| E-mail this to a friend | Printable version |
|
|||||
| Session No | Seating No | Contribution Date | Contribution To | ||
|---|---|---|---|---|---|
| 8 | 5 | 19 June 2012 | Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2011/2012 Pamoja na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka 2012/2013 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka 2012/2023 | ||
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi hii ya kwanza asubuhi hii ya leo. Hoja iliyoko mbele yetu ya Hoja ya Bajeti waswahili wanasema kupanga ni kuchagua. Ukilinganisha Bajeti hii na Bajeti zilizotangulia, alipokuwa anawasilisha maoni ya Kamati Mheshimiwa Mtemi Andrew Chenge alisema thamani ya shilingi yetu mwaka jana ukilinganisha na dola iliwa ni shilingi 1449.5/- kwa dola moja. Mwaka huu shilingi yetu imeshuka thamani, kwa sasa ni shilingi 1599.98/- kwa dola moja. Ukilinganisha na anguko la thamani ya fedha yetu na mfumko wa bei kutoka asilimia nane mpaka asilimia 18.7 ni kwamba Bajeti ya mwaka huu haina nyongeza ya aina yoyote. Haipo. Ukiweka kwenye uwiano huo utaona kwamba Bajeti hii ungechukua thamani ya shilingi kama ilivyo trilioni 13.5 za mwaka jana itakuwa ni sawa sawa na trilioni 14.9 ambayo ni karibu trilioni 15 hizi zinazoombwa na Serikali leo hii hapa. Mheshimiwa Naibu Spika, ukisikia michango iliyotolewa na Wabunge wote tangu jana, Tanzania ni yetu sote, ningeshauri kwamba mchango uliotoka kwa Wabunge wote uzingatiwe kwa sababu naamini wazo zuri ni zuri tu hata kama lingetoka kwa mtu ambaye hupendi sura yake. Mheshimiwa Naibu Spika, sikufurahishwa sana jana na michango yote iliyotolewa na Kambi ya Upinzani si lolote si chochote, siyo sahihi kabisa. Tanzania watu tunao, takribani milioni arobaini na tano. Kwa hivyo Human Resources tuliyonayo tukiitumia vizuri, tukatumia ardhi tuna kilomita za mraba zaidi ya laki tisa arobaini na saba elfu na mia tatu, ardhi ipo, tukirejea kauli ya mwalimu kwamba ili tuendelee tunahitaji Watu, Ardhi, Siasa Safi na Uongozi Bora, kuna tatizo kubwa kwenye siasa zetu na tuna tatizo kubwa kwenye uongozi wetu. Ninasema hivyo kwa sababu ukiangalia makusanyo yetu ya humu ndani trilioni nane, inaonesha utamaduni wetu sisi Watanzania au utamaduni uliowasilishwa hapa, yaani tuseme ni Bajeti ya utamaduni wa Watanzania wa kupenda kutumia zaidi na siyo kwenye maendeleo. Kwa sababu huwezi ukatumia zaidi ya asilimia sabini na maendeleo ukayawekea asilimia thelathini na zaidi ya asilimia hamsini ya Bajeti yenyewe ya maendeleo ikawa ni fedha ya kutoka nje. Sasa ni kwamba Je, Bajeti hii tunategemea wafadhili ili tuweze tukafanya shughuli zetu, tunategemea wafadhili ili tuweze tukasomesha watoto wetu, tunategemea wafadhili ili tuweze kufanya shughuli zetu ambazo hata za kujihudumia sisi wenyewe kwa miaka yote tangu tumepata uhuru wa Taifa hili. Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2015 tutapimwa kwa malengo ya Milenia, lengo la kwanza la milenia ni kupunguza umaskini, lengo la pili ni elimu kwa wote, lengo la tatu ni masuala ya jinsia na kuwawezesha akina mama, lengo la Nne ni masuala ya vifo vya watoto wadogo, vifo vya akina mama ni lengo la Tano, magonjwa ya Ukimwi na mengineyo, mazingira na global partnership ya nane. Je, Bajeti hii imeweka namna gani kwenye jedwali dogo tu la kuonyesha kwamba malengo ya milenia tumefikia wapi moja baada ya jingine, au ni historia ndefu tu ambayo ina confuse hata Wabunge katika kuisoma Bajeti hii. Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma zile Volumes, volume (I) mpaka (IV) inaonekana ni kuchanganya changanya tu,ingewekwa jedwali dogo zuri, hata kama mtu siyo mchumi kama mimi hapa niweze nikalielewa vizuri. Lakini kuja na tarakimu nyingi tu. Je, efficiency ya Bajeti ya mwaka jana ilifanikiwa kwa kiasi gani. Je, Bajeti hii naweza nikadiriki kusema kwamba ukisoma kwa makini na ukiangalia Bajeti hii imeshindwa hata kuondoa msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam. Mheshimiwa Naibu Spika, ninaamini kwamba Jiji la Dar es Salaam kwa takwimu ambazo zipo miaka mitatu iliyopita tunapoteza zaidi ya shilingi bilioni nne kila siku na hii inatokana na mafuta tunayotumia, muda wa kazi ambao ni zaidi ya asilimia thelathini unapotea tukiwa kwenye foleni barabarani,uchafuzi wa mazingira tunaoufanya cabondioxide inayotoka kwenye magari haya, ukiangalia uzalishaji yaani man power efficiency ya wafanyakazi wetu takribani sasa tunasema milioni kumi wanaoishi katika Jiji la Dar es Salaam, tunajiongezea umaskini siku hadi baada ya siku. Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini Bajeti hii uwezo kama ni trilioni kumi na tano, hapa nilinganishe kwamba yupo Daktari ambaye ana wagonjwa wa malaria wapo mia moja na uwezo wake wa kuwatibu ni wagonjwa ishirini na tano tu. Je, utatibu wa wagonjwa 25 ili wapone au utagawa robo robo ili utibu wagonjwa wote mia moja ili wapone? Mheshimiwa Naibu Spika, Bajeti ya miundombinu inasikitisha sana, usafiri ambao ni rahisi kuliko wote duniani wa kwanza ni maji, wa pili ni reli na watatu ni barabara na wa nne ni anga. Lakini ukiangalia Bajeti hii kwenye bandari, kwenye reli kwenye anga ni bilioni takribani mia tatu tu. Hii ni Bajeti ya kuongeza umaskini kwa Watanzania na wala siyo Bajeti ya kuleta ahueni kwa Watanzania. Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia misamaha ya kodi tunayoizungumzia, hii misamaha ya kodi ukiangalia zile taasisi ambazo zinasamehewa kodi, ukiangalia kama NGOS unaweza ukachukulia NGOs kama Aghakan Foundation, imekuwa ikipewa misamaha ya kodi tangu Serikali ya awamu ya kwanza mpaka leo hii. Je, hospitali za Aghakan zinatoa huduma zilizo bora zaidi kuliko hospitali nyingine na aghali zaidi. Je, zinawasaidia maskini hapana! Je, haki inatendeka? Je, wazawa wa Taifa hili wanaolima pamba, wanaofanya biashara ya pamba, watu wanasema no buku no cotton nakubaliana nao kabisa. Je, wanasaidiwa namna gani akina ndugu Gungu na wenzake? Je ukiwasaidia wazawa ukatoa upendeleo wa maksudi kwa wazawa ambao Watazalisha zaidi humu humu ndani, ukawa wazawa takribani kama elfu mbili ambao wana uwezo kama akina Reginald Mengi, wakaweza kuajiri watu labda elfu tano tano kila mwaka ni kwamba tatizo la ajira tutakuwa tunaajiri zaidi ya watu milioni kumi na tutakuwa tumeondokana na tatizo la ajira. Tatizo la ajira siyo la Serikali peke yake. Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kuna msemo unaosema makosa yetu ya jana japo yanasikitisha sana ni mafundisho yetu ya leo, sioni dhamira yangu inapinga. Tumeanza hapa kwa kusoma dua ya kusema ewe Mwenyezi Mungu atujalie ili tuweze kufanya maamuzi yaliyo sahihi mimi siungi mkono kabisa Bajeti hii. Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali ikubali, Waziri na Serikali yote collectively wakae, maoni yanayotolewa yote hapa warekebishe Bajeti hii kwa maslahi ya Taifa la Tanzania kwa kuwa Tanzania ni yetu sote na hakuna watu wenye Hati miliki ya kuwaongoza Watanzania milele. Hili tukilisema vizuri kwa utaratibu tutaelewana, isionekane kwamba kuna mtu mwenye mawazo bora kuliko mwingine au kila wazo lichukuliwe kwa ubora wake, kila wazo lisikilizwe kwa ubora wake na tukisikilizana vizuri ninaamini masuala ya MKUKUTA, sioni hata suala la MKURABITA huku mnasema mabenki yawepo, MKURABITA iko wapi, watu wana samani gani za kuweza kurasilisha mali zao. Kwa hivyo kuna mambo mengi ya kinadharia zaidi kuliko vitendo ndani ya Bajeti hii. Niombe efficiency, na reliability tutaweza tukafika. Mheshimiwa Naibu Spika, siungi mkono hoja hii, ahsante sana. |
|||||