Parliament of Tanzania

Mkutano wa Kumi na Tatu wa Bunge waanza Jijini Dodoma

Mkutano wa Kumi na Tatu wa Bunge umeanza tarehe 6 Novemba, 2018 na unatarajiwa kuahirishwa tarehe 16 Novemba, 2018 ambapo shughuli ya kwanza iliyofanyika ni Wabunge wateule wanne kuapishwa. Wabunge hao ni;-

(i) Mhe. Timotheo Paul Mnzava (Jimbo la Korogwe Vijijini – (CCM)

(ii) Mhe. Mwikwabe Mwita Waitara (Jimbo la Ukonga – (CCM)

(iii) Mhe. Julius Kalanga Laizer (Jimbo la Monduli – (CCM)

(iv)Mhe. Zuberi Mohammed Kuchauka (Jimbo la Liwale – (CCM).

Akizungumza na Waandishi wa Habari siku moja kabla ya kuanza kwa Bunge Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai (Mb) amesema kuwa shughuli nyingine zinazotarajiwa kufanyiwa kazi katika mkutano huu ni kama ifuatavyo;-

1. Maswali

Kuhusu Maswali yatakayoulizwa Bungeni, Mhe. Spika amesema kuwa Maswali 125 ya Kawaida yanatarajiwa kuulizwa na Wabunge. Aidha, wastani wa Maswali 16 ya papo kwa papo kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu yanatarajiwa kuulizwa siku za Alhamisi tarehe 8 na 15 Novemba, 2018.

2. Kamati ya Mipango

Kwa mujibu wa Mhe. Spika madhumuni makubwa ya Mkutano huu wa Bunge ni kwa ajili ya Waheshimiwa Wabunge kujadili na kuishauri Serikali kuhusu Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020.

“Katika Mkutano huu sehemu kubwa ya mijadala ya Wabunge ni kuhusiana na huu Mpango utakaowasilishwa Bungeni na Waziri wa Fedha na Mipango,” alisema Mhe. Ndugai.

Aidha, Mhe. Spika aliongeza kuwa Mpango huu utajadiliwa kuanzia tarehe 6 hadi 12 Novemba, 2018.

Kwa mujibu wa Kanuni ya 94 ya Kanuni za Bunge, Toleo la Januari, 2016 Bunge litakaa kama Kamati ya Mipango ili kukidhi matakwa ya Ibara ya 63 (3) (c) ya Katiba kwa kujadili na kuishauri Serikali kuhusu Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali katika Mwaka wa Fedha husika.

3. Miswada ya Sheria ya Serikali

Mhe. Ndugai amesema pia kuwa katika Mkutano huu wa kumi na Tatu Serikali itawaailisha Bungeni Miswada ya Sheria ifuatayo ambayo itasomwa kwa mara ya kwanza:-

(i) Muswada wa Sheria ya Maji na Usafi wa Mazingira ya Mwaka 2018;

(ii) Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 4) wa Mwaka 2018; na

(iii) Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa Mwaka 2018;

(iv) Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania wa Mwaka 2018; na

(v) Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Usimamizi wa Nchi Kavu wa Mwaka 2018.

Kwa upande mwingine Mhe. Spika amesema kuwa, Muswada wa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha wa Mwaka 2018 (The Microfinance Bill, 2018) ambao umewasilishwa kwa hati ya dharura utasomwa Mara ya Kwanza na hatimaye kupitishwa na Bunge katika Mkutano huu.

4. Maazimio

Spika Ndugai amesema pia kuwa Serikali imewasilisha Maazimio yafuatayo kwa ajili ya kufanyiwa kazi na Bunge:-

(i) Azimio la kuridhia Itifaki ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika kuhusu kulinda Hatimiliki za Wagunduzi wa Aina Mpya za Mbegu za Mimea (Protocol for Protection of New Varieties of Plant [Plant Breeder’s Rights] in the Southern African Development Community – SADC);

(ii) Azimio la kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Kuzuia Matumizi ya Silaha za Kibaiolojia na Sumu [Convention on Prohibition of Development, Production and Stockpiling of Bacteriological (biological) and Toxin Weapons and on Destruction – BTWC]; na

(iii) Azimio la Kuridhia Mkataba wa Takwimu wa Afrika (African Charter on Statistics).

Bofya hapa kusoma ratiba ya mkutano huu wa Bunge

Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's