sana katika Bunge hili na mimi nasikitika sana, Waziri Mkuu anachaguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na anathibitishwa katika Bunge hili. Kwa hiyo, Waziri Mkuu anachaguliwa na Rais na kuthibitishwa na Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dau jana alisema kwamba kuna Waziri mmoja wa Ujenzi alimwambia habari ya boti lakini akajibiwa majibu mabaya na Waziri wa Ujenzi. Sasa hiyo siyo mara moja tu, Mheshimiwa huyu Waziri wa Ujenzi alikuja Kilwa hivyo hivyo nikamwambia kuna mradi wa maji wakati huo alikuwa Naibu Waziri wa Maji, nikamwambia nimeonana na Waziri Mkuu na yeye akanijibu kama alivyojibiwa Bwana Dau, akasema Waziri Mkuu nani, bwana! Mimi namtambua Mheshimiwa Magufuli tu. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuseme Waziri Mkuu ambaye amechaguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wwa Tanzania na kuthibitishwa na Bunge hili na mimi nilimpigia kura ili awe Waziri Mkuu. Halafu kuna mtu mmoja ambaye anachaguliwa tu lakini wala hathibitishwi na Bunge anamdhalilisha Waziri Mkuu. Mimi nikifikiri anadhalilisha ninaposema mimi mpinzani tu, kumbe hata akisema Mheshimiwa Dau wa Mafia naye anaambiwa hivyo hivyo hii siyo desturi nzuri Waheshimiwa, huyu ni Waziri Mkuu asidharauliwe na najua watu wa CCM nimewaambia jana vipi wamesema bwana sisi tukisema sana tunaitwa katika maadili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nanukuu ya jana. Jana hiyo hiyo kuna Mheshimiwa Sugu hapa kasema kwamba watu wanauliwa akatoka Waziri mwingine akasema hajauliwa. Sasa nina ushahidi kwamba Polisi wa Tanzania wameua watu wangu Kilwa ndani ya msikiti na yule Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani alisema kwamba kama kuna ushahidi atoe, mimi ushahidi ninao kwamba Polisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walimuua Ismail Bweta katika Msikiti Chumo.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mwigulu akaniita wakati huo akiwa Waziri wa Mambo wa Ndani akaniambia niwalete hao watu, nikaja nao watu kwa Waziri Mwigulu, baba wa marehemu na yule mtu aliyetolewa jicho na Polisi. Mheshimiwa Mwigulu alipopewa taarifa akasema jambo hili zito umpeleke kwa Waziri Mkuu. Namwambia tu huyo Mheshimiwa anasema kwamba Polisi hawajaua watu. Nikawapeleka wale watu Waziri Mkuu wakamwambia, kidogo alie akasema kweli Serikali imefanya kosa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hayo mambo yapo nchi hii na mnaua, mnateka na mimi ushahidi ninao, hii yote tunasema ili tuendelee tunahitaji vitu vingapi vinne ardhi, watu, siasa safi na uongozi bora. Kitendo cha watu kuuliwa na taarifa mnapata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa tena! Tunapanga mipango ya nchi kwamba kama siasa itakuwa mbaya. Nimeanza kusema kwamba siasa mbaya mipango yote itakuwa hakuna kama siasa itakuwa mbaya sasa uelewi tu, mzee mwenzangu huelewi ninachokisema?… (Makofi/Kicheko)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya namalizia kwamba, naomba sana Serikali muwe makini, muwe wakweli, kwa sababu Mtume anasema utakuja wakati viongozi watakuwa waongo na watu watawajua kuwa waongo, lakini watawapigia makofi na kuwachinjia nyama ili hali watakuwa waongo viongozi hao. Basi msitegemee rehema kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo mwisho wa yote, naomba korosho zote wakanunue kwa sababu waliahidi wakanunue ili mambo…watu wetu wa Kusini mipango yao iende vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake mipango bila korosho kununua hakuna mipango. Ahsante sana.