| E-mail this to a friend | Printable version |
|
||||||
| Session No | Question Number | To the Ministry of | Sector | Date Asked | ||
|---|---|---|---|---|---|---|
| 5 | 105 | WORKS | Transport/Road | 17 November 2011 | ||
| Mheshimiwa Spika, ninashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, ninayo maswali madogo mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:- (a) Mheshimiwa Spika, nionavyo kiasi cha shilingi milioni 93 ni kidogo kwa kazi ya usanifu, lakini hata hivyo kwa sababu amesema ni kwa ajili ya kukamilisha, ninaamini wataalam walikuwa makini katika hilo. Je, kazi hii ya usanifu itakamilika lini na ni nani anayeifanya? (b) Mheshimiwa Spika, Barabara ya kutoka Mpemba mpaka Kasumulu Boarder kule Kyela inapita mpakani mwa Malawi na Tanzania na ni barabara ya Kihistoria; umuhimu wake ni mkubwa kwa uchumi kwa hivi sasa. Mwanzoni ilijengwa kama ya ulinzi lakini sasa ni ya uchumi. Ninaomba kuuliza kwa kuwa Wananchi wa Kyela wanategemea bidhaa mbalimbali kutoka Ileje na vivyo hivyo Wananchi wa Ileje wanaitegemea Barabara hiyo; na kwa kuwa Barabara hiyo inapita kwenye miteremko mikali na inahitaji kuweka utengenezwaji ambao utakuwa wa kudumu; je, inaweza kuingizwa kwenye Mpango wa Serikali kuwekewa lami hapo baadaye? |
||||||
| ANSWERS TO SUPPLEMENTARY QUESTION # 105 SESSION # 5 | ||||||
|
||||||
| WAZIRI WA UJENZI (BARABARA NA VIWANJA VYA NDEGE): Mheshimiwa Spika, ninapenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kibona, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, fedha zilizotengwa kwa ajili ya kufanya feasibility study kwa Barabara aliyoitaja ya Mpemba hadi Isongole zinatosha. Mhandisi Mshauri anayefanya kazi hiyo ni Inter Consult Ltd. ya Dar es Salaam kwa gharama ya shilingi milioni 232.184 na fedha hizi zote zilizotolewa ni fedha za ndani. Katika fedha hizo, tumepanga pia fedha zingine ambazo zitatumika kwa ajili ya kufanya matengenezo ya kawaida katika kuhakikisha kwamba, hii barabara inapitika. Katika bajeti ya mwaka huu kuna shilingi milioni 182.5. Mheshimiwa Spika, kuhusu kutengeneza tena barabara nyingine ya lami ya kutoka Isongole kupitia Ngana hadi Kasumulo ambayo ameiomba Mheshimiwa Mbunge; ni vigumu kwa barabara zote za Tanzania kutengenezwa kwa kiwango cha lami. Kwa mfano, Barabara ya Mpemba hadi Isongole imepandishwa daraja mwaka 2009 na kuwa Barabara Kuu; lakini kuna Barabara Kuu nyingi nchini ambazo bado hazijajengwa kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, ninamwomba Mheshimiwa Mbunge, tusubiri kwanza tumalize Barabara Kuu za kutoka Tunduma – Sumbawanga, Mpanda - Kigoma zitengenezwe kwa kiwango cha lami, Barabara ya kutoka Babati – Dodoma - Iringa imalizike kwa kiwango cha lami na Barabara zingine Kuu, halafu zingine za kwenda Isongole na Kasumulu zitafuata baadaye. Ninaomba Wananchi waelewe hivyo, kwa sababu uwezo wa Serikali hauwezi ukatengeneza barabara zote kwa kiwango cha lami. |
||||||