You are using an older version of Internet Explorer.

In order to get the most out of our website, you can get a free update of Internet Explorer.
If you're using a work computer, please contact your IT administrator.

[CLOSE]
  email E-mail this to a friend email Printable version

Contributions

Session No Seating No Contribution Date Contribution To
7 7 18 April 2012 Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.

Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye leo imempendeza kwamba Nassari na yeye nae ni Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niwashukuru sana wananchi wa Arumeru Mashariki kipekee ambao waliamua kuchagua utu dhidi ya fedha, ambao waliamua kumchagua yule ambaye hajaoa kwa sababu hakuja kusuluhisha ndoa Bungeni, ambao waliamua kumchagua asiyekuwa na kitambi kwa sababu hatujaja kucheza mieleka na ambao walimchagua kijana mdogo wakiamini anaweza kuwa dogo janja akayafikisha matatizo yao Serikalini na panapohusika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeipitia taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu ya Serikali Kuu na kwa kweli wakati nikiisoma nikajiuliza maswali mengi sana; nikajiuliza hivi hii ni nchi au ni SACCOS? Kwa sababu unashangaa kwamba watu kila siku wanachota pesa kama unavyoweka kwenye SACCOS kesho unakuja unachota, keshokutwa unachota. Ukienda China, wanadai kwamba ukila rushwa, ikisadikika kwamba umekula au umetoa rushwa adhabu yako unanyongwa. Leo tunasema kwamba bidhaa za Kichina ni fake, lakini sheria zao sio fake, za kwetu ndio fake.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona mapungufu kwenye matumizi mabaya ya fedha za umma. Manunuzi yanafanyika bila kufuata taratibu na kanuni au sheria zilizowekwa. Ukiangalia kwenye kitabu hiki, naomba kunukuu, tunaelezwa kwamba kwa mwaka wa fedha 2009/2010 manunuzi ya umma shilingi bilioni 50, milioni 685 na vilaki kadhaa na pesa zingine kwamba hizi zote zilitumika kufanya manunuzi ambayo hayakufuata taratibu au sheria ya manunuzi ya umma na kwenye hizi fedha unaambiwa kwamba Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali, iliongoza kwa kutumia shilingi bilioni 49. Sasa hii ni Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali ambayo Watanzania wanaamini kwamba ndio wanaofahamu vizuri Sheria za Manunuzi na ndio wanaopaswa kuzifuata kwa usahihi, halafu ndio wanaoongoza kutokuzifuata sheria hizi wakati wakifanya manunuzi kwa kutumia fedha za umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile ripoti inaonesha kwamba kumekuwa hakuna kumbukumbu, kumbukumbu za fedha za manunuzi hazitunzwi. Leo ni aibu unakuta shilingi bilioni 362 hizi fedha ukiongeza kidogo tu ni sawasawa na nusu trilioni ambazo zina uwezo wa kulipa walimu mishahara zaidi ya 100,000 kwa mwaka mzima kwenye nchi yetu. Lakini hizi fedha zimetumika na kumbukumbu hazitunzwi yaani hazionekani, nyaraka ni pungufu maana yake ni nini? Hatuna uhakika kama kweli haya manunuzi yalifanyika au hizi fedha ziliishia kwenye
mifuko ya watu wachache.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sio hayo peke yake, kumekuwa na matumizi ysiyokuwa ya ulazima. Ripoti inaonesha kwamba mpaka tarehe 30 Juni, 2010 magari ya Serikali yenye thamani ya shilingi trilioni tano, ina maana Serikali yetu inamiliki magari yenye thamani ya shilingi trilioni tano na kila siku baada ya siku magari yanazidi kununuliwa, magari ya gharama kubwa na magari ambayo uendeshaji wake vilevile ni wa gharama kubwa kupindukia. Sasa hii ni aibu kwamba tunaambiwa tunamiliki magari ya shilingi trilioni tano, wakati ukienda kwenye Majimbo yetu, ukienda Arumeru Mashariki, hakuna magari ya wagonjwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sio hivyo peke yake, lakini vilevile unakuta kwamba hata haya magari yanavyonunuliwa Japan, gharama ambayo Serikali inatumia ni tofauti na gharama halisi ambayo mtu binafsi akienda kununua magari haya anakuwa analipa. Hii inaonesha kwamba kuna wizi mkubwa tena wa mchana kweupe. Sasa hii inasikitisha sana kwamba unakuta Wizara mbili kwenye Serikali yetu hazina majengo zinapanga; wanapanga na kwa Wizara ya Afya peke yake wanalipa shilingi milioni 38 kila mwezi. Maana yake kwa mwaka wanalipa shilingi milioni 456. Kwa miaka mitatu, miaka minne peke yake kwa hizi fedha ambazo wanalipa kwenye pango, Wizara ina uwezo wa kujenga ofisi na ikajitosheleza, zikatumika kwa miaka mingi ijayo tukaacha kuendelea kulipa
kodi kuliko kulipa pango. Hii ni aibu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndio sababu tunafika mahali tunaingia huku Bungeni mahali ambapo tunaamini kwamba hili ndilo jengo kuu la kufanya maamuzi kwenye nchi yetu, halafu anakuja Waziri siku ya jana anakwambia hajaiona ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwenye ukaguzi maalum wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS). Halafu leo asubuhi anakuja Naibu wake anatuambia kwamba hiyo ripoti anayo. Halafu cha ajabu, mimi hapa mkononi hiyo ripoti ninayo, ni Mbunge mpya, nimeingia huku juzi; halafu Waziri, anasema hana. Sasa mimi hii inanishangaza na kwa kweli napata wasiwasi sana, sijui ni mahali gani tunapolipeleka Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi nakubaliana kabisa na mapendekezo yote yaliyotolewa na Kamati. Mapendekezo yote yaliyotolewa na Kamati, nafikiri yanapaswa kuungwa mkono na Wabunge wote across parties bila kujali tofauti ya vyama vyetu kwa sababu kazi tuliyotumwa huku ni kuja kuwasimamia Watanzania na ninasikitika kwamba leo tunajadili fedha za wananchi lakini Waziri wa Fedha hayupo. Jana tulikuwa tunachagua Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki, hili Bunge lilikuwa limejaa, Mawaziri wote walikuwepo; leo tunaikanyaga Serikali kuisimamia kuhusu fedha zetu, Mawaziri hawapo. Kwa hiyo, kwa kweli, mimi inanishangaza sana kwamba kwenye uchaguzi wa Wabunge
tupo, lakini kwenye kusimamia fedha zetu hatupo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi niseme tu
kwamba naungana na ninakubaliana kabisa na mapendekezo ya Kamati na ninaomba tusivunje hili Bunge, kabla hatujaondoka, tukubaliane kwa sauti moja kwamba lazima Serikali iwajibike na sitegemei kama alivyosema Mheshimiwa Kangi Lugola kwamba yeye ameomba Mungu ndege ya Rais isije ikawekwa mafuta ikaanguka; mimi wala siombi ya Rais, zile ndege zinazopandwa na walalahoi za Watanzania ambazo leo hii zinawekwa mafuta ambayo pengine yamechakachuliwa, niombe Mungu kwa leo isianguke hata moja wakati tukisubiri Waziri kesho akitoa tamko na pengine achukue maamuzi magumu. Kama Wizara imemshinda, aachie ngazi Watanzania na watu wengi ambao wana uwezo wa kufanya kazi na wako committed. Nakushukuru sana.