Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Naomba niseme tu kwamba kwa mara ya kwanza nasimama kwenye Bunge lako Tukufu kuchangia nikiwa mtu huru sana. I will speak out my mind. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, neno la kwanza ni kwamba unajua life is real, kuna maisha halisi na kuna maisha ya kuigiza. Kwa hiyo, kwenye mijadala humu Bunge, Mheshimiwa Mpango na Serikali wajue kwamba kuna watu wanazungumzia maisha ya watu na kuna watu wanazungumzia maisha yao. Wale waliopewa dhamana hiyo ya kuzungumza mambo ya Watanzania, wanyonge, maskini wafanye hivyo, wasikilize kidogo wa-base kwenye mambo ambayo wameamua wao ambao ndiyo mkataba kati yao na Watanzania walio wengi, hili ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hiyo naunga mkono miradi yote ambayo imetajwa hapo ya kimkakati, ujenzi wa reli, Shirika la Ndege na umeme wa maji wa Rufiji. Ni muhimu watu wajue kwamba haya yote, kujenga reli, kuliboresha shirika la ndege na umeme wa maji ya Rufiji wala hauhitaji Katiba Mpya. Kwa hiyo, haya yatekelezwe mapema, wale ambao wanasubiri Katiba Mpya watafanya watakapopata Katiba Mpya, kwa sasa haya yafanyike, huhitaji Katiba Mpya katika kutekeleza haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini liko suala la maji. Wenzangu walipokuwa wanazungumza, maana leo nimepata uzoefu mpya kabisa, mimi ni Mwalimu, yaani ni kama ulikuwa unawafundisha wanafunzi halafu unampa mmojawapo swali halafu unakaa unamsikiliza, nimewa-enjoy sana ndugu zangu wale watasubiri kweli, watasubiri sana. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mchangiaji mmoja anasema kuna mradi wa maji kule Njombe haujakamilika au umekamilika lakini hautoi maji lakini anasema hatua hazikuchuliwa. Mwingine anasema watu hawana amani, watu wana vinyongo yaani wana hofu hofu. Kwa nini mtumishi wa umma, kama ni Mkuu wa Idara ya Maji, Injinia wa Maji una hofu wakati ni mtaalam na umepewa dhamana katika eneo lako? Unasema mradi umekamilika lakini hautoi maji, huyo ambaye amekula pesa awajibishwe na hapo ndiyo inakuja dhana ya kutumbuana, hHuyu hawezi kuonewa huruma. Kama tunazungumza habari ya maji hayapatikani lazima miradi ya maji ikamilike na wale ambao hawakutimiza wajibu wao wawajibishwe na hiyo ndiyo kazi ya Serikali ya Awamu ya Tano, naunga mkono jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo la maji likifanyika nchi nzima, kila jimbo, kila wilaya, kila mkoa maana yake habari ya upinzani haitasikika, watu wataimba CCM wataimba Magufuli, wataimba Majaliwa, wataimba Ndugai, hakuna mjadala, watu wanataka maji hawataki Katiba Mpya. Nani ameitisha mkutano watu wakawaambia alete Bungeni suala la Katiba Mpya, watu wanataka maji, barabara, hayo maneno ya Katiba Mpya ni yao, wananchi kule mtaani wanataka waondolewe kero zao. Hiyo ndiyo kazi Mheshimiwa Magufuli anayoifanya na sisi tunamuunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwamba kule Ukonga kuna shida ya majia miradi inaendelea na kwenye mpango huu imetajwa katika Mkoa wa Dar es Salaam kuondoa kero ya maji ikiwepo Jimbo la Ukonga, Temeke, Kigamboni na Ubungo. Hata na Majimbo mengine kule ambayo wenzangu wapo, akina Mheshimiwa Mnyika na wengine na CCM kwa kweli pale haijabagua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la elimu. Kuna mwenzangu mmoja hapa amesimama akasema hakuna ajira, mimi nilikuwa naangalia kwenye mtandao wa ajira. Kwa mfano Serikali imekarabati Shule Kongwe za Jangwani, Azania, Pugu, Kilakala, Vyuo vya Ualimu, Tarime TCC, Mbeya kule Mpuguso, hii kazi imefanyika na mabilioni ya fedha zimetumika. Tunapozungumza kuna walimu wapya wa sekondari wameajiriwa zaidi ya 4,800 wa hesabu na masomo ya sayansi. Kuna nyumba za walimu zimejengwa, maabara, hosteli za wasichana, kule kwangu Mbondole imejengwa. Haya mambo lazima ukubali na upongeze kidogo. Sisi wengi hapa ni Wakristo hasa upande ule unatakiwa ushukuru hata kwa kidogo. Kuipongeza Serikali ni kuipa moyo kwamba hapa umetatua kero hii lakini bado kuna hili na lile si dhambi. Sasa ukikaa hapa unajadili habari ya kupongeza inaonekana siyo sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la elimu. Elimu, kwa maana ya shule ya elimu ya awali, shule za msingi na sekondari Serikali imefanya vizuri sana baada ya kuondoa ada na kutoa ile elimu bure. Sasa kuna vyuo vya ufundi na teknolojia, kuna vyuo vya elimu ya juu, hapa inabidi Serikali iweke nguzo. Unapozungumza habari ya ajira, ukiwa na vyuo maana yake ni kwamba utapata vijana wengi wakimaliza form four, form six, watakuwa na ujuzi watajiajiri hawatasubiri ajira ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile lazima Serikali ichukue hatua. Kuna mchingiaji mmoja jana amesema kwamba mikopo ya elimu ya juu itolewe na benki, benki haiwezi, hawa ni vijana wamemaliza shule hawana kazi, wanakaa mtaani muda mrefu. Kwa hiyo, lazima Serikali yenyewe ichukue wajibu wa kusomesha Watanzania watoto wa maskini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vigezo vya mikopo ya elimu ya juu, naipongeza sana Serikali kwa sababu wakati nikiwa Rais wa Mlimani 2005/2006 tulikuwa tunagoma ndipo unapata mkopo. This time around vijana wanakaa kwenye mabweni yao, fedha zinaingia, wanaenda kwenye mitandao Serikali imefanya kazi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, cha muhimu vigezo viangaliwe habari ya kuambiwa tu kwama baba yake alikuwa mtumishi amestaafu amesoma private sasa hawezi kupata mkopo siyo sawasawa. Mimi hapa ni Mbunge na wenzangu kesho nikistaafu maana yake kipato hiki hakipo, mwanangu atakosa mikopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nadhani vigezo viangaliwe na hali halisi ya mazingira kulingana na wakati. Suala la kuwasomesha vijana wa Tanzania, ni jambo mahsusi, ni jambo maalum lisimamiwe na litekelezwe. Watoto ambao wamefaulu kwenda vyuo vikuu wasibaki mitaani hawasomi itakuwa si sawa, hilo tunaliunga mkono lifanyike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, afya. Kuna mtu jana anasema kwa nini mnazungumza habari ya vifaa tiba. Tukubaliane kuwa wakati tunapanga kupunguza maradhi ya aina mbalimbali katika hii nchi ni lazima pia haya yaliyopo tuyatibu na kujipanga vizuri, hili jambo ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naangalia takwimu, kwa mfano wamejenga nyumba za madaktari 313, vituo vya afya 350, zahanati mpya 38, hospitali za wilaya 221 na Kivule Ukonga ipo na Bunda kule kwa Mheshimiwa Ester Bulaya ipo, imetajwa hapa na fedha zimepelekwa. Sasa katika eneo hili lazima tukubali kwamba kazi inafanyika kubwa, tuunge mkono wenzetu lakini tuboreshe namna ya kwenda mbele, hilo ni jambo la msingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo la vijana, wanawake na walemavu...

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema kwamba life is real na niko kwenye maisha halisi, nimerudi kwenye enzi zangu na I will speak out my mind throughout this Bunge, kwa hiyo hakuna shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali itajitahidi, kuna suala la vijana, akina mama na walemavu, zile asilimia nne kwa akina mama, nne kwa vijana na mbili kwa walemavu, changamoto kubwa ni kwamba mahitaji ni makubwa kuliko uwezo uliopo na halmashauri zetu hazina uwezo kwa kuwa zina shughuli nyingi sana. Serikali iangalie namna ya kupata fedha iwezeshe makundi haya maalum, hawa ndiyo wapiga kura na ndiyo Watanzania. Hawa akina mama, vijana na walemavu wakiwezeshwa watapungaza utegemezi, wakienda kupiga kura wataiunga mkono Serikali kwani imewawezesha. Hili lifanyiwe kazi haraka sana na halihitaji Katiba Mpya, linahitaji utashi na maamuzi na fedha itafutwe ifanye kazi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utawala bora, hapa nina maneno kidogo. Kuna watu hapa wamesimama mtu anaita mkutano wa hadhara anatukana mwanzo mpaka mwisho, akikamatwa anasema ameonewa, nani kamtuma akatukane watu kwenye mkutano wa hadhara? Ameita waandishi wa habari anasema watu wameuawa, sisi tunakwambia tusaidie uthibitishe waliouawa unasema unaonewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wanazungumza utawala bora, tarehe 4 Novemba, Kambi Rasmi ya Upinzani ya CHADEMA walikutana maana wana urafiki wa mashaka kati yao na CUF walikutana. Yuko Mheshimiwa Zitto, Mheshimiwa Mbowe, Mheshimiwa Nyarandu, yuko na mwingine wanapanga namna ambavyo Bunge hili, yaani kikao chako hiki Mheshimiwa Mwenyekiti kitavurugwa na maazimio yao wanapanga hata kwenda nje.Sasa kama mnakubaliana, mnapanga namna ya kuvuruga mahusiano ya kimataifa na mnamtuma Nyalandu aende, halafu hapa mnatuambia habari za utawala bora, mnataka mwongozo wa Spika; nakushukuru Mwenyekiti kwa kupiga chini taarifa zisizo na maana hawawezi kutuingiza huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nashukuru. Unapozungumza habari utawala bora ni lazima uanzie ndani. Ni muhimu sana na lazima tukubaliane. Hatuwezi kuwa na Watanzania wanakutana kwenye magenge yao, wanapanga kuvuruga amani ya nchi, wanapanga kuvuruga mahusiano, halafu wanakuja Bungeni ili tupoteza muda kujadili mambo yao. Wamepanga wao, wamejadili wao, watupoteze muda, hatuwezi kuruhusu mjadala ukafanyika humu ndani. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mambo ambayo tunamuunga mkono Mheshimiwa Dkt. Magufuli ni namna ambavyo anaweza kuchukua hatua kwa watu ambao wamefuja mali za nchi.

Kama kuna watu wanafanya biashara hawafuati utaratibu, hawalipi kodi wamevuruga miradi wakikamatwa wanasema hawana amani, wahalifu lazima washughulikiwe, hata Mwalimu Nyerere alifanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Azimio la Arusha lilikuja kuwawajibisha watu ambao ni wazembe, sasa Mheshimiwa Dkt. Magufuli amewaelekeza watendaji wenzake na hili linahusu ma-DC na Wakuu wa Mikoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya Mbunge ni tofauti na kazi ya DC na RC, wale ni executive, kama kuna mahali kuna mradi haujafanyika mtu amesimamia jengo limekuwa hovyo hovyo anakamatwa anaisaidia Serikali ili kazi ifanyike.

Kwa hiyo, nidhamu ni muhimu sana.

Naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais amefanya ziara kule Nyamongo, amesema wananchi watalipwa fedha zao za muda mrefu. (Makofi)

Sasa yameshughulikiwa wananchi wanaishi kwa amani. Mheshimiwa Dkt. Kigwangala nenda ukashughulikie mambo haya msingi yaishe. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na kwa mara ya kwanza katika historia ya Bunge, naomba niunge mkono hoja kwa nguvu zote asilimia mia moja, ahsante sana.