You are using an older version of Internet Explorer.

In order to get the most out of our website, you can get a free update of Internet Explorer.
If you're using a work computer, please contact your IT administrator.

[CLOSE]
  email E-mail this to a friend email Printable version

Contributions

Session No Seating No Contribution Date Contribution To
8 11 27 June 2012 Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka 2012/2013 – Ofisi ya Waziri Mkuu na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia fursa hii ili kwa niaba ya wananchi wa Arumeru Mashariki niweze
kutoa mchango wangu kwenye hotuba ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nianze na tatizo ambalo limekuwa sugu kwenye sehemu mbalimbali kwenye nchi yetu na hususan kwenye Jimbo langu na Wilaya yetu ya Arumeru ambalo ni tatizo la ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, utakubaliana nami kabisa kwamba ndani ya siku chache zilizopita migogoro ya ardhi imejitokeza tena kwenye Jimbo langu la Arumeru Mashariki na mpaka kupelekea
baadhi ya watu kupoteza maisha. Nimeitafuta hotuba ya Waziri Mkuu ya mwaka jana nikalinganisha na ya mwaka huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hotuba yake ya mwaka jana Waziri Mkuu alizungumzia sana suala la ardhi na akapendekeza kwamba, Serikali inakuja na mipango ya matumizi bora ya ardhi ili kuweza kuzuia maafa ambayo yanaweza yakatokana na migogoro
ya ardhi. Lakini kitabu cha mwaka huu kwenye suala hilo hilo la ardhi kinachoonyeshwa ni hati kwenye vijiji zaidi 11,000 yaani mipaka ambayo imepimwa, lakini haioneshi ni migogoro mikubwa mingapi kati ya wawekezaji au wamiliki wa mashamba na wananchi
ambayo yametatuliwa wala hatua ambazo Serikali imechukua badala yake, suala hili limekuwa likichukuliwa kisiasa na watu wanasema kwamba vurugu zinafanyika Arumeru kwa sababu ya CHADEMA wakati mwaka 1952 kabla ya Tanganyika kupata uhuru
Arumeru walikusanya pesa wakamtuma Ayo Japhet Kiriro Umoja wa Mataifa ikiwa UNO kwenda kwa sababu ya Meru Land Case, sasa sijui kama mwaka 1952 hata kabla ya kupata uhuru sijui kama Japhet Kiriro naye alikuwa CHADEMA au CHADEMA ilikuwepo
kipindi hicho.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la ardhi tulichukue kwa umakini mkubwa sana, tumekuwa na migogoro mikubwa kwenye madini kwenye nchi yetu lakini migogoro hii iko kwenye maeneo husika yale ambayo yana madini, lakini tatizo la ardhi limekuwa ni kubwa
kabisa kwenye nchi yetu kila kona ya nchi hii na kama tukiendelea kulifumbia macho kuna tatizo kubwa mbele yetu litakuja na maafa yatazidi kujitokeza kwa wingi.

Kuna barua hapa kutoka Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, tangu mwaka 1999 na inaainisha mashamba 11 ndani ya Wilaya ya Arumeru ambayo yalipata kibali cha Rais ili yaweze kufutiwa hati, lakini mpaka leo tunapozungumza mashamba
yale yapo yamemilikiwa na watu, wananchi hawajayapata na mpaka leo yanaendelea kuzusha migogoro na watu wanaendelea kupoteza maisha.

Niseme tu kwamba sitakuwa tayari kuunga mkono hoja
kama Ofisi ya Waziri Mkuu isipotueleza kinagaubaga kwamba ni hatua gani zimechukuliwa au Serikali inakwenda kuchukua ili kuweza kuzuia matatizo haya ya ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Halmashauri zetu Madiwani wamekaa na wataalam wakaunda timu, wakaenda wakafanya utafiti na wakatoa mapendekezo yao tangu mwaka jana mwezi wa tatu, kipindi hicho sijawa Mbunge lakini mpaka leo hii ile
taarifa inaonekana haijafika Wizarani na wala Serikali haijaipata kwa ajili ya kuweza kuchukua hatua stahiki.

Niseme tu wakati mwingine tunawakatisha tamaa Madiwani na Wataalam wetu kwenye Halmashauri kwa sababu wanafanya kazi zao lakini Serikali inakuwa haiwachukulii maanani.

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee kidogo suala la matumizi yasiyokuwa ya lazima. Jana Mheshimiwa Wenje ameongea hapa na mimi leo nitaongea kuweka msisitizo kwamba leo tunazungumza kwamba nchi ina hali mbaya kiuchumi na kifedha halafu tunajadili bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Wakuu wa
Mikoa wote wako Dodoma, wasaidizi wao wako Dodoma, Madereva wao wako Dodoma, Ma-RAS wako Dodoma, wapo hapa sijui wanafanya nini!

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini simaanishi kwamba sitaki kuonana na Mkuu wangu wa Mkoa lakini tunaonana kwenye RCC, tunaonana kwenye Road Board na tunaonana Mikoani. Sasa kuna haja gani ya wao kuwa hapa ndani wakati ofisi zao
hazifanyi kazi sasa hivi mikoani? Hizi ni kazi za televisheni
ambazo tumenunua ambazo zipo kwenye Ofisi za Wakuu wa Mikoa, wakae kule waangalie kama wanataka kufuatilia Bunge waangalie huko wakati wanaendelea kuwatumikia wananchi kwani hakuna sababu yoyote ya msingi ya wao kuwa hapa, walipiwe
hoteli, per diem, chakula na wasaidizi wao pia. Kwa kweli nafikiri ni matumizi mabaya ya fedha za Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini siyo hivyo tu kwamba leo hii tunazungumzia hali mbaya kwenye nchi halafu bado tunazidi kuongeza Baraza la Mawaziri, halafu kama haitoshi Rais anamteua mtu anampa Uwaziri asiyekuwa na Wizara Maalum, sasa nikajiuliza hivi huyo plate number ya gari lake
itaandikwa Waziri wa nini, sijui ofisi yake iko wapi, sijui
anawahudumia akina nani? Sijui tunaongea nini hapo
kwa sababu matumizi mabaya ya mali za umma imekuwa ni tatizo kubwa na linaimbwa kila siku kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee suala la uwekezaji na uwezeshaji. Kuna suala linaitwa EPZ na kwenye Jimbo langu la Arumeru Mashariki kwenye Kata ya Kirero, eneo la Marura wananchi mashamba yao yamechukuliwa, ni kwa miaka sasa na mpaka leo hakuna hata mmoja amepata fidia na hatujui
wanapewa lini fidia na kwa rate ipi. Napenda Ofisi ya Waziri Mkuu ituambie kwamba ni lini watu hawa wanakwenda kupewa fidia zao na kama Serikali haipo tayari watu warudishiwe ardhi ili waendelee kufanya kilimo mpaka pale Serikali itakapokuwa tayari.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee suala la rada, chenji ya wizi wa fedha za rada. Zaidi ya shilingi bilioni sabini kwa mujibu wa kauli ya Waziri Membe zina uwezo wa kujenga nyumba za Walimu zaidi ya 1196, zina uwezo wa kujenga vyoo 200,000
kwenye shule zetu pia. Hizi fedha pia zingekuwa na uwezo hata wa kuchonga na kununua madawati kwa ajili ya shule zetu lakini mpaka leo hii tunavyozungumza bado wananchi vijijini wanasumbuliwa kila mwaka madawati, mtoto anakwenda shule akimaliza mdogo wake naye anaingia shule naye anaambiwa aje na dawati, kila siku! Na kuna watu tunajiuliza…

Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo ni kengele ya kwanza!

Mheshimiwa Naibu Spika, tunajiuliza kwamba hizi fedha wanadai
zinarudishwa na nakupongeza Mheshimiwa Naibu Spika kwamba na wewe ulikwenda ukahakikisha kwamba unazirudisha na kwa sababu wewe ni Naibu Spika, huwezi kuzungumza humu ndani, lakini sisi tutakusemea na watu wa Kongwa kwamba hata kule
nyumba za Walimu zitajengwa, vyoo vitajengwa na mabati vile vile yapelekwe. Lakini ni lazima tufahamu kwamba, hawa watu wamechukuliwa hatua gani au wanachukuliwa hatua gani kwa sababu itakuwa ni tendency ya kila siku kwenye nchi, watu wanapiga pesa zisipostukiwa poa, zikishtukiwa zinarudishwa
chenji, lakini hatua stahiki hazichukuliwi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri tuna kila sababu ya kuwa serious zaidi katika hili suala la watu waliohusika wachukuliwe hatua za kisheria ili kwamba tujiridhishe ili wengine wasiendelee kufanya hivyo kwa sababu huu utakuwa ni wizi wa kila siku na hii biashara itakuwa ni business as usual na hatupo tayari
kuendelea na suala hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, niungane na Wabunge wenzangu wanaotokea kwenye Majimbo yanayolima Kahawa. Kumekuwa na tatizo kubwa sana kwenye kilimo cha kahawa na wananchi wananyanyasika kwani gharama za utunzaji na kulima kahawa
zinakuwa kubwa kuliko ile bei wanayokwenda kununua sana sana kwa sababu ya soko huria, watu ambao wameruhusiwa kwenda kununua kahawa mbichi.

Watu wanajipangia bei, hao hao ndiyo Mawakala, halafu ukienda kwenye soko hao hao ndiyo wahusika vile vile.

Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri kuna haja ya Serikali kutoa kauli kwamba wakulima wasiuze kahawa mbichi yaani ya maganda kwa mawakala wa soko huria ili waweze kupata stahiki zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niongelee suala la utalii. Kwenye hotuba ya Waziri Mkuu ameongelea suala la kukuza utalii na kuutangaza utalii kupitia Balozi zetu. Juzi nilikuwa Marekani na nilikwenda kwenye Ubalozi wetu wa Tanzania nilichokikuta pale ni
brochure ambazo zimewekwa pale kwa wale ambao wanatembelea ni sisi wenyewe Watanzania, sasa sijui kama tunakwenda kujifunza utalii Marekani ili tuje kwenda Ngorongoro Tanzania, sielewi.

Mheshimiwa Naibu Spika, halafu unakwenda sehemu kama Arusha kwenye eneo la Kisongwe, kwenye jengo la TANAPA unakuta imewekwa ile screen kubwa ya fedha nyingi ambayo inatangaza mbuga za wanyama wakati mzungu anayepita ile barabara ni yule ambaye tayari yuko barabarani kwenda safari.
Nafikiri hizi screen ziwekwe kwenye airport kubwa kama Heathrow, JFK na hata Amsterdam kwamba tutangaze utalii wetu nje ya nchi, lakini mnakwenda kutuwekea screen Kisongwe wakati tupo safarini kuelekea mbugani sasa sijui tunatangaza utalii gani na ni utalii gani unaotangazwa Tanzania wakati tunaifahamu
Ngorongoro vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba sitakuwa tayari kuunga mkono hoja mpaka maswali yote yapatiwe majibu sahihi.