Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Maftaha Abdallah Nachuma

Supplementary Questions
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza;

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini ujenzi ule kimsingi umesimama na hakuna kinachoendelea pale Hospitali ya Mitengo.

(a) Je, ni lini sasa Serikali itaanza kuendeleza ule ujenzi wa Hospitali ya Kanda pale Mitengo?

(b) Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ujenzi wa hospitali hii bado umesimama na wananchi wa Kanda ya Kusini na hasa wale wa Mtwara Mjini wana changamoto za kupata matibabu bora ya tiba, lakini kimsingi kwamba Hospitali ya Ligula, hospitali ambayo ni Hospitali ya Mkoa hakuna x-ray, x-ray zimeharibika na ni muda mrefu hivi sasa wananchi wanahangaika kutembea umbali mrefu kwenda kufuata x-ray Mkoa wa Lindi na Dar es Salaam. Je, Serikali ipo tayari hivi sasa kuleta x- ray mpya ambazo zitaweza kutumika kwa ajili ya kuboresha tiba za wananchi wa Mtwara?
MHE. ABDALLAH N. MAFTAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Naomba niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kwa muda mrefu Serikali ilikuwa na mpango wa kuhakikisha inatoa huduma za afya bure kwa wazee, lakini kumekuwa na mkakati na utaratibu wa kutoa bima ama kadi za matibabu kwa wazee ambazo zina mipaka. Kwa mfano, mzee wa Mtwara Mjini akienda Mtwara Vijijini kule hana nafasi ya kutibiwa japokuwa ana zile kadi. Je, Serikali ina mkakati gani sasa hivi wa kuondoa mipaka ya kadi za matibabu za wazee? (Makofi)
MHE ABDALLAH N. MAFTAHA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
(a) Kwa kuwa Mtwara Mjini kila kipindi cha masika maji huwa yanajaa na mafuriko yanatokea na Serikali inatoa kilo 16 za unga, je, Serikali iko tayari hivi sasa kusema tarehe ngapi itaanza ujenzi wa miundombinu Mtwara Mjini?
(b) Kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri kadanganywa katika jibu lake nililiouliza kwamba Barabara ya Mikindani- Lwelu itajengwa lini kwa kiwango cha lami, yuko tayari hivi sasa kufuatana na mimi kama Mbunge ili aweze kujionea mwenyewe kwamba kadanganywa? Ahsante
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Nashukuru Mheshimiwa Spika, kwa kiasi kikubwa swali langu lilikuwa na sehemu mbili hivi, lakini limejibiwa swali moja tu.
Nilikuwa nimezungumza kwamba tatizo la maji kwa Mikoa hii ya Kusini na hasa miundombinu yake ambayo imejengwa tangu ukoloni ni miundombinu hafifu sana. Kwa mfano, mradi ule wa maji wa Makonde umejengwa mwaka 1953 na mpaka hivi sasa navyozungumza unatoa maji kwa asilimia 30 tu kwa sababu ya miundombinu yake ni hafifu. Naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Kwa kuwa katika majibu yake ya msingi Mheshimiwa Waziri amezungumzia suala zima la mradi wa maji wa Mto Ruvuma na akasema kwamba upembuzi yakinifu umekamilika na wananchi watapata maji na vijiji takribani 25 vinavyopitia lile bomba ambalo linatarajiwa kujengwa wataweza kunufaika na mradi huu wa maji.
Mheshimiwa Spika, swali tangu mwaka 2015 mpaka hivi sasa navyozungumza wale wananchi wameambiwa maeneo yale ambayo maji yatapita au ule mradi utapita wasiendeleze yale maeneo na hawajalipwa fidia hata senti moja mpaka hivi sasa, je, ni lini wale wananchi watapewa fidia ili waweze kutumia zile fedha kwenda kununua maeneo mengine waweze kuendeleza kilimo?
Mheshimiwa Spika, imekuwa ni kilio kikubwa sana Mtwara Mjini na maeneo mengine ya Kusini, kwamba watendaji wa Idara za Maji wanavyokuja kusoma mita hawasomi zile mita na wamekuwa wakikadiria malipo ya mita kila mwezi, wanaona usumbufu kwenda kuzipitia mita wakati mwingine na kuleta usumbufu mkubwa kwa wananchi na kuwabambikia fedha nyingi za kodi ya maji kinyume na taratibu na kanuni. Naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri kwamba mwaka huu mwezi wa pili Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maji alitembelea kule Mtwara na wananchi waliandamana kwa ajili ya tatizo hili, naomba atoe majibu ya uhakika kwamba ni lini sasa Serikali itakoma kukadiria mita za maji...
SPIKA: Mheshimiwa Nachuma yaani umehutubia.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: ...na badala yake waende kusoma mita?
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa shule hii ni siku nyingi sana imezungumzwa na Serikali kwamba itapandishwa hadhi kuwa shule ya Kidato cha Tano na Kidato cha Sita, lakini siyo kweli kwamba hii shule ina upungufu wa matundu ya vyoo, mimi shule hii naifahamu sana. Mwaka jana yamejengwa matundu 16, tatizo ni mabweni.
Swali langu la kwanza; je, Serikali ipo tayari hivi sasa kutenga bajeti ya kutosha ili shule hii ya Mchinga Sekondari waweze kujenga mabweni kwa ajili ya kupokea wanafunzi wa Kidato cha Tano na cha Sita? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, amezungumza hapa Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba shule ya Kidato cha Tano na cha Sita, mwanafunzi kutoka Lindi na maeneo mengine anaweza kupangiwa mkoa wowote, lakini shule hizi za Kidato cha Tano na cha Sita Tanzania zina matatizo mengi ya chakula na wanafunzi wanakula milo ambayo siyo kamili, wanakula maharage ya kuoza maeneo mengi. Swali langu; Serikali iko tayari hivi sasa kuhakikisha kwamba inapeleka bajeti ya kutosha ili wanafunzi wa Kidato cha Tano na cha Sita Tanzania waweze kupata milo kamili?
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza. Nimesikitishwa sana na maelezo ya Mheshimiwa Naibu Waziri pale alivyoeleza kwamba Manispaa ya Mtwara Mikindani imetenga maeneo kama vile Likonde, Mbae na Mjimwema.
Mheshimiwa Naibu Spika, ikumbukwe maeneo haya ni Tarafa mbili tofauti; na siku ya tarehe 21 mwezi wa Nane, Serikali iliweza kubomoa vibanda vidogo vidogo ambavyo vimejengwa katika Kata ya Jangwani, Tarafa ya Mikindani ambapo ni kilometa takribani 10 kwa maeneo aliyoyataja ambapo kuna akinamama wafanyabiashara wadogo wadogo wanauza samaki kihalali kabisa katika maeneo yale. Cha ajabu wale samaki wao wamevunjwavunjwa na kumwagwa. Akinamama wale walikopa pesa kutoka katika mabenki na taasisi mbalimbali za kifedha na mpaka hivi sasa ninavyozungumza hawana uwezo wa kulipa mikopo ambayo wamekopa.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu ni kwamba, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari hivi sasa afuatane na Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini ambaye anazungumza, aje kuangalia mazingira yale ambayo wale akinamama wamebomolewa maeneo yao ya kuuza samaki ambapo ni mbali takriban kilometa 10 kutoka eneo ambalo amelitaja yeye?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. MAFTAH A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru niweze kuuliza swali la nyongeza. Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua kabisa kwamba Serikali iliweka mkakati wa kuhakikisha ya kwamba maeneo yote ambayo limepita bomba la gesi kitaalam wanaita mkuza wa gesi, kwamba vijiji vile na mitaa ile itakuwa imepatiwa umeme kupitia REA Awamu ya Kwanza, Pili na ya Tatu. Lakini mpaka sasa hivi ninavyozungumza maeneo mengi ya vijiji na vitongoji vya Mtwara Mjini na Lindi kwa mfano Dimbozi, Mbawala Chini, Mkunjanguo na Naulongo kule kote bado hakujapelekewa umeme. Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa Serikali ukoje kuhakikisha kwamba wanamaliza tatizo hili katika ule mkuza wa gesi kwamba wapate umeme wale wananchi?
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante, nishukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, hata hivyo nina maswali mawili ya nyongeza.
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2013 wananchi wa Mtwara waliweza kuandamana kwa kiasi kikubwa sana Mtwara na Lindi wakidai namna gani kwamba rasilimali hii gesi inaweza kuwanufaisha na tunashukuru hivi sasa manufaa
hayo yanaanza kuonekana. Nilikuwa naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba ule mpango wa kuwapa wawekezaji ambao wana nia ya kuwekeza Mtwara gesi waweze kutengeneza ama wajenge viwanda vya mbolea umefikia wapi mpaka hivi sasa?
(b)Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naomba kujua, kulikuwa na mkakati na mwaka jana tulielezwa ndani ya Bunge hili kwamba kuna usambazaji wa gesi asilia kwenda majumbani kwa mana kwamba mikoa ya Dar es Salaam na maeneo mengine. Nilikuwa naomba kujua mkakati huu kwa Mkoa wa Mtwara na Lindi upoje kwa sababu tulipewa tu taarifa kwamba upembuzi yakinifu umeshaanza nataka kujua mimi kama Mbunge sina taarifa nao. Ahsante sana.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Ahsante Mheshimiwa Mwenyekiti naomba kwa namna ya kipekee nishukuru kwa sababu suala hili la ulipaji wa maeneo haya fidia hii ni suala la muda mrefu sana kwa kuwa Wizara hii ya TAMISEMI na Wizara ya Ardhi imekubali sasa kulimaliza suala hili tunashukuru kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini, lakini hata hivyo nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, nilikuwa naomba kujua sheria inatueleza kwamba kwa kuwa maeneo haya yamechukuliwa mwaka 2012/2013 ni muda mrefu hivi sasa wananchi wale wamekosa maeneo ya kulima na kufanya shughuli zao za kimaendeleo, je, Serikali ipo tayari kulipa pamoja na fidia ya nyongeza?
Swali la pili, kwa kuwa ahadi hii ya kuwalipa wananchi hawa Jimbo la Mtwara Mjini ni la muda mrefu, je Mheshimiwa Waziri yupo tayari kulithibitishia Bunge hili kwamba wananchi wa Mtwara Mjini wa maeneo haya ya Mji mwema na Tangira kwamba tarehe hizo walizotaja ni kweli wataenda kulipa fidia? Ahsante.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo hili la kutokuwa na mawasiliano katika jimbo hilo la Momba linafanana kabisa na barabara ya ulinzi ambayo inaanzia Mtwara Mjini na kuzunguka Mikoa yote ya Kusini kwamba mvua zilizonyeesha hivi sasa barabara hii haipitiki na hasa katika maeneo ya kijiji cha Kivava na Mahurunga mvua imeweza kukata madaraja na barabara hii hivi sasa haipitiki. Je, Serikali hivi sasa ipo tayari kuharakisha ujenzi wa barabara hii ya ulinzi? Ahsante.
MHE. MAFTAH A. NACHUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kabla sijauliza swali la nyongeza, naomba nifanye masahihisho kidogo. Mheshimiwa Naibu Waziri kasema eneo la Libya ni shamba la chumvi.
Mheshimiwa Spika, mgogoro huu siyo shamba la chumvi ni makazi ya watu ambao nilizungumza wakati wa bajeti hapa kwamba waliamka asubuhi wakakuta wamewekewa beacon kwamba eneo lao limeuza. Siyo shamba la chumvi. Naomba Mheshimiwa Naibu Waziri afanye masahihisho.
Mheshimiwa Spika, sasa naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, Machi 5 mwaka huu wa 2017, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikuwa Mtwara, pamoja na mambo mengine Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi alikuwepo Mtwara Mjini na alilalamikiwa kuhusu suala la mgogoro wa ulipaji wa fidia katika maeneo ambayo yamechukuliwa mwaka 2013; Mji Mwema. Akaahidi kwamba wananchi wale watalipwa pesa zao mwishoni mwa mwezi Julai, lakini mpaka leo tunapewa taarifa kwamba yule CEO wa UTT amesema hawezi kuwalipa wale watu.
Mheshimiwa Spika, naomba kujua majibu ya Wizara hii kwamba ni kweli inawatendea wananchi hawa wa Mtwara Mjini haki? Kwa sababu tangu mwaka 2013 wamechukuliwa maeneo yao, halafu leo Serikali inasema haiwezi kulipa zile pesa. Naomba tupate ufafanuzi.

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, eneo hili la Libya ambalo ni maarufu kama Mangowela, lakini wale waliochukua lile eneo kwa kuwanyang’anya wananchi eti wanawaeleza wawahamishe, wamebatiza jina wakaita Libya, lakini asili yake ni Mangowela. Sasa naomba kujua, yule mtu ambaye amewanyang’anya wananchi wale ni taasisi inaitwa Azimio na Serikali imemchukulia hatua maeneo mengi. Je, Serikali iko tayari hivi sasa kumnyang’anya ardhi ile ambayo ameidhulumu kwa wananchi na badala yake wananchi wale wameambiwa waende Mahakamani wakati wanajua kabisa kwamba anafanya ujanja kule Mahakamani? Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tatizo hili la Morogoro Kusini linafanana kabisa na Jimbo la Mtwara Mjini ambako umeme unatoka pale lakini bado kuna vijiji vingi kwa mfano Naulongo, Mkunjanguo, Namayanga na Mawala Chini kule kote mtandao wa umeme haujafika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa nimemweleza Mheshimiwa Waziri mara nyingi sana, je, yupo tayari hivii sasa kutoa kauli ya mwisho kwamba ni lini mtandao wa umeme utapita kwenye vijiji hivi nilivyovitaja? Ahsante. (Makofi)
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Kakunda, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kumekuwa na malalamiko mengi sana kwa Wakazi wa Dodoma wakiwemo Wabunge na Taasisi mbalimbali za Kiserikali kwamba ili waweze kupata huduma ya ardhi Manispaa ya Dodoma, basi kuna mzunguko mkubwa sana na mlolongo mkubwa sana.
Je, Serikali ipo tayari hivi sasa kufanya uchunguzi maalum na kuchukua hatua kwa kuwa, sasa Manispaa ya Dodoma ni Mji Mkuu kwamba tunahitaji huduma hizi ziende kwa haraka? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, zipo Taasisi za Serikali ambazo zinahamia Dodoma hivi sasa, zinataka kujenga ofisi zao hapa Dodoma, lakini bado kumekuwa na urasimu mkubwa sana taasisi hizo kupewa ardhi pale Manispaa.
Je, Serikali ipo tayari hivi sasa kuweka utaratibu maalum ili Taasisi hizi za Kiserikali ama Taasisi za Umma ziweze kupewa maeneo ya kuweza kujenga ofisi zao? (Makofi)
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, asante sana nilikuwa naomba kuuliza swali la nyongeza kwamba sasa hivi Tanzania kuna dawa hizi ambazo zinaitwa tressa medicines ambazo zinatolewa kwenye Hospitali za Rufaa ama Hospitali za Mikoa tu na kwamba kule vijijini kwenye Zahanati na Vituo vya Afya hizi dawa hazitolewi za magonjwa kama BP, magonjwa HIV, Kifua Kikuu sasa swali langu; nilikuwa naomba kujua kwa sababu wananchi wanapata tabu sana kusafiri umbali mrefu kwenda kutafuta dawa hizi kwenye Hospitali za Mikoa na Hospitali za Rufaa.
Je, Serikali ipo tayari hivi sasa kufundisha wale Medical Assistant’s kule vijijini ili dawa hizi ziweze kutolewa kule vijijini? Ahsante sana.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa tatizo la maji la Mji wa Tukuyu linafanana kabisa na Manispaa ya Mtwara Mjini, ambako kwa muda mrefu Serikali imekuwa na mpango wa kutoa maji kutoka Mto Ruvuma, lakini ule mradi mpaka hivi sasa umekwama kwa sababu kibali bado hakijasainiwa na Waziri husika. Je, ni lini Serikali itatoa kibali hiki ili zile pesa ziweze kutoka Exim Benki ya China na ule mradi uweze kutekelezwa mara moja Mtwara Mjini, kwa sababu kuna tatizo kubwa la maji? Ahsante
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, uwanja wa ndege wa Kanda ya Kusini ni uwanja ambao upo Mtwara Mjini na ule uwanja wa Mtwara Mjini nimekuwa nazungumza sana kwenye Bunge hili kwamba ni uwanja ambao hauruhusu ndege kuweza kutua wakati wa usiku, miaka ya nyuma huko taa zilikuwepo zikaondolewa. Je, mpango wa Serikali wa ahadi inazotoa kila mwaka wa kukarabati na kuweka taa za kuongozea ndege Mtwara Mjini kiwanja hiki cha Kanda ya Kusini utaanza lini.
MHE. MAFTAH A. NACHUMA: Mheshimiwa Spika, naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri, tatizo hili la maji katika Wilaya ya Nyang’hwale linafanana kabisa na tatizo la maji Mtwara Mjini na kwa kiasi kikubwa Mtwara Mjini kuna mradi ambao ulipangwa kutekelezwa kwa kupata pesa kutoka Benki ya Uchina ambapo mpaka sasa bado hizp pesa hazijapatikana.
Juzi nilikuwa namuuliza Mheshimiwa Waziri akaniambia kuna pesa zingine zimesainiwa maji yatoke Bonde la Ziwa Kitele mpaka Mtwara Mjini.
Je, Serikali iko tayari hivi sasa kutekeleza mpango wa muda mfupi wa kuchimba visima kwa kutumia gari za Idara ya Maji ambazo zipo pale Mtwara katika maeneo ambayo maji hakuna kama Kata ya Ufukoni na Likombe?
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pia nashukuru kwa majibu sahihi ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri kazungumza hapa kwamba Bandari hiyo ya Mtwara ndiyo itakuwa chanzo cha ufunguzi wa kitu tunachoita Mtwara Corridor, maendeleo ya Kusini mwa Tanzania na Afrika kwa ujumla. Naomba kujua kwamba hili gati linajengwa hivi sasa ni gati moja tu. Mkakati wa Serikali ukoje kuhakikisha kwamba wanamaliza ujenzi wa magati matatu yaliyobaki ili yaweze kukamilika magati manne?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, naomba kujua kwa kuwa Bandari ya Dar es Salaam hivi sasa ina msongamano mkubwa sana na Mtwara sasa hivi hii bandari inajengwa. Je, Serikali ipo tayari hivi sasa kuhakikisha kwamba inapunguza cargo on transit kutoka Bandari ya Dar es Salaam waweze kuruhusu Bandari ya Mtwara ili kuweza kuondoa msongamano hivi sasa? Ahsante.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza swali langu halijajibiwa. Niliuliza kwa nini Serikali haisemi ukweli ndani ya Bunge? Kwa sababu hapa nina Hansard mbili Serikali ikiahidi kulipa fidia wananchi hawa, lakini pia kuna maelezo ambayo siyo sahihi sana kwenye maelezo ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Hata hivyo nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Serikali hii ya Awamu ya Tano inafanya mambo makubwa sana, imeweza kununua ndege, imeweza kuwa na mkakati wa kujenga standard gauge, lakini pia imeweza kuweka mkakati wa kujenga Stiegler’s Gorge, inashindwaje kulipa fidia ya shilingi bilioni nane kwa wananchi wa Jimbo la Mtwara Mjini maeneo ya Mjimwema? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, naomba kujua, katika kuilazimisha Halmashauri sasa kuwaeleza wananchi waweze kupimiwa viwanja, wapo wananchi waliokubali na wengine hawajakubali. Je, kwa kuwa hili suala la Taasisi ya UTT-PID ipo ya chini ya Serikali Kuu, Serikali iko tayari hivi sasa kuja Mtwara Mjini na kuweza kutoa elimu kwa wananchi hao wa Mjimwema na Tangira ili waweze kukubaliana na maamuzi ya Serikali? Ahsante.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kumekuwa na ahadi nyingi sana na za muda mrefu kwenye mitaa ya pembezoni mwa Manispaa ya Mtwara Mikindani ambayo hakuna mawasiliano maeneo hayo na nimekuwa nikichangia ndani ya Bunge hili na kuyataja maeneo hayo kwa muda mrefu kwamba maeneo ya Namayanga, maeneo ya Naulongo, Mkunjanguo, Mbawala Chini na Mkangara, mawasiliano hayapo kabisa ya simu. Je, ni nlini Serikali hii itapeleka mawasiliano kwenye mitaa hii ambayo ni muhimu ndani ya Manispaa ya Mtwara Mikindani? (Makofi)
MHE. MAFTAH A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mtwara Mjini kuna Mradi wa Maji ambao unatekelezwa na Serikali kutoa maji Kijiji cha Lwelu kuelekea Kata za Ufukoni, Magomeni na maeneo mengine ya Mtwara Mjini lakini mkandarasi yule anasuasua sana na tayari kasha-rise certificate Wizara bado haijamlipa na mradi umesimama. Je, Serikali inatoa kauli gani ili kuhakikisha mkandarasi yule analipwa na mradi ule unaendelea haraka ili wananchi wa Mtwara Mjini wapate maji? Ahsante. (Makofi)
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Serikali ina wajibu wa kulinda mipaka yake yote ya nchi hii kwa ajili ya kujilinda na maadui mbalimbali wanaovamia ndani ya nchi yetu na ili uweze kulinda mipaka ni lazima kuwe na barabara kwenye mipaka yote, barabara ambazo zinapitika kwa muda wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka wa kusini unaoanzia Mtwara Mjini kupita Mahurunga – Kitaya – Tandahimba – Newala mpaka Ruvuma, hii barabara ilipandishwa hadhi kwa muda mrefu sasa na inaitwa Barabara ya Ulinzi. Mpaka leo Serikali inasuasua kujenga. Naomba kujua ni lini barabara hii ya ulinzi ambayo nimeitaja itajengwa kwa kiwango cha lami ili kulinda mpaka wa kusini sawasawa?
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa sababu Serikali imeweza kutambua angalau kwamba kuna shilingi milioni 92.4 ambazo Manispaa ya Mtwara Mikindani inadaiwa, kwa maana ya shule za msingi na shule za sekondari. Naomba kuuliza maswali yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, Shule ya Sekondari Sabasaba, Raha Leo, Chikongola na Shule zote za Msingi za Manispaa ya Mtwara Mikindani zinadaiwa hizi stationery kabla Serikali haijaanza utaratibu wa kupeleka elimu bure. Siku za nyuma ilikuwa michango inakusanywa kupitia kwa wazazi then zinalipwa stationery hizi ambazo zinatumika katika shule za msingi na sekondari. Ni lini Serikali italeta hizi shilingi bilioni 92.4 kwa ajili ya kulipa kwenye hizi shule ambazo zinadaiwa pale Mtwara Mjini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Mkuu wa Shule ya Sekondari na Mwalimu Mkuu wa Shule za Msingi ndiyo wanaobeba haya madeni kama yao, ni declare tu interest nilikuwa Mkuu wa Shule, nafahamu kila Mkuu wa Shule anavyotembea anadaiwa yeye. Je, Serikali inawasaidiaje hawa Wakuu wa Shule za Sekondari na Walimu wa Shule za Msingi ili haya madeni yasionekane kama ni ya kwao yawe ni madeni ya Serikali na Serikali iweze kulipa kwa wakati? Ahsante (Makofi)
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Manispaa ya Mtwara Mikindani ina mitaa mingi ambazo nguzo za umeme hazijafika na nimekuwa nikiitaja hapa Bungeni kwa muda mrefu sana, kwa mfano, Kijiji cha Mbwala Chini, Mtaa wa Naulongo, Mkunja Nguo, Kata ya Magomeni, Kata ya Ufukoni na Kata ya Mitengo maeneo mengi hayana nguzo za umeme. Nilikuwa naomba kujua kwa sababu nimeongea kwa muda mrefu ndani ya Bunge hili, kwa nini Serikali haitaki kuwapatia wananchi hawa umeme? (Makofi)
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Wakati tunapitisha bajeti hapa nilizungumza juu ya barabara muhimu sana Kanda ya Kusini inayopita mikoa yote ya Kusini, kwa maana ya Lindi, Mtwara na Ruvuma, barabara ya Ulinzi. Kwa kuwa bajeti haijasema chochote juu ya barabara hii kwamba imetengewa kiasi gani, Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara hii ili huu mpaka wa Kusini unaoanzia Mtwara Mjini maeneo ya Mahurunga, Kitaya, Tangazo, Tandahimba, Newala mpaka kule Ruvuma uweze kulindwa sawasawa pale ambapo maadui wa nchi hii wanaweza wakatokea? Ahsante.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Spika, asante. Nashukuru kwa majibu mafupi na precise ya Mheshimiwa Naibu Waziri, hata hivyo nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa utaratibu wa manunuzi ni mchakato na majibu yake hayajaeleza kwamba exactly timeframe ni lini Serikali imempa huyu mkandarasi kukamilisha mchakato wake ili ujenzi na ukarabati uanze mara moja.
Sasa nilikuwa naomba kupata majibu kwamba ni lini hasa, ni baada ya miezi mingapi huyu mkandarasi atakuwa amemaliza?
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na utaratibu huko miaka ya nyuma kwamba baadhi ya vitu vinahamishwa mikoa ya Kusini na baada ya uhuru tu mapema ilihamishwa reli lakini pia na taa za Uwanja wa Ndege wa Mtwara. Sasa nilikuwa naomba kujua kwamba ukarabati ambao unatarajiwa kufanyika katika uwanja huu utahusisha pamoja na uwekaji wa taa za kuongozea ndege ambazo zilizoondolewa miaka ya nyuma? Ahsante. (Makofi)
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Spika, asante, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini bado kuna changamoto moja ameiacha katika Korosho ambayo ni changamoto ya malipo kwamba mpaka leo Serikali inasuasua kuwalipa Wakulima waliouza Korosho zao. Wapo Wakulima ambao wamepeleka Korosho zao ghalani lakini wamelipwa pesa ambayo haikidhi au hailingani na kiwango walichopeleka. Lakini pia wapo Wakulima ambao mabodi display zinaonesha kwamba wamelipwa tayari lakini wakienda benki pesa hizo hazipo, kwa hiyo kuna malipo hewa. Kwa hiyo, nilikuwa naomba kujua Serikali kwa nini haielezi ukweli juu ya malipo ya Korosho kwa Wakulima wa Korosho.

Mheshimiwa Spika, swali la pili nilikuwa naomba kujua kwamba Serikali imekusanya Korosho hizi zikawekwa kwenye maghala Mtwara na Lindi na maeneo mengine na Korosho zinahifadhiwa haizidi miezi mitatu, Korosho zimeanza kuota hivi sasa zingine. Je, Serikali haioni kwamba inalitia hasara Taifa hili kwa kuziweka Korosho hizi bila kuzibangua?
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kuuliza swali la nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa kumekuwa na operesheni ambayo inafanywa na Jeshi la Polisi ya kusaka watu ambao wanasema hawana kazi mtaani. Cha ajabu hawa watu wanakamatwa kipindi kile cha jioni tayari wamesharudi makazini wakiwa wamepumzika barazani huko Dar es Salaam na maeneo mengine ya Tanzania hali ambayo inapelekea kujaza mahabusu zetu katika maeneo mengi ya nchi hii. Serikali inatoa tamko gani kuhusu operesheni hii inayofanywa na Jeshi la Polisi ambayo inapelekea kujaza mahabusu bila sababu?
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Naomba kujua mara nyingi nimekuwa naongea Vijiji vya Manispaa ya Mtwara Mjini nimekuwa nikivitaja vijiji hivi katika Bunge hili miaka yote mitatu na Serikali ikiwa inaahidi kwamba, inatekeleza suala la kupeleka umeme. Vijiji hivi ni Mkangara ambako Naibu Waziri alishaenda kule na akaona hali halisi, Naulongo, Mkunjanguo, Namayanga na maeneo…

NAIBU SPIKA: Uliza swali Mheshimiwa Maftah, uliza swali.

MHE. MAFTAH A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujua kwa nini Serikali haitaki kutenga bajeti ili kupeleka umeme katika vijiji hivi au mitaa hii?
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kumekuwa na utaratibu wa hizi AMCOS zetu kuajiri ama kutokuwa na vigezo vya wale ambao wanaajiriwa kwamba hawawekewi elimu ni kiwango gani na kwa kiasi kikubwa wahasibu ndiyo wanakuwa ni watu pekee wenye elimu kiasi ambacho kinapeleka kufanya hujuma nyingi sana kwenye hizi AMCOS. Naomba kujua Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba wale ambao wanafanyia kazi hizi AMCOS wanawekewa vigezo vya kielimu ili wakulima wasiweze kuibiwa kama ilivyo hivi sasa?
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kuna Wilaya ambazo zina Majimbo mawili na Wilaya hizi ziligawanywa Majimbo kwa sababu ya ukubwa wa zile Wilaya na idadi kubwa ya watu, lakini hivi sasa kuna tetesi ambazo zinatembea chini kwa chini huko Serikalini kwamba yale Majimbo ambayo yaligawanywa kutokana na ukubwa lakini pia na wingi wa watu yanataka kurudishwa kuwa Jimbo moja moja.

Je, kama hilo ni kweli, hatuoni kwamba Serikali ita-hinder utendaji wa Majimbo hayo?
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza imeelezwa kwamba TFDA ndiyo Mamlaka ambayo inashughulikia chakula na dawa, lakini kwa hali ya uhalisia TFDA yenyewe capacity yake ni ndogo sana ya kuweza kupima vinasaba vyote Tanzania nzima kwa sababu Ofisi yao Kuu iko pale Dar es Salaam na wana vifaa vichache sana.

MWENYEKITI: Uliza swali.

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu, je, ni lini Serikali itaiongezea vifaa TFDA iweze kufanya kazi yake sawasawa nchi nzima?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuna dawa pia ambazo inasemekana na wataalam wa afya, kwamba zinapelekea kuharibu miili ya binadamu na hasa zile dawa za kufanya rangi ya watu weusi iweze kuwa nyeupe, je, Serikali imechukua hatua gani mpaka hivi sasa ili kuwafanya Watanzania wengi wanaotumia dawa hizi wasiweze kupata madhara?
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Mtwara kimejengwa enzi ya Mkoloni na hivi sasa ukiingia mle ndani kinakaribia kubomoka, kinauliza kabisa niue nikuache, niue nikuache? Kila mwaka tunazungumza ndani ya Bunge na Serikali inasema imetenga bajeti. Kwa nini mpaka leo Serikali haileti fedha kwa ajili ya kukarabati kituo hiki ambacho hivi sasa kinatarajia kubomoka?
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; ili haya makampuni ya kihandisi yapate usajili, inasemekana na wahandisi wenyewe kwamba kumewekwa tozo kubwa sana na hii Bodi. Je, Serikali iko tayari hivi sasa kupunguza tozo hizo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ili uweze kujenga nyumba, angalau ghorofa moja Tanzania ni lazima upate vibali vya makampuni ya kihandisi na vibali hivyo ni lazima uwe na kibali cha architect, structure, quantity QS, Contractor na pia ulipe malipo ya halmashauri na TRA. Sasa, je Serikali haioni kwa sababu ili upate vibali hivi, fedha ya tozo ya vibali vya wahandisi inaizidi fedha uliyokuwa nayo ya ujenzi. Je, haioni kwamba Serikali kwa kuruhusu suala hili wananchi wengi wanashindwa kujenga nyumba bora nzuri?
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; hivi sasa Manispaa ya Mtwara Mikindani kumekuwa na baadhi ya Viongozi wa vyama vya siasa wa wilaya na mkoa ambao wameweza kuratibu vikundi mbalimbali kwa ajili ya kufanya uhalifu kwenye uchaguzi unaotarajia kufanyika mwaka huu 2020. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, je Serikali Mheshimiwa Waziri yuko tayari hivi sasa kuja Mtwara kuweza kuchukua ushahidi ambao nitampatia kwa mikono yangu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili Manispaa ya Mtwara Mikindani kuna baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wanachukua na kuwatumia baadhi ya askari polisi kwenda kuwafanyia hujuma Wapinzani usiku saa nane, saa tisa na kuwagongea majumbani kwao na kuwakamata bila sababu yoyote ya msingi na kwenda kuwaweka ndani eti kwa sababu tu wanafanya kazi ya kunadi Chama cha Wananchi - CUF na vyama vingine vya Upinzani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali iko tayari hivi sasa kuwachukulia hatua Askari wa aina hiyo wanaotumika kwa ajil ya Chama Tawala? (Makofi)
MHE. MAFTAH A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nimekuwa nayataja maeneo kadhaa ambayo yapo jimbo la Mtwara mjini kwa muda mrefu ndani ya Bunge hili na maeneo hayo, Naulongo, Mkunjanguo, Namayanga, na Mbawala Chini ambapo hakuna mawasiliano ya simu kabisa. Nilikuwa naomba commitment ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba ni lini atafanya ziara ya Mtwara Mjini kuja kukagua mguu kwa mguu maeneo haya ili aweze kudhibitisha kwamba maeneo haya yanahitaji mawasiliano kwa simu?
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri pale Mtwara Mjini Manispaa ya Mtwara mjini nimekuwa naulizia barabara kwa muda mrefu barabara ya kutoka Mikindani, Lwelu mpaka Dimbuzi lakini barabara ya kutoka kata ya ufukoni, Mbaye mpaka Mbawala chini. Lakini barabara ya kutoka Mtawanya mpaka Namayanga. Barabara hizi nimekuwa nikizungumza ndani ya Mbunge hapa kwa muda mrefu na hivi sasa TARURA imekuwa inasuasua kuzitengeneza barabara hizi ambazo ni muhimu kwa wananchi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuzitengeneza barabara hizi kwa kiwango cha lami?
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na matengenezo ya mara kwa mara ambayo hayakidhi haja ya barabara kubwa inayotoka Mtwara Mjini mpaka pale Mnazi Mmoja, Manispaa ya Lindi kwa sababu barabara hii imekuwa inaharibika sana kwa magari yanayosafirisha saruji kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam na Serikali inaahidi kutengeneza kwa kiwango kikubwa lakini mpaka leo barabara hii ina mashimo, wanaweka viraka vidogo vidogo lakini hairekebishwi vile ambavyo inatakiwa kujengwa.

Je, ni lini Serikali inatekeleza ahadi yake ya kutekeleza na kutanua barabara hii kwa kiwango cha lami kutoka Mtwara Mjini mpaka Mnazi Mmoja na kule Nanganga?
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza kwa kuwa hawa Wenyeviti wa Serikali za Vijiji na Mitaa wanafanya kazi inayofanana kabisa na hawa Watendaji wa Vijiji na Mitaa, lakini Serikali inawalipa Watendaji tu. Je, Serikali haioni kwamba inawabagua Wenyeviti hawa?

Mheshimiwa Spika, swali la pili kwa kuwa Halmashauri nyingi hivi sasa mapato yake yamechukuliwa na Serikali ikiwemo kodi ya majengo pale Mtwara Mjini na nchi nzima kiujumla ambayo ilikuwa inasaidia sana kupata makusanya ili kuweza kuwalipa posho kwa mujibu wa sheria hawa Wenyeviti wa Vijiji Serikali ama Vijiji vingi ama Halmashauri nyingi zinashindwa kutoa hata posho ya shilingi 20,000 kwasababu haina vyanzo vya mapato ikiwemo kodi ya majengo.

Je, Serikali ni lini itarudisha kodi hii ili halmashauri nyingi ziweze kukusanya na kuwapa posho Wenyeviti wa Mitaa?

Hon. Dr. Tulia Ackson

Speaker

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Ms. Nenelwa J. Mwihambi

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's