Parliament of Tanzania

Questions By: Hon. Atupele Fredy Mwakibete

Supplementary Questions
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini pia niseme tu kwamba barabara hii katika maeneo mengi, kama ulivyokiri kwenye jibu lako la msingi kuna baadhi ya maeneo inateleza, kuna utelezi mkali. Je, Serikali ina mipango gani kuhakikisha kwamba kwa kipindi hiki cha mvua ambapo haipitiki inaweza kujengwa kwa haraka iwezekanavyo?
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu ya Serikali ambayo wananchi wa Busekelo hawajaridhika nayo, kwa sababu wananchi hawa wako pale tangu miaka ya 1950 na mipaka imefanyika mwaka 2006/20007, ni mwaka wa tisa sasa bado wananyanyaswa sana na watu wa TANAPA.
Je, Serikali inatoa kauli gani kuhusiana na watumishi wa TANAPA ambao wanawanyanyasa wananchi na wanashindwa hata kuendeleza maeneo yao ya kilimo, shule pamoja na makanisa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, atakuwa tayari tuongozane twende akajionee kuanzia mwanzo mpaka mwisho wa Bonde la Mwakaleli ili ukajithibitishe hiyo mipaka?
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, asante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, lakini kwa mujibu wa swali nilivyouliza pamoja na majibu ambayo yametolewa ni dhahiri kwamba kwa vijiji ama Kata ambazo amezisema mimi mwenyewe ni shahidi kwamba kuna hela ambazo hazijafika hadi sasa hivi na katika jibu lake la msingi amesema zimefika. Kwa mfano Kata ya Mpata, nimepeleka mabomba zaidi ya milioni 10 lakini Serikali mpaka sasa hivi haijatoa chochote. Mheshimiwa Waziri unaweza ukathibitishia wananchi wa Mpata kwamba hizo fedha zimefika kule? Hilo ni swali la kwanza.
Swali la pili, kuna baadhi ya Kata ya Ntaba, kijiji cha Ilamba wananchi pamoja na wakazi wa eneo la pale wananyang’anyana maji, wananchi na mamba, na zaidi ya wananchi kumi na moja wameshauawa na mamba ama kuliwa na mamba kwa sababu ya kutafuta maji, je, Serikali inatoa tamko gani kwa ajili ya wananchi hawa na ikizingatiwa kwamba kuna mradi ambao umeshafanyiwa upembezi yakinifu tangu mwaka 2008 hadi leo hii kwa thamani ya shilingi milioni 100, haikufanya kitu chochote.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa niweze kuuliza swali moja la nyongeza. Mkoa wa Mbeya umebarikiwa sana kuwa na madini pamoja na vyanzo mbalimbali vya umeme. Nataka nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa mfano, kuna vyanzo vya umeme vya jotoardhi kule Busokelo lakini pamoja na Lake Ngozi, kuna makaa ya mawe, kuna maporomoko ya maji na vitu vingine katika sehemu nyingine mbalimbali. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri, ni lini vyanzo hivi vitaanza kufanya kazi ili wananchi wa Mbeya na Tanzania kwa ujumla ipate umeme wa kutosha?
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali moja. Kwa kuwa tatizo la Barabara ya Kalambo linakwenda sambamba na tatizo la barabara iliyopo Jimbo la Busokelo Wilayani Rungwe inayotoka pale Tukuyu Mjini kuanzia Katumba – Suma – Mpombo – Isange – Ruangwa – Mbwambo hadi Tukuyu Mjini; na barabara hii imekuwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi zaidi ya miaka 10: Je, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami Kilometa 73 zilizobaki?
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa Sera ya Afya inasema, kila Kijiji kijenge Zahanati na kila Kata ijenge Kituo cha Afya; nakumbuka mwaka 2007 tulikuwa na program ya kujenga sekondari kwa kila Kata na kulikuwa na uhaba mkubwa sana wa watumishi; tulikuwa tunasema ni Vodacom ama Voda faster kwa sababu tu walikuwa wanamaliza Form Six na kwenda kufanya kazi. Je, Serikali imejipangaje ukizingatia hii ni afya kwa ajili ya watumishi watakaoajiriwa kwa vituo ama vijiji 12,000 na kitu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Halmashauri ya Busokelo ni changa sana; tuna Hospitali moja tu, nayo hiyo Hospitali ni CDH kwa maana ya kwamba ni Council Designated Hospital; na tuna Kituo kimoja tu cha Afya. Je, Serikali ipo tayari sasa kushirikiana na wananchi nguvu kazi tunazozifanya ili iweze ku-upgrade Kituo cha Kambasegela, Kituo cha Afya Isange pamoja na Kanyerere?
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kwanza nimpongeze kwa jinsi ambavyo amekuwa akifuatilia suala la afya kwa Jimbo langu la Busokelo, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, je, ni lini hasa hospitali hii itaanza kujengwa ikizingatia kuwa wananchi wa Jimbo la Busokelo pamoja na Mbunge wao tupo tayari kushirikiana na Serikali kujenga hospitali hii?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, pamoja na kwamba hizi shilingi bilioni mbili ambazo zimetamkwa kwenye jibu la msingi yalikuwa ni maombi maalum, je, Mheshimiwa Naibu Waziri unaweza ukawathibitishia wananchi wa Jimbo la Busokelo kwamba hizi fedha sasa na maombi yao yamekubaliwa?
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa niweze kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tatizo la Shule ya Sekondari Ndembela linaendana sana na tatizo la Shule Sekondari ya Kandete Wilayani Rungwe ambapo sasa tumeanza kujenga ili iwe ya wasichana pekee. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anaweza akawadhibitishia wananchi wa Busokelo kwamba Serikali itashiriki kikamilifu ili ianze mapema mwakani?
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa kuwa, tatizo la Karagwe linaendana sana na tatizo la maji lililopo Jimboni Busokelo, Wilaya ya Rungwe. Je, Serikali ina mpango gani hasa katika Kata za Ntaba, Itete, Isange pamoja na Kandete kuwapelekea maji ukizingatia Kata ya Ntaba kuna bwawa la asili ambapo wananchi 12 wameuawa kwa sababu ya kutafuta maji?
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kwa masikitiko makubwa sana na nisononeke moyoni mwangu kwamba Mheshimiwa Waziri majibu aliyoleta hapa sio niliyouliza kwenye swali langu la msingi. Nimeuliza, barabara itajengwa lini ya Mkoa wa Mbeya na Njombe yeye amenitajia barabara za Katumba – Lusanje – Kandete. Nilikuwa namaanisha barabara inayotoka Mwakaleli kwenda mpaka Makete halafu iunganishwe na Njombe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini zaidi swali la pili nimeuliza Jimbo la Busokelo litaunganishwa na Jimbo la Rungwe. Lakini Waziri anasema Serikali haifikirii kufungua barabara kuunganisha maeneo hayo kutokana na milima mikali, hivyo barabara ziendelee kutumika zilizopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nisikitike kwa sababu wananchi wa Jimbo la Busokelo katika Vijiji nilivyovitamka Suma pamoja na Kilimansanga ni zaidi 5,000. Akisema kwamba waendelee kutumia barabara hizo hizo wakati tayari hakuna muunganisho wa hizo barabara nashindwa kuelewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hili swali ningeomba liweze kujibiwa kwa mara nyingine tena kwa sababu majibu aliyojibu hapa sio, hayaniridhishi.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na
majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naipongeza Serikali kwa jinsi
ambavyo wameushughulikia mradi huu wa masoko na miradi mingine iliyo ndani
ya Wilaya ya Rungwe. Nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza; kwa kuwa,
mradi huu wa maji umechukua muda mrefu na Mkandarasi aliyekuwa amepewa kazi hiyo Osaka, baada ya kutangazwa tenda ya mara ya pili anaondolewa.
Tungependa kufahamu ni sababu gani zimesababisha Mkandarasi huyu wa
mara ya kwanza ashindwane na Halmashauri?
Swali la pili; kwa kuwa, miradi hii ya maji ni ya thamani kubwa, zaidi ya
bilioni tano tungependa tumwombe Mheshimiwa Naibu Waziri aweze
kuitembelea hii miradi pamoja na ya Mwakaleli One pamoja na Kapondelo
ikiwemo na hii ya Masoko. Ahsante.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Serikali kwamba Halmashauri ya Busokelo haijakidhi vigezo vya kuwa Wilaya, nina maswali mawili kwa Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo vigezo anavyosema haijakidhi sijui ni vipi kwa sababu vigezo ambavyo vinazingatiwa, hasa ni idadi ya watu pamoja na jiografia ya eneo husika, kwetu kwa sababu hii tathmini ilishafanyika tangu miaka 2013 na sasa hivi ni 2017. Hauoni kwamba kuna
umuhimu sasa wa kuanzisha hiyo Halmashauri ya Busokelo iwe inaitwa Wilaya ya Busokelo badala ya sasa ilivyo? Swali la pili, kwa kuwa Mkuu wa Wilaya pamoja na DAS wanafanya kazi nzuri katika Wilaya ya Rungwe, kwa bahati mbaya kwa sababu ya jiografia ya Rungwe ilivyo kuna zaidi ya kata 40 na huyu Mkuu wa Wilaya hawezi kusimamia ama kufuatilia zote kwa wakati mmoja kufuatana na jiografia ilivyo.
Je, hauoni pia ni miongoni mwa sababu ambayo
inaweza ikasababisha ianzishwe Wilaya ya Busokelo na hivyo iweze kuanzishwa haraka iwezekanavyo?
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa niweze kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, wewe ni miongoni mwa
watu ambao ni washabiki na wapenzi wa ngoma za asili, pamoja na kwamba wewe ni mpenzi wa ngoma za asili, hata huku Dodoma kuna ngoma za asili zinaitwa Chigogo.
Je, Serikali imejipangaje kuwezesha wale wote ambao wanaanzisha ngoma za asili katika mashindano hayo? (Makofi)
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina swali moja tu la nyongeza. Taifa lolote duniani ili lisonge mbele linahitaji watu waliosoma kada mbalimbali, iwe ni sanaa, sayansi au biashara.
Je, Serikali ina mpango gani wa ku-balance wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi, pamoja na wanafunzi wanaosoma sanaa ili isitokee kama sasa tuna ziada ya wanafunzi wa sanaa zaidi ya 7,463 na inapelekea kutokuwa na ajira. Serikali ina mpango gani kwa miaka ya hivi karibuni na baadaye? (Makofi)
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa furda hii niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri Dkt. Mary Mwanjelwa Dada yangu niipongeze Serikali katika majibu haya.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa katika jibu lake la msingi amekiri kwamba Serikali ina vituo ama vyuo 14 kwa ajili ya kilimo hapa nchini, lakini chuo/kituo hiki kilianza kujengwa tangu 2009 na kilikabidhiwa kwa halmashauri na halmashauri imeshindwa kukiendeleza. Je, hauoni kuna umuhimu sasa kupitia Wizara yako muweze kuchukua jukumu hili ili chuo hiki kiweze kukamilika maana ni zaidi ya miaka nane hadi sasa?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, pamoja na kwamba kuna vyuo hivyo 14, tumekuwa tukitoa wataalam na watafiti mbalimbali na wanakuwa wanazalisha kwa tija; lakini changamoto kubwa iliyopo ni kwamba anapokwenda kufanya kazi ama kwenye field changamoto kubwa ni kwamba masoko ya mazao wanayozalisha yanakuwa hayapo. Wizara imejipangaje, ni mechanism gani itatumika kutafutia masoko kwa bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nchini hasa hasa katika kilimo ukizingatia kwamba mahindi sasa hivi yameshuka bei, viazi mviringo vimeshuka bei, choroko zimeshuka bei na mazao mbalimbali? Ahsante. (Makofi)
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Mbunge wa Rungwe Mheshimiwa Saul Henry Amon, Mji wa Tukuyu ni miongoni mwa miji mikongwe katika nchi hii hata utaitwa Tokyo. Lakini mradi wa Masoko aliousema Mheshimiwa Naibu Waziri una changamoto nyingi na hadi umepelekea Mkandarasi wa mara ya kwanza walipelekeana Mahakamani pamoja na Halmashauri na hata sasa amepatikana Mkandarasi mwingine, lakini Mkandarasi huyu wa pili bado naye hajalipwa fedha zake na wanakoelekea inawezekana ikawa kama Mkandarasi wa kwanza. Je, Serikali inatoa kauli gani ili akinamama ambao wanatoka mabondeni na maeneo mengine mbalimbali tuwatue ndoo kichwani ili huyu Mkandarasi aweze kulipwa fedha zake.
Swali la pili, Mji wa Tukuyu una milima, mabonde pamoja na mlima Rungwe, tuna maji ya kutosha. Hatuna sababu yoyote Serikali kutopeleka maji kule kwa sababu hata maji ya gravity tu yanatosha kwa ajili ya wananchi waweze kupata maji. Serikali inatoa kauli gani ili wananchi wa eneo hilo waweze kupata maji? (Makofi)
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa niulize swali moja la nyongeza. Ugonjwa wa UKIMWI siyo tishio kwa maana ya kuua, tishio kubwa ni magonjwa nyemelezi. Kwa bahati mbaya Serikali imekuwa ikinunua dawa hasa hasa kwa ajili ya kufumbaza Virusi vya UKIMWI aina ya TLA (Tenofovir, Lamivudine na Efavirenz). Je, ni lini Serikali itaanza kununua dawa kwa ajili ya magonjwa nyemelezi (Opportunistic Infections -OI drugs) hasa hasa Azithromycin, Fluconazole na Co- trimoxazole?
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante, wananchi wa Busekelo kwa kushirikiana na mimi nikiwa Mbunge wao tumeamua kulima barabara inayounganisha Mkoa wa Njombe na Mkoa Mbeya kwa kutumia zana za jembe la mkono.
Je, ni lini Serikali itatupa support ili tuweze kukamilisha barabara hii ambayo ni muhimu sana kwa wananchi wa Busekelo na Makete na ukizingatia kwamba…
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kabla sijauliza maswali yangu mawili ya nyongeza nataka niweke kumbukumbu sahihi kwamba mimi ni Mbunge wa Busokelo ambayo iko ndani ya Wilaya ya Rungwe.
Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba kuna sera, kuna miongozo kuna vitengo mbalimbali vya kufuatilia forensic wizi wa mitandaoni, lakini bado wizi unaendelea; Je, Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kuwatumia wataalam wetu wa ndani kushirikiana na nchi ambazo zimefanikiwa kutatua tatizo hili la wizi wa mtandaoni ikiwemo Israel ama India?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, sekta ya mawasiliano inachangia asilimia 13 ya pato la Taifa. Kwa msingi huo sekta hii ni muhimu sana, lakini Serikali bado haijaanzisha Bodi ya TEHAMA. Nchi ambazo zimefanikiwa katika TEHAMA kwa mfano Finland wamefanikiwa kugundua Nokia ukienda Korea Kusini kuna Samsung, ukienda Marekani akina Job Steve - Apple na Mataifa mengine mbalimbali. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuanzisha hii Bodi ya TEHAMA ili professionals ambao wamesoma hii TEHAMA waweze kutambulikana na kuongeza Pato la Taifa zaidi? (Makofi)
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa niweze kuuliza swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa Mkoa wa Mbeya una vivutio vya asili kama ulivyo Mkoa wa Iringa na vivutio hivyo vya asili ni kama Mlima Rungwe, Mlima Kejo, Ziwa Nyasa na maeneo mengine kama Maziwa ya Masoko, Kingururu, Iramba pamoja na Daraja la Mungu.
Je, Serikali ina mpango gani kuvitangaza vivutio hivi ili wananchi wanaoishi maeneo hayo waone umuhimu wa uwepo wa vivutio hivyo? (Makofi)
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ili niweze kuuliza swali moja la nyongeza. Mkoa wa Mbeya ni mkoa wa pili kwa wananchi wake kuwa na pato la Taifa ukitanguliwa na Mkoa wa Dar es Salaam, lakini miundombinu yake si rafiki kwa wananchi wake. Je, ni lini Serikali itatengeneza barabara iliyoahidi kutoka mchepuo wa Uyole kwenda Mbalizi pamoja na barabara kutoka Katumba, Ruangwa, Masoko mpaka Mbambo na Tukuyu yenye kilometa 83? (Makofi)
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa nami niweze kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme unaotokana na joto ardhi ama geothermal ni endelevu na sustainable ama renewable na Serikali ingeweza kutumia vyanzo vyote tungepata zaidi ya Megawati 5,000. Je, ni lini Serikali itaweza kukamilisha mradi wake ambao ilikuwa inaendelea kuufanya wa kuchoronga visima katika Ziwa Ngosi lililopo Wilayani Rungwe pamoja na Mto Mbaka uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo? (Makofi)
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali kuhusiana na swali hili, hasa hasa ujenzi wa Kiwanda cha Maziwa kule Isange, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, wananchi wa Jimbo la Busokelo hasa Kata za Lupata, Kandete, Luteba, Mpombo, Isange, Lwanga, Kabula pamoja na Itete, wanafuga sana ng’ombe wa maziwa wapatao zaidi ya 35,000 na wanazalisha lita zaidi ya milioni 54 kwa mwaka lakini mbegu walizonazo bado ni ng’ombe wale wa zamani. Je, Serikali itawasaidiaje kupata ng’ombe wapya ambapo inaweza kufanyika kitu kinaitwa uhimilishaji kwa ajili ya uzalishaji zaidi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wananchi hawa pamoja na ufugaji wao wanajitahidi sana kukusanya maziwa na kupeleka sehemu ambapo kuna matenki kwa njia ya baiskeli pamoja na pikipiki. Je, Serikali itawasaidiaje kutafuta ama kupata gari la kisasa lenye tenki ili liwasaidie kwa ajili ya kukusanya kwa wakulima na wafugaji ambao wanafuga ng’ombe hawa wa maziwa mpaka sehemu ya viwanda?
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa niweze kuuliza swali moja la nyongeza.
Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kuweza kupata nafasi ya kuja katika Jimbo langu la Busokelo, lakini nina swali moja tu kwamba ulivyokuja wana Busokelo tulikuomba kwamba vijiji vyote ambavyo vipo kwenye scope ya REA III na kwa bahati mbaya sana hivi vijiji baadhi yao vina nyumba za nyasi lakini hii leo ninavyouliza swali kwako Mheshimiwa Waziri ni kwamba vile vijiji vimerukwa. Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya Vijiji 8 ambavyo vimerukwa kwenye scope ambayo ipo sasa kwa REA III? (Makofi)
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, napenda kuweka kumbukumbu sahihi kwamba mimi ni Mbunge wa Jimbo la Busokelo na si Rungwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Halmashauri ya Busokelo ina utajiri mkubwa sana wa madini aina ya marble pamoja na carbondioxide gas. Serikali imekiri hapa kwamba madini ya marble yanapatikana katika Kijiji cha Kipangamansi, Kata ya Lufilyo. Je, ni lini Serikali itakuja kufanya tafiti katika milima ya safu za Livingstone kwani inasadikika pia kuwa kuna madini aina ya dhahabu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Waziri tumekuwa tukiongea mara nyingi kwamba atutembelee Halmashauri ya Jimbo la Busokelo ili apate kushuhudia wananchi wangu wanaojishughulisha na hizo shughuli za marble. Ni lini Waziri atakuja kuwatembelea wananchi wa Jimbo langu na kuona shughuli hizo za madini? (Makofi)
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na nimpongeze pia Waziri mwenye dhamana kwa namna ambavyo waliweza kutembelea Jimbo langu la Busokelo na kufanya mikutano mingi na wananchi wale.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa mradi huu umechukua muda mrefu, ni zaidi ya miaka 21 sasa tangu upembuzi yakinifu ufanyike, je, Serikali haioni umuhimu wa kuharakisha mradi huu ili ifikapo 2022 uweze kukamilika badala ya mwaka ambao Mheshimiwa Waziri ameusema?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa umeme wa jotoardhi ni umeme endelevu kwa maana ya renewable na tumeona katika nchi yetu na tafiti zimeonyesha tunaweza kupata megawatts zaidi ya 5,000 kwa vyanzo vyote ambavyo vimeainishwa kwa nchi nzima ya Tanzania. Je, Serikali ina mpango gani wa kuviendeleza vyanzo hivyo ili Tanzania ifikapo 2025 iwe ni nchi ya uchumi wa kati?
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwanza nisikitike kwa niaba ya wananchi wa Busokelo kwa sababu barabara hii aliitembelea aliyekuwa Naibu Waziri wa Ujenzi kipindi hicho, Mheshimiwa Eng. Ngonyani tangu tarehe 21 Novemba, 2016 na aliahidi kwamba ingetengenezwa kwa kiwango cha changarawe kilometa 7.5. Hili swali nimeliuliza Bungeni zaidi ya mara tatu na kila jibu linalokuja linakuwa tofauti na jibu lililotangulia. Wananchi wa Busokelo wanataka kujua ni lini Serikali itaunga mkono juhudi za wananchi wa Jimbo la Busekelo, Kata ya Luteba ambao wameanza kutengeneza barabara hii kwa kilometa 4 wao wenyewe kwa jembe la mkono pamoja na Mbunge wao?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa barabara hii imeanzishwa na nguvu za wananchi na kwa maana hiyo Serikali haitambui kama iko TARURA, TANROADS ama kwenye vijiji. Ni lini sasa Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari kuunganisha nguvu za pamoja za TANROADS na TARURA ili tujue ni nani atakayehusika na barabara hii? Ahsante.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nipongeze Serikali kwa juhudi pekee ya kuinua bei ya zao la chai kutoka 241 kwa kilo ya majani mabichi chai mpaka kufikia 315, na nimpongeze kipekee Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Mheshimiwa Rais kwa kutembelea Jimbo hili la Busokelo na concern yetu ya zao la chai tuliwaambia na kuunda Tume kwa ajili ya kushughulikia tatizo hili.

Mheshimiwa Spika, Bonde la Mwakaleli tuna Kiwanda cha Chai ambacho kimekuwa kikizalisha chai lakini kwa msimu, kuanzia mwezi wa Disemba mpaka Juni kila mwaka na hivyo miezi Sita mingine huwa hakifanyi kazi; Je, Serikali ina mpango gani mkakati wa kukifanya kiwanda hiki cha chai cha Bonde la Mwakaleli kiweze kufanya kazi mwaka mzima badala ya sasa tunaki- underutilize. (Makofi)

Swali la pili, hivi sasa katika Jimbo langu la Busokelo tunalima viazi mviringo na ni wakati wa msimu wa mavuno lakini bei yake ipo chini sana, kiasi kwamba hata wanunuzi wa viazi hivi wanawaibia zaidi wakulima wana-collude kwa kushirikiana na yale makampuni yanayotengeneza mifuko kwa kufanya kitu kinachoitwa lumbesa. Kwa mfano, mfuko mmoja ambao una debe tano wao wanafanya debe sita na nusu na wananchi hawa wanakuwa wamekopa wamenunua pembejeo, wamelima kwa shida, lakini bei zao ziko chini na kiasi hiki kinafanya mkulima akate tamaa kabisa kuendelea kulima zao hili la viazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, je, Serikali inatoa tamko gani wewe ukiwa Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara kuja site ili uone namna mateso ya wananchi wangu wa Bonde la Mwakaleli, Busokelo pamoja na Wilaya nzima ya Rungwe hadi Uyole - Mbeya kwamba wanahitaji masoko ya uhakika katika zao hili la viazi. (Makofi)
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Pamoja na juhudi nzuri za Serikali zilizofanywa pamoja na Kampuni hii ya Tanzania Oxygen Limited kuweza kuzuia baadhi ya wanyama watambaao pamoja na binadamu kwenda kwenye eneo hili la kisima ambacho mara nyingi miaka ya nyuma Wananchi na wanyama wengine walikufa kutokana na kuvuta gesi hii ya carbondioxide. Swali la kwanza; je, ni lini Serikali itaendelea kutoa elimu kwa wananchi ambao wanazunguka kisima hiki na kwa kuwa nguvu za asili za volcano bado zipo na volcano nii ni hai ili kuzuia madhara yatokanayo na kuvuta gesi hii ya carbondioxide?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa Serikali imeonesha nia njema kwa ajili ya kujenga viwanda hapa nchini lakini kumekuwa kuna changamoto kubwa kuingiza gesi hii ya carbondioxide ndani ya Nchi yetu ya Tanzania tukitambua kwamba carbondioxide gas inatumika katika mazingira ama kwenye vitu vingi ikiwemo vyakula pamoja na vinywaji ili visiharibike. Ni kwa kiwango gani Serikali itavutia zaidi wawekezaji kwenye maeneo mengine ambayo gesi hii ya carbondioxide bado haijaanza kuchimbwa.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa niulize swali moja la nyongeza. Matatizo ya Korogwe Mjini yanafanana sana na matatizo ya Wilaya ya Rungwe hususan Busokelo kwa kukatika katika umeme. Kwa siku umeme unaweza kukatika zaidi ya mara 10 na tatizo kubwa lililokuwepo ni kwamba, nguzo za umeme chini yake kuna miti.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru Wizara pamoja na Waziri kwa maana ya kuleta timu maalum kwenda ku-clear ama kukata hiyo miti, lakini bado tatizo kubwa limeendelea kuwepo. Ni mikakati gani Serikali iko nayo kuhakikisha kwamba wananchi wa Jimbo la Busokelo wanapata umeme masaa 24 kwa siku kuliko hivi ilivyo kwa sasa? (Makofi)
MHE. FRED A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa fursa niweze kuuliza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Wilaya ya Rungwe ni miongoni mwa wilaya ambazo zina maji mengi ya kutosha na vyanzo vingi lakini wananchi wetu hawana maji ya kutosha. Je, ni lini Serikali itakamilisha miradi ambayo imeanzisha ya maji hususan miradi ya Mwakaleli I pamoja na miradi ya masoko na Kandete pamoja na Kata za Rwangwa. (Makofi)
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa niulize swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto zilizopo Same Magharibi zinafanana sana na changamoto zilizopo Jimbo la Busokelo. Kata ya Ntaba tuna Daraja ambalo linaitwa Mto Ngubwisya, liliondolewa na maji tangu tarehe 30 Aprili, 2019 na daraja hili linaunganisha Kata za Kisegese, Itete, Kambasegera pamoja na Luangwa.

Je, ni lini Serikali inakwenda kujenga daraja hili ili wananchi wangu wa Busokelo waunganishwe kama ilivyokuwa zamani? (Makofi)
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Serikali nataka kufahamu ni hatua gani za kinidhamu zinazoweza kuchukuliwa na Serikali kwa wataalam wetu wanaosababisha variation ya miradi kuwa na gharama kubwa, kwa mfano, daraja hili la Mbaka ambalo limechukua muda mrefu sana. Kuna kitu tunaita geotechnical investigation hakikufanyika na ndiyo maana imechukua muda mrefu zaidi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa daraja hili litakapokamilika kutakuwa kuna madaraja mawili, kutakuwa kuna daraja hili ambalo linajengwa pamoja na lililokuwepo la chuma.

Je, Serikali ipo tayari kulichukua hili daraja la chuma kupeleka katika mto huo huo Mbaka lakini kwa kuweza kuunganisha kati ya Majimbo ya Busokelo, Kyela pamoja na Rungwe katika Kijiji cha Nsanga? (Makofi)
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwepo na malalamiko mengi ya wanafunzi wenye sifa za kupata mikopo ya elimu ya juu lakini hawapati hiyo mikopo; na mimi ni shuhuda kwa kuwaleta wanafunzi wa jimbo langu, kwenda Bodi ya Mikopo lakini hawakuweza kufanikiwa kupata Bodi ya Mikopo, zaidi ya wanafunzi 20.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa swali je, serikali ni lini itahakikisha kwamba wanafunzi wenye sifa hakika wanapata mikopo badala sasa takwimu zinaonesha wanapata lakini uhalisia hawapati mikopo hiyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa wale waliofanikiwa kupata mikopo, kwa maana ya ukimaliza umeweka kanuni ama utaratibu kwamba mwanafunzi akimaliza chuo kikuu mara tu baada ya kumaliza aanze kurudisha huo mkopo na baada ya miezi 24, kwa maana ya miaka miwili, asipoanza kurudisha huo mkopo mmeweka kanuni kwamba atatozwa riba ya asilimia 10.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali, kwa wanafunzi ambao hawajapata ajira na sasa ajira ni changamoto, pengine miaka mitano, mingine kumi, wengine 20 na wengine hawapati kabisa; Serikali imejipangaje kuhakikisha kwamba wanawawezesha kwanza hao wanafunzi kuwa-link na mashirika na taasisi ili fedha zilizokopwa na wanafunzi hawa zisipotee? Ahsante.
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa changamoto za stendi katika Jimbo la Arusha Mjini, zinafana sana na changamoto za kukosekana stendi katika Jimbo la Busokelo. Je, ni lini Serikali itajenga stendi za Miji ya Ruangwa, Ruangwa Mjini pamoja na Kandete?
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kabla sijauliza maswali mawili ya nyongeza naomba kwanza nikushukuru sana pamoja na Serikali kwa changamoto ambazo tulizipata Jimbo la Busokelo kwa mafuriko ambayo yalisababisha nyumba zaidi ya 30 pamoja na mtu mmoja kufariki, lakini wewe pamoja na timu yako mlikuja kutoa msaada. Ahsanteni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa niulize maswali mawili ya nyongeza, pamoja na majibu ya Serikali, huu Mradi wa Mto Rumakali upo katika halmashauri mbili kati ya Halmashauri ya Busokelo pamoja na Mkoa wa Njombe, lakini mradi huu katika utekelezaji wake inaonyesha kwamba licha ya kwamba megawati hizo zitazalishwa tunahitaji kujua wananchi wa Busokelo, je, ni kwa kiwango gani kupitia Corporate Social Responsibility ya mradi huu watanufaika wananchi wa Busokelo pamoja na Kata hii ya Lufilyo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa mradi huu utaanza kuzalishwa hivi karibuni na tunafahamu kwamba Halmashauri ya Busokelo ni halmashauri changa, je, ni kwa kiwango gani Serikali imejipanga kuboresha miundombinu kufikia sehemu ya uzalishaji wa mradi huu kupitia Halmashauri ya Busokelo hususani madaraja ya Mto Lufilyo pamoja na madaraja ya Mto Malisi? Ahsante.(Makofi)
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Serikali nina maswali mawili ya nyogeza.

Mheshimiwa Spika, kutokana na kwamba mipaka ya Hifadhi hii ya Kitulo ilikosewa kwa sababu walikuwa wanatumia vijana ambao walikuwa wakibeba zile zege au beacon na kwa kuwa zilikuwa ni nzito sana walikuwa wanatua mahala ambapo siyo mipaka. Maana wanapotua ndiyo hapo hapo wanafanya mpaka na kusababisha baadhi ya taasisi kama shule mbili pamoja na jamii/familia/kaya kuwa ndani ya hifadhi. Je Serikali iko tayari sasa kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi kwenda kurekebisha mipaka hii ili iwe na uhalisia ama original yake ilivyokuwa inatakiwa iwe? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Hifadhi ya Kitulo inajulikana kama bustani ya Mungu kwa sababu ina maua ambayo yanachua na ni hifadhi pekee kwa Afrika ambayo ina maua mazuri sana na kwa bahati mbaya sana haijatangazwa ipasavyo. Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba Hifadhi hii ya Kitulo inatangazwa ili ijulikane kama zilivyo hifadhi nyingine? (Makofi)
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa niulize swali moja la nyongeza.

Barabara ya kutoka Katumba - Suma – Mwakareli - Luwanga - Mbambo mpaka Tukuyu yenye urefu wa Kilometa 82, imeanza kujengwa kipande cha kutoka Luhangwa – Mbambo – Tukuyu.

Je, ni lini kipande cha kutoka Luhangwa - Mwakareli - Suma - Katumba kitajengwa? Ahsante. (Makofi)
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina swali moja la nyongeza. Kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa barabara hii kwa kilomita 27 na sasa bado kilomita 56. Je, ni lini hizi kilomita zilizobaki zinakwenda kusainiwa ukizingatia kwamba Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi kaka yangu Innocent Bashungwa pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Fedha walitembelea Jimbo la Busokelo tarehe Mosi Oktoba na walifanya mkutano mzuri sana. Tunawashukuru sana kwa kuja, ninyi ni mashuhuda wazuri kwamba barabara hii inahitaji kujengwa kwa kiwango cha lami. Je, ni lini itasainiwa? (Makofi)

Hon. Dr. Tulia Ackson

Speaker

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Ms. Nenelwa J. Mwihambi

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

Member of the Parliament

Hon. Zubeida Khamis Shaib

Mfenesini (CCM)

Profile

Hon. Mohamed Abdulrahman Mwinyi

Chambani (CCM)

Questions / Answers(4 / 0)

Supplementary Questions / Answers (4 / 0)

Profile

View All MP's