Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Luhaga Joelson Mpina

Supplementary Questions
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi hii. Kwa kuwa barabara ambayo ameitaja Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Meatu Mheshimiwa Leah Komanya ni barabara ambayo pia inaungana na barabara ya kutoka pale Mwabuzo ikaenda Kabondo, Itinje, Mwandwitinje mpaka Mwaukoli na inaunganisha na zote hii inatoka Bariadi nyingine inatoka Meatu zinaenda zote Mkoa wa Tabora na Wilaya ya Igunga.

Mheshimiwa Spika, sasa kwa sababu mapendekezo haya yote tuliyapeleka kwa pamoja kama ambavyo Naibu Waziri wa Ujenzi amejibu, sasa anaweza kunihakikishia kwamba haya maombi yote yanafanyiwa kazi kwa pamoja na muda mfupi ujenzi utaanza wa barabara hizi sasa kuwa za mkoa na baadaye ujenzi kuanza mara ili kuondoa changamoto zilizopo kwa sasa kutokana na TARURA kushindwa kumudu kukidhi mahitaji yake?
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijauliza swali langu la nyongeza nimeshindwa kujizuia kumpongeza Dkt. Tulia Ackson kwa kuchaguliwa kwa kura zote kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Mwenyezi Mungu ambariki ili atekeleze haki za Watanzania hapa Bungeni. Baada ya hayo, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa majibu haya yaliyotolewa, mrai wetu huu wa kufua umeme wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere hauwezi kukamilika kama mkataba ulivyosema. Tulipokuwa kwenye Kamati ya Bajeti mwezi wa 11 Waziri alikuja mbele ya Kamati akaieleza kwamba sababu za mradi huu kuchelewa ni Mkandarasi kukaidi dizaini iliyowekwa na wataalam ya kujenga mahandaki matatu kwa ajili ya kuchepusha maji, lakini badala yake alijenga handaki moja, jambo ambalo lilimfanya achelewe sana kukamilisha kazi hiyo, kwa hiyo ndiyo sababu kubwa ya msingi; na sababu za UVIKO-19 zilikataliwa; na majibu haya yako kwenye Hansard za Kamati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tena wamekuja na majibu mengine, wanasema kwamba ni kuchelewa kwa mitambo ya kubebea ile milango ya vyuma (hoist crane system), ndiyo iliyochelewa kufika na mradi huu kuchelewa kwa sababu ya UVIKO-19.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa sababu majibu haya yanakanganya, kwenye Kamati chini ya Hansard waliyakataa majibu hayo kwamba hayana ukweli wowote na wakasema kwamba majibu sahihi ni kwamba huyo alikuwa mzembe na kwamba watam-penalize kwa ucheleweshaji atakaoufanya wa kuchelewesha mradi huu ambao unacheleweshwa na Watanzania. Sasa Mheshimiwa Waziri atuambie; Kamati ni sehemu ya Bunge, na hapa wamekuja na majibu mengine, na ushahidi wa Hansard upo. Nini majibu ya Serikali ya kuchelewesha mradi huu, kwa sababu majibu mawili tayari yametolewa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni kuhusu katakata ya umeme inayoendelea na mgao wa umeme unaoendelea hivi sasa. Mwanzo tulielezwa kwamba sababu ya mgao wa umeme unaoendelea sasa hivi ni kwa sababu ya matengenezo ambayo hayakufanyika kwa miaka mitano, ndiyo maana wako kwenye maintenance. Baada ya muda mfupi tena tukaambiwa kwamba ni kwa sababu ya mabwawa yanayotumika kufua umeme kukauka na yamekauka kwa sababu ya mifugo pamoja na ukaidi wa binadamu. Sasa hivi tena, wakati huo huo TANESCO nao wanasema kwamba hakuna mgao wa umeme, baadaye TANESCO wanatangaza mgao wa umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hebu tuelezwe na Serikali; kwa sababu suala la katakata ya umeme na mgao wa umeme hivi sasa linaathiri sana Watanzania; viwanda vinafungwa, wananchi wako kwenye dhiki kubwa, huduma za afya zimevurugika, huduma za maji zimevurugika. Kwa ujumla Taifa liko kwenye hali ngumu ya ukosefu wa umeme…

MWENYEKITI: Umeeleweka Mheshimiwa, umeeleweka.

MHE. LUHAGA J. MPINA: …tupate majibu sahihi ya Serikali ni nini kinachosababisha hali hii ya kukatikakatika kwa umeme kuendelea?
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nasikitika sana kwa majibu haya yaliyotolewa na Serikali. Kipindi cha miaka minne toka mwaka 2018 mpaka leo Serikali inazungumzia suala la tathmini, inazungumzia suala la upembuzi yakinifu, miaka minne! Wananchi wa Simiyu wamechoka na hizi danadana za Serikali, leo tunataka tuambiwe nini sababu zilizozuia mradi huu kujengwa ili tujue, kwa sababu huwezi kutuambia hadi miaka minne unazungumzia tathmini, unazungumzia upembuzi yakinifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni nchi yetu imekuwa ikiagiza bidhaa za nguo kutoka nje ya nchi kutokana na ukosefu wa viwanda kama hivi, tunaagiza bidhaa za nguo kutoka nje tunatumia fedha nyingi za kigeni kuagiza bidhaa za nguo nje ya nchi. Lakini pia wananchi wa Tanzania wanateseka kwa kukosa soko zuri la pamba kwa sababu ndani ya nchi hakuna viwanda na kugeuka kuwa soko la wakulima wa nchi zingine kwa kununua bidhaa zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ajira zetu tunazi-export kila leo; Serikali ituambie ni lini Serikali itachukizwa na mambo haya na kuingia kwenye uwekezaji wa viwanda vya pamba ili wakulima wa pamba waweze kupata bei nzuri na tuweze kunufaika na valua addition la zao la pamba? (Makofi)
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Taarifa ya CAG ya mwaka 2019/2020 na mwaka 2020/2021 kesi hizo nilizozitaja zimesajiliwa katika Mabaraza yetu; Baraza la Rufani za Kodi (TRAT) na Bodi ya Rufani za Kodi (TRAB) zilisajiliwa kesi hizi zenye thamani ya trilioni 360 na hivyo kama majibu ya Serikali kwamba hakuna kesi ya trilioni 360 wakati kwa mujibu wa Taarifa ya CAG hizi kesi zilikuwa zimesajiliwa na Mabaraza haya; hizi kesi zipo wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, zipo taarifa za uhakika kwamba katika mwaka huu wa fedha Serikali iliamua kupokea shilingi bilioni 700 kupitia katika hizo kesi za shilingi trilioni 360 na katika kipindi cha Disemba, 2021 na Februari, 2022 Serikali ilipokea fedha hizo na kuzifuta kesi zenye thamani ya shilingi trilioni 360. Kwa nini Serikai iliamua kupokea fedha bilioni 700 badala ya shilingi trilioni 360 kama madai halali ya nchi? (Makofi)
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, kwanza nasikitika kwamba swali limeuliza shilingi trilioni 360 lakini limejibiwa shilingi trilioni 4.21. Hata hivyo, ninayo maswali mawili ya nyongeza: -

La kwanza, kwa nini Serikali iliamua kukubali kupokea shilingi bilioni 700 kutoka katika kesi za malimbikizo ya makampuni ya madini maarufu “makinikia” badala ya shilingi trilioni 360 ambayo ni madai halali katika nchi yetu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, nini kilichowafanya TRA washindwe kukusanya malimbikizo ya kodi yasiyo na kesi ya shilingi trilioni 7.54 na kusababisha ongezeko hili la malimbikizo ya kodi kufikia asilimia 94.6 lakini wakati huo huo uwezo wa TRA wa kukusanya malimbikizo hayo umekuwa ukishuka kila wakati na kufikia asilimia 10 tu na wakati huo TRA ikijivuna kwamba inaongeza makusanyo ya kodi?

SPIKA: Mheshimiwa Mpina kwanza nipate ufafanuzi; swali linazungumzia kesi 1,097; shilingi trilioni 360 na hizo Dola za Kimarekani milioni 181.4.

Mheshimiwa Naibu Waziri jibu linazungumzia mashauri kuwa 854 ambayo thamani yake ni shilingi trilioni 4.21 na dola za Kimarekani milioni 3.48. Haya ndiyo mashauri yaliyopo ambayo Serikali inayajua ambayo ni tofauti na ya Mbunge au mmechagua kati ya yale ambayo yapo, mmeamua kuyajibia haya ambayo mmeleta majibu? Nataka kuelewa kwanza hapa. (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Hayo ni mashauri ambayo yapo na Serikali tunayatambua.

SPIKA: Mheshimiwa Waziri, naona umesimama. Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, ufafanuzi wa hiyo sehemu ya kwanza, halafu nimpe fursa ya kujibu yale maswali mawili.
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza suala la kuvunja sheria hapa halipo kwa sababu tayari hawa wananchi wameshashinda kesi mahakamani na Mahakama ikawapa ushindi na ikaamuru mifugo yao warejeshewe.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; Waziri wa Maliasili na Utalii wakati anahitimisha bajeti yake alisema mifugo hiyo itarudishwa mara moja; na Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokutana na kikao cha wafugaji wote nchini aliagiza mifugo hiyo wairejeshwe lakini sasa hivi…

SPIKA: Uliza swali Mheshimiwa Mpina ulishatoa maelezo marefu sana.

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, swali ninaloliuliza hapa orodha ipo Wizarani na Waziri anayo orodha kwa nini anakwepa hapa kuwalipa hao wafugaji wanyonge ambao wameshashinda kesi mahakamani na kutudanganya hapa kwamba hiyo orodha hana?
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Moja; Serikali ina makakati gani wa dharura wa kudhibiti biashara holela, uingiaji wa mikataba mibovu na usimamizi hafifu wa sheria ambazo kasoro hizo zinasababisha ajira nyingi za Watanzania kupotea?

Mbili; kwa nini Serikali isiachane na utaratibu wa sasa hivi wa baadhi ya ajira kupatikana kwa njia ya uteuzi na badala yake ajira zote zikapatikana kwa njia ya ushindani, ajira za Viongozi na ajira za Watendaji, Mawaziri, Wakurugenzi na Makatibu Wakuu na Watendaji wengine wote wa Serikali ili kuiwezesha Serikali kupata Viongozi wenye uwezo usiotiliwa mashaka katika nafasi mbalimbali za Serikali? (Makofi)
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Moja, kwa nini Wizara na TRC waliacha bei ya ushindani ya shilingi bilioni 9.1 kwa kilometa moja ya standard gauge na kuamua kumpa kampuni ya CCECC kwa shilingi bilioni 12.5 kwa kilomita moja ya standard gauge na kuisababishia hasara Serikali ya shilingi trilioni mbili ambayo ni kinyume na matakwa ya single source kama alivyoeleza?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Ni kwa nini Serikali isivunje huo mkataba baina ya TRC na CCECC wa ujenzi wa kipande cha Tabora - Kigoma kwa sababu hata hiyo Lot III, Lot IV anayoi-refer CAG ameshatuambia kwamba tayari walikiuka utaratibu wa sheria. Kwa nini Serikali isifute huu mkataba wa kinyonyaji?
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu hayo mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, kwa kuwa tathimini iliyofanywa na Wizara Novemba 2021 ilibaini kwamba jumla ya bilioni 83 za bidhaa za dawa pamoja na bidhaa za afya zilikuwa zimeibiwa.

Je, Serikali ilichukua hatua gani na imechukua hatua gani kwa hao watumishi ambao wamefanya ubadhilifu wa dawa hizo kwa ajili ya wananchi kwa ajili ya kutolea huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa, uwezo wa Bohari ya Dawa (MSD) kusambaza dawa pamoja na bidhaa nyingine za afya ni asilimia 59 tu. Hii inatokana na malimbikizo ya madeni ambayo ni zaidi ya bilioni 259, lakini pia mtaji wa bilioni 593. Je, Serikali inatoa tamko gani kumaliza matatizo haya, ili kuiwezesha taasisi yetu ya MSD kuwa na uwezo mkubwa wa kusambaza dawa pamoja na bidhaa nyingine za afya kwa maslahi ya wananchi wetu?
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi. Kwa kuwa chanzo kikubwa cha migogoro ya wananchi na wanaoishi katika maeneo ya hifadhi na wahifadhi ni mipaka pamoja na alama zinazoonekana, lakini pia ni pamoja na kuzuia matumizi mseto katika maeneo ya WMA kinyume na mikataba iliyofungwa katika uanzishaji wa WMA hizo: Je, Serikali ina mkakati gani mahususi wa kuondoa changamoto hizo ili kuwezesha wananchi kuishi kwa ushirikiano mwema na wahifadhi?
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Kwa kuwa, Serikali imeendelea kukaidi na kukiuka sheria katika uingiaji na usimamizi wa mikataba ya uziduaji ambayo ni madini gesi na mafuta na pamoja na matakwa yale ya TEITI lakini pia kuna matakwa ya Sheria Kifungu 12 cha (The Natural Wealth and Resources (Permanent Sovereignty) No. (5) Act, 2017) ambayo…

MWENYEKITI: Mheshimiwa swali.

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ambayo inataka mikataba yote iletwe hapa Bungeni. Kwa nini Serikali inaendelea kukiuka matakwa haya ya kisheria? (Makofi)
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, Serikali kupitia TARURA, Mkoa wa Simiyu iliahidi kujenga Daraja la Mto Sanjo linalounganisha Itilima na Meatu na Daraja la Mto Sanga linalounganisha Maswa na Meatu kwa muda mrefu. Je, ni lini Serikali itatimiza azma yake hiyo?
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi. Kwanza niipongeze sana TRA kwa hatua walizozichukua kuongeza uwezo wa kukagua hii miamala ya transfer pricing, ikiwemo ununuzi wa Kanzidata ya Orbis na kuiwezesha Serikali kupata mapato stahiki. Sasa ninayo maswali mawili ya nyongeza:-

Swali la kwanza; hizo hatua ambazo amezizungumza Mheshimiwa Naibu Waziri zimesaidia kwa kiwango gani kuongeza mapato ya Serikali?

Swali la pili; ni kauli gani Serikali inatoa juu ya ongezeko kubwa la taarifa shuku juu ya fedha haramu ambapo miamala ya usafirishaji wa fedha kwa njia ya kielektroniki na fedha taslimu imeongezeka kutoka trilioni 123 hadi trillioni 280 mwaka wa 2023. Sasa ishara hii inaonesha kwamba, kuna ongezeko kubwa la rushwa, ufisadi, transfer pricing, elicit financial flow, capital flight, sasa haya matukio haya kwa ongezeko hilo la hizi takwimu Serikali inatoa kauli gani kama FIU ilivyotoa taarifa? (Makofi)
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi. Kwa kuwa Serikali katika Jimbo la Kisesa ilishaahidi kujenga mnara katika Kata za Isengwa, Mbugabanya, Mwabusalu, Mwakisandu, Lingeka na Mwabuma: Ni lini Serikali itatimiza azma yake hiyo ili kuboresha mawasiliano katika kata hizo? (Makofi)
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa hili tatizo la ajira ni tatizo kubwa sana hapa nchini hivi sasa. Je, kwanini Serikali isifanye tracer study na kuandaa database ya vijana wote wanaohitimu mafunzo ili kuweza kuwatambua, kuweza kuwafuatilia na kujua namna nzuri ya kuwapatia ajira Serikalini pamoja na sekta binafsi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwanini Serikali isiandae mfumo mzuri wa kuwakopesha hawa vijana, wale wanaotaka kuingia kwenye ujasiriamali hata walau mtaji wa Milioni 20 wa kuanzia na wakajidhamini kwa vyeti vyao vya vyuo? (Makofi)
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa usambazaji na ugawaji wa mbolea katika msimu wa kilimo 2022/2023 uligubikwa na changamoto nyingi ikiwemo wakulima kuuziwa mbolea feki, mbolea nyingi kutoroshwa lakini wakulima wengi kupelea mbolea na kusababisha hasara kubwa.

Je, katika msimu huu wa kilimo 2023/2024 Serikali imejipanga vipi kutatua changamoto zilizojitokeza mwaka jana na kuleta hasara kubwa kwa wakulima?
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa sababu kubwa ya kushuka kwa bei ya pamba ni makato makubwa yanafanywa na Bodi ya Pamba, ambapo mwaka 2021 kwa kilo moja walikata shilingi 400; mwaka 2022 walikata shilingi 300 kwa kilo moja; na mwaka huu 2024 napo watakata.

Je, ni nani anayeruhusu viwango hivi kukatwa na kusababisha wananchi kupata bei ndogo ya pamba?
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa usambazaji na ugawaji wa mbolea katika msimu wa kilimo 2022/2023 uligubikwa na changamoto nyingi ikiwemo wakulima kuuziwa mbolea feki, mbolea nyingi kutoroshwa lakini wakulima wengi kupelea mbolea na kusababisha hasara kubwa.

Je, katika msimu huu wa kilimo 2023/2024 Serikali imejipanga vipi kutatua changamoto zilizojitokeza mwaka jana na kuleta hasara kubwa kwa wakulima?
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri kwa kweli ya Naibu Waziri lakini ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, maboresho aliyoyasema Mheshimiwa Naibu Waziri ni makubwa. Je, hayo maboresho yametusaidia kuongeza kaguzi kiasi gani ikilinganishwa na kaguzi zilizokuwepo ambayo ilikuwa ni asilimia 1.2 kati ya makampuni 504 yanayojihusisha na miamala ya transfer pricing?

Swali la pili, Je, maboresho hayo yaliyofanywa na TRA yametuwezesha kuokoa fedha kiasi gani zilizokuwa zinapotea kutokana na kukosekana uwezo ndani ya nchi wa kukagua miamala ya transfer pricing?

Hon. Dr. Tulia Ackson

Speaker

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Ms. Nenelwa J. Mwihambi

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's