Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Dr. Jasmine Tiisekwa Bunga

Supplementary Questions
MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukarabati unahitaji fedha za kutosha na Chuo Kikuu cha Mzumbe kwa muda mrefu kina madai halali sana kutoka Serikalini ambapo chuo kinaidai Serikali kama vile fedha za ada kutoka Bodi ya Mikopo. Fedha hizi zingeletwa mapema zingeweza kusaidia kufanya ukarabati. Je, ni lini sasa Serikali itaweza kulipa madeni haya ili Chuo Kikuu cha Mzumbe kiweze kufanya marekebisho haya madogo madogo na kukifanya chuo hiki kiweze kuwa na muonekano mzuri kuliko ilivyo sasa hivi?
MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu haya, maana kwa siku nyingi sana tulikuwa tumeahidiwa na majibu yalikuwa hivi hivi, lakini haya mpaka tumepewa date kwamba Juni tutapata hiyo x-ray digital tunashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri napenda kuuliza maswali ya nyongeza kwamba; kwa kweli pamoja na kupata hiyo digital x-ray lakini bado kuna huduma nyingine ya mashine za kisasa ambazo zitasaidia hawa majeruhi kuweza kuchunguzwa zaidi. Kwa mfano tumeshuhudia hivi majuzi Waheshimiwa wenzetu Wabunge walivyopata ajali ilibidi wakimbizwe haraka sana kwenda Muhimbili kule kwa ajili ya uchunguzi zaidi, lakini kama tungekuwa na mashine hizi tungesaidia hata wagonjwa kuokoa usumbufu na maisha yao na gharama; mashine hizo ni MRI na CT-Scan.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ninaomba kuuliza, je, Wizara ni lini sasa mtatuletea pia katika Hospitali hii ya Mkoa wa Morogoro mashine za MRI na CT-SCAN ili kupunguza hata rufaa kule Muhimbili na kupunguza msongamano lakini pia kuokoa maisha ya wagonjwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia pale Morogoro kama tunavyoona ile hospitali inapokea wagonjwa wengi sana wa ndani ya mkoa lakini pia na mikoa mingine. Sasa bado kuna huu usumbufu ambao unapata wagonjwa kwamba operating theatre ya mifupa haipo wanatumia theatre moja, je, ni lini sasa pia Serikali itatenga fedha za kujenga theatre hii ili kuokoa maisha ya wagonjwa na kuondoa usumbufu? Ahsante.
MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante Naibu Waziri kwa majibu mazuri, napongeza Serikali kwa mpango mzuri ambao wameueleza. Hata hivyo, kama alivyozungumza kwenye majibu yake, ameonesha kabisa kwamba milima hii ina ikolojia ya pekee, bioanuai adhimu, lakini kuna mifuko ambayo imeanzishwa kwa Hifadhi ya Tao la Mashariki na utekelezaji wa mradi wa miaka mitano kuanzia 2016 – 2021 pamoja na vijiji vinavyozunguka, napongeza kwa hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia sasa kwenye hii Milima ya Uluguru, kwa sababu uhifadhi sio lazima uwe pale kwenye chanzo, maana yake pamoja na hills yaani vijilima vyake. Lakini ukiangalia kwa sasa hivi pale Manispaa ya Morogoro ile milima iliyozunguka kuanzia maeneo ya Kilakala, Bigwa, Kigurunyembe na Pangawe ambayo hapa kuna vyanzo vikubwa sana vya maji ambao wakazi hawa wote niliowataja wa Bigwa, Kigurunyembe na Kola tunategemea maji kutoka kwenye milima hii, lakini mito hii imekauka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inasababishwa na uharibifu mkubwa ambao unaendelea sasa hivi kwenye milima hii ya Bigwa, Kigurunyembe, Pangawe ambapo sasa watu wanajenga kwa kasi kubwa sana ndani ya ile misitu, wanakata ile misitu yaani… (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba kwa sababu pia pale kuna Mbega wale weupe na ndege ambao ni adimu. Je, Serikali imechukua hatua gani kusimamisha na kudhibiti ujenzi huu holela ambao unaendelea katika milima hii ambayo ni vyanzo vikubwa vya maji? Ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri bado kidogo ayajaniridhisha kwa sababu mimi nilitembelea Mikumi pale 2016 na majibu niliyopewa ni haya haya kwamba mwekezaji amepatikana na ukarabati unaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa namwomba Mheshimiwa Naibu Waziri anihakikishie hapa huu ukarabati utamalizika lini ili tuweze kupata mapato ya uhakikika? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili ni kwamba mbuga hii ya Mikumi ipo katikati ya barabara ambayo inaenda mikoani na nje ya Tanzania. Kulikuwa na mpango wa kuanzisha road toll ili kuweza kupata mapato zaidi katika mbuga hii ambayo inakumbana na changamoto nyingi, miundombinu na hata magari ya kuzuia ujangili.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kujua, ni lini Serikali itaanzisha ushuru huu kwa sababu mchakato ulishaanza, sasa kuna kigugumizi gani? Hii itasaidia mbuga hii iweze kupata mapato na kukabiliana na changamoto ili iweze kuboresha na kuongeza mapato zaidi? Ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Mheshimiwa Naibu Waziri nakushukuru sana kwa majibu mazuri. Kwa kweli hicho ni kilio cha muda mrefu kwa wananchi kuhusu bili na kuhusu upatikanaji wa hizi pre-paid meters.

Mheshimiwa Spika, katika jibu la Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba Serikali imeagiza Mamlaka zote nchini kuendelea kuwafungia wananchi; swali langu ni kwamba: Je, ni lini sasa wamewaagiza muda wa kumaliza kufunga hizi meters? Maana isije ikachukua muda mrefu, tuweze kuwapunguzia adha hii ya bili kubwa na wananchi waweze kupata maji kwa bili ambayo ni ya uhakika.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza. Namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri yenye matumaini hasa kwa mwaka huu kutengewa hizo shilingi milioni 34, lakini hii barabara ya Kidiwa - Tandali imeshafanyiwa upembuzi yakinifu, ingawa sasa hizo fedha zitatafutwa mpaka lini? Hapo sasa napenda kufahamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri kwamba Tarafa ya Mgeta kama alivyotembelea miaka ya nyuma, landscape yake bado ni ile ile ya milimani na watu wanaishi milimani. Kwa sasa tunategemea barabara hii kubwa moja toka Sangasanga kwenda mpaka Nyandila - Kikeo. Barabara hii ni mbovu sana hasa wakati wa masika; na tulishaahidiwa. Nakumbuka miaka ya 1970s alipokuja Mheshimiwa Abdu Jumbe aliahidi kwamba tutatengenezewa kwa kiwango cha lami. Ni kweli naweza nikalia.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Rais Mstaafu, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete alipokuja aliahidi kwamba barabara hii itatengenezwa kwa kiwango cha lami kulingana na ubovu wake na nauli inakuwa kubwa: Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi yake ya kujenga barabara hii ya Sangasanga mpaka Nyandila kwa kiwango cha lami?

Swali la pili. Katika kutatua changamoto za usafiri katika Tarafa hii ya Mgeta, wananchi wamejitolea kutengeneza barabara nyembamba za kupita pikipiki, lakini wanakutana na changamoto ya utaalamu; wakati mwingine hawajui barabara iende hivi, kwa hiyo, wanakutana na changamoto hizo, lakini pia wanakutana na changamoto sehemu nyingine inabidi ijengwe madaraja au karavati.

Je, Serikali sasa iko tayari kuungana na wananchi hawa wa Tarafa ya Mgeta ili kupeleka wataalam pamoja na kuwajengea madaraja ili tuweze pia kutumia usafiri wa pikipiki kuunganisha vijiji na Kata? Ahsante.
MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake kuonyesha kwamba Serikali inatambua mchango wa wazazi ambao wamehangaika kutulea hadi kufikia hapa tulipo. Tukumbuke kwamba hata vitabu vitakatifu vya Mungu, kwa mfano amri kumi za Mungu ni amri ya nne pekee ambayo inatoa na ahadi kwamba ukiheshimu wazazi utapata baraka na utaishi miaka mingi duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kutatunza wazazi, wenzetu ambao wazazi wapo hai ni vizuri, it is a blessing. Tuendelee kuangalia wazazi wetu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nina maswali mawili ya nyongeza kwamba Je, Serikali ipo tayari kutunga sheria itakayowabana watoto hawa wanaotelekeza, ili waweze kuwatunza wazazi wao?

Mheshimiwa Spika, swali la pili: Je, wakati tunasubiri hiyo sheria kutungwa, Serikali ipo tayari kuweka Dawati la Wazee ili waweze kusikilizwa katika malalamiko yao, hasa kwa wale ambao wanatelekezwa na watoto wao? Ahsante.

Hon. Dr. Tulia Ackson

Speaker

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Ms. Nenelwa J. Mwihambi

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's