Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Eng. Atashasta Justus Nditiye

Supplementary Questions
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, itakumbukwa kwamba miaka ya 1990 tulipokea wakimbizi kutoka Burundi na wakawekwa kwenye kambi ya wakimbizi ya Nduta. Baada ya hali ya amani kurejea, ile kambi ilifungwa, Serikali ikawapatia wananchi kuanzisha kijiji cha mfano cha Nduta.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wakimbizi hali ya amani iliyokuwa siyo nzuri tena Burundi, wakimbizi tena walirejea na Serikali ikawaomba wale wananchi waondoke kwa ahadi kwamba itawalipa fidia. Sasa ni lini wananchi hao watalipwa fidia yao? Swali la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ujio wa wakimbizi mara nyingi pamoja na mambo mengine huwa ina athari za kimazingira na kimiundombinu hasa barabara na maji. Kuna ombi ambalo Kiwilaya tulitoa na Serikali ya Mkoa ikatuunga mkono kuhusu miundombinu ya maji kwa kuwa ujio wao umesababisha kuongezeka kwa watu wanaotumia miundombinu ile ile ya maji na barabara…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa naomba uulize swali tafadhali.
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Mheshimiwa Naibu Waziri anajua, juzi juzi alikuwa Kibondo na akajua kwamba tumepeleka ombo UNHCR kwa ajili ya kupata maji.
Je, Serikali imefanya msukumo gani hadi sasa hivi ili tuweze kupatiwa maji?
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Mimi nilitaka kujua kuhusu kipande cha barabara kutoka Kibondo kwenda Mabamba kilometa 45 ambacho Mheshimiwa Waziri alizungumza kwamba kitajengwa kwa kiwango cha Lami. Lakini katika vitabu vyake vya bajeti imetengewa milioni 80, hiyo ni kwa ajili gani? Ahsante.
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina swali moja la nyongeza.
Ninaamini Mheshimiwa Waziri anafahamu kwamba zahanati karibu nane zimekwishapata umeme kupitia mradi wa REA Awamu ya Kwanza na ya Pili, lakini hazijaunganishwa.
Je, ni lini Wizara ina mpango wa kuunganisha umeme kwenye Zahanati hizo nane?
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nataka kujua, kwa kuwa sekondari nyingi sasa zina maabara na baadhi ya sekondari hizo kata zake zimekwishapitiwa na umeme, lakini Sekondari hazina umeme ni jukumu la Wizara au ni nani mwenye jukumu la kuingiza umeme kwenye shule hizo? Ahsante.
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Katika Wilaya yangu ya Kibondo, Jimbo la Muhambwe, kuna Chuo cha MCH ambacho kwa muda mrefu sasa karibu miaka mitano wamejaribu kujenga maabara, wamekwishafikia mpaka ngazi ya kupaua, wamekwishaweka mbao mwaka wa pili na nusu sasa na hakijapauliwa. Ni lini Serikali itapeleka pesa kwa ajili ya kupaua jengo hilo la maabara?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya kutia moyo ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Kwa kuwa migogoro ya ardhi katika Halmashauri zetu na hasa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo imekuwa mingi sana, je, Serikali ina mpango gani wa kuziwezesha ofisi za Kanda ku-speed up utoaji wa hati ili kupunguza migogoro ya ardhi? (Makofi)
Sehemu ya pili, moja kati ya vitu vinavyosababisha migogoro mikubwa sana ya ardhi, hasa mijini ni uwepo wa baadhi ya watumishi wa Idara ya Ardhi wasiokuwa waaminifu katika Halmashauri zetu, watumishi hawa wamekuwa wakikaa muda mrefu sana sehemu moja ya kituo cha kazi. Je, Serikali ina mpango wowote wa kuwabadilisha mara kwa mara ili kujenga mahusiano mazuri kati ya wananchi na watumishi hao wa Idara ya Ardhi? Ahsante.
MHE. ENG. ATASHASTA J.NDITIYE: Mheshimiwa Mwenyekiti nashukuru sana, jina langu ni Atashasta Justus Nditiye au Engineer Nditiye inatosha. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wawekezaji wazawa Green Field Plantations walianza mchakato wa kufuatilia eneo hilo toka mwezi wa pili mwaka jana na tuliwapa ushirikiano namshukuru sana Mkuu wa Wilaya pamoja na wananchi wa Jimbo la Muhambwe, lakini ilipofika mwezi wa nane ameondoka mpaka sasa hivi ninapoongea hajarudi. Tunadhani ni muhimu sana tupate mwekezaji competitor kwa ajili ya ku-speed up suala la yeye kuja kufanya shughuli za uwekezaji kama tunavyotarajia ili wananchi wasije wakakata tamaa. Ni lini Serikali inafikiria kutafuta mwekezaji mwingine ikiwezekana hata wa kutoka nje ili kuweza kuwekeza katika Kiwanda cha sukari? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika kuelekea kwenye sera ya viwanda katika nchi yetu tuna wabunifu wengi sana na katika Wilaya yetu ya Kibondo kwa mfano, kuna kijana amebuni magodoro yanayotumia mifuko ya plastic na kila alipojaribu kuwasiliana na COSTECH kwa ajili ya ushauri wamekuwa hawampi ushirikiano wa kutosha. Ni lini Serikali inajipanga kuwaongezea uwezo COSTECH ili wanapopata maswali kutoka kwa wabunifu wadogo wadogo waweze kuwatembelea na kuwapa ushauri? Ahsante.
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Gereza kuu la Wilaya ya Kibondo pamoja na kuhudumia Watanzania na mahabusu kwa wafungwa, linahudumia vile vile mahabusu na wafungwa kutoka nchi jirani ya Burundi kwa maana ya Wakimbizi kwa wingi sana. Lina upungufu mkubwa sana wa maji na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la UNHCR liliahidi kwamba litasaidia kuleta mradi wa maji kwa Gereza lile na taarifa tulishazitoa mpaka kwa Waziri wa Mambo ya Ndani. Je, Srikali imefikia hatua gani kuwalazimisha sasa wale watu wa UNHCR walete maji katika Gereza hilo la Kibondo? Ahsante. (Makofi)
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwa kuwa Hospitali ya Wilaya ya Kibondo ndiyo hospitali vilevile inayotumika kama Hospitali ya Rufaa kwa Wilaya ya Kakonko, lakini inatumika kama Hospitali ya Rufaa kwa wakazi kutoka nchini Burundi, kwa maana ya wakimbizi wapatao laki mbili. Serikali ina mpango gani wa kuongeza majengo kwenye hospitali hiyo ambayo hayajawahi kuongezwa kutoka mwaka 1971?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwa sababu hiyo hiyo Serikali ina mpango gani wa kuongeza mgawo wa dawa ili kuweza kukidhi mahitaji ya wananchi wa Wilaya ya Kibondo?
MHE. MHANDISI ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba tu kwanza nimpe taarifa tu kwamba maji yalitoka ndani ya miezi sita tu kama na siku nane halafu mpaka sasa hivi toka 2010 lile gereza halina maji ya uhakika na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wakati huu mradi unatengenezwa kipindi kile tulikuwa hatuna wakimbizi sasa hivi ninapoongea 2015 tumepokea wakimbizi 120,000 na kati ya hao kuna wahalifu mbalimbali ambao nao wanatumia gereza hilo hilo ambalo kipindi hicho kulikuwa na upungufu wa lita 39,000. Tunapozungumzia kwamba maji ni uhai na kwa kuwa na idadi ya wafungwa sasa imeongezeka, Serikali ina mpango gani wa dharura hata wa kuwashirikisha UNHCR ambao ndiyo wana dhamana ya wakimbizi katika kutatua tatizo hilo? Hilo ni swali la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa sheria inawapa kinga wafungwa wa kisiasa na wafungwa wengi ambao wanatoka kwa wakimbizi siyo wa kisiasa, ni wafungwa wa makosa ya kawaida na kwa kuwa sasa wameanza kurudishwa makwao, Serikali haioni umuhimu sasa wa kuwarudisha wale wafungwa ambao wako kwenye gereza ili kupunguza idadi ya wafungwa? Ahsante. (Makofi)
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwa miaka mingi sana hadi mwaka jana mwanzoni, wananchi waliruhusiwa kufanya shughuli za uvuvi ndani ya hifadhi pamoja na ufugaji nyuki. Lakini toka mwaka jana mwanzoni Serikali ilipiga marufuku na wananchi wakiingia kule wananyanyaswa sana ikiwa ni pamoja na kupigwa na wafanyakazi wa Idara ya Wanyamapori na Wahifadhi.
Je, ni lini Serikali itaruhusu wananchi, waendelee kufanya shughuli za uvuvi na ufugaji nyuki, kwa kuwa kwa kufanya hivyo, itajenga mahusiano mazuri kati ya Serikali na wananchi?
Swali la pili, sehemu kubwa ya hifadhi hiyo ya Moyowosi haina alama kwenye mipaka yake na kwa kuwa wananchi wanakuwa wakinyanyaswa sana kwa ajili ya kufanya shughuli zao ambazo walikuwa wamekwisharuhusiwa na Serikali, ni lini sasa Serikali itakuwa tayari kuweka alama hizo za mipaka? Ahsante.
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mepesi mepesi ya ndugu yangu Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, inaonyesha jinsi ambavyo mtiririko wa project management engineering pattern usivyokuwepo katika majibu yake ya swali ya msingi. Haiwezekani leo Serikali inapanga kuchukua kufanya usanifu wa kina na kuandaa vitabu vya zabuni halafu wakati huo huo mtaalam mshauri anaendelea na usanifu ambao unatakiwa kwisha mwezi Julai, 2017, wakati mtu wa Environmental Impact Assessment hajafanya kazi yake. Hiyo inanipa mashaka kama kweli huu mradi upo au haupo. Sasa naomba Serikali itoe tamko kama kweli huu mradi upo na utaanza lini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, amezungumzia kiasi cha shilingi milioni 300 zilizotolewa kwa ajili ya Mji wa Kibondo kupanua miundombinu. Hata hivyo, ninayo uhakika na yeye Mheshimiwa Naibu Waziri niliwasiliana naye mwezi wa Aprili mwanzoni, kwamba kuna milioni 300 zilizotolewa kwa ajili ya Mji wa Kibondo toka mwaka jana bajeti iliyopita hii tunayoimalizia, lakini ziliendelea kuchezewa chezewa pale Mkoani mpaka sasa hivi tunavyoongea pesa haijaenda Kibondo. Lakini tunaambiwa tuna milioni 300 zina…

MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka nijue hiyo milioni 300 anayoizungumza kwamba itatolewa mwaka huu ni ile tuliyodhulumiwa Kibondo mwaka jana au inakuwa carried forward au ni ya mwaka huu? Naomba kujibiwa. (Makofi)

Hon. Dr. Tulia Ackson

Speaker

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Ms. Nenelwa J. Mwihambi

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's